Sura ya 02 : Urithi wa Tanzania

Utangulizi

Katika sura hii utajifunza dhana ya urithi na maeneo yenye urithi wa kihistoria nchini Tanzania. Pia, utajifunza wajibu wa jamii katika kulinda urithi wa kihistoria. Umahiri utakaoupata utakusaidia kuthamini urithi uliopo nchini na kutumia fursa zinazopatikana kutokana na urithi huu kwa maendeleo ya jamii.

Fikiri

Urithi uliopo Tanzania.

Maana ya Urithi

Kazi ya kufanya namba 1

Soma vyanzo mbalimbali, ikiwemo vitabu na mitandao, kuhusu maana ya neno urithi.

Urithi unajumuisha vitu vyenye thamani na kumbukumbu zilizohifadhiwa au kuwepo katika eneo fulani kutoka vizazi vilivyopita. Urithi huu unaweza kuwa ule unaoshikika kama vile, masalia ya binadamu wa kale, michoro ya mapangoni, magofu na masalia ya miji na majengo, vitu vya thamani kama shanga na zana zilizotumiwa na watu walioishi kale.

Urithi wa asili kama vile wanyama, milima, mito ya asili na maziwa ni sehemu ya urithi unaoshikika. Pia, urithi unaweza kuwa ule usioshikika kama vile mila, desturi, miiko, maarifa, dini na elimu ya jadi. Hivi vyote ni sehemu ya urithi kwani huonesha asili yetu, chimbuko letu au matukio yaliyotokea katika jamii zetu. Aidha, urithi umebeba utambulisho wa asili, tamaduni, mila na desturi zetu.

Maeneo yenye urithi unaoshikika

Tanzania ni nchi mojawapo duniani yenye urithi mwingi na adhimu unaoshikika.

Kazi ya kufanya namba 2

Tembelea maeneo yenye urithi kama vile magofu ya miji, misikiti, makanisa, masalia ya binadamu, zana za mawe, mbuga za wanyama, milima, mito ya asili na misitu katika maeneo unayoishi, kisha orodhesha urithi uliopo.

Masalia ya binadamu wa kale, michoro ya mapangoni, magofu na masalia ya miji na majengo, mbuga za wanyama, milima, mito ya asili, misitu na vitu vya thamani kama shanga na zana zilizotumiwa na watu walioishi kale ni sehemu ya urithi unaoshikika.

Urithi unaohusu binadamu wa kale na shughuli zake Tanzania ina urithi adhimu kuhusu shughuli za binadamu wa kale na masalia yake. Mfano, Kondoa Irangi, Dodoma kuna kumbukumbu za michoro ya mapangoni yenye urithi wa kihistoria unaoonesha shughuli za jamii za kale (chunguza Kielelezo namba 1).


Kielelezo namba 1: Michoro ya mapangoni, Kondoa Irangi

Eneo la Oldupai, Arusha ni mahali ambako kuligunduliwa masalia ya fuvu la binadamu wa kale. Mabaki haya yaligunduliwa na Dkt. Louis Leakey na Mary Leakey mwaka 1959. Huu ni urithi mkubwa kwa sababu inaaminika kuwa ndipo alipoishi binadamu wa kwanza duniani (chunguza Kielelezo namba 2).


Kielelezo namba 2: Fuvu la binadamu aliyeishi kwa miaka mingi zaidi

Pia, eneo la Laetoli, Arusha lina nyayo za binadamu anayeaminika kuishi kwa miaka mingi zaidi duniani (chunguza Kielelezo namba 3). Huu ni urithi mkubwa kwa nchi yetu. Wageni huja nchini kutembelea maeneo hayo ili kujifunza historia ya watu wa kale.


Kielelezo namba 3: Nyayo za binadamu wa kale, katika eneo la Laetoli

Eneo la bonde la Isimila, Iringa kuna urithi wenye historia unaohusu Zana za Mawe zilizotumiwa na binadamu wa kale. Zana hizi za mawe zina mfanano na mikuki, mishale, shoka, visu na nyundo kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 4. Zana hizi zilitumika kuwinda, kuchimbia mizizi na kupondea vitu mbalimbali Urithi huu wa Zana za Mawe ni adhimu na

muhimu kwa historia ya binadamu duniani.


Kielelezo namba 4: Baadhi ya Zana za Mawe katika Makumbusho ya Isimila

Zoezi la 1

1. Eleza kwa nini urithi huu uliopo eneo la Laetoli, Kondoa Irangi, Isimila na Oldupai ni muhimu?

Urithi wa kihistoria kuhusu wageni kutoka Mashariki ya Mbali na Kati

Jamii za Tanzania hapo Kale zilifanya biashara na wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali na ya Kati. Nchi hizo ni India, Irani, Iraki, Kuwait, China na Saud Arabia. Biashara hii ilifanyika katika miji iliyopo katika mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi kama vile Dar es Salaam, Bagamoyo, Tanga, Kilwa na Zanzibar. Biashara hizi zilifanyika kwa kubadilishana bidhaa. Bidhaa kubwa katika biashara hii kutoka nchini ilikuwa dhahabu na pembe za ndovu. Dhahabu ilitoka Zimbabwe kupitia bandari ya Sofala, Msumbiji. Kutoka kwa wageni kuja nchini, bidhaa kubwa zilikuwa shanga na vyombo vya ndani kama vile mabakuli na sahani za udongo. Baadhi ya mabaki ya bidhaa hizi yapo katika Makumbusho hapa nchini, kama vile makumbusho ndogo iliyopo Kaole, Bagamoyo.

Biashara hizi zilisababisha wafanyabiashara hawa watajirike na kujenga miji, majengo, misikiti na makaburi. Majengo na miji hiyo kwa sasa vimebaki kama magofu na masalia yenye kumbukumbu ya kihistoria kuhusu wafanyabiashara hao. Kielelezo namba 5 kinaonesha mojawapo ya magofu ya mji uliotumiwa na wafanyabiashara hao.


Kielelezo namba 5: Magofu ya mji wa Tongoni, Tanga

Pia, eneo la Kunduchi lililopo Dar-es-salaam lina mabaki ya mji uliotumiwa na wafanyabiashara hao (chunguza Kielelezo namba 6).


Kielelezo namba 6: Magofu ya mji wa Kunduchi, Dar es salaam

Vilevile, eneo la Kilwa, Lindi lina mabaki ya magofu ya mji, majengo na ikulu za viongozi waliojihusisha na biashara hii. Kilwa Kisiwani, ndio mji uliokuwa kituo muhimu na kikubwa wakati wa biashara zilizofanywa na watu kutoka Mashariki ya Kati. Kilwa kuna masalia ya jengo la mfalme wa Kilwa liitwalo Husuni Kubwa. Jumba hili lilikuwa ikulu ya sultani wa Kilwa (chunguza Kielelezo namba 7). Masalia haya yapo Kilwa, mkoa wa Lindi mpaka leo.


Kielelezo namba 7: Magofu ya Husuni Kubwa, Kilwa

Maeneo ya Kilwa kuna gofu la ngome ambalo lilijulikana kama ngome ya gereza. Ngome hii ilianza kujengwa na wageni kutoka Mashariki ya Kati, na baadae kumaliziwa kujengwa na Wareno kutoka Ulaya. Gofu la ngome hii nalo ni sehemu ya urithi nchini Tanzania (chunguza Kielelezo namba 8).


Kielelezo namba 8: Gofu la ngome ya gereza Kilwa, Lindi

Vilevile, kuna urithi wa magofu ya misikiti iliyotumiwa na wafanyabiashara hao kwa ajili ya ibada. Jamii hizi zilishika dini ya Kiislamu. Miongoni mwa misikiti hii ipo Kilwa Kisiwani, Lindi na Kaole Bagamoyo, mkoa wa Pwani (angalia Kielelezo namba 9).


Kielelezo namba 9: Gofu la msikiti mkuu Kilwa Kisiwani, Lindi

Pia, Kaole kuna magofu ya msikiti, makaburi na kisima kilichotumiwa na wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Kati. Angalia magofu hayo katika Kielelezo namba 10.


Kielelezo namba 10: Magofu yaliyopo Kaole, Bagamoyo

Vilevile, Kaole kuna urithi wa bidhaa kama sahani na shanga zilizoletwa na wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali na Kati. Urithi wa bidhaa hizo upo katika makumbusho ndogo iliyopo Kaole. Makumbusho mbalimbali nchini zina bidhaa kama vile vigae, vyombo na shanga zilizoletwa na wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali na Kati.

Ushirikiano wa kibiashara baina ya wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali na Kati na jamii zetu ulisababisha kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya maneno ya lugha ya Kiswahili yamekopwa kutoka katika lugha zilizotumiwa na wafanyabiashara hao. Maneno kama vile, sadaka, mwalimu, akili, tisa, ahadi, shikamoo, marahaba, ahsante, madrasa na kitabu yamekopwa kutoka katika lugha ya Kiarabu. Pia, maneno kama gunia, dunia, pesa na gari yamekopwa kutoka katika lugha ya Kihindi. Haya ni baadhi tu ya maeneo tunayotumia katika lugha ya Kiswahili kwa sasa. Lugha ya Kiswahili ni urithi nchini.

Pia, jamii zilizoshirikiana na wafanyabiashara hao zimerithi tamaduni za kigeni kama vile dini ya Kiislamu, mavazi na maadili yao. Jamii hizi ni zile zilizopo hasa katika maeneo ya mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi. Kielelezo namba 11 kinaonesha mfano wa mitindo ya mavazi hayo. Maadili haya ya kigeni yamekuwa sehemu ya urithi wa jamii zetu mpaka sasa.


Kielelezo namba 11: Mitindo ya mavazi iliyoletwa na Waarabu

Aidha, ujio wa wageni hao ulileta viungo mbalimbali vya chakula nchini kama vile mdalasini, iliki, pilipili manga, karafuu na binzari nyembamba kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 12. Mdalasini Iliki Karafuu Pilipili manga Binzari nyembamba


Kielelezo namba 12: Viungo vya chakula vilivyoletwa na wageni

Pia, baadhi ya mapishi ya vyakula kama vile pilau, jamii zetu zimerithi kutoka kwa wageni hao.

Kazi ya kufanya namba 3

Fanya uchunguzi maeneo ambayo wageni kutoka nchi za Mashariki ya Mbali na Kati walikaa, kisha andika maadili ambayo jamii hizo zimerithi.

Urithi wa Kihistoria unaohusu biashara ya utumwa nchini

Maeneo ya Bagamoyo kuna urithi wa magofu unaotokana na biashara ya utumwa. Wafanyabiashara wa biashara ya utumwa walitoka nchi za Uarabuni. Bagamoyo kuna jengo la Caravan Serai ambalo lilikuwa hoteli ya wafanyabiashara wa watumwa (chunguza Kielelezo namba 13).


Kielelezo namba 13: Jumba la Caravan Serai, Bagamoyo

Pia, maeneo ya Zanzibar kuna magofu na majengo yaliyotumiwa kwa ajili ya kuhifadhi watumwa na kuishi wafanyabiashara wa biashara ya watumwa (chunguza Kielelezo namba 14).


Kielelezo namba 14: Chumba cha chini kilichotumika kuweka watumwa, kilichopo eneo la kanisa la Anglikana Unguja, Zanzibar

Urithi wa Kihistoria unaohusu wageni kutoka nchi za Ulaya

Tanzania ina urithi wa kihistoria ulioachwa na wageni waliokuja kutoka katika nchi za Ulaya. Baadhi ya wageni hawa walikuwa wamisionari. Awali, wageni hawa walikuja kueneza dini ya Kikristo. Hivyo, walijenga makanisa kadhaa katika maeneo waliyoishi. Ujio wa wageni hao uliacha urithi wa kihistoria wa makanisa yaliyojengwa kwa ajili ya ibada.

Makanisa waliyoyajenga wamisionari hao bado yanatumika kwa ibada hadi sasa. Mfano wa makanisa hayo ni kanisa Katoliki la zamani lililopo Bagamoyo na kanisa la Anglikana

lilipo Mkunazini, Zanzibar (chunguza Kielelezo namba 15).


Kielelezo namba 15: Kanisa la Anglikani, Zanzibar lililojengwa eneo la soko la watumwa

Kuna makanisa mengine yaliyojengwa baadae wakati wa ukoloni hapa nchini. Mfano wa makanisa hayo ni Kanisa la Mtakatifu Yosefu na kanisa la Azania Front, yaliyopo Dar es Salaam. Pia, makanisa haya ni sehemu ya urithi wa kihistoria nchini kwa sasa. Licha ya urithi wa makanisa, wageni hawa walikuwa ndio chanzo cha kuingia Ukristo na maadili ya dini ya Kikristo nchini. Dini na maadili ya Kikristo ni sehemu ya urithi nchini hata leo.

Pia, tuna urithi wa mazao yaliyoletwa nchini na wageni kutoka nchi mbalimbali. Mazao hayo ni kama vile mahindi, maembe, viazi mviringo, mihogo na mapera. Mazao haya yanalimwa mpaka sasa na yamebaki kama sehemu ya urithi nchini. Urithi uliopo katika makumbusho Makumbusho ya Taifa yamehifadhi urithi wa kihistoria wa aina mbalimbali. Makumbusho haya ni; Kijiji cha Makumbusho kilichopo Kijitonyama, Dar es Salaam, Makumbusho ya Vita vya Majimaji, Songea mkoa wa Ruvuma, Makumbusho ya Azimio la Arusha, Arusha na Makumbusho ya Mwalimu Nyerere, Butiama mkoa wa Mara. Makumbusho mengine ni Makumbusho ya Elimu Viumbe, Arusha, Makumbusho na Nyumba ya Sanaa iliyopo Dar es Salaam na Makumbusho ya Kumbukumbu ya Rashidi Mfaume Kawawa iliyopo Songea. Pia, kuna makumbusho ya watu binafsi yenye taarifa za kihistoria kama vile makumbusho ya Bujora, Mwanza. Hizi ni baadhi za makumbusho nchini.

Kazi ya kufanya namba 4

Soma vyanzo mbalimbali ikiwemo tovuti na vitabu kuhusu Makumbusho yaliyopo nchini na eleza urithi uliopo kwenye makumbusho hayo.

Urithi wa asili

Tanzania ina urithi wa asili kama vile misitu, mbuga za wanyama, milima, mabonde, maziwa na mito.

Kazi ya kufanya namba 5

Fanya uchunguzi, kisha andika maeneo yenye urithi wa mbuga za wanyama, mito, mabonde, maziwa na milima kutoka katika mazingira unayoishi na taifa kwa ujumla.

Eneo la bonde la Isimila lililopo mkoani Iringa lina nguzo za asili zilizodumu kwa miaka mingi. Chunguza Kielelezo namba 16.


Kielelezo namba 16: Nguzo za asili katika bonde la Isimila, Iringa

Pia, Tanzania ina mbuga za wanyama kama vile Serengeti, Ngorongoro, Mikumi, Tarangire, Ruaha, Mkomazi, Udzungwa, Nyerere na Manyara ambazo ni urithi wa asili uliopo nchini. Angalia mfano katika Kielelezo namba 17.


Kielelezo namba 17: Mbuga ya wanyama Ngorongoro, Arusha

Hizi ni baadhi tu ya mbuga za wanyama zilizopo nchini. Wanyama waliopo katika mbuga hizi ni urithi wa asili uliopo Tanzania.

Kazi ya kufanya namba 6

Fanya uchunguzi, kisha andika mbuga nyingine zilizopo nchini na baadhi ya wanyama waliopo katika mbuga hizo.

Vilevile, kuna milima mikubwa nchini ambayo ni urithi wa asili. Mfano wa milima hiyo ni mlima Kilimanjaro, ambao ndio mlima wa kwanza kwa urefu barani Afrika (chunguza Kielelezo namba 18). Kuna milima mingine ambayo ni urithi wa asili, kama vile mlima Meru, milima ya Udzungwa na mlima Rungwe.

Kazi ya kufanya namba 7

Fanya uchunguzi na andika milima mingine zaidi ambayo ni urithi wa asili nchini.


Kielelezo namba 18: Mlima Kilimanjaro

Tanzania kuna maziwa na mito ya asili ambayo ni alama ya urithi nchini. Baadhi ya maziwa yaliyopo nchini ni ziwa Victoria, ziwa Tanganyika, ziwa Manyara, na ziwa Nyasa. Pia, kuna mito mikubwa ya asili mfano, mto Ruaha, Kilombero, Malagarasi, Rufiji, Wami na Ruvuma. Hii ni baadhi ya mito mikubwa ya asili ambayo ni urithi wa asili nchini. Vilevile, misitu na uoto wa asili ni sehemu ya urithi nchini.

Kazi ya kufanya namba 8

Fanya uchunguzi na orodhesha mito na maziwa mengine ambayo ni urithi wa asili nchini.

Urithi usioshikika

Urithi usioshikika unahusu masuala ya kijamii yaliyorithiwa kutoka kizazi hadi kizazi ambayo hayawezi kuonekana au kushikika. Urithi huu unahusisha masimulizi kama vile hadithi, miiko, ngano, nyimbo, midundo ya ngoma, methali na lugha za asili. Pia, unahusisha shughuli za kijamii kama vile matambiko, dini na matamasha ya jadi. Vilevile, unahusu maarifa ya jadi kuhusu kilimo, uvuvi, uhunzi, ufugaji na elimu ya mazingira.

Sanaa za maonesho kama vile maigizo na tafsiri za sanaa za ufundi kama vile uchoraji na uchongaji ni sehemu ya urithi usioshikika (angalia mfano katika Kielelezo namba 19). Vitu hivi kwa pamoja ni mfano wa urithi usioshikika wenye kubeba mila, desturi, maarifa na ujuzi wa asili wa jamii za kale.


Kielelezo namba 19: Uchongaji wa vinyago vyenye tafsiri mbalimbali

Kazi ya kufanya namba 9

Fanya uchunguzi na andika urithi usioshikika uliopo katika maeneo yanayokuzunguka.

Urithi uliopo nchini kwa ujumla ni maarufu kwa utalii kwa sasa. Wageni wengi kutoka nje na ndani ya nchi huenda kutembelea urithi huu.

Umuhimu wa urithi katika taifa Urithi una umuhimu kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Urithi huu ni muhimu katika:

  1. Kutambulisha urithi uliopo nchini;
  2. Kutupa ushahidi wa chimbuko na asili za jamii na maadili yake;
  3. Kupata historia ya jamii zetu;
  4. Kutambulisha maarifa na ujuzi wa asili wa jamii za Kitanzania;
  5. Kutoa ufahamu juu ya asili na mabadiliko ya jamii za Kitanzania;
  6. Kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia utalii;
  7. Kutoa ushahidi wa chimbuko la tamaduni zetu;
  8. Kupata taarifa za mabadiliko ya jamii na jinsi ya kuyaendeleza; na
  9. Kupata pato la Taifa kwa njia ya utalii.

Kazi za kufanya namba 10

Andika mambo uliyojifunza kuhusu urithi wa kihistoria.

Wajibu wa jamii katika kutunza maeneo ya urithi wa Tanzania

Kazi ya kufanya namba 11

Fanya uchunguzi na kisha andika urithi uliopo katika maeneo ya karibu na andaa mpango wa kutunza na kulinda urithi huo.

Maeneo yenye urithi yanapaswa kuhifadhiwa na kuthaminiwa. Jamii ya Kitanzania ndiyo yenye wajibu wa kutunza maeneo haya. Maeneo yenye urithi yanapaswa kutunzwa na kulindwa kwa kufanya mambo yafuatayo:

(a) Kuhifadhi kumbukumbu halisi ya wakati, eneo, na matumizi ya urithi huo;

(b) Kufanya usafi na ukarabati ili kuzuia uharibifu wa urithi uliopo;

(c) Kuheshimu ubunifu wa miundo, aina na mbinu wakati wa ujenzi ili kuendeleza uhalisi wa urithi uliopo; na

(d) Kuweka mandhari ya mazingira salama ili kuzuia uharibifu.

Zoezi la jumla

1. Andika neno NDIYO mbele ya sentensi ambayo ni kweli na neno HAPANA mbele ya sentensi ambayo si kweli.

  1. Makanisa yenye urithi wa historia hayatumiki kwa sasa.
  2. Kilwa ulikuwa mji maarufu kwa biashara ya watumwa.
  3. Bagamoyo na Zanzibar ilikuwa miji iliyohusika na biashara ya utumwa.
  4. Magofu ya mji wa Kunduchi yalijengwa wakati wa biashara kati ya jamii zetu na nchi za Mashariki ya Mbali na Kati.
  5. Maadili ya jamii za mwambao wa Bahari ya Hindi yamechangiwa na wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali na Kati.

2. Oanisha kipengele kutoka sehemu A na maeneo yaliyopo sehemu B kwa kuandika herufi ya jibu sahihi katika sehemu uliyopewa.

Sehemu A Jibu Sehemu B

(i) Jumba la wafanyabiashara ya utumwa

(ii) Makumbusho ya Vita vya Majimaji

(iii) Maeneo yenye historia ya watumwa

(iv) Maarufu kwa michoro ya mapangoni

(v) Makanisa yanayotumika ambayo ni urithi wa Tanzania

(vi) Eneo lenye magofu na masalia yenye miji iliyotumiwa na wafanyabiashara kutoka Mashariki ya Mbali na Kati

(vii) Gofu la ikulu ya sultani wa Kilwa

(viii) Urithi wa misikiti ya kale

(ix) Kuligundulika binadamu wa kale zaidi

(x) Kuna nyayo za binadamu wa kale


A. Kilwa Kisiwani, Kaole

B. Husuni Kubwa

C. Oldupai

D. Bagamoyo na Zanzibar

E. Kilwa, Tongoni, Pangani na Kunduchi

F. Laetoli

G. Tanga

H. Kondoa Irangi

I. Anglikani Mkunazini, Zanzibar, Azania Front

J. Caravan Serai

K. Songea

3. Andika umuhimu wa urithi wa Tanzania.

4. Andika mambo uliyojifunza kuhusu urithi uliopo nchini.

5. Andika urithi wa kimaadili na kitamaduni tuliorithi kutoka kwa wageni waliokuja nchini.

Msamiati

  • Husuni jumba lililotumiwa na wafalme au sultani kama makazi
  • Kale huhusisha zamani au miaka mingi iliyopita Maadili tabia, mienendo, kanuni, nidhamu za jamii husika
  • Magofu mabaki ya majengo ya kale yanayoonekana
  • Makumbusho maeneo yenye kuhifadhi vitu vyenye urithi wa kiasili na kiutamaduni
  • Oldupai eneo hili hujulikana pia kama bonde la olduvai
  • Sultani ni mfalme au mtawala wa nchi, jina lilitumiwa na watawala wa Kiarabu
  • Utumwa mfumo ambao binadamu alitumikishwa bila malipo na kumilikiwa na mtu mwingine.
  • Mtumwa hana uhuru wa mali, hata watoto walikuwa ni mali ya aliyemmiliki.


www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256