Sura Ya Pili : Kuipenda shule yetu

Utangulizi

Katika sura hii, utajifunza kutunza mazingira ya shule na muundo wa uongozi wa shule. Vilevile, utajifunza sheria na kanuni za shule, na shughuli zenye kuiletea shule sifa nzuri. Umahiri utakaoupata katika sura hii utakuwezesha kutii sheria na kanuni zilizowekwa katika jamii. Muundo wa uongozi wa shule

Ni vyema utambue kuwa viongozi wa shule wana mchango mkubwa katika ujifunzaji shuleni. Viongozi hao wanasaidia kuboresha nidhamu yenu, maendeleo ya kitaaluma na mazingira ya shule yenu. Viongozi wa shule yako hutofautiana kwa majukumu mbalimbali. Mpangilio wa viongozi katika nafasi na majukumu yao huitwa muundo wa uongozi wa shule.

Je, unawafahamu viongozi wa shule yako? Unaufahamu muundo wa uongozi katika shule yako? Je, viongozi wa shule yako wana majukumu yapi?

Soma habari ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Shule ya Msingi Maendeleo ni moja ya shule kongwe nchini. Je, ungependa kufahamu uongozi wa shule hii? Uongozi wa shule hii unaundwa na kamati ya shule, mwalimu mkuu, mwalimu mkuu msaidizi, mwalimu wa taaluma, mwalimu wa nidhamu, walimu, na viranja.

Muundo wa Uongozi wa Shule

Kielelezo namba 1: Muundo wa uongozi wa shule za msingi


Zoezi la 1

1. Je. ni viongozi gani wa shule wanaotajwa kwenye habari hii?

2. Nini faida ya kuwa na viranja shuleni?

3. Je, unapata faida gani kwa kuwafahamu viongozi wa shule yako?

Kazi ya kufanya

Jadiliana na mwalimu wako wa somo kuhusu majukumu ya Kamati ya shule, Mkuu wa shule, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Mwalimu wa Taaluma, na Mwalimu wa Nidhamu.

Majukumu ya viranja wa shule

Je, ni yapi majukumu ya viranja wa shule?

Soma majigambo yafuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Kiranja wa usafi: Mimi nina majukumu mazito, shule inavutia na kupendeza.

Kiranja wa taaluma: Wapi wewe! Mimi majukumu yangu ni zaidi ya majukumu yako. Usimamizi wangu ndio unaifanya shule ijulikane kwa ufaulu wa wanafunzi wengi.

Kiranja wa nidhamu: Wote mnajidanganya. Hivi mazingira mazuri na ufaulu mkubwa vinapatikanaje bila ya nidhamu nzuri? Mimi jukumu langu ndilo kubwa zaidi.

Kiranja wa usafi: Kusimamia usafi wa shule yakiwemo maeneo ya nje na vyoo ni kazi ndogo eeh!

Kiranja wa nidhamu: Afadhali wewe. Mimi nasimamia wanafunzi kuwahi shuleni. Pia, nahakikisha wanavaa sare za shule zinazotakiwa. Vilevile, wanaingia darasani na kuonesha tabia njema muda wote.

Kiranja wa taaluma: Taaluma ndiyo kila kitu. Mimi nasimamia maendeleo ya taaluma ya wanafunzi. Pia, nafuatilia ufundishaji na ujifunzaji darasani na ufaulu katika masomo. Vilevile, natoa ushauri kwa uongozi wa shule kuhusu namna ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Kiranja mkuu: Jamani! Majukumu yenu ni muhimu katika kuiendeleza shule yetu. Nawapongeza nyote kwa usimamizi mzuri unaofanya shule yetu ipate sifa nzuri. Ninayo furaha kuwa msimamizi wenu katika majukumu yote.

Zoezi la 2

1. Je, ni kiranja gani mwenye jukumu la kusimamia usafi wa mazingira shuleni?

2. Taja kazi ya kiranja wa darasa.

3. Je.wewe ungependa kuw akiranja unayesimamia majukumu gani?

Kuzingatia sheria na kanuni za shule

Ni wajibu wa kila mwanafunzi kuzingatia sheria na kanuni za shule anaposoma. Je, shuleni kwako kuna sheria na kanuni za shule?

Hebu tafakari matendo yafuatayo:

1. Mwanafunzi amegongwa na pikipiki akiwa amevaa shati lisilokuwa na nembo ya shule.

2. Mwanafunzi anazingatia muda wa kufika na kuondoka shuleni.

3. Mwanafunzi hakufanya mitihani kwa sababu ya tabia yake ya utoro.

Soma kisa kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.

Shule ya Msingi Amani husifiwa kwa kuwa na wanafunzi wenye nidhamu. Wanafunzi wake wanazingatia sheria na kanuni za shule. Sheria hizo ni kuwahi shuleni, kuhudhuria vipindi vyote, na kuvaa sare zenye nembo ya shule.

Wanafunzi wote hufika shuleni saa moja asubuhi wakiwa wamevalia sare safi za shule. Baada ya paredi vipindi vya masomo huanza rasmi. Vipindi hivyo huanza saa mbili asubuhi hadi saa saba na dakika arobaini mchana.

Mnyate na Asifiwe ni wanafunzi wa darasa la nne katika shule hii. Wanafunzi hawa walikuwa na tabia ya kutoroka shuleni muda wa vipindi. Mara kwa mara mwalimu wa darasa aliwaadhibu na kuwashauri waache utoro lakini hawakuzingatia. Siku moja gari la matangazo lilipita karibu na shule yao. Mnyate na Asifiwe walikuwa makini kusikiliza matangazo hayo. Unadhani ni kwa nini walionesha umakini? Wao walikuwa na tabia ya kutoroka shuleni na kwenda kucheza muziki. Tangazo la siku hiyo lilikuwa ni la uzinduzi wa bendi ya muziki. Uzinduzi huo ulikuwa unafanyika mchana wa siku hiyo. Mnyate na Asifiwe walitoroka kwa kuruka ukuta. Kundi kubwa la watu lilihudhuria uzinduzi huo. Mnyate na Asifiwe walisukumwa katikati ya kundi hilo. Walikanyagwa na kupoteza fahamu. Kwa kuwa sare zao za shule zilikuwa hazina nembo ilikuwa ni vigumu kuitambua shule wanayotoka. Hivyo watu wema waliwaweka kando ya barabara na kuwapa huduma ya kwanza.

Punde mwalimu Masumbuko alipita akaona mkusanyiko wa watu. Alisogea karibu ili kujua kilichokuwa kimetokea. Alielezwa kuwa wanafunzi wawili walikanyagwa kwenye uzinduzi wa bendi ya muziki. Mwalimu aliuliza, ”Je, wanafunzi hao mmeshawatambua?”. ”Bado kwa kuwa sare zao hazina nembo ya shule”, alijibu mmoja wa watu hao. Basi mwalimu Masumbuko alisogea pale walipo wanafunzi wale. ”Aaah jamani! Hawa ni wanafunzi wangu”, alisema. Muda huohuo alimpigia simu mwalimu mkuu. Mwalimu mkuu aliagiza wanafunzi wenzao waende kuwabeba na kuwaleta shuleni. Mnyate na Asifiwe walikuwa wameshapata fahamu.

Zoozi la 3

1. sheria zipi za shute zilizovunjwa na Mnyale na Asifiwe?

2. Je. utawasaidiaje wanafunzi wenye tabia kama hizi shuleni kwako,

3. Ni athari zipi zinazoweza kumpata mwanafunzi asiyezingatia sheria na kanuni za shule?

Kazi ya kufanya

Angalia matendo ya kuvunja sheria za shule darasani kwako. Orodhesha kwenye daftari lako matendo yaliyojitokeza mara nyingi.

Zoezi la 4

Oanisha maneno ya kifungu A na yale ya kifungu B ili kupata maana sahihi.

Kifungu A

Kifungu B

1. Uongozi wa shule

2. Kiranja Mkuu

3. Sheria za shule

4. Medali

5. Sifa nzuri za shule



(a) Msimamizi mkuu wa majukumu ya viranja

(b) Kuwahi shuleni, kuhudhuria vipindi vyote na kuvaa sare zenye nembo ya shule

(c) Zawadi anayopewa mshindi inayovaliwa shingoni

(d) Kamati ya shule, mwalimu mkuu na mwalimu wa taaluma
(e) Kiranja wa taaluma

(f) Wingi wa wanafunzi na walimu

(g) mwalimu mkuu, diwani na viranja

(h) Vikombe

(i) Kufanya vizuri katika taaluma, michezo na nidhamu

Kushiriki shughuli zenye kuiletea shule sifa nzuri

Ni vyema ukatambua kuwa kila mwanafunzi ana jukumu la kushiriki katika shughuli mbalimbali. Shughuli hizo ziwe zenye kuiletea shule yake sifa nzuri.

Ni mambo gani yanayoifanya shule yako isifike vizuri kuliko shule za jirani? Je, wewe unashiriki vipi kuiletea sifa shule

Angalia picha zifuatazo:

Kilelezo namba 2: Matendo ya kuiletea shule sifa nzuri


Zoezi

1. Je, ni matendo gani yanaonekana katika picha?

2. Umejifunza nini kutokana na matendo katika picha?

3. Ni matendo gani zaidi ya hayo yanayoweza kuiletea shule yako sifa nzuri?

4. Utatenda matendo gani iii kuiletea shule yako sifa nzuri?

Soma ngonjera ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.

Hodi hodi twaingia, tunene tuliyonayo,

Elimu mliyopata, muitumie maishani,

Uhodari mloonesha, shule inajivunia,

Sio tu kwenye masomo, tamaduni na michezo,

Hamasa tumeipata, mfano tutatumia,

Kuletea shule sifa, hiyo ni dhamira yetu.

Mmeitangaza shule, hakuna asiyejua,

Zawadi mlizopata, shule inajivunia,

Nasi pia tutaenzi, sifa shule kujengea,

Ufaulu kuongeza, medali kushindania,

Hakika hatutashindwa, mikakati twaiweka,

Kuletea shule sifa, hiyo ni dhamira yetu.

Endelezeni vipaji, dua tunawaombea,

Nchi yawategemea, mkae mkitambua,

Mmetuonesha njia, nasi tunaipitia,

Epukeni na maovu, msije kuangamia,

Mafanikio mpate, Taifa lifaidike,

Kuletea shule sifa, hiyo ni dhamira yetu.

Zoezi la 6

1. Unapata ujumbe gani kutokana na ngonjera hii?

2. Ni matendo gani yaliyomo kwenye ngonjera hii yanaweza kuiletea shule sifa nzuri?

3. Je, ni mambo gani mengine yanayoweza kuiletea shule yako sifa nzuri?

Kazi ya kufanya

Zungumza na marafiki, walezi au wazazi kuhusu mambo waliyoyafanya kuziletea shule zao sifa nzuri. Taja shughuli ambazo hujawahi kuzifanya ili kuiletea shule yako sifa nzuri.

Zoezi la 7

1. Andika ndiyo kwa sentensi sahihi au hapana kwa sentensi isiyo sahihi katika sentensi zifuatazo:

(a) Kushirikiana na wanafunzi wenzetu huweza kuiletea shule sifa nzuri

(b) Kusimamia nidhamu ya wanafunzi siyojukumu la viranja wa shule

(c) Utoro wa mwanafunzi huchangia kufeli mitihani

(d) Jukumu la kuiletea shule sifa nzuri siyo la wanafunzi bali ni la walimu tu

(e) Tabia njema za wanafunzi ni baadhi ya mambo yanayo iletea shule sifa nzuri

2. Andika habari fupi ukieleza utakavyomhamasisha rafiki yako kushiriki kwenye shughuli zitakazoiletea shule sifa nzuri.

Msamiati

Athari

matokeo mazuri au mabaya yampatayo mtu au kitu baada ya kupitia hatua fulani

Katibu

mwandishi wa taarifa za vikao

Kuenzi

kuonesha thamani ya jambo zuri lililokwishafanyika

Malezi

mwongozo mwema anaopewa mtu katika maisha

Medali

zawadi anayopewa mshindi inayovaliwa shingoni iliyotengenezwa kwa madini ya dhahabu, shaba au fedha

Miundombinu

vitu vinavyowezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma kama vile barabara na majengo

Ufanisi

matokeo mazuri

Unasihi

ushauri anaopewa mtu mwenye tatizo fulani


www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256