SURA YA KWANZA

KUWAPENDA WENZETU KATIKA JAMII

Msamiati

 • Baa- Balaa linalomfika mtu, aghalabu husababisha hasara au maafa
 • Uhitaji- ukosefu wa mahitaji ya msingi ya binadamu

KUELIMISHA JAMII NAMNA YA KUTOA MISAADA KWA WAHITAJI

 • Wahitaji ni watu waliopungukiwa na mahitaji muhimu kama vile, chakula, mavazi, fedha, mavazi au afya njema.
 • Ni muhimu kushiriki katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji.
 • Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia iii kuelimisha na kuhamasisha jamii kutoa misaada kwa wahitaji:
 1. Kubaini makundi mbalimbali ya wahitaji katika jamii tunamoishi;
 2. Kufahamu aina mbalimbali za misaada kwa wahitaji wa kila kundi;
 3. Kubaini njia za kuhamasisha jamii kutoa misaada kwa wahitaji;
 4. Kuelewa namna ya kuwahudumia na kuwafariji wahitaji katika jamii;
 5. Kubaini aina za huduma na faraja tunazoweza kuwapatia wahitaji;
 1. Kufahamu umuhimu wa kuwahudumia na kuwafariji wahitaji katika jamii; na
 2. Kupanga mikakati ya kuwatambua watu wenye uhitaji.

Kubaini makundi mbalimbali ya wahitaji katika jamii

 • Wahitaji katika jamii ni pamoja na watoto yatima, watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, watu wenye ulemavu, na wazee.
 • Kundi jingine la watu wenye uhitaji ni waathirika wa majanga mbalimbali katika jamii, kwa mfano, baa la njaa, janga la moto, mafuriko, magonjwa ya mlipuko, na tetemeko la ardhi.


Picha: Waanga wa mafuriko

Aina za misaada kwa wahitaji

 • Misaada inayofaa kutolewa kwa wahitaji ni ya aina mbalimbali kutegemeana na uhitaji wa wahusika.
 • Baadhi ya misaada hiyo ni
 • chakula,
 • mavazi,
 • malazi,
 • huduma za afya,
 • na vifaa mbalimbali kama vile; vifaa vya michezo, usafiri, na huduma ya kwanza.
 • Pia, ipo misaada ya ushauri na unasihi, ya kisheria, ya fedha, na ya malezi.
 • Misaada hii hutolewa pale uhitaji unapotokea katika jamii. Kwa mfano, wakati wa baa la njaa au mafuriko, watu huchangia chakula, dawa, mavazi, na malazi kwa wahitaji.
 • Pia, wanafunzi waliokumbwa na majanga wanaweza kuwa na uhitaji wa vifaa vya shule kama vile, sare za shule, madaftari, na vifaa vya michezo kama; mipira, viatu, sare za michezo na vifaa vya riadha.
 • Vilevile, wahitaji wanaweza kupatiwa ushauri na unasihi ili waweze kuhimili changamoto wanazokutana nazo shuleni na katika mazingira wanamoishi.
 • Aidha, msaada wa kisheria ni muhimu ili kutoa haki kwa wanajamii wanaopeleka mashitaka au kushitakiwa mahakamani.
 • Kwa mfano, msaada wa kisheria unahitajika kwa watoto yatima wanaonyanyaswa, kuporwa mali za wazazi wao, kufanyishwa kazi ngumu na kukosa huduma za afya au elimu bora. Ushauri wa kisheria kwa kawaida hutolewa na wataalamu wa sheria.
 • Wataalamu hawa hutoa mchango wao kwa kusaidia kufungua kesi na kuwatetea bila gharama.

Njia za kuhamasisha jamii kutoa misaada kwa wahitaji

Watu au taasisi mbalimbali za kijamii hufanya jitihada za kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wahitaji. Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kuhamasisha wanajamii kushiriki katika kutoa misaada kwa wahitaji. Baadhi ya njia hizo ni pamoja na:

 1. Kutumia vyombo vya habari: Vyombo mbalimbali vya habari vinaweza kutumika kuhamasisha wanajamii kushiriki katika utoaji wa misaada kwa wahitaji mbalimbali. Vyombo vya habari ni pamoja na
 • televisheni,
 • magazeti, na
 • redio ambavyo vinaweza kufikisha taarifa au ujumbe kwa watu wengi zaidi na kwa urahisi.
 • Kwa mfano, kupitia televisheni, watu wanaoshiriki kutoa misaada wanaweza wakaoneshwa na kusikika. Jambo hili litasaidia kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kushiriki kutoa misaada kwa wahitaji.
 • Redio inaweza kutumika kutoa matangazo mbalimbali yanayohamasisha juu ya kusaidia kundi fulani linalohitaji msaada.
 • Vilevile, redio na televisheni huweza kutumika kuibua wahitaji na kuhamasisha jamii kuwasaidia kwa njia mbalimbali.
 1. Kutumia mitandao ya kijamii:
 • Mitandao ya kijamii ni njia ya mawasiliano inayowezesha kundi la watu kupeana taarifa. Taarifa hizo huibua mijadala mbalimbali. Kwa kutumia mitandao ya kijamii, wahitaji wanaweza kuchangiwa mawazo au michango mingine ya hali na mali.
 • Baadhi ya mitandao ya kijamii ni "Facebook", "WhatsApp", "Instagram", na "Twitter". Mitandao ya kijamii inaweza kutumika kuhabarisha jamii juu ya ushiriki wa watu au kundi fulani katika kutoa misaada kwa wenye uhitaji.
 • Pia, mijadala huweza kuendeshwa kuhusu umuhimu wa kusaidia wahitaji. Vilevile, mitandao ya kijamii hutumika kuhamasisha watu kushiriki katika kuwahudumia watu wenye uhitaji.
 • Vikundi au taasisi mbalimbali zinaweza kushiriki kwenye harakati za kuisaidia jamii. Kwa njia hii, washiriki wengine kwenye mitandao ya kijamii wanaweza wakahamasika na kutoa misaada.
 1. Midahalo na makongamano:
 • Hizi ni njia zinazoweza kutumika kuelimisha na kuhamasisha jamii kushiriki katika kuwasaidia watu wenye uhitaji.
 • Katika midahalo na makongamano, mada kuhusu watu wenye uhitaji zinaweza kuwasilishwa na kujadiliwa ikiwa ni pamoja na kupendekeza namna ya kusaidia wahitaji.
 • Mambo yanayohusu watu wenye uhitaji kama wazee, walemavu, yatima, wajane na wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi huweza kupewa kipaumbele ili kuijengea jamii moyo wa kuwasaidia na kubadili hall zao.
 1. Mabango na vipeperushi:

Mabango na vipeperushi vinaweza kutumiwa ili kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwasaidia watu wenye uhitaji. Ujumbe katika mabango na vipeperushi huweza kudumu kwa muda mrefu, hivyo, kuhamasisha jamii hatua kwa hatua.

 1. Kutembelea nyumba kwa nyumba:

Matembezi ya nyumba kwa nyumba ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa wanajamii. Pia, njia hii hutumiwa na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu katika kusaidia wanajamii kuelewa haki zao. Matembezi ya nyumba kwa nyumba huweza kuwa na malengo matatu tofauti. Kwanza, kubaini wenye uhitaji. Pili, kukusanya misaada kisha kugawa kwa wenye uhitaji na tatu, kuhamasisha watu kujitolea kusaidia wenye uhitaji.

 1. Semina na mikutano ya hadhara: Ili kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwasaidia wenye uhitaji, viongozi wa Serikali na taasisi zake hutumia njia hii kutoa maelekezo na hamasa kwa wananchi na jumuiya zinazowazunguka.
 2. Majadiliano ya vikundirika: Watu wa rika moja huwekwa pamoja na kufanya majadiliano jinsi ya kuhamasisha na kuwasaidia wenye uhitaji. Njia hii ni nzuri kwani watu wa rika moja ni rahisi kujadiliana bila vikwazo kutokana na kuwa katika umri mmoja na maono yanayokaribiana.
 3. Matumizi ya sanaa: Sanaa za maonesho ni nyenzo muhimu ya kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki katika kutoa misaada kwa watu wenye uhitaji. Matumizi ya sanaa kama vile nyimbo, maigizo na majigambo, hubeba ujumbe uliokusudiwa kuwafikia walengwa kwa haraka kwa kuwa kazi za sanaa huvutia.
 4. Vikundi vya kujitolea katika shule: Shule inaweza kuwa na vikundi vya kujitolea. Kazi ya vikundi hivi ni kuhamasisha wanafunzi wengine kujitolea na kusaidia watu wenye uhitaji.


Kuwahudumia na kuwafariji wahitaji katika jamii

 • Huduma na faraja ni vitu muhimu sang kwa watu wenye uhitaji. Hii ni kwa sababu watu wenye uhitaji huwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
 • Vitendo vya kuwasaidia wahitaji huenda sanjari na huruma, faraja na upendo kwa mtoa huduma. Wahitaji huhitaji kufarijiwa iii kuwasaidia kufurahia maisha kama watu wengine.
 • Mtu hufarijika au kupata utulivu baada ya kupewa maneno mazuri ya faraja na ya kutia moyo iii aweze kukabiliana na hali aliyonayo.

Baadhi ya huduma na faraja zinazoweza kutolewa kwa wahitaji ni kama ifuatavyo:

 1. Huduma ya kisheria: Hii ni huduma anayopewa mhitaji wa mambo yanayohusu sheria kama vile; kubambikwa kesi, kudhulumiwa mirathi, na unyanyasaji wa kijinsia. Huduma hii humsaidia aliyeonewa kupata haki na kufarijika. Kwa kawaida, huduma za kisheria hutolewa na watu au taasisi yenye wataalamu wa sheria. Huduma ya kisheria inapotolewa bila malipo hujulikana kama "msaada wa kisheria".
 2. Makazi: Huduma hii hutolewa kwa wahanga wa majanga yanayoharibu makazi. Kwa mfano, watu ambao nyumba zao zimebomolewa na mafuriko kipindi cha mvua, kuungua moto au paa kuezuliwa na upepo, hupewa hifadhi ya makazi ili kuwasitiri kwa muda. Aidha, wanaweza kupewa viwanja na vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ujenzi wa makazi mapya.
 3. Huduma muhimu za kiafya: Wahitaji hupewa huduma hii ill kukabiliana na matatizo ya kiafya yanayowakumba. Misaada ya kiafya inaweza kuwa vifaatiba, dawa, huduma za matibabu au elimu ya afya.
 4. Ushauri: Huduma hii hutolewa kwa mtu mwenye jambo linalomtatiza na linalohitaji ufumbuzi wa haraka iii aweze kuendelea na mipango yake au ndoto zake. Ndoto au mipango inaweza kuwa inayohusu elimu, afya, kazi, biashara au kilimo. Pia, ushauri huu unaweza kuwa ni wa namna ya kuhimili changamoto za maisha kama vile, kufiwa na wazazi, watoto, kupata magonjwa ya kudumu au wazazi kufukuzwa kazi. Ushauri unaotolewa kwa watu wenye hali hizi huitwa unasihi.

Umuhimu wa kuwahudumia na kuwafariji wahitaji katika jamii 

Utoaji wa huduma na faraja una faida nyingi ikiwa ni pamoja na:

 1. Kujenga upendo: Huduma anayopatiwa mhitaji husaidia kujenga upendo. Kwa mfano, mtu aliyepata ajali ya gari, moto, mafuriko na majanga mengine, hujenga upendo mkubwa kati yake na wale waliomsaidia. Upendo huu hutokana na ile hall ya kuona kwamba wanajamii wengine wanajali na kujitolea kumsaidia bila malipo.
 2. Kujenga umoja na mshikamano: Kushirikiana kwa pamoja katika kuwasaidia watu wenye uhitaji hujenga na kudumisha umoja na mshikamano kwa wanajamii. Ushirikiano huwaweka watu pamoja iii kutatua changamoto zinazowakabili.
 3. Kulinda haki za binadamu: Vitendo vya kuwahudumia wahitaji huwajengea wanajamii utayari na utashi wa kulinda haki za binadamu. Kwa mfano, haki ya kuishi hulindwa na wanajamii kwa kuwapatia wahitaji huduma mbalimbali kama vile; malazi, mavazi, chakula, na matibabu ili kujikimu kimaisha.
 4. Kudumisha udugu: Kuwahudumia na kuwafariji wahitaji, hujenga udugu katika jamii. Wanajamii wanapotoa misaada ya kijamii hujenga tabia ya upendo, ushirikiano na kujali wenzao, hivyo kuwafanya waishi kama ndugu.
 5. Kuthamini utu: Kutoa msaada na kuwafariji watu wenye uhitaji ni kitendo cha kuthamini utu wao. Mfano wa vitendo vya kujali utu ni kumsaidia mwanafunzi asiyeona kwa kumshika mkono anapokwenda maliwato au sehemu hatarishi kama vile kuvuka barabara na sehemu nyinginezo.Kwa kushirikiana na wenzako katika kikundi, chambueni makundi ya wahitaji yasiyopungua matano yanayohitaji huduma na faraja shuleni kwenu, kuijini au mtaani. Kisha, watembelee au buni mbinu mtakazotumia kuwapa huduma na faraja na wasilisha darasani kwa majadiliano.

Mikakati ya kuwatambua watu wenye uhitaji

 • Ili kuweza kuwapatia misaada na faraja watu wenye uhitaji, ni muhimu kubaini mahali walipo na mahitaji yao. Mikakati ya kuwatambua watu wenye uhitaji husaidia kuwajua na kuwapa misaada stahiki. Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na:
 1. Mikutano ya hadhara: Kuwapo kwa mikutano ya hadhara katika vijiji na mitaa husaidia kutambua wahitaji katika jamii. Mikutano huwapa wanajamii fursa ya kuibua changamoto zinazowakabili; kwa mfano, watoto waliopo katika mazingira hatarishi, wajane waliodhulumiwa mirathi, na wanajamii wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
 2. Makongamano na mihadhara ya kidini: Mikusanyiko ya kidini huhudhuriwa na watu wenye mahitaji mbalimbali. Ushirikiano wa viongozi wa dini na wanajamii katika mihadhara na makongamano husaidia kuwatambua wahitaji waliopo katika jamii na kuwapa misaada. Kwa mfano, makanisani au misikitini, vipo vikundi mbalimbali vinavyoweza kushiriki kubainisha wahitaji.
 3. Vyombo vya habari: Vyombo vya habari hutambua na kutangaza changamoto za watu mbalimbali wenye uhitaji. Vilevile, wanajamii hutumia vyombo vya habari kutoa taarifa za watu wenye uhitaji. Mifano ya vyombo vya habari ni televisheni, redio na magazeti. Kupitia vyombo vya habari, watu wenye uhitaji hutambulika na jamii kisha kupatiwa misaada.

(d) Kushirikiana na taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali: 

 • Ushirikiano na taasisi hizi ni muhimu kwa kuwa taasisi hizi hujihusisha na shughuli mbalimbali katika jamii Mikakati ya kuwatambua watu wenye uhitaji katika jamii huweza kufanywa kupitia taasisi kama vile shule, zahanati au ofisi za Serikali za mitaa na taasisi za kidini. Taasisi hizi huwa na taarifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na taarifa za wahitaji, hivyo ni rahisi kuwatambua wanajamii wenye uhitaji.

(e) Mitandao ya kijamii:

 • Hii ni njia inayotumiwa na wanajamii kutoa na kupokea taarifa mbalimbali. Hivyo, inaweza kutumika kwa urahisi kuwatambua watu wenye uhitaji. Kwa mfano, kupitia mitandao ya kijamii kama vile "Twitter", "Instagram", na "WhatsApp" watu wenye uhitaji wanaweza kubainishwa na watu kujitokeza kuwasaidia.

www.learninghubtz.co.tz

MTIHANI WA MWISHO WA MADA

URAIA NA MAADILI LA SABA

KUWAPENDA WENZETU KATIKA JAMII

MADA YA KWANZA

Chagua jibu sahihi.

 1. Huduma za kisheria kwa wahitaji huweza kupatikana sehemu gani?
 1. Asasi binafsi za utetezi wa haki za binadamu, mahakamani na magereza
 2. Kwa mwanasheria, mahakamani, na asasi binafsi za utetezi wa haki za binadamu
 3. Shuleni, vituo vya polisi na vituo vya afya
 4. Mahakamani, ofisi za vijiji na magereza
 1. Nini umuhimu wa kuwahudumia na kuwafariji wahitaji katika jamii?
 1. Kujenga upendo na kuthamini utu
 2. Kudumisha udugu na kujitangaza
 3. Kulinda haki za binadamu na haki za kisiasa
 4. Kukuza utegemezi kwa wahitaji
 1. Ni njia zipi zinazoweza kutumika kwa haraka kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutoa misaada kwa wahitaji?
 1. Televisheni, redio na mitandao ya kijamii
 2. Semina, mikutano ya hadhara na makongamano
 3. Mikutano ya hadhara, semina na vipeperushi
 4. Redio, mikutano ya hadhara na mitandao ya kijamii

Andika “kweli” kwa sentensi iliyo sahihi na “si kweli” kwa sentensi isiyo sahihi.

 1. Watu waliokumbwa na majanga ya moto na mafuriko ni miongoni mwa wahitaji………….
 2. Televisheni huchangia wahitaji wasipate msaada kwa haraka…………..
 3. Vyakula, malazi, huduma za afya na Faraja ni baadhi ya mahitaji kwa wahitaji…………..
 4. Msaada wa kisheria ni muhimu kwa wahitaji katika jamii………..
 5. Nyimbo, redio na mitandao ya kijamii husaidia kufikisha ujumbe kwa jamii ili kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji……………
 6. Faraja ni kitendo cha kuwaliwaza watu au mtu aliyepatwa na matatizo………….

Oanisha kipengele kutoka sehemu A na maneno yaliyopo sehemu B kisha andika herufi ya jibu sahihi katika nafasi uliyopewa.

Sehemu A

Jibu

Sehemu B

 1. Misaada kwa wahitaji
 2. Mabango na vipeperushi
 3. Watoto yatima na wazee
 4. Utu
 5. Mitandao ya kijamii
 1. Wahitaji katika jamii
 2. Wavuti ambapo watu hujumuishwa Pamoja na kutumiana ujumbe au kuwa na mijadala kupitia simu za mkononi au kompyuta
 3. Ubinadamu, upendo na huruma
 4. Vyakula, mavazi, huduma za afya, vifaa mbalimbali na makazi
 5. Njia ya kutoa elimu kwa wahitaji
Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256