Sura Ya Kwanza : Kujipenda na kuwapenda watu wengine

Utangulizi

Katika sura hii, utajifunza kubaini matendo ya kujipenda na kuwapenda watu wengine katika jamii. Pia, utajifunza kubaini matendo yanayohatarisha usalama wa watoto na wanajamii. Aidha, utajifunza namna na umuhimu wa kuzingatia maelekezo na miongozo sahihi unayopewa nyumbani na shuleni. Umahiri utakaoupata katika sura hii utakuwezesha kutambua wajibu wako wa kuheshimu na kuwapenda watu wote katikajamii yako.

Matendo yanayoonesha upendo katika jamii

Kuna matendo mengi yanayoonesha kujipenda na kuwapenda watu wengine katika jamii. Baadhi ya matendo hayo ni kujiheshimu na kuwaheshimu watu wengine, kujijali na kuwajali watu wengine pamoja na kujikinga na kuwakinga watu wengine dhidi ya mambo yanayoweza kuwadhuru. Pia, kuwasaidia walemavu, wagonjwa na wazee.

Matendo yanayoonesha upendo kwa familia

Katika familia kuna watu mbalimbali kama vile baba, mama, dada na kaka. Pia wapo babu na bibi, mama wadogo na wakubwa, wajomba, binamu na wengine. Sisi wanafamilia tunapaswa kujipenda na kuwapenda wanafamilia wenzetu. Katika familia, watu wanapaswa kuishi kwa upendo na mshikamano. Wanafamilia wanapaswa kula pamoja, kufanya kazi pamoja na kusaidiana katika shida na raha.

Katika mila na desturi ni mwiko kumchukia ndugu yako wa damu.Vipo vitendo mbalimbali vinavyofanywa na wanafamilia kuonesha upendo. Kwa mfano kusaidiana kwenye shida mbalimbali kama vile njaa, maradhi na mengineyo. Pia, tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwakosoa ndugu zetu wanapokosea ili waweze kujirudi katika mwenendo stahiki. Je, ni matendo gani ya upendo ungependa utendewe na wanafamilia? Ni matendo gani ya upendo unayowatendea wanafamilia?

Miongoni mwa matendo yenye kuonesha upendo katika familia ni kushiriki katika shughuli za nyumbani. Je, ni shughuli gani unazifanya ukiwa nyumbani?

Soma mazungumzo yafuatayo, kishajibu maswali yanayofuata.

Mama Sikitu:

Habari za nyumbani rafiki yangu.

Mama Furaha:

Nzuri tu, vipi mwanao Sikitu hajambo?

Mama Sikitu:

Hajambo! Furaha anaendeleaje?

Mama Furaha:

Furaha anaendelea vizuri na ananisaidia sana katika shughuli za nyumbani. Kila alfajiri anapoamka anaosha vyombo na kufagia uwanja. Pia huchota maji ndipo aende shuleni. Akirudi jioni humwagilia bustani ya mboga na kunisaidia kuandaa chakula.

Mama Sikitu:

Heri yako mwenzangu, binti yangu Sikitu ni mvivu sana. Hafanyi kazi yoyote nyumbani, si kufagia, wala kuosha vyombo. Hata nguo zake namfulia na kumpigia pasi.

Mama Furaha: Pole mwenzangu! Inawezekana unamdekeza sana Sikitu.
Mama Sikitu: Hapana rafiki yangu. Nimejitahidi kumwelekeza hadi nimechoka. Sikitu hanielewi hata kidogo.
Mama Furaha: Usikate tamaa. Jaribu kukaa naye na kumshauri. Mfanye kuwa rafiki yako wa karibu. Mueleze faida za kushiriki katika kazi za nyumbani. Muelekeze kwa upendo na si kwa kumfokea, taratibu atabadilika tu.


Zoezi la 1

1. Taja matendo matatu yanayoonesha kujipenda mbali na yaliyoelezwa katika kitabu.

2. Taja matendo matatu yanayoonesha kuwapenda watu wengtne katika jamii.

3. Mama Sikitu anavutiwa na matendo gani anayoyafanya Furaha?

4. Je. ni matendo yapi mengine ya upendo yanayofaa kuigwa na wanafamilia?

5 Je, ni mambo gani ya upendo unayopenda kufanyiwa na familia yako?

6. Kama wewe ungekuwa rafiki yaks Sikitu ungefanya nini kumsaidia?


Kazi ya kufanya

Andika kwenye daftari lako matendo mengine matano yanayoonesha upendo katika familia. Kisha kusanya kazi hiyo.


Kuwahudumia wanafamilia wenye mahitaji maalumu

Familia zetu hujengwa na watu wenye mahitaji mbalimbali. Watu hao ni kama watoto wadogo, walemavu, wazee, wagonjwa na wajawazito. Ni vyema kujifunza mahitaji yao ili kuwasaidia.

Hebu tafakari matendo yafuatayo:

1. Mtoto anapika chakula cha mama yake ambaye ni mgonjwa.

2. Kaka anampeleka mdogo wake hospitali.

3. Dada anafua nguo za mdogo wake anayeumwa.

4. Watoto wanamnyanyua baba yao mlemavu na kumsaidia kukaa kwenye baiskeli.

5. Mtoto anampelekea bibi maji ya kunywa.

Je, umejifunza nini kupitia matendo haya?

Soma kisa kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.

Bwana na Bibi Sheuta wanaishi kijiji cha Soni, wilaya ya Lushoto. Wana watoto watatu; Bakari, Sharifa na Amina. Bakari anasoma darasa la Pili. Amina anasoma darasa la tatu, na Sharifa anasoma darasa la nne. Bakari ni mlemavu wa miguu. Kila siku asubuhi Sharifa na Amina humsaidia mdogo wao kuvuka barabara wanapokwenda shuleni. Hufanya hivyo tena wanaporudi kutoka shuleni. Pia, familia hii huishi na bibi Saufa ambaye ni mzee sana, na macho yake hayaoni vizuri. Sharifa humshika mkono bibi Saufa na kumsindikiza anapoenda bafuni kuoga. Pia humwandalia chakula na maji ya kunywa. Amina humsaidia mama yake kupika chakula na kufua nguo za wanafamilia. Vilevile, humsaidia Bakari kujenga stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.

Zoezi Ia 2

1. Je, ni tabia zipi zinazofaa kutokana na kisa hiki?

2. Je, wewe unafanya matendo yapi kuwahudumia wanafamilia wenye mahitaji maalumu?

3. Utamshauri nini mwenzako asiyependa kuwahudumia wanafamilia wenye mahitaji maalumu?

Kuwasaidia wanafamilia wanapopatwa na matatizo

Ni muhimu kuwasaidia watu wengine katika familia ili kutatua matatizo yao. Utafanya nini iwapo;

1. Mdogo wako amejikata na wembe kwenye kidole na damu inamtoka?

2. Mama au baba yako ameugua ghafla mkiwa peke yenu nyumbani?

3. Mdogo wako amejisaidia kwenye kaptula?

4. Dada au kaka yako amepoteza daftari lake?

Soma ngonjera ifuatayo, kishajibu maswali yanayofuata.

Bahati:

Habarini ndugu zangu,

Ujumbe nawaletea,

Ndugu kusaidiana,

Na siyo tu kufanana.

Salama:

Mbona unanichanganya,

Wataka kunidanganya,

Msaada huo ni upi?

Mbona sikuelewi?

Bahati:

Wazazi kuwauguza,

Wanapokuwa wagonjwa,

Ndugu kuwahudumia,

Wanapokuwa na shida

Zawadi:

Faraja tunapeana,

Panapokuwa na tabu,

Suluhisha ugomvi, Pale unapotokea.

Salama:

Sasa nimewaelewa,

Elimu nimeipata,

Familia tuijali,

Ikiwa na matatizo.

Zoezi la 3

1. Unapata ujumbe gani kutokana na ngonjera hii?

2. Ni kwa namna gani unaweza kuwasaidia wanafamilia wenzako wanapokuwa na matatizo?

3. Kuna umuhimu gani mwingine ambao haukutajwa katika ngonjera hii unaotokana na kuwasaidia wanafamilia wanaopatwa na matatizo?

Kazi ya kufanya

Orodhesha kwenye daftari lako matendo matano yanayofaa kuwatendea wanafamilia.


Kusaidia kulea wadogo zako

Katika sehemu hii utajifunza matendo na umuhimu wa kuwajali na kuwalea wadogo zako. Ukifanya hivyo utawasaidia wakue vyema.

Angalia picha zifuatazo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Kielelezo namba 1: Matendo ya kusaidia kulea wadogo zako

Zoezi Ia 4

1 . Ni matendo yapi yanayoonekana kwenye picha ya kwanza hadi ya tatu?

2. Je, ni matendo yapi kati ya hayo unayafanya ukiwa nyumbani?

3. Ni matendo yapi tofauti na yaliyopo kwenye picha unayafanya ukiwa nyumbani?

Kazi ya Kufanya

Zungumza na wazazi, walezi au ndugu zako kuhusu matendo unayotakiwa kufanya kuwalea wadogo zako. Andika matendo hayo nyuma ya daftari lako. Chora jedwali linaloonesha matendo ya kulea wadogo zako. Kisha onesha kwa idadi jinsi ulivyotenda matendo hayo kwa Wiki moja. Zingatia mfano ufuatao:

Mfano wa jedwali


Baada ya Wiki moja, muoneshe jedwali lako mwalimu wa Uraia

Matendo yanayohatarisha usalama katika jamii

Ni jukumu letu kuhakikisha kuwa familia na wanajamii wanakuwa salama wakati wote. Hii ina maana kuwa, ni muhimu kuyatambua na kuyaepuka matendo yanayohatarisha usalama katika jamii. Matendo hayo ni pamoja na kupuuza sheria za barabarani, kushiriki ajira za utotoni na kujiunga na makundi yanayotumia vilevi kama vile pombe, bangi na vinginevyo.

Kazi ya kufanya

Angalia matendo yanayohatarisha usalama wa mtoto yanayofanyika katika maeneo yanayokuzunguka. Andika matendo hayo kwenye daftari lako.

Madhara ya matendo yanayohatarisha usalama watoto

Bila shaka unatambua kuwa matendo yanayohatarisha usalama wa watoto yana madhara mbalimbali.

Soma mazungumzo haya, kisha jibu maswali yanayofuata.

Babu:
Hamjambo wajukuu zangu?
Wajukuu:
Hatujambo! Shikamoo babu.

Babu:

Marahaba! Leo nataka tujadili kuhusu vitendo vinavyohatarisha usalama wa watoto. Je, kuna anayeweza kutaja moja ya vitendo hivyo?

Samata:

Kushiriki katika ajira za utotoni.

Babu:

Vizuri Samata. Je, umewahi kuona watoto wakishiriki kwenye ajira za utotoni?

Selina:

Ndiyo babu. Nimewaona watoto wakishiriki ajira za utotoni, kwa mfano; kubeba mizigo mizito, kuponda kokoto za ujenzi, na kuchimba madini.

Babu:

Aahh! Hii ni hatari sana kwa afya zao. Ni jambo gani jingine linaweza kuhatarisha maisha ya mtoto?

Fatuma:

Kupuuza sheria za barabarani kunakosababisha ajali kwa wanafunzi.

Babu:

Ndiyo mjukuu wangu Fatuma, umejibu vizuri sana. Baadhi ya madereva hupuuza sheria za barabarani wanapoendesha magari na pikipiki. Hivyo wanaweza kuwagonga watoto na kuwasababishia vifo au ulemavu wa kudumu.

Yakobo:

Mimi nadhani pia, watoto wanaweza kujihusisha na makundi hatarishi.

Babu:

Ndiyo Yakobo. Unaweza kueleza zaidi kuhusu makundi hatarishi?

Yakobo:

Haya hujumuisha makundi ya watumiaji wa vilevi kama pombe au dawa za kulevya. Pia, watoto huweza kushiriki ngono wakiwa na umri mdogo.

Babu:

Nani anaweza kutueleza madhara ya kushiriki ngono katika umri mdogo?

Upendo:

Watoto wanaweza kupata mimba za utotoni na kukatisha masomo yao. Pia, wanaweza kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile UKIMWI na Kaswende.

Babu:

Vitendo hivi ni hatarishi kwa usalama wa watoto na raia wengine. Wajukuu zangu ninawaasa muwe na tabia njema. Msihatarishe usalama wa maisha yenu.

Samata :
Asante babu kwa nasaha zako.

Zoezi la 5

1 . Je, ni vitendo gani hatarishi kwa usalama wa watoto?

2. Ni madhara yapi yanayotokana na vitendo vinavyohatarisha usalama wa watoto?

3. Je, ni vitendo gani kati ya vilivyotajwa kwenye mazungumzo ni hatarishi zaidi?

4. Unafikiri ni ushauri gani zaidi babu angetoa kuhusu ulinzi na usalama?

5. Utawasaidiaje wenzako kuepuka vitendo hatarishi?

Zoezi la 6

Andika ndiyo mbele ya sentensi sahihi au hapana mbele ya sentensi isiyo sahihi.

1 . Ni vyema kuwatendea wengine vitendo usivyopenda kutendewa

2. Wanafunzi wanapaswa kuzingatia maelekezo wanayopewa na walimu tu

3. Njia bora ya kumfundisha mwanafunzi mvivu ni kumchapa

4. Watoto wadogo, wagonjwa na walemavu wanahitaji kuhudumiwa

5. Wanafamilia wanapaswa kusaidiana wakati wa matatizo tu

6. Kutumia vilevi na kushiriki ngono katika umri mdogo ni vitendo hatarishi

Matendo yanayoharibu upendo katika jamii

Tafakari matendo yafuatayo:

1. Mwanafunzi anamrushia jiwe mwenzake.

2. Mwanafunzi anamsengenya rafiki yake.

3. Mwanafunzi anamtukana mwenzake.

4. Mtoto anasema uongo ili apewe fedha na mzazi au mlezi wake.

Bila shaka umewahi kuona watu wakitenda matendo yanayoharibu upendo katika jamii. Matendo hayo ni kama vile ugomvi, kusengenya na kutukana. Pia matendo mengine ni uchoyo, wizi na udanganyifu.

Soma kisa kifuatacho, kishajibu maswali yanayofuata.

Shukuru na Sekela ni wanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Jitegemee. Kila asubuhi Sekela hupewa fedha kwa ajili ya nauli na matumizi mengine. Licha ya kupewa fedha za kutosha, Sekela huwadanganya wazazi wake ili apewe fedha zaidi. Akiwa shuleni, hununua sharubati na vitumbua na kula peke yake. Siku moja Shukuru alipoteza kalamu yake, akamuomba Sekela amsaidie. Sekela alikuwa na kalamu mbili, lakini alikataa kumsaidia Shukuru. Wakati wa mapumziko, Shukuru hupenda kucheza na marafiki zake. Wote huacha mifuko ya madaftari yao darasani. Sekela hubaki darasani kwa sababu hapendi kucheza na wenzake. Siku moja wakati wa mapumziko, Shukuru na wenzake walikuwa wakicheza nje. Sekela alichungulia dirishani na kuona kuwa hakuna mtu anayemuona. Akafungua mfuko wa Shukuru na kuiba rula. Baada ya mapumziko, Shukuru alirudi darasani akashangaa kuona mfuko wake ukiwa wazi. Alipoangalia ndani hakuiona rula yake. Alikimbia ofisini na kumtaarifu mwalimu wa darasa kuhusu kupotea kwa rula yake.

Mwalimu alikuja darasani na kuwakagua wanafunzi katika mifuko yao. Ahhh! Rula ilikuwa imefichwa ndani ya mfuko wa Sekela. Mwalimu alimuonya Sekela aache tabia ya wizi.

Halafu akasisitiza kwamba, mwanafunzi inakupasa utambue kuwa si vyema kuwatendea wengine matendo usivyopenda kutendewa. Hivyo basi, yakupasa kutenda matendo yanayofaa kila wakati katika maisha yako.

Zoezi Ia 7

1. Je, ni matendo yapi yasiyofaa kumtendea mtu yaliyo katika kisa hiki?

2. Una maoni gani kuhusu matendo ya Sekela?

3. Utafanya nini kumsaidia mwenzako kuepuka tabia kama ya

4. Ni matendo yapi mengine yasiyofaa kumtendea mtu zaidi ya haya yaliyooneshwa kwenye kisa ulichosoma?

Kazi ya kufanya

Zungumza na wazazi au walezi au wanafunzi wenzako kuhusu umuhimu wa kuepuka matendo yasiyofaa kumtendea mtu. Andika mazungumzo hayo kwenye daftari lako.

Kuzingatia maelekezo ya walimu, wazazi na walezi

Je, umewahi kupewa maelekezo na mzazi, mlezi au mwalimu?

Soma kisa kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.

Adila ni mtoto wa Mzee Shokolo. Anasoma Shule ya Msingi Kirore. Mzee Shokolo humuelekeza Adila kazi za nyumbani. Mara nyingi maelekezo hufanyika kabla ya kwenda shule na baada ya kurudi nyumbani. Kazi hizo ni kufagia uwanja, kuosha vyombo na kuteka maji. Kazi nyingine ni kumwagilia bustani ya mboga na maua. Pia humuelekeza kufua na kunyoosha nguo zake na kufanya kazi alizopewa shuleni.

Kila siku asubuhi, Adila huosha vyombo na hufagia uwanja. Aidha, Adila hufika shuleni mapema, hufanya usafi kisha humwagilia maua. Wakati wa jioni, Adila hurejea nyumbani na humwagilia bustani. Walimu, wazazi na jamii hufurahishwa sana na tabia ya usikivu wa Adila. Kwa sababu hiyo, Adila hupokea zawadi nyingi kutoka kwa wazazi, walezi, walimu na wanajamii.

Zoezi la 8

1 . Je, ni matendo yapi ya Adila yanayofaa kuigwa?

2. Je, ni maelekezo gani Adila hupewa nyumbani na shuleni?

3. Kwa nini ni muhimu kuzingatia maelekezo sahihi unayopewa?

4. Utamsaidiaje mwenzako asiyependa kuzingatia maelekezo ya walimu, na wazazi au walezi?

5. Orodhesha faida tatu za kufuata maelekezo unayopewa na wazazi, walezi au walimu.

Kazi ya kufanya

Andika orodha ya shughuli unazofanya kila siku. Bainisha shughuli unazofanya kwa kufuata maelekezo ya mzazi, mlezi, au mwalimu. Bainisha shughuli unazofanya bila kufuata maelekezo ya mzazi, mlezi au mwalimu.

Msamiati

Ajira

kazi ya kulipwa mshahara au kujiajiri

Dhamira

jambo analokusudia mtu kufanya

Hatarishi

yenye kuleta madhara

Nasaha

maneno mazuri yanayotolewa kushauri jambo

Sharubati

kinywaji kinachotengenezwa kwa maji ya matunda

Wanajamii

ni jumuiya ya watu wanaoishi katika eneo fulani


www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256