KISWAHILI SURA YA KWANZA : KUIPENDA NCHI YANGU

KUIMBA WIMBO WA KIZALENDO

Mungu ibariki Afrika

Wabariki Viongozi wake

Hekima Umoja na Amani

Hizi ni ngao zetu

Afrika na watu wake.

Kiitikio:

Ibariki Afrika, Ibariki Afrika

Tubariki watoto wa Afrika.

Mungu ibariki Tanzania

Dumisha uhuru na Umoja

Wake kwa Waume na Watoto

Mungu Ibariki Tanzania na watu wake.

Kiitikio:

Ibariki Tanzania, Ibariki Tanzania

Tubariki watoto wa Tanzania.

SHAIRI LA TANZANIA YANGU.

1. Sauti yangu napaza, namuomba Rahamani,

Nianze kuzungumza, sikizeni kwa makini,

Haya niliyoyawaza, humu kwangu akilini,

Naisifu Nchi yangu, kwa nudhumu maarufu.

2. Kwa nudhumu maarufu, na vina kupangila,

Mizani kama mkufu, beti kuzishikilia,

Na mishororo mirefu, mantiki kupangilia,

Karibu utiririko, malengo nikupeleke.

3. Nchi yangu ya thamani, mimi kweli naipenda,

Wale wasioithamini, naona wafanya inda

Hata sijui kwa nini, kwa nchi yao wakonda,

Hakika tuithamini, kwa moyo mweupe kwabu.

4. Nchi ninayoipenda, popote ulimwenguni,

Kila utakapokwenda, Nchi yetu ina shani,

Kila mtu anaipenda, Nchi yetu ya thamani,

Kwa kweli usipopenda, nakuona hayawani.

5. Nakuona hayawani, mimi ninakuheshimu,

Unachfanya ni nini, na wala huoni tabu,

Hat ng’ambo hupaoni, umekua kama dubu,

Nchi ya kujivunia, wala sioni aibu.

6. Wala sioni soni, Nchi yangu kuisifu,

Hebu chunguza amani, hakika ni utukufu,

Hata uvue miwani, utauona mkufu,

Nchi hii burudani, imenikuna mtima.

7. Mtima imenikuna, kwa dafina teletele,

Samaki wa kumimina, changu, sato, kolekole,

Ziwa la kina kirefu, kina kirefu milele,

Thamani ya Nchi yangu, haithithiliki kamwe.

8. Kamwe haithithiliki, ikitazama bahari,

Bandari hazipimiki, mimi naona fahari,

Uvuvi haushikiki, pwani yote i tayari,

Nani bado haelewi? Ajikune nimuone.

9. Ajikune nimuone, aone ule mlima,

Kwanza mawenzi aone, kilele kimesimama,

Kisha kibo apaone, theluji isiyohama,

Kuipenda Nchi yangu, hakika ni maridadi.

10. Ni maridadi hakika, wala sioni hiyana,

Unguja inashikika, historia bayana,

Pemba nayo kwa hakika, marashi yake mwanana,

Nchi yangu maridadi, sichoki kujivunia.

11. Sichoki kujivunia, wanyama wa kupendeza,

Mikumi najivunia, Serengeti yapendeza,

Wanyama wang’ang’ania, mbugani wajipenyeza,

Nani bado ana swali, mwambieni aulize.

12. Aulize mwambieni, nimpeleke ruaha,

Au mikumi twendeni, akaipate furaha,

Hata gombe mwambieni, twendeni aonje raha,

Nchi yangu kusifia, mimi naona fahari.

13. Fahari bado naona, kuzungumzia mito,

Malagarasi mwaona, Rufiji siyo kijito,

Ruvu kagera mwanana, pangani pia ni mito,

Hakika siwezi choka, mimi ninajivunia.

14. Nchi ninajivunia, ni hakika na ni wajibu,

Vito vya kujivuna, almasi na dhahabu,

Tanzaniti sikia, rubi na gesi nasibu,

Asiyejua ni nani, tumwonyeshe mashujaa.

15. Mashujaa wa uhuru, Nyerere naye Karume,

Wengine walio huru, Mwinyi na tena Karume,

Mkapa, Jakaya, Nuru, Sheni, Pombe wanaume,

Amani wameitunza, viongozi wetu safi.

16. Viongozi walitamba, sera wakaziansisha,

Ujamaa ukapambana, azimio likatisha,

Utandawazi twaomba, kasi mpya nakumbusha,

Ikafata hapa kazi, matokeo yote chanya.

17. Matokeo yote chanya, mijini na vijijini,

Umeme ninawatonya, hadi huko vijijini,

Barabara nawakanya, msilime kwa mpini,

Nani ambaye haoni, ujenzi wa reli mpya?

18. Ujenzi mpya wa reli, na wa anga usafiri,

Watalii mbalimbali, salama wataabiri,

Hakuna tena pa mbali, wala ya mbali safari,

Nchi inasonga mbele, vijiji na mijini.

19. Vijijji na mijini, elimu b ila malipo,

Afya hata vijijini, zahanati sasa zipo,

Tunaona na mijini, madaraja sasa yapo,

Tazama fahari yangu, kuitwa mtanzania.

20. Kuitwa mtanzania, fahari yangu na yako,

Utaifa ndiyo nia, umoja ndiyo mashiko,

Nchi nitapigania, vurugu kwetu ni mwiko,

Yapo mengi ya msingi, siwezi kuyamaliza.

21. Siwezi kuyamaliza, hadi yale ya kilimo,

Ardhi yajitambaza, rutuba isokikomo,

Hata mvua ya kusaza, tena bila ya kikomo,

Niishilie kunena, kaditama nifichame.

22. Kaditama nafichama, sala nampa Rabani,

Tuepushie nakama, madhila kwetu hapana,

Fanaka kwetu adhama, nakuomba maulana,

Kwa fuadi natuama, amani utujalie.

Maswali:

  1. Wimbo wa Taifa una beti ngapi?
  2. Taja ujumbe uliopo kwenye wimbo wa Tanzania.
  3. Taja mashujaa waliotajwa kwenye shairi.
  4. Tajs sifa za Tanzania zilizotajwa katika shairi.
  5. Taja vilele viwili vya mlima Kilimanjaro.
  6. Kwa nini unasisitizwa kuipenda Nchi yako?
  7. Orodhesha shughuli za kiuchumi zinazotajwa katika shairi.
  8. Nini maana ya “marashi yake mwanana”?
  9. Shairi hili linahusu nini?
  10. Nini maana ya kujivunia Nchi?
  11. Umejifunza nini kutokana na shairi ulilolisoma?
  12. Taja viongozi walioitawala Tanzania.
  13. Mbuga zipi za wanyama zilizotajwa kwenye shairi?
  14. Tanzania ni Nchi mashuhuri, thibitisha ukweli wa kauli hii.

ZOEZI LA 2.

Oanisha maneno ya sehemu A na maana yake katika sehemu B.

Sehemu A

Sehemu B

  1. Nudhumu
  2. Inda
  3. Hayawani
  4. Dafina
  5. Mithili
  6. Saza
  7. Kaditama
  8. Fichama
  9. Adhama
  10. Fuadi
  1. Mwisho au kikomo cha jambo
  2. Tabia ya mtu kutopenda mafanikio ya mtu mwingine
  3. Mfano wa
  4. Utungo wa kishairi
  5. Jambo kubwa la heshima na fahari
  6. Moyo
  7. Mtu asiye na ubinadamu
  8. Mali iliyofukiwa chini ya ardhi kwa lengo la kufichwa.
  9. Bakiza sehemu ya kitu unachotumia au unachokichukua.
  10. Jificha kwa kujibanza ili kutoonekan na watu kwa urahisi.

ZOEZI LA 3.

Kamilisha methali zifuatazo:

  1. Manahodha wengi_______________
  2. ________________hutumbua usaa.
  3. Kutoa ni moyo_______________
  4. _______________hakuna wajenzi
  5. Asa ya mja hunena__________________
  6. _____________vya kuchinja haviwezi
  7. Achezaye na tope_______________________
  8. __________________haanguliwi na mti
  9. Amani haiji________________________
  10. _________________akichoka keshapata.

ZOEZI LA 4. VITENDAWILI:

Tegua vitendawili vifuatavyo:

  1. Gari langu halitumii mafuta___________________
  2. Shamba langu kubwa lina kisiki kimoja__________________
  3. Saa yangu haijasimama tantu itiwe ufunguao_________________
  4. Wanangu hawapandi mlima bali huteremka daima_______________
  5. Garimoshi reline________________
  6. Mavuno ya shamba nzima hayajazi kiganja__________________
  7. Maisha yako ni furaha kwa watu_______________________
  8. Chungu cha mwitu hakiwapiki wapichi wake wakaiva_________________
  9. Kwa mfalme hawa hawatoki, hawa hawaingii________________________
  10. Nacheza ngoma lakini wapigaji wake wako ughaibuni_____________

ZOEZI LA 5.

A: Andika maneno yenye maana sawa na maneno yafuatayo:

  1. Fuadi___________________
  2. Kaditama_________________
  3. Jibanza__________________
  4. Bakiza__________________
  5. Onya___________________
  6. Husuda_________________
  7. Shujaa__________________
  8. Mshororo________________
  9. Kera____________________
  10. Nakama_________________

B: Ni neno lipi lililo tofauti?

  1. Mpasuko, mshikamano, ushirikiano, umoja.
  2. Figo, mtima, fuadi, moyo.
  3. Kazi, saza, shughuli, wajibu.
  4. Mzalendo, mzaha, mwenyeji, mzawa.
  5. Kodi, Rushwa, ushuru, ada.
  6. Kubali, shawishi, bembeleza, hamasisha.
  7. Dhahabu, lulu, udongo, almasi.
  8. Tiririka, miminika, mwagika, zoleka.
  9. Bashiri, pata, kisia, tabiri.
  10. Paramia, pindua, dandia, panda.

C: Jaza nafasi zilizoachwa wazi kwa kutumia maneno yaliyo kwenye kisanduku.

Mzalendo, kaulimbiu, kibwagizo, rasilimali, mtiifu, kusoma, samani, bustani, misitu.


  1. Fedha au kitu anachopewa mtu kama pole anapofiwa huitwa______________
  2. Mtu anayeipenda nchi yake na kuitumikia kwa moyo na uadilifu huitwa__________________
  3. ___________za viongozi mbalimbali hulenga katika kihamasisha watu kufanya kazi kwa bidii.
  4. Wananchi wasingalichoma________________kusingalikuwa na ukame.
  5. Shule yetu ina______________nzuri ya maua.
  6. _____________ni maneno yanayojirudia katika wimbo au shairi.
  7. Tunatakiwa kutunza ________________ya Nchi yetu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vya baadaye.
  8. _____________kwa bidii ni mbini ya kufaulu mtihani.
  9. Ofisi ya mwalimu mkuu ina_____________za aina mbalimbali
  10. Musa angelikuwa______________asingelifukuzwa shule.

www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256