JIOGRAFIA STANDARD III SUBJECT NOTES
CHAPTER : 1  Jiografia na Mazingira

Sura ya 01 : Dhana ya Jiografia na Mazingira

Utangulizi

Binadamu anapaswa kuielewa Jiografia na kuyafahamu vema mazingira yanayomzunguka ili kujua namna bora ya kuhusiana nayo. Jiografia inamwezesha binadamu kuyaelewa mazingira yanayomzunguka, jinsi ya kuyatumia na kuyahifadhi sasa na kwa vizazi vijavyo.

Katika sura hii, utajifunza kuhusu maana ya Jiografia na Mazingira, uhusiano baina ya Jiografia na Mazingira, na umuhimu wa kujifunza Jiografia na Mazingira. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuthamini somo la Jiografia na Mazingira.

Fikiri

Vitu vinavyomzunguka binadamu

Maana ya Jiografia

Jiografia ni somo linalohusu binadamu na mazingira yake. Hivyo, Jiografia inahusu dunia, angahewa, na vitu vilivyopo juu ya uso wa dunia, mtawanyiko wake na jinsi vinavyohusiana na binadamu. Uso wa dunia una mandhari kuu mbili ambazo ni mabara, na bahari. Mandhari hizi zinahusisha maumbo mbalimbali ambayo ni sehemu ya mazingira. Jiografia imejikita katika kumwezesha binadamu kujenga stadi za msingi zitakazomwezesha kuyafahamu mazingira yake na kuhusiana nayo kwa njia endelevu. Kielelezo namba 1 kinaonesha mandhari ya uso wa dunia.


Kielelezo namba 1: Mandhari ya uso wa dunia

Maana ya mazingira

Binadamu anavyoishi juu ya uso wa dunia anazungukwa na vitu mbalimbali. Vitu hivi vyote pamoja na binadamu mwenyewe ni sehemu ya mazingira. Hivyo, mazingira ni vitu vyote vinavyomzunguka binadamu. Vitu vinavyomzunguka binadamu vinaweza kuwa ni vya asili ambavyo huunda mazingira ya asili au vilivyotengenezwa na binadamu. Vitu vya asili ni vile ambavyo havijatengenezwa na binadamu kama vile milima, mabonde, misitu, wanyama, mito, bahari, ardhi, na hewa. Vitu vilivyotengenezwa na binadamu ni kama vile nyumba, barabara, bustani, meza, magari na vitu vingine vyote ambavyo siyo vya asili. Maelezo kuhusu vitu vinavyounda mazingira yanaweza kufupishwa kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 2.


Kielelezo namba 2: Vipengele vya mazingira

Vitu vyote vya asili na vilivyotengenezwa na binadamu vinaweza kupatikana nyumbani, shuleni, au mahali popote. Binadamu hutegemea mazingira kufanya shughuli zake zote zinazomwezesha kuishi. Hivyo, binadamu ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira kwa matumizi endelevu. Kielelezo namba 3 kinaonesha baadhi ya vitu vinavyopatikana katika mazingira.


Kielelezo namba 3: Baadhi ya vitu vinavyopatikana katika mazingira

Mazingira ya shule yetu

Kazi ya kufanya namba 1

Chunguza vitu vilivyomo katika mazingira ya shule, kisha:

1. Bainisha vitu vya asili na visivyo vya asili ulivyoviona; na
2. Eleza faida ya vitu ulivyovibaini.

Mazingira ya shule ni vitu vyote vinavyopatikana shuleni. Vitu hivyo ni kama vile madarasa, ofisi za walimu, nyumba za walimu, miti, bustani za maua, viwanja vya michezo, bendera ya taifa, na vyoo vya wanafunzi na vya walimu. Pia, mazingira ya shule yanaweza kuwa na mabweni, maktaba, maabara za masomo na vitu vinginevyo vya asili kama vile mito na vilima. Ndani ya darasa kunaweza kuwa na vitu kama vile madawati, viti, meza, vitabu, ubao na vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia. Vilevile, wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wa shule ni
sehemu ya mazingira ya shule.

Mazingira ya shule moja yanaweza kutofautiana au kufanana na ya shule nyingine kutokana na vitu vilivyomo katika shule husika. Kimsingi, vitu vinavyounda mazingira ya shule vina umuhimu katika ufundishaji na ujifunzaji hivyo, vinapaswa kutunzwa.

Kazi ya kufanya namba 2

Chunguza Kielelezo namba 4, kisha jibu maswali yanayofuata:


Kielelezo namba 4: Mazingira ya shule

Maswali

1. Ni vitu gani unaviona katika Kielelezo namba 4?

2. Ni vitu gani muhimu ukiviondoa katika Kielelezo namba 4 vitaathiri mazingira ya shule? Toa sababu.

Mazingira ya nyumbani

Kazi ya kufanya namba 3

Chunguza Kielelezo namba 5, kisha jibu maswali yanayofuata:


Kielelezo namba 5: Mazingira ya nyumbani

Maswali

1. Ni vitu gani unaviona katika Kielelezo namba 5?
2. Ni vitu gani katika Kielelezo namba 5, vipo katika mazingira ya nyumbani kwenu?

Mazingira ya nyumbani ni vitu vyote vinavyopatikana mahali tunapoishi. Vitu hivyo vinaweza kuwa nje au ndani ya nyumba. Mazingira ya nje ya nyumba yanaweza kuwa na vitu kama miti, magari, maua, ndege, wadudu, wanyama, mito, milima, mabonde na vitu vingine kulingana na mahali tunapoishi. Pia, mazingira ya ndani ya nyumba yanaweza kuwa na vitu kama kitanda, makochi, vyombo vya kupikia, vifaa vya usafi, pamoja na vitu vingine vyote vinavyopatikana ndani ya nyumba.

Kwa kawaida, mazingira yanaweza kufanana au kutofautiana kutokana na vitu vinavyopatikana katika eneo hilo. Hivyo, siyo lazima mazingira ya nyumba moja yafanane na ya nyumba nyingine. Pia, siyo lazima mazingira ya eneo moja yafanane na ya eneo lingine.

Zoezi la 1

1. Eleza tofauti iliyopo baina ya mazingira ya nyumbani na mazingira ya shuleni.

2. Mazingira ya nyumbani yanaweza kubadilika kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika nyumbani.

(a) Eleza shughuli zinazoweza kuboresha mazingira ya nyumbani kwenu.

(b) Eleza shughuli zinazoweza kuharibu mazingira ya nyumbani kwenu.

Kazi ya kufanya namba 4

Ukiwa unaelekea shuleni kwako fanya yafuatayo:

1. Chunguza mazingira ya njia unayopita kuelekea shuleni kwako.

2. Bainisha vitu unavyoviona.

3. Bainisha vitu ulivyoviona ambavyo havipo katika mazingira ya nyumbani kwenu.

Uhusiano wa Jiografia na Mazingira

Jiografia na Mazingira ni dhana zinazohusiana na ni vigumu kuzitenganisha. Tumejifunza kwamba mazingira ni vitu vyote vinavyotuzunguka, wakati Jiografia inapambanua kuhusu vitu hivyo. Kwa hiyo, Jiografia inatupatia uelewa kuhusu mazingira yanayomzunguka binadamu na namna tunavyoweza kuhusiana nayo. Vitu kama vile misitu, milima, maziwa, mito, bahari, hali ya hewa, ardhi, na wanyama ni sehemu ya Jiografia na Mazingira. Kwa hiyo, ni muhimu kujifunza dhana hizi mbili kwa pamoja.

Kazi ya kufanya namba 5

Chunguza Kielelezo namba 6, kisha jibu maswali yanayofuata:


Kielelezo namba 6: Shughuli mbalimbali katika mazingira

Maswali

1. Bainisha shughuli zinazofanyika katika Kielelezo namba 6.
2. Eleza mazingira ambayo shughuli hizo hufanyika.
3. Ni shughuli zipi ulizozibaini katika Kielelezo namba 6 hufanyika katika mazingira unayoishi?
4. Kwa nini baadhi ya shughuli katika Kielelezo namba 6, hazifanyiki katika mazingira unayoishi?

Umuhimu wa kujifunza Jiografia na Mazingira

Kujifunza Jiografia na Mazingira kunatuwezesha kuyaelewa mazingira yetu. Pia, Jiografia na mazingira inatuwezesha kutambua rasilimali zilizopo katika mazingira yetu na namna ya uzitumia, kuzitunza na kuzilinda. Mifano ya rasilimali hizo ni wanyama pori, mito, maziwa, bahari, misitu, ardhi, madini na milima. Vilevile, kujifunza Jiografia na Mazingira kunatuwezesha kujua shughuli za binadamu zinazoweza kufanyika katika maeneo mbalimbali. Mfano, maeneo yenye mito, maziwa, na bahari yanaweza kutumika kufanya shughuli za uvuvi, usafiri wa majini au utalii. Maeneo ya tambarare yenye udongo wa rutuba na mvua ya kutosha yanafaa zaidi kwa kilimo na ufugaji. Maeneo yenye misitu yanaweza kutumika kufanya shughuli za kupasua mbao na ufugaji wa nyuki.

Aidha, kujifunza Jiografia na Mazingira kunatuwezesha kuelewa kuhusu hali ya hewa na tabianchi iliyopo mahali fulani. Mfano, eneo lenye miti mingi huwa na hali ya hewa nzuri na mandhari yenye kuvutia. Vilevile, maeneo yenye milima yanaweza kuwa na hali ya hewa yenye baridi kwa sababu ya mwinuko mkubwa. Binadamu hulazimika kuvaa nguo nzito kama sweta kujikinga na baridi. Maeneo ya Tanzania yaliyopo karibu na mwambao wa bahari mara nyingi huwa na hali ya joto zaidi kuliko maeneo ya bara. Hivyo, watu katika maeneo hayo wanaweza kuvaa nguo nyepesi ili kuepuka au kupunguza madhara ya joto. Hata hivyo, hali ya joto katika maeneo ya pwani inaweza kutofautiana kutegemeana na mwinuko wa ardhi na mwelekeo wa upepo.

Jiografia na Mazingira inasaidia kubaini na kuelewa majanga ya asili kama vile mafuriko na vimbunga, na jinsi ya kuepuka athari za majanga hayo. Pia, inasaidia katika kupanga na kutekeleza ujenzi wa miundombinu na huduma za jamii. Mifano ya miundombinu na huduma za jamii ni barabara, hospitali, na shule. Hivyo, elimu ya Jiografia na Mazingira, inamwezesha binadamu kujua maeneo yanayohitaji kupatiwa huduma hizo. Kwa ujumla, kuna umuhimu wa kujifunza somo la Jiografia na Mazingira ili kuwa na matumizi sahihi na endelevu ya vitu vilivyomo katika mazingira. Mfano, matumizi endelevu ya maji, misitu na ardhi.

Zoezi la 2

1. Kwa nini tunajifunza kuhusu Jiografia na Mazingira?
2. Uelewa kuhusu majanga ya asili unasaidia nini?
3. Ni rasilimali zipi za asili zinapatikana katika mazingira unayoishi?

Zoezi la marudio

Chagua herufi ya jibu sahihi

1. Mazingira ya asili yanaweza kuwa endelevu kwa kufanya nini?

 1. Kuchimba madini
 2. Kuyatunza na kuyahifadhi
 3. Kujenga nyumba za kisasa
 4. Kuanzisha viwanda

2. Unaweza kufanya shughuli gani tofauti na uvuvi kama unaishi maeneo yenye mito, mabwawa, na maziwa?

 1. Kilimo cha umwagiliaji
 2. Uvunaji wa mazao
 3. Utengenezaji wa mbao
 4. Uwindaji na uuzaji wa ngozi

3. Jiografia na Mazingira inasaidia kupata ufahamu wa namna binadamu anavyoweza ______

 1. kuhusiana na vitu vinavyomzunguka
 2. kutengeneza mizinga ya nyuki
 3. kupanga mtawanyiko wa vitu katika mazingira
 4. kutengeneza samaki

4. Tabianchi ya sehemu moja hutofautiana na ya sehemu nyingine kwa sababu ya_________

 1. watu waliopo katika mazingira
 2. sura ya nchi na uoto uliopo katika mazingira
 3. wanyama waliopo katika mazingira
 4. wadudu waliopo katika mazingira

5. Ufugaji wa nyuki hutegemea uwepo wa rasilimali gani muhimu?

 1. Maji, majani na miamba
 2. Miti, maua na misitu
 3. Milima, mabonde na bahari
 4. Mvua, magogo na majani

6. Maeneo ya Tanzania yaliyopo karibu na bahari mara nyingi huwa na hali ya hewa gani?

 1. Baridi
 2. Baridi na joto
 3. Joto
 4. Unyevunyevu

7. Jirani na nyumbani kwenu kuna mto wenye maji mnayoyatumia katika matumizi mbalimbali. Je, ni ujuzi gani katika Jiografia na Mazingira utakuwezesha kuwa na matumizi endelevu ya mto huo?

 1. Hali ya hewa
 2. Utunzaji wa mazingira
 3. Kilimo cha umwagiliaji
 4. Uvuvi na utalii

Maswali ya majibu mafupi

8. Tunapata faida gani kwa kupanda miti katika mazingira ya shule?

9. Endapo mzazi au mlezi wako atanunua eneo kubwa lenye msitu, utamshauri afanye shughuli gani?

10. Ni sababu zipi za kijiografia na kimazingira zitakuongoza kuchagua eneo la kuanzisha kilimo?

11.Jiografia inatuwezesha kufahamu namna sahihi ya kutumia vitu vilivyopo katika mazingira. Bainisha matumizi sahihi ya ardhi katika mazingira unayoishi.

Msamiati

 • Ardhi sehemu ngumu ya uso wa dunia ambayo haijafunikwa na maji.
 • Bahari eneo kubwa la maji ya chumvi ambalo hufunika sehemu kubwa ya uso wa dunia.
 • Bustani eneo lililopandwa miti, maua, nyasi, matunda au mbogamboga.
 • Hali ya hewa hali ya anga katika eneo fulani maalumu kwa wakati fulani.
 • Miundombinu jumla ya njia za usafiri, majengo na huduma ambazo hutoa msingi na usaidizi wa shughuli mbalimbali katika eneo maalumu.
 • Rasilimali vitu muhimu na vya thamani vilivyopo katika mazingira.
 • Shughuli za binadamu kazi au matendo mbalimbali ambayo watu hufanya katika maisha yao ya kila siku.

www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256