KISWAHILI

SURA YA PILI

SHAIRI

Soma na ghani shairi lifuatalo kisha jibu maswali.

1. Elimu kwa wanadamu, ndio silaha imara,

Imekuwepo dawamu, hata kwa wale sonara,

Tajua wake utamu, ukipitishwa kwa sura,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

2. Nakupatia nudhumu, taona nayo tijara,

Ujifunze na elimu, ya kuucheza mpira,

Uione yako timu, kisha kuanza ziara,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

3. Na ving’ora vya kudumu, adui kuteka nyara,

Kwa yote yalo magumu, ni shime kuyazingira,

Kukazania elimu, kuuzika ufukara,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

4. Kusoma kunawakimu, vijana kuwa imara,

Kupambana na magumu, kwenye uwanja wa dura,

Watu kushika hatamu, huwa na nyingi fikira,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

5. Rafiki yangu Adamu, kwepa ya ujinga nira,

Usijekosa fahamu, kupata ari na ghera,

Mkumbo ni kama sumu, atakukosesha dira,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

6. Liyotukuka elimu, hufunza na biashara,

Yafaa kuwa timamu, kujipatia ajira,

Maisha hana karimu, ukikosa ubora,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

7. Sheria ni msumeno, hukosa huku na huku,

Elimu nayo ni meno, pia ni kama sumaku,

Yaweza leta unono, mithili ngoma chiriku,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

8. Aliye moyo mgumu, hatimi katia fora,

Kaitunga na hukumu, ya kuhimiza fikira,

Kaupata ufahamu, na kung’amua taswira,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

9. Ukiwepo darasani, mwalimu msikilize,

Kisichotiwa mizani, angalia usimeze,

Kilopita kipimoni, ndicho ukitekeleze,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

10. Mazoezi darasani, yatakufanya uweze,

La kufanya akilini, kuchagua ipendeze,

Ujuzio ubaini, jamii isipumbaze,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

11. Utakuwa hatiani, masomo kuyapuuza,

Kuishi kama kunguni, hakika inaumiza,

Bora uishi porini, na majini kama pweza,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

12. Kwa walimu na wazazi, nidhamu uidumishe,

Na mambo yalo azizi, pekee jishughulishe,

Tabia ya uchokozi, kamwe usijifundishe,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

13. Tabia mbaya ya wizi, elimu iikomeshe,

Madhara ya udokozi, jamii uifundishe,

Mwenendo kama wa mbuzi, daima jiepushe,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

14. Fanikiwa hatimaye, ni mfano maishani,

Tegemea cha nduguye, hufa hali masikini,

Mwanafunzi asomaye, apaswa awe kifani,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

15. Kijana nakuusia, usiachie na hisa,

Masomo kung’ang’ania, nakupatia hamasa,

Ndani ya historia, jinalo lipate nasa,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

16. Ya viwandani elimu, lazima uzingatie,

Wanafunzi wahitimu, ujuzi washikirie,

Wa viwanda ufahamu, hakika wakumbatie,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

17. Naweka chini kalamu, tamati nimefikia,

Labaki lako jukumu, nasaha, kucharukia,

Usiache ufahamu, sukari kukimbilia,

Usilikose darasa, kwa kufuata mkumbo.

ZOEZI LA 1: UFAHAMU.

  1. Shairi hili lina jumla ya beti ngapi?
  2. Taja vina vya mwisho katika ubeti wa nne.
  3. Taja vina vya kati na vya mwisho katika ubeti wa kuni na nne.
  4. Kila ubeti wa shairi hili una mishororo mingapi?
  5. Mstari unaojirudiarudia katka kila ubeti unaitwaje?
  6. Taja mambo matatu (3) yanayozungumziwa katika shairi hili.
  7. Mshairi anaposema katika ubeti wa tisa kuwa, “kisichotiwa mizani, angalia usimeze” anamaanisha nini?
  8. Taja mambo mawili katika ubeti wa kumi na tatu ambayo hayafai kuigwa na jamii.
  9. Taja faida tatu za kuwepo kwa viwanda nchini.
  10. Pendekeza kichwa cha shairi hili.

ZOEZI LA PILI. MSAMIATI:

Tunga sentensi kwa kutumia misamiati ifuatayo:

  1. Mkumbo
  2. Dura
  3. Chiriku
  4. Usia
  5. Hamasa
  6. Nira
  7. Mizani
  8. Dawamu
  9. Tujara
  10. Azizi

ZOEZI LA TATU. METHALI:

Kamilisha methali zifuatazi:

  1. Mgegemea cha nduguye_________________________________
  2. _____________________uonekana asubuhi
  3. _____________________katika tumbo la heri
  4. Sheria ni msumeno_____________________________________
  5. Elimu bila adili________________________________________
  6. ____________________hawiki penye jogoo
  7. Udugu wa nazi________________________________________
  8. Nguvu ya mamba______________________________________
  9. ____________________si mwisho wa uhunzi
  10. ____________________ukosa yote.

ZOEZI LA NNE. MAZOEZI YA LUGHA:

A: Pigia msitari neno lenye maana tofauti na mengine: -

  1. Shairi, utendi, hadithi, ngonjera.
  2. Kunde, njegere, maharage, mahindi.
  3. Kengele, king’ora, tarumbeta, mlio.
  4. Gazeti, sheria, kanuni, katiba.
  5. Vina, silabi, mizani, aya.
  6. Gilasi, bilauri, kikombe, sahani.
  7. Sangara, kamongo, pweza, chiriku.
  8. Ujangili, wizi, ulevi, ujambazi.
  9. Kunguni, panzi, nzige, senene.

B: Chagua jibu sahihi katika maswali haya: -

(i) Mtu anayetunga mashairi anaitwa?

  1. Mghani
  2. Muhunzi
  3. Mshairi
  4. Mwandishi

(ii) Shairi huweza kuimbwa au?

  1. Kughaniwa
  2. Kuchezwa
  3. Kutambwa
  4. Kutegwa

(iii) Kituo ni mstari wa _____ unaojirudiarudia katika kila ubeti wa shairi.

  1. Kwanza
  2. Pili
  3. Kati
  4. Mwisho

(iv) Katika shairi la kimapokeo _______ vya kati na vya mwisho hufanana.

  1. Beti
  2. Vina
  3. Mizani
  4. Silabi

(v) Idadi ya silabi katika mshororo huitwa?

  1. Mizani
  2. Kituo
  3. Vina
  4. Herufi

(vi) Kila ubeti wa shairi lazima ubebe angalau wazo _____ muhimu.

  1. Tata
  2. Shinikizi
  3. Moja
  4. Kinzani

(vii) Ubeti wa shairi wenye mistari minne huitwa?

  1. Kibwagizo
  2. Kituo
  3. Mshororo
  4. Tarbia.

(viii) Mistari katika ubeti wa shairi inaweza pia kuitwa?

  1. Nudhumu
  2. Mshororo
  3. Mizani
  4. Kituo

(ix) Ni nini maana ya kughani shairi?

  1. Kusoma shairi
  2. Kuimba shairi
  3. Kuelezea shairi
  4. Kuandika shairi.

(x) Utungo wa kifasihi unaotumia lugha ya mkato kuwasilisha ujumbe kwa hadhira huitwa?

  1. Insha
  2. Sanaa
  3. Fasihi
  4. Shairi.

C: Eleza maana ya taswira zilizotumika katika shairi ulilolisoma.

  1. Ukipitishwa kwa sura.
  2. Mpira
  3. Uwanja wa dua
  4. Nira
  5. Meno
  6. Mizani
  7. Kunguni
  8. Udokozi
  9. Mbuzi
  10. Maumeno.

D: Kanusha sentensi zifuatazo:

  1. Shairi linaigizwa
  2. Nikiwa mkubwa nitakuwa mcheza masumbwi
  3. Baba ana kiwanda cha sabuni
  4. Kiswahili ni lugha ya kigeni Tanzania.
  5. Nimepata maswali
  6. Mwanafunzi anasoma kamusi ya kiswahili
  7. Nyumbani kwetu ni mbali
  8. Eva anapalilia bustani ya babu yake.
  9. Mwandiko mzuri ni wa chausiku tu.

E: Tumia maneno uliyopewa kwa kula sentensi kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

  1. Watoto ______ chakula kitamu (wanapenda, watalia, wanaimba, walitenda)
  2. Otaigo alipofika sokoni_________mjomba anauza viatu (atamkuta, hukuta, alimkuta, angemkuta)
  3. Baba yake Eliza_____________ akida (ataita, anaitwa, anaitika, ameitwa)
  4. Kesho jioni___________ mtoni (nitakwenda, nilienda, nimekwenda, nimeenda)
  5. Leo Mwalimu __________elimu kwa vitendo. (himiza, alihimiza, huhimiza, anahimiza)
  6. Mwasije atakapokuwa mkubwa_________ ghorofa (anajenga, hujenga, atajenga, akijenga)
  7. Kijana yule angalighani shairi__________mtukutu (asingalikuwa,asingelikuwa, asingekuwa,angekuwa)
  8. Mama____________sasa hivi kwenda dukani (aliondoka, alikwishaondoka, ameondoka, keshaondoka)
  9. Kila siku ________ shuleni kwa miguu. (tulikwenda, tumekwenda, tunakwenda, tutakwenda.)
  10. Jana ________kitabu kinachoelezea utii wa watoto kwa wazazi na walimu. ( nimesoma, nilisoma, nitasoma anasoma.)

www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256