URAIA NA MAADILI: SURA YA KWANZA

KUJIPENDA NA KUWAPENDA WATU WENGINE.

Msamiati

 1. Balehe Mabadiliko yanatokea kwa motto wa kiume na kike anapoingia utu uzima.
 2. Haiba Tabia nzuri na mwenendo wa kupendeza unaowafanya wengine wawe na mvuto kwako.
 3. Hedhi Damu inayomtoka mwanamke katika sehemu za siri anapo balehe.
 4. Jinsia Uhusiano wa kiutendaji kati ya mwanamke na mwanaume kwa mtazamo wa kijamii.
 5. Jinsi Tofauti kati ya mwanamke na mwanaume zinazotokana na maumbile yao.
 6. Kaniki Aina ya kitambaa cheusi cha nguo ya pamba, huvaliwa na wanawake badala ya kanga au kitenge.
 7. Kudhibiti Kuweka kitu chini ya mamlaka au kutawala kitu barabara.
 8. Mgolole Shuka ndefu inayovaliwa na baadhi ya viongozi wa kimila.
 9. Muktadha Mazingira ambamo tukio au jambo hutendeka.
 10. Staha Heshima au adabu.

Umahiri

Baada ya mada hii, mwanafunzi aweze,

 • Kuonyesha upendo kwake mwenyewe
 • Kuwapenda wengine hasa wenye mahitaji maalum
 • Kuwa na haiba na staha
 • Kuvaa mavazi ya heshima
 • Kutunza utamaduni wa jamii yake.

Utangulizi.

 • Ulipokuwa darasa la nne ulijifunza matendo ya kujipenda na kuwapenda watu wengine.
 • Katika sura hii, utajifunza matendo yenye kuonesha upendo kwa watu wenye mahitaji maalumu, kuheshimu jinsi na kuvaa mavazi yenye staha katika miktadha mbalimbali kulingana na utamaduni wa mtanzania.
 • Hii itakuwezesha kuishi vyema na watu katika jamii.

Kuwapenda watu wenye mahitaji maalumu

 1. Je, umewahi kusikia mtu akisema kuwa inakupasa kuwapenda wenzako? Je, upendo ni nini?
 2. Upendo ni tabia na matendo ya kutojiumiza au kutowaumiza watu wengine kwa makusudi, kimwili, kiroho au kisaikolojia. Mara nyingi, huwa tunasema kuwa upendo halisi hauna mipaka.
 3. Kwa kutambua hilo, inatupasa kujipenda na kuwapenda watu wengine bila ubaguzi. Watu wenye mahitaji maalumu wanahitaji upendo zaidi kwa sababu ya hali zao. Hivyo, inatupasa tusifanye matendo ya kuwaumiza.
 4. Mifano ya watu wenye mahitaji maalumu ni wazee, watu wasioona, watu wenye uoni hafifu, watu wenye ulemavu wa ngozi, watu wenye ulemavu wa akili na wenye ulemavu wa viungo vingine vya mwili. Mifano mingine ni watoto yatima na watu masikini.

Kutenda matendo yenye kuheshimu jinsia nyingine

 • Je, umewahi kusikia katika maisha yako neno jinsia? Mara nyingi watu hushindwa kutofautisha neno jinsi na jinsia. Wewe unafikiri maneno hayo yang maana moja?
 • Ipo tofauti kati ya maneno jinsi na jinsia. Neno jinsi lina maana ya tofauti za kimaumbile zilizopo kati ya mwanaume na mwanamke.
 • Tofauti za kijinsi na majukumu yake hayabadiliki kwa sababu ni ya kimaumbile.
 • Jinsia ni uhusiano uliopo kati ya mwanamke na mwanaume ulioundwa na jamii husika. Jinsia inahusu mgawanyo wa majukumu kati ya wanawake na wanaume katika jamii.
 • Japokuwa wanawake na wanaume wanatofautiana kimaumbile, wanaweza kushirikiana majukumu mbalimbali. Kwa mfano, wote wanaweza kuwa viongozi bora na pia wote wanaweza kufanya kazi za kitaalamu. Tofauti za kijinsia zinaweza kubadilishwa kulingana na uelewa wa haki za binadamu. Yapo matendo mengi yanayoonesha kuheshimu jinsi na kujali jinsia.

Hebu tafakari matendo yafuatayo:

 1. Mwanafunzi wa kike akimwelekeza mwanafunzi wa kiume kukokotoa maswali ya hisabati.
 2. Mwanafunzi wa kiume na wa kike wakiosha vyombo pamoja.
 3. Mwanafunzi wa kiume akimtua mwanafunzi wa kike ndoo ya maji kichwani.
 4. Mwanafunzi wa kiume akikataa kuketi katika dawati moja na wanafunzi wa kike.
 5. Wanafunzi wakigombana na kutumia lugha ya matusi kwa kutaja viungo vya maumbile ya kijinsi.

Je, ni matendo gani kati ya hayo ambayo hayaheshimu jinsi nyingine?

Matendo ya kudhalilisha kijinsi yanaonesha kuvunjiana heshima. Matendo kama haya yanapotokea, unapaswa kuyakemea na kutoa taarifa kwa walimu, wazazi, au walezi.

Matendo yanayoonesha usawa wa kijinsia:

 • Kutoa elimu sawa kwa mtoto wa kike na wa kiume
 • Kutambua kuwa mwanaume na mwanamke wote ni binadamu
 • Kutobaguana katika kutekeleza majukumu mbalimbali nyumbani na shuleni
 • Katika ukuaji wako utapitia hatua mbalimbali. Katika kila hatua unawajibika kujitambua, kujua majukumu yako, kujiheshimu na kuwaheshimu wenzako wa jinsi nyingine.
 • Kwa mfano, kuna hatua ya kuanza kupata hedhi kwa watoto wa kike na kubalehe kwa watoto wa kiume. Hiki ni kipindi cha kupevuka kimwili, kiakili na kimawazo.
 • Mabadiliko haya husababisha hisia ambazo zinaweza kuathiri mwenendo na haiba yako.
 • Hivyo, ni vyema kufikiri kabla ya kusema au kutenda. Maneno unayozungumza yasiwaudhi wenzako wa jinsi tofauti.
 • Pia, matendo unayotenda yasisababishe wao kuumia au kujiona wanyonge.
 • Inafaa kujenga uhusiano chanya kati ya wasichana na wavulana kwa kutambua mipaka ya uhusiano huo na umuhimu wa kuthamini utu wa mwingine.
 • Kwa mfano, siyo vizuri kumcheka mwenzako kutokana na kubalehe na kupata hedhi. Vilevile, si vizuri kutumia lugha za matusi au kumgusa mvulana au msichana viungo vyake vya maumbile ya kijinsi na kumbagua.
 • Mara zote, pale ambapo unabalehe au kupata hedhi mambo yanayoendana na jinsi yako yanaanza kubainika katika mwili. Kwa mfano, msichana anaweza kutoka chunusi usoni, kupata hedhi, kuota matiti na kupata mimba. Mvulana kwa upande wake anaweza kutoka chunusi usoni, sauti inaweza kuwa nzito, anaweza kuota ndoto nyevu na huweza kusababisha mimba.
 • Ili kuepuka madhara, kila jinsi iwajibike kujitunza kwa kutambua kuwa wakati huo siyo wa uhusiano wa kimapenzi. Hivyo basi, katika kipindi cha balehe unatakiwa kujijengea uwezo wa kudhibiti hisia zako.
 • Ili kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha madhara, ni vyema kujiepusha na mazingira hatarishi kama vile, kupita vichochoroni peke yako au matembezi yasiyo ya lazima ya usiku. Pia, wasichana wajiepushe na kupenda kupokea zawadi kutoka kwa wavulana au wanaume.

Soma kisa hiki, kisha jibu maswali yanayofuata.

Ana alikuwa msichana mwenye uwezo mkubwa sana darasani. Alikuwa mchangamfu, akishiriki kikamilifu kwenye michezo na ngoma mbalimbali shuleni. Alikuwa na marafiki aliokuwa akicheza nao. Alipofika darasa la tano alibadilika ghafla. Siku moja, nguo yake ilionekana imechafuka. Wenzake darasani walimcheka na wavulana wakaanza kumbeza kwa miluzi. Mvulana mmoja alimbinyia jicho.

Ana alianza kusononeka. Uchangamfu ulipungua na hakuwa anashiriki tena vizuri kwenye michezo. Alianza kujitenga na kutokushirikiana na wenzake katika kujifunza.

 • Mwanzoni Ana alikuwa mtoto wa aina gani shuleni?
 • Ana alipata mabadiliko gani?
 • Ana alifanyiwa vitendo gani ambavyo vilikiuka haki zake za kijinsi?
 • Una ushauri gani kwa wanafunzi wenzako wenye tabia kama ya wale waliomzomea na kumcheka Ana?
 • Kuna tofauti gani kati ya neno jinsi na jinsia?
 • Taja matendo ambayo ukitendewa utakuwa umedhalilishwa kijinsia.
 • Orodhesha matendo yanayofanyika shuleni kuonesha usawa wa kijinsia.
 • Taja matendo yanayoonesha kuheshimu jinsi nyingine.
 • Orodhesha matendo ya nyumbani yasiyoonesha usawa wa kijinsia. ,

Tofautisha kati ya udhalilishaji wa kijinsi na udhalilishaji wa kijinsia.

Kuvaa mavazi yenye staha katika miktadha mbalimbali

 1. Je, ni mavazi gani huwa unayavaa mara nyingi? Mavazi tunayovaa huwa yanabeba au yana tafsiri namna tuiivyo.
 2. Mavazi yenye staha yanaonesha tabia ya kujiheshimu na kujithamini. Je, unafikiri ni mavazi gani huonesha staha?
 3. Mavazi yenye staha kwa wasichana ni sketi ndefu isiyobana, gauni refu lisilobana, blauzi isiyoonesha matiti wala kitovu, suruali ambayo ni ndefu na isiyobana.
 4. Kwa upande mwingine, mavazi yenye staha kwa wavulana ni kama vile suruali ambazo hazibani maungo ya mwili wala zisizochanwa, au kuvaliwa chini ya kiuno.
 5. Uvaaji wa mavazi yenye staha huendana na miktadha. Kwa mfano, sehemu za ibada zina aina yake ya mavazi, shuleni huvaliwa sane zenye staha, michezoni huvaliwa mavazi ya aina yake kwa ajili ya michezo.
 6. Baadhi ya nguo huvaliwa na jinsi zote kama vile; suruali, kaptura na koti. Lakini mtoto wa kiume havai gauni wala sketi. Hali kadhalika, hall ya hewa huainisha aina ya mavazi yafaayo kuvaliwa. Kuna mavazi yanayotakiwa kuvaliwa wakati wa joto na yale yanayovaliwa wakati wa baridi. Mavazi yavaliwayo wakati wa baridi ni koti, sweta, mashati ya mikono mirefu na suti.
 7. Mavazi yanayovaliwa wakati wa joto ni kama vile, kaptura, magauni na mashati yenye mikono mifupi.
 8. Pia, baadhi ya watu huvaa mavazi kama magauni mapana, baibui, misuli na kanzu kwa mikoa yenye joto kama Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Hata hivyo, tuepuke kisingizio cha hall ya hewa kwa lengo la kuvaa mavazi yasiyo na staha.

Mavazi ya utamaduni

 1. Mavazi ya kiutamaduni ni mavazi ambayo hubeba utambulisho wa jamii fulani. Mavazi hayo hutambulisha mila na desturi za kabila fulani.
 2. Kuna baadhi ya mavazi ambayo huonesha tamaduni mbalimbali. Mavazi hayo ni kama lubega hasa kwa watu wa jamii ya kimasai; kanzu, msuli, koti na baraghashia hasa kwa jamii ya watu wa pwani.
 3. Vilevile, yapo mavazi maalumu yanayovaliwa na viongozi wa kimila kama vile watemi na machifu. Kwa mfano, machifu wa makabila ya Wangoni na Wahehe huvaa migolole.
 4. Pia, kuna mavazi maalumu wakati wa kucheza ngoma za kiasili. Mfano, kaptura nyeupe na shati jeupe huvaliwa rla watu wa kabila la Wanyasa kwenye ngoma ya mganda na nguo ya kaniki huvaliwa kwenye ngoma za asili za Kigogo.
 5. Kutokana na utandawazi, Tanzania imekuwa ni soko la mavazi yanayotoka kwenye tamaduni za nchi mbalimbali. Pamoja na matokeo ya utandawazi ambayo hayaepukiki, tunawajibika kuchagua mavazi yasiyotudhalilisha wala kushusha heshima yetu na ya nchi yetu.

www.learninghubtz.co.tz

URAIA NA MAADILI DARASA LA TANO: MTIHANI WA MWISHO WA MADA:

SURA YA KWANZA

1. Chagua jibu ambalo ni sahihi.

(i) Tunapaswa kuonesha upendo kwa watu

 1. Wenye mahitaji maalum
 2. Ndugu wa karibu
 3. Watu wanotupenda
 4. Watu wote bila ubaguzi.

(ii) Wafuatao wana mahitaji maalum isipokuwa:

 1. Wazee
 2. Watoto
 3. Watu wenye ulemavu wa akili
 4. Yatima na maskini.

(iii) Tofauti gani sio ya kimaumbile kati ya mwanaume na mwanamke?

 1. Kupata hedhi
 2. Kupata mimba
 3. Uwezo wa kuzaa
 4. Kunyonyesha

(iv) Tendo gani kati ya haya halionyeshi usawa wa kijinsia.

 1. Kutoa elimu sawa kwa mtoto wa kike na kiume
 2. Kutambua kuwa mwanaume na mwanamke wote ni binadamu
 3. Majukumu ya jikoni kuachiwa wasichana
 4. Kutobagua wasichana katika elimu

(v) Moja ya mabadiliko ya wasichana wanapo balehe ni

 1. Kuongezeka kwa kimo
 2. Kuonyesha heshima zaidi
 3. Kupata hedhi
 4. Kuwa na mpenzi wa jinsia tofauti.

(vi) Wasichana wanaweza kujiepusha na mimba za mapema kwa;

 1. Kuwa na marafiki waaminifu
 2. Kwenda disko na jamaa zao
 3. Kupokea zawadi kutoka kwa wavulana
 4. Kuepuka matembezi yasiyo ya lazima usiku.

(vii) Kwanini tunapaswa kuvaa mavazi yaliyo na staha?

 1. Yanaonyesha kujiheshimu
 2. Yanasaidia kuepuka magonjwa
 3. Ili tupendwe
 4. Ili tuvutie watu

(viii) Kabila gani huvaa kaniki kwenye ngoma za asili?

 1. Maasai
 2. Wagogo
 3. Wanyasa
 4. Wasukuma

(ix) Mabadiliko ya kimwili ya mtoto wa kiume na wa kike kuingia utu uzima huitwa

 1. Jinsia
 2. Kuvunja ungo
 3. Utu uzima
 4. Balehe

(x) Ipi sio staha katka jamii

 1. Kuvalia nguo inayokustiri
 2. Kucheza na wavulana sehemu za uchochoro
 3. Kuwasalimia watu kwa heshima
 4. Kupenda watu wote

2. Andika kweli au si kweli kwa matendo yafuatayo.

 1. Upendo halisi ni kujipenda mwenyewe_____________
 2. Watu wenye ulemavu wana mahitaji maalum_______________
 3. Moja ya mahitaji ya kwanza ya mtu ni upendo__________________
 4. Majukumu ya kujinsia hubadilika_______________
 5. Majukumu ya kijinsia hubadilika kutokana na mtazamo wa jamii husika____________
 6. Watoto wa jinsia zote wanapaswa kujiheshimu na kuheshimiwa _____________
 7. Wanaume wote hawashiriki kabisa kupika chakula cha nyumbani___________
 8. Mavazi ya heshima yanaonyesha tabia ya kupitwa na wakati na ushamba___________
 9. Mavazi mengine huvaliwa na wanawake na wanaume_________________
 10. Vazi la lubega huvaliwa na wamasai_______________

3. Taja mabadiliko yanayotokea kwa wasichana wakati wa kubalehee

4. Je unapaswa kufanya nini ili kujiepusha na hatari za mimba kama msichana?

5. Taja makundi manne ya watu wenye mahitaji maalum ambao wanahitaji upendo wako.

6. Kwanini tunapaswa kuvaa mavazi yenye heshima?

7. Tunawezaje kuwaonyesha upendo watu walio na mahitaji maalumu?

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256