URAI NA MAADILI : SURA YA PILI

KUJIVUNIA SHULE NA KUIPENDA NCHI YETU

Msamiati.

  • Dola Chombo chenye mamlaka ya kuendesha utawala au siasa ya nchi.
  • Dukuduku Machungu, wasiwasi au mfundo unaomsonga mtu moyoni.
  • Dumisha Kuendeleza Jambo Fulani kama mila
  • Katiba Kanuni, taratibu au sheria ambazo huwezesha serikali itawale au chama au kampuni iendeshe shughuli zake.
  • Maslahi manufaa au faida aipatayo mtu baada ya kufanya kazi, biashara au kumaliza tendo lolote.
  • Mhimili Nguzo au kitu kinachozuia kingine kisianguke
  • Minajili Kwa ajili ya..
  • Thamini Kukipa kitu hadhi..

Umahiri.

Baada ya kujifunza mada hii, mwanafunzi anatakiwa aweze;

  • Kuonyesha upendo kwa shule na nchi yake
  • Kujivunia nchi yake na shule yake
  • Kujitolea katika shughuli mbalimbali
  • Kuendeleza utamaduni wa watanzania.
  • Kuheshimu Katiba ya Nchi.

Kujivunia shule na kuipenda nchi yetu

Utangulizi.

Karibu katika sura pili. Katika sura ya kwanza, ulijifunza matendo yenye kuonesha upendo kwa watu wenye mahitaji maalumu, kuheshimu jinsi na kuvaa mavazi yenye staha. Katika sura hii, utajifunza mambo yanayoiletea shule sifa nzuri. Pia, utajifunza umuhimu wa kuenzi tunu za taifa letu ambazo ni tamaduni, mila na desturi zetu. Vilevile, utajifunza alama za utambulisho wa taifa letu pamoja na sikukuu za kitaifa.

Kuipenda na kujivunia shule yetu

Hebu jiulize, je, unaipenda shule yako? Je, unajivunia shule yako? Unajivunia vitu gani katika shule yako?

  1. Sifa nzuri za shule zinajumuisha tabia njema za wanafunzi na walimu, majengo safi na mazingira yanayovutia.
  2. Hivyo, sifa nzuri ya shule inatokana na shule kuwa na mazingira yanayotunzwa kwa kupandwa miti ya vivuli, miti ya matunda pamoja na maua.
  3. Vilevile, sifa nzuri ya shule huchangiwa na wanafunzi kuwa nadhifu kwa kutunza sare zao na vifaa wanavyotumia katika mchakato wa kujifunza. Wanashirikiana kutunza rasilimali na samani za shule kama vile majengo, madawati, viti, vitabu na madaftari yao.
  4. Hali kadhalika, wanafunzi wanajituma na kuwajibika ipasavyo bila kusukumwa na mtu mwingine. Uwepo wa mambo yote haya husababisha ufaulu mzuri na kujenga sifa nzuri ya shule.
  5. Sifa mbaya za shule zinajumuisha tabia zilizopo shuleni ambazo hazikubaliki miongoni mwa jamii inayoizunguka.
  6. Sifa mbaya ya shule inachangiwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na uchakavu wa miundombinu na mazingira machafu.
  7. Pia, kuna vitendo vya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya wanafunzi, kama vile kutovaa sare ya shule kikamilifu, kushindwa kufua sare zao na kuchana madaftari na vitabu.
  8. Vilevile, baadhi ya wanafunzi wana tabia ya utoro, uvivu na kuchelewa kufika shuleni. Hali hii huchangia sifa ya shule kuwa mbaya. Aidha, matendo ya baadhi ya walimu kuonesha Labia za uvunjifu wa taratibu na sheria za kazi.
  9. Mfano wa vitendo hivyo ni ugomvi baina ya walimu, walimu na wanafunzi, walimu kutotumia lugha yenye staha wawapo mazingira ya shule au katika jamii. Mambo yote hays yanaweza kusababisha shule kuwa na sifa mbaya.

Nembo ya shule yetu

  • Nembo ni alama maalumu inayotambulisha kitu fulani. Nembo ya shule ni alama inayoitambulisha shule inayohusika.
  • Kwa kawaida nembo ya shule hujumuisha kauli mbiu ya shule, shughuli mbalimbali za shule kama vile shughuli za kitaaluma, elimu ya kujitegemea na mazingira ya shule.

image

Kielelezi namba 1: Nembo ya shule

  • Je, shule yako ina nembo inayoitambulisha? Je, nini kauli mbiu ya shule yako? Ili kuifaharnu vizuri nembo ya shule yako mwalimu atakuonesha na pia atakuongoza kuichora.

Kufanya shughuli mbalimbali za kujitolea shuleni

  1. Je, umewahi kufanya kazi za kujitolea shuleni kwako? Ufijisikiaje ulipofanya hivyo? Ilikuwa shughuli gani? Kujitolea ni tabia ya kufanya jambo kwa hiari bila kushurutishwa na pasipo kujali maslahi binafsi.
  2. imageKwa mfano, unaweza kujitolea kupanda miti na maua katika mazingira ya shule au kuanzisha bustani za mboga. Pia, unaweza kuanzisha na kushiriki katika kiabu mbalimbali kwa mfano skauti, klabu ya mazingira, klabu ya UKIMWI, klabu ya kutoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa na kiabu ya elimu kwa mlipa kodi.
  3. Kielelezi namba 2: wanafunzi wakijitolea kufanya usafi.
  4. Aidha, unaweza kushiriki katika shughuli ya kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa ofisi, madarasa na vyoo vya shule
  5. Pia, unaweza kushiriki katika shughuli mbalimbali shuleni hasa za elimu ya kujitegemea iii kuleta maendeieo katika shule na kuongeza kipato.
  6. Baadhi ya shughuli hizo ni kilimo na ufugaji, kuanzisha vitalu vya kuotesha miche ya miti na kujiunga na masomo ya ziada ya ufundi stadi endapo shule yako ina masomo hayo.

Tunu za nchi yetu

  • Tunu ni mambo yote ya thamani ambayo watu hujionea fahari kuwa nayo. Je, tunu za nchi ya Tanzania ni zipi?
  • Tunu za nchi yetu ya Tanzania ni;
  • lugha yetu ya Kiswahili,
  • umoja,
  • uzalendo,
  • uwajibikaji,
  • upendo,
  • heshima,
  • utu na kuwajali wazee.
  • Sisi sate yatupasa kuipenda na kujivunia nchi yetu kwa kuzienzi tunu zinazoitambulisha. Vilevile, ni muhimu kuheshimu mila na desturi zetu na kudumisha tamaduni zetu kama sehemu ya tunu za taifa.

Mila na desturi za Kitanzania

  • Je, umewahi kusikia mtu akikuambia tudumishe mila na desturi zetu? Ulielewa kuwa anamaanisha nini?
  • Mila na desturi ni namna tulivyozoea kufanya mambo katika jamii yetu tangu zamani. Mila na desturi vinaweza kutafsiriwa kama ni mapokeo ambayo jamii hurithishana kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

image

Kielelezi namba 3: Utamaduni wa Watanzania.

  • Mila na desturi hujenga au kuunda utamaduni ambao ndio utambulisho wa jamii hiyo.
  • Nchini Tanzania kuna mila na desturi mbalimbali ambazo hubeba utambulisho wa jamii mbalimbali.
  • Kuna mila na desturi zinazofaa na zisizofaa, kama ilivyobainishwa katika Jedwali namba 1.

Mila na desturi zinazofaa

Mila na desturi Zisizofaa

  1. Vijana kwendo jandoni na kujifunza majukumu ya utu uzima.
  2. Kuhimiza watu wote kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano.
  3. Zinazohimiza wanafamilia kufanya kazi za nyumbani bila kujali jinsia.
  4. Mgawanyo wa kazi unaozingatia usawa wa kijinsia.
  5. Haki za watoto zinaheshimiwa.
  1. Mila zinazohimiza wanawake kubeba majukumu ya familia na kuacha familia.
  2. Kukeketa wasichana na kucheza ngoma zisizo na maadili.
  3. Kuhimiza uvivu na jinsia moja kutojishughulisha sawa sawa katika majukumu.
  4. Mgawanyo wa kazi usio zingatia usawa wa kijinsia.
  5. Watoto kutokua na haki.

Jedwali namba 1: Sikukuu za Kitaifa

  • Ili kuimarisha utamaduni wa taifa, inatupasa kudumisha mila na desturi zinazofaa na kutokomeza mila na desturi zisizofaa ambazo ni kikwazo kwa maendeleo ya familia, jamii na hata taifa kwa ujumla.

Kudumisha utamaduni wa taifa

  • Umewahi kusikia neno utamaduni? Je, umewahi kuwaza maana ya neno
    hili? Tunaweza kuutafsiri utamaduni kuwa ni mwenendo wa maisha unaohusisha asili, mila, desturi, jadi, au itikadi inayotawala katika jamii fulani.
  • Pia, ni mtindo wa jurnia wa maisha ya jamii fulani. Hivyo, kudumisha utamaduni wa taifa ni kuzingatia mila na desturi zinazofaa, pamoja na mambo mengine yote yanayojenga umoja katika jamii na taifa.

Umuhimu wa utamaduni

  • Utamaduni ndio unaobeba utambulisho wa taifa letu. Pia, utamaduni unajenga moyo wa kujiamini na kujithamini.
  • Kwa mfano, lugha ya Kiswahili hulitambulisha taifa la Tanzania. Wasanii wanapokwenda nje ya nchi hulitambulisha taifa letu kwa sanaa wanayoipeleka huko.
  • Vilevile, utamaduni hujenga umoja, upendo, ushirikiano, kuthaminiana na kuheshimiana.
  • Utamaduni hudumisha mila na desturi za jamii kwa kupitia mafunzo mbalimbali ya vijana, kwa mfano mafunzo ya jando na unyago katika jamii fulani kulingana na wakati.
  • Mafunzo hayo huwawezesha kuishi maisha yanayokubalika katika jamii husika. Pia, utamaduni huhimiza kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, iii kupanua fursa za ajira.
  • Kazi za sanaa kama vile maigizo, muziki, michezo, ngoma na kuchonga vinyago huimarisha kipato cha mtu binafsi, jamii na taifa.
  • Aidha, kwa kupitia utamaduni tunapata burudani katika miktadha mbalimbali; mfano, nyimbo na ngoma za asili zinapochezwa.
  • Nyimbo na ngoma za asili pia hutumiwa na makabila mbalimbali kama kichocheo cha kuhamasisha kufanya kazi kwa bidii, kujenga tabia nzuri na nidhamu katika maisha. Kwa mfano, kabila la Wasukuma hupiga ngoma wakati wa kulima iii kuhamasisha ari ya kufanya kazi.
  • Tunaweza kudumisha utamaduni wetu kwa njia mbalimbali. Njia mojawapo ni kwa kushiriki katika mambo ya sanaa na ngoma za asili.
  • Njia nyingine ni kutumia lugha zetu za asili, kuitumia na kuienzi lugha ya Kiswahili katika matukio mbalimbali mfano, shughuli za kiserikali na za kijamii. Aidha, tunatakiwa kujivunia, kutumia na kuyaenzi mavazi yetu ya asili, kudumisha mila na desturi zinazofaa, kutumia na kuvitangaza vyakula vyetu vya asili. Pia, tunatakiwa tuzienzi mila na desturi zetu hasa zile zinazoimarisha uhusiano mwema.
  • Vilevile, ni muhimu kuidumisha heshima na uhusiano kwa kuzingatia taratibu za kusalimiana katika jamii. Kwa mfano, kwa kawaida mtu mwenye umri mdogo ndiye anayepaswa kuanza kumsalimia mtu mwenye umri mkubwa. Utamaduni ni kielelezo cha uhai wa jamii yetu.

Alama za taifa

Ulipokuwa darasa la nne ulijifunza matendo ya kuipenda nchi yetu kama vile kuonesha heshima kwa wimbo wa taifa na bendera ya taifa, pamoja na kuthamini fedha ya Tanzania. Katika sura hii, utajifunza kwa undani zaidi matumizi ya alama hizi za taifa. Aidha, utajifunza matumizi ya bendera ya taifa, wimbo wa taifa, mnyama wa taifa (twiga), nembo ya taifa. fedha ya taifa, bendera ya rais, mwenge wa uhuru, katiba ya Jamhuri ya Muunaano wa Tanzania na ramani ya Tanzania.

Matumizi ya alama za taifa

Je, ulishajiuliza umuhimu wa alama za taifa? Alama hizi hutumika wakati fulani, kwenye mazingira fulani na kwa lengo fulani. Hebu tuyabaini matumizi ya alama za taifa la Tanzania.

Bendera ya taifa

Bendera ya taifa inaitambulisha nchi ya Tanzania miongoni mwa mataifa
mengine. Bendera yetu ya taifa hupepea katika nchi zote ambako Tanzania

imefungua ofisi za ubalozi. Pia, viongozi na baadhi ya Watanzania wanaposafiri nje ya nchi kwa lengo Ia kuiwakilisha Tanzania, hubeba bendera yetu ya taifa.

  1. Bendera ya taifa hutambulisha pia vyombo vya usafiri vinavyosajiliwa Tanzania. Vyombo hivyo ni meli, ndege, magari na pikipiki. Vilevile, bendera ya taifa hutambulisha ofisi au taasisi za serikali kama vile shule, ofisi ya serikali ya kata, wilaya na mkoa, majengo ya mahakama na ofisi za wizara mbalimbali.

image

Kielelezi namba 4: Bendera ya Taifa

  1. Pia, bendera ya taifa hutumika kuonesha majonzi pale inapotokea msiba au janga Ia kitaifa. Mifano ya majonzi hayo ni kama vile kifo cha baba wa taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ajali ya MV Bukoba iliyotokea tarehe 21 mwezi wa 5 mwaka 1996 na Kivuko cha MV Nyerere iliyotokea tarehe 20 mwezi wa 9 mwaka 2018 katika Ziwa Viktoria ambapo meli na kivuko hicho vilizama na kusababisha vifo vya watu wengi. Katika maombolezo ya matukio kama hayo bendera ya taifa hupepea nusu mlingoti.

Wimbo wa taifa

  1. Kwa kiasi kikubwa matumizi ya wimbo wa taifa yanafanana na yale ya bendera ya taifa. Wimbo wa taifa huimbwa wakati viongozi wa nchi wanapotembelea nchi nyingine.
  2. Pia, huimbwa wakati vikundi vya utamaduni na michezo wanapocheza michezo ya kimataifa ndani na nje ya nchi. Pia, wimbo wa taifa huimbwa kabla ya tangazo Ia msiba wa kiongozi mkuu wa nchi, kama vile rais, makamu wa rais na waziri mkuu.
  3. Hali kadhalika, kabla ya rais kufanya uzinduzi wa jambo muhimu linalogusa maslahi mapana ya taifa, huimbwa wimbo wa taifa. Mfano wa matukio hayo ni uzinduzi wa meli mpya au ndege mpya. Aidha, wimbo wa taifa huimbwa katika taasisi mbalimbali kama vile, shuleni na katika vikosi vya majeshi yetu ili kukuza uzalendo.
  4. Vilevile, wimbo wa taifa huimbwa katika matukio muhimu ya kitaifa, kama vile sikukuu za kitaifa na hafla zinazohusisha viongozi wakuu wa serikali.

Mnyama wa taifa

Je, unamfahamu mnyama wa taifa? Anaitwa nani ? Na ulimwona wapi? Mnyama wa taifa la Tanzania anaitwa twiga. Mnyama huyu hutumika kama alama kificho katika fedha ya noti ya Tanzania. Pia, hutumika pamoja na alama ya bendera ya taifa kutambulisha ndege inayomilikiwa na Serikaya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile, alama ya twiga hutumika kama kielelezo cha utajiri wa maliasili iliyopo Tanzania.

image

Kielelezi namba 5: Mnyama wa Taifa

Nembo ya taifa la Tanzania

Je, umewahi kuiona nembo ya taifa? lna vitu gani? Uliiona wapi? Nembo ya taifa ina jumla ya alama 13 ambazo ni: mwanamke na mwanaume, mwenge wa uhuru, pembe za ndovu, mlima Kilimanjaro, mawimbi ya bahari, bendera ya taifa, mkuki, mazao ya pamba na karafuu, jembe na shoka, ukanda wenye maneno uhuru na umoja, rangi ya njano na nyekundu.

image

Kielelezi namba 6: Nembo ya Taifa

  1. Nembo ya taifa inatumika kuonesha umiliki wa mali na nyaraka za Serikali ya Tanzania. Alama hiyo huonekana katika vitabu na machapisho mbalimbali ya serikali, hati za kusafiria nje ya nchi na mavazi ya viongozi wa juu wa kijeshi. Pia, hutumika katika mawasiliano rasmi ya kiserikali kama vile barua za kiserikali na matamko ya kiserikali. Nembo ya taifa la Tanzania hutumika pia kama muhuri wa rais.

Fedha ya Tanzania

Alama nyingine ya kitaifa ni fedha ya Tanzania. Fedha ya Tanzania inaitwa shilingi. Fedha hutumika kwa namna mbili. Hutumika kuitambulisha Tanzania kama nchi huru. Pia, hutumika kuthamanisha vitu na mall. Fedha ya Tanzania iko katika sura mbili: noti na sarafu.

image

Kielelezi namba 7: Fedha ya Taifa

Bendera ya Rais

Alama hii hutumika kutambulisha mamlaka rasmi ya rais katika shughuli rasmi ambazo rais anahudhuria ndani au nje ya nchi. Vilevile, hutumika katika chombo cha usafiri anachokitumia rais.

Mwenge wa uhuru

Mwenge wa uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza juu ya kilele cha mlima Kilimanjaro siku ambayo Tanganyika ilipata uhuru tarehe 9 mwezi wa 12 mwaka 1961. Mwenge huu wa uhuru hutumika kukumbuka na kuitambulisha Tanzania kama nchi huru. Hutumika pia kuonesha mshikamano wa kitaifa. Mwenge wa uhuru hutumika katika matukio ya kuzindua baadhi ya miradi ya maendeleo nchini pindi unapokimbizwa kwenye maeneo husika. Vilevile, mwenge wa uhuru hutumika kuhamasisha na kudumisha uzalendo kwa Watanzania. Wakati wa kukimbiza mwenge wa uhuru, kuna wimbo maalumu unaoimbwa iii kuwakumbusha Watanzania jukumu lao la kuulinda uhuru wao.

image

Kielelezi namba 8: Mwenge wa Uhuru


Mbio za mwenge hufanyika mara moja kila mwaka kuzunguka nchi nzima.

Hebu imba, kisha tafakari maudhui ya wimbo huu wa "Kuwasha mwenge."

"Sisi tumekwisha kuwasha Mwenge, Tumekwisha kuwasha Mwenge,

Na kuuweka juu ya mlima,

Mlima Kilimanjaro.

Kuwasha Mwenge,

Kuwasha Mwenge,

Na kuuweka Kilimanjaro.

Umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini,

Pale ambapo hakuna matumaini, Upendo mahali ambapo pana chuki, Na heshima ambapo pamejaa dharau."

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

  1. Je, umewahi kuiona katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Je, umewahi kuisoma?
  2. Katiba ni sheria, kanuni na taratibu zinazotumika kuendesha shughuli za nchi, chama au kikundi cha watu wenye malengo yanayofanana.
  3. Tanzania tunatumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo ni sheria mama inayoainisha misingi mikuu ya kisiasa na kuonesha muundo, madaraka na majukumu ya serikali. Katiba huonesha pia haki na wajibu wa raia wa Tanzania.
  4. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni alama mojawapo miongoni mwa alama zinazolitambulisha taifa letu.
  5. Katiba hutumika kuhifadhi na kulinda sheria zote zinazotungwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inaeleza bayana mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili mikuu mitatu ya dola ambayo ni serikali, bunge na mahakama.
  6. Katiba hutumika wakati viongozi wanapoapishwa baada ya kuteuliwa na kuchaguliwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi. Wanaapishwa na katiba ill kuitetea na kuilinda katiba hiyo. Vilevile, katiba hueleza bayana madaraka na mipaka ya viongozi iii kuepusha migogoro na matumizi mabaya ya madaraka.
  7. Aidha, katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huhifadhi sheria zinazotetea imaslahi na haki za binadamu.

Ramani ya Tanzania

  1. Alama hii hutumika kutambulisha na kuonesha mipaka ya nchi yetu na nchi nyingine zilizo jirani yetu. Upande wa mashariki,Tanzania inapakana na Bahari ya Hindi, upande wa magharibi inapakana na nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Rwanda.
  2. Upande wa kaskazini Tanzania imepakana na nchi za Kenya na Uganda. Upande wa kusini.

 

 Kielelezi namba 9: Ramani ya Tanzania

 

Sikukuu za kitaifa

  1. Je, unazifahamu sikukuu gani za kitaifa? Kama mwanafunzi umeshawahi kushiriki sikukuu gani za kitaifa?
  2. Sikukuu za kitaifa ni zile siku zinaadhimishwa kitaifa kila mwaka, ili kukumbuka matukio muhimu ya kitaifa. Ifuatayo ni orodha ya sikukuu zinazoadhimishwa kitaifa nchini Tanzania:

Jedwali namba 2: Sikukuu za Kitaifa

Tarehe

Sikukuu

1 Januari

Mwaka Mpya

12 Januari

Kumbukumbu ya siku ya Mapinduzi Zanzibar

07 Aprili

Kumbukumbu ya kifo cha rahisi wa kwanza Zanzibar- Sheik Abeid Amani Karume.

26 April

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar

01 Mei

Siku ya wafanya kazi Duniani

07 Julai

Maonyesho ya Kibiashara ya kimataifa

08 Agosti

Sikukuu ya wakulima Tanzania

14 Agosti

Kumbukumbu ya kifo cha Raisi wa Kwanza wa Tanzania- Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

09 Disemba

Uhuru wa Tanganyika

Pia, kuna sikukuu nyingine za dini ya Wakristo kama vile Krismas. ljumaa Kuu, Pasaka na Jumatatu ya Pasaka. Vilevile, kuna sikukuu za Waislamu, mfano Eid - El Fitri, Eid - El Haji na Maulid.

Umuhimu wa sikukuu za kitaifa

  • Sikukuu za kitaifa hutumika kuenzi matukio ya kitaifa na kudumisha ujumbe ulio katika matukio kayo.
  • Sikukuu za kitaifa, hutoa fursa kwa viongozi kueleza mafanikio na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi.
  • Wakati wa maadhimisho ya sikukuu hizo, viongozi hutumia nafasi hizo kuchanganua na kufafanua mambo ya kitaifa na kutafakari mwelekeo wa nchi.
  • Pia, hutoa elimu mbalimbali kwa wananchi kuhusu mambo yanayohusu maendeleo ya nchi yao.
  • Kwa mfano, wakati wa sherehe za wakulima ambazo huadhimishwa tarehe 8 mwezi wa 8 kila mwaka, viongozi wetu wa kitaifa huwahamasisha wakulima kutembelea maonesho mbalimbali yatakayo wasaidia wakulima kupata mbinu na njia za kisasa za kuboresha kilimo na ufugaji.
  • Vilevile, sikukuu hizi huwasaidia wananchi kupata fursa ya kuwasiliana na viongozi wao.
  • Aidha, kwa kupitia sikukuu hizi wananchi hupata fursa ya kusherehekea mafanikio na kutafakari changamoto mbalimbali. Mfano, katika sikukuu ya Mei Mosi wafanyakazi hutoa dukuduku zao kuhusu changamoto zinazowakabili.

www.learninghubtz.co.tz

KUJIVUNIA SHULE NA KUIPENDA NCHI YETU : MTIHANI WA MWISHO WA MADA

SURA YA PILI

1. Chagua jibu sahihi kwa kuandika herufi ya jibu kwenye nafasi iliyo hapo chini.

(i) Maana ya utamaduni ni:-

  1. Ushabiki wa kitu au jambo unalolipenda
  2. Mtindo wa jumla wa maisha ya watu katika jamii au taifa Fulani
  3. Shughuli za asili zinazofanywa na watu

(ii) Baadhi ya alama zipatikanazo kwenye fedha ya Tanzania ni

  1. Twiga Tembo, Nembo ya taifa na sura ya rais
  2. Nembo , nyumbu na kifaru
  3. Mwenge , twiga na sokwe

(iii) Umuhimu wa bendera ya rais ni

  1. Kutembelea katika ziara mbalimbali tu
  2. Kuonyesha mamlaka ya rais
  3. Kuhamasisha mwenge wa uhuru

(iv) Chimbuko la sheria zote nchini Tanzania ni;

  1. Fedha ya Tanzania
  2. Katiba ya Jamhuri wa muungano wa Tanzania.
  3. Vyama vya siasa

(v) Rangi ya bluu iliyopo katika bendera ya taifa uwakilisha;

  1. Watanzania
  2. Madini
  3. Maji ambayo ni mito, maziwa na bahari nchini Tanzania

(vi) Alama ambayo hutumika kuonyesha umiliki wa mali na nyaraka za serikali tu ni;

  1. Picha ya makamu wa rais
  2. Bendera ya taifa
  3. Nembo ya Taifa

(vii) Ni ishara gani inayoonyesha kwamba taifa limepatwa na msibu mkubwa?

  1. Bendera zote kupepea nusu mlingoti
  2. Bendera ya taifa kupepea nusu mlingoti
  3. Bendera ya taifa kutopandishwa kabisa siku ya tukio

(viii) Ni siku ambazo viongozi hupata fursa kueleza mafanikio na changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi

  1. Siku za kukimbizwa mwenge wa uhuru tu
  2. Sikukuu ya mapinduzi ya Zanzibar tu
  3. Sikukuu za kitaifa

(ix) Zipi kati ya hizi ni mila zisizofaa katika jamii?

  1. Kufanya kazi kwa ushirikiano
  2. Kuwakeketa wasichana
  3. Kuhamasisha wanaume na wanawake kushirikiana kufanya kazi za nyumbani hili kujiongezea kipato.

(x) Mifano ya vikundi vinavyoweza kuundwa shuleni ni kama;

  1. Skauti, klabu za mazingira, klabu ya TAKUKURU. Klabu za masomo
  2. Upatu, ushirikiano na vyama vya siasa
  3. Skauti, singeli na ngoma za asili.

2. Andika kweli au si kweli kwa maswali yafuatayo:-

  1. Ikiwa nchi ina sifa mbaya hatupaswi kuipenda.
  2. Nembo ya shule hujumuisha kauli mbiu ya shule
  3. Tunapaswa kutopoteza muda kwa kushiriki kazi za kujitolea
  4. Umoja na upendo ni mojawapo ya tunu za Taifa letu.
  5. Mila na tamaduni husaidia kutambulisha jamii fulani
  6. Kutumia lugha zetu za asili kunavunja utaifa.
  7. Moja wapo kati ya alama za taifa ni twiga
  8. Bendera zote hupandishwa nusu mlingoti wakati wa msiba wa Taifa.
  9. Mwenge wa Uhuru uliwashwa mara ya kwanza tarehe 9 mwezi wa 12 mwaka 1961
  10. Tanzania inapakana na nchi Tisa.

3.

  1. Ni nini maana ya alama ya Taifa
  2. Taja alama za Taifa

4.

  1. Nembo ya Taifa ina alama ngapi?
  2. Orodhesha tunu za Taifa za Tanzania.
  3. Eleza manufaa ya katiba kwa watanzania.

5.

  1. Nembo ya shule ni nini?
  2. Eleza umuhimu wa nembo ya shule
  3. Bainisha mambo ya msingi yaliyo kwenye nembo ya Taifa

6.

  1. Utamaduni ni nini?
  2. Eleza umuhimu wa utamaduni katika Taifa.
Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256