Sura ya 02 :Sura ya nchi

Utangulizi

Uso wa dunia umefunikwa kwa tabaka gumu ambalo huitwa ardhi. Ardhi ina maumbo mbalimbali. Maumbo hayo huunda sura ya nchi ya eneo fulani. Katika sura hii utajifunza kuhusu maana ya sura ya nchi, maumbo makuu ya sura ya nchi, mtawanyiko na umuhimu wa maumbo ya sura ya nchi. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuhusiana vema na maumbo ya sura ya nchi yaliyopo katika mazingira unayoishi.

Fikiri

Maumbo tofauti ya ardhi uliyowahi kuyaona

Maana ya sura ya nchi

Sura ya nchi ni mwonekano wa maumbo mbalimbali ya ardhi katika uso wa dunia. Maumbo haya huunda mandhari tofauti za sehemu mbalimbali. Sura ya nchi huwa na mtawanyiko wa maumbo kama vile milima, vilima, tambarare, uwanda wa juu, besini na mabonde. Shughuli za binadamu kama vile kilimo, ujenzi wa makazi, na ufugaji hutegemea maumbo ya sura ya nchi ya mahali fulani. Hivyo, ni muhimu kuyafahamu maumbo ya sura ya nchi ili tuweze kuhusiana nayo kwa njia ambayo ni endelevu.

Kazi ya kufanya namba 1

1. Chunguza Kielelezo namba 1, kisha bainisha maumbo ya sura ya nchi yaliyopo katika kielelezo hicho.


Kielelezo namba 1: Maumbo mbalimbali ya sura ya nchi

2. Chunguza na eleza maumbo ya sura ya nchi yaliyopo katika mazingira unayoishi.

Maumbo makuu ya sura ya nchi

Kazi ya kufanya namba 2

Tumia vyanzo vya mtandaoni kutafuta video zinazohusu maumbo makuu ya sura ya nchi ya Tanzania. Angalia au sikiliza video hizo kisha, andika ufupisho.

Sura ya nchi ya mahali hutokana na uwepo wa maumbo mbalimbali ya ardhi katika eneo husika. Maumbo hayo hujulikana kama maumbo ya sura ya nchi. Maumbo ya sura ya nchi hutofautiana kimuonekano kulingana na urefu na umbo. Ili kuelewa tofauti za maumbo ya ardhi katika maeneo mbalimbali, inatupasa kujifunza kuhusu maumbo makuu ya sura ya nchi. Maumbo hayo ni milima, mabonde, vilima, uwanda wa juu, besini na tambarare. Kielelezo namba 2 kinaonesha muonekano wa maumbo makuu ya sura ya nchi.


Kielelezo namba 2: Maumbo makuu ya sura ya nchi

Mtawanyiko na umuhimu wa maumbo makuu ya sura ya nchi ya Tanzania Kila eneo la ardhi lina sura yake kutokana na maumbo mbalimbali yanayoonekana. Kwa mfano, sura ya nchi ya Tanzania ni ya kipekee kutokana na muonekano wake. Uwepo wa milima, mabonde, tambarare, vilima, besini, na uwanda wa juu ni fahari ya Tanzania. Maumbo haya yote hupatikana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kazi ya kufanya namba 3

Tumia vitabu na vyanzo vya mtandaoni, soma au sikiliza kuhusu mtawanyiko wa maumbo makuu ya sura ya nchi ya Tanzania. Kisha, bainisha shughuli zinazofanyika katika maumbo ya sura ya nchi ya Tanzania na yale yaliyopo katika mazingira unayoishi.

Mlima

Mlima ni umbo la ardhi lenye mwinuko mrefu zaidi juu ya uso wa dunia. Sehemu ya juu ya mlima huitwa kilele cha mlima. Kilele cha mlima kinaweza kuwa na theluji au barafu au kisiwe nazo. Pia, mlima huwa na miteremko mikali. Tanzania ina milima mingi inayotofautiana kwa urefu. Mfano; mlima mrefu kuliko yote Tanzania ni mlima Kilimanjaro, ambao upo katika mkoa wa Kilimanjaro. Mlima Kilimanjaro una urefu wa mita 5,895. Kilele cha mlima Kilimanjaro kimefunikwa na barafu na theluji. Hii ni kwa sababu kadiri mwinuko wa ardhi unavyoongezeka joto hupungua. Pia, mlima Kilimanjaro ni wa kwanza kwa urefu barani Afrika. Kielelezo namba 3 kinaonesha mandhari ya mlima Kilimanjaro.


Kielelezo namba 3: Mlima Kilimanjaro

Milima mingine iliyopo Tanzania ni mlima Meru uliopo mkoa wa Arusha wenye urefu wa mita 4,566, na mlima Rungwe uliopo mkoa wa Mbeya wenye urefu wa mita 2,981. Milima mingine ni safu za milima ya Uluguru iliyopo mkoa wa Morogoro yenye urefu wa mita 2,630, na safu za milima ya Usambara iliyopo mkoa wa Tanga yenye
urefu wa mita 2,290.

Vilima

Vilima ni umbo la ardhi lililoinuka kwa urefu wa wastani. Vilima vina urefu mdogo kuliko milima na havina miteremko mikali kama milima. Hata hivyo vilima vina kilele kama mlima. Vilima hupatikana katika maeneo mbalimbali ya Tanzania. Mfano wa vilima ni kama vile: vilima vya Ngorongoro vilivyoko Arusha, vilima vya Mererani vilivyoko Manyara, vilima vya Sao na Kitonga vilivyoko Iringa. Pia, kuna vilima vya Sekenke vilivyoko mkoa wa Singida. Kielelezo namba 4 kinaonesha vilima.


Kielelezo namba 4: Vilima

Umuhimu wa milima na vilima

Maumbo mbalimbali ya sura ya nchi ni muhimu katika maisha ya binadamu. Mara nyingi, milima, na vilima huwa ni vyanzo vizuri vya maji. Maji hayo hutumiwa na binadamu na viumbe wengine kwa matumizi mbalimbali. Pia, milima husababisha aina mojawapo ya mvua. Vilevile, milima na vilima ni sehemu za vivutio vya utalii. Watalii hupanda milimani na vilimani kuona misitu, maporomoko ya maji na viumbe mbalimbali wa porini. Aidha, watu hujipatia kipato kutokana na shughuli za utalii. Kielelezo namba 5 kinaonesha maporomoko ya maji kutoka kwenye vilima.

Kielelezo namba 5: Maporomoko ya maji

Pia, katika miteremko ya milima, kuna misitu minene yenye wanyama ambao ni vivutio vya utalii. Vilevile, miti iliyopo katika misitu hiyo inatupatia mbao, na vifaa vingine vya ujenzi. Baadhi ya miti ni dawa zinazotumiwa na binadamu kutibu magonjwa mbalimbali.

Zoezi la 1

Chagua herufi ya jibu sahihi

1. Zipi kati ya sifa zifuatazo zinatofautisha mlima na kilima?
(a) Urefu na miteremko
(b) Urefu na rutuba
(c) Miamba na udongo
(d) Ufupi na wingi wa theluji

2. Kwa nini vilele vya baadhi ya milima kama vile mlima Kilimanjaro vimefunikwa na barafu?

(a) Kuna joto kali
(b) Kuna mvua nyingi
(c) Kuna baridi kali
(d) Kuna maji mengi

Maswali ya majibu mafupi

3. Unafikiri ni changamoto zipi wanazozipata mafundi wa ujenzi wanapojenga nyumba maeneo yenye vilima au milima?

4. Athari zipi za mazingira zitatokea endapo kilimo kitafanyika kwenye miteremko ya milima?

5. Ni milima gani ipo katika mikoa ifuatayo:

(a) Arusha
(b) Mbeya
(c) Morogoro

Mabonde

Mabonde ni maumbo ya ardhi yenye kina kirefu. Mara nyingi mabonde huwa katikati ya milima au vilima kama inavyooekana katika Kielelezo namba 6.


Kielelezo namba 6: Bonde

Baadhi ya mabonde huwa na maji ambayo hutengeneza mito, mabwawa au maziwa. Mfano, katika nchi ya Tanzania kuna bonde kuu la ufa la Afrika Mashariki. Katika bonde hilo, kuna Ziwa Natron lililopo mkoa wa Arusha, Ziwa Eyasi na Manyara yaliyopo mkoa wa Manyara. Pia, kuna Ziwa Tanganyika linalopatikana katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Ziwa Tanganyika lina kina kirefu kuliko maziwa yote yanayopatikana Tanzania na Afrika kwa ujumla. Vilevile kuna Ziwa Nyasa linalopatikana mikoa ya Ruvuma, Njombe na Mbeya.

Umuhimu wa mabonde

Mabonde ni muhimu kwa sababu hukusanya maji kutoka kwenye milima na vilima. Hii inayafanya mabonde kuwa vyanzo vya maji. Sehemu zenye mabonde zilizo na maziwa, mito na mabwawa ni makazi ya viumbe wa majini wakiwemo samaki. Hivyo, sehemu hizi hutumika kwa shughuli za uvuvi. Pia, maeneo yenye mabonde ya mito huwa na udongo wenye rutuba hivyo hutumika katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji. Vilevile, mito na mabwawa hutumika kuzalisha umeme. Aidha, maziwa na baadhi ya mito hutumika kwa usafiri wa vyombo vya majini kama vile meli na boti.

Uwanda wa Juu

Uwanda wa juu ni sehemu ya ardhi yenye mwinuko wenye umbo la tambarare. Kielelezo namba 7 kinaonesha uwanda wa juu.


Kielelezo namba 7: Uwanda wa juu

Nyanda za juu zinaweza kutofautiana kwa umbo na kwa ukubwa. Mfano wa uwanda wa juu Tanzania ni uwanda wa juu wa kusini ambao unapatikana katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, na Njombe.

Umuhimu wa uwanda wa juu

Baadhi ya maeneo ya uwanda wa juu hutumika kujenga makazi na kuhifadhiwa kama vivutio vya utalii kutokana na uzuri wa mandhari na hali ya hewa. Mfano, hifadhi ya taifa ya Kitulo ipo katika uwanda wa juu kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Mbeya na Njombe. Hifadhi hii ipo kati ya vilele vya milima ya Kipengele, Uporoto na Safu za milima ya Livingstone. Hii ni hifadhi ya kwanza barani Afrika kuanzishwa kwa lengo la kutunza mimea yake ya asili jamii ya maua. Sehemu nyingine ya uwanda wa juu hutumika kwa kilimo.

Tambarare

Tambarare ni umbo la ardhi lisilokuwa na miinuko. Maeneo tambarare hayana milima, vilima, au miinuko mikubwa. Sehemu kubwa ya tambarare huwa na ardhi inayofanana kwa mwinuko wake kwa kiasi kikubwa kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 8. Mifano ya maeneo tambarare Tanzania ni baadhi ya maeneo ya mbuga ya Serengeti na Tarangire.


Kielelezo namba 8: Tambarare

Umuhimu wa maeneo ya tambarare

Sehemu za tambarare huwa na udongo wenye rutuba unaofaa kwa kilimo na shughuli za ufugaji. Kielelezo namba 9 kinaonesha kilimo katika eneo tambarare.


Kielelezo namba 9: Kilimo katika eneo tambarare

Pia, sehemu za tambarare hutumika kujenga makazi ya watu, na miundombinu mingine kwa kuwa maeneo haya hayahitaji usawazishaji mkubwa wa ardhi kwa vile hayana vilima na miinuko. Vilevile, maeneo ya tambarare ni mazuri kwa shughuli za michezo na usafiri wa ardhini. Aidha, maeneo haya yanaweza kuwa na misitu inayohifadhi wanyama na viumbe wengine wa porini ambao pia ni vivutio vya utalii.

Besini

Hii ni sehemu ya ardhi iliyobonyea na kutengeneza umbo kama la beseni. Besini inaweza kuwa na maji au kutokuwa na maji. Besini yenye maji hutengeneza ziwa. Mfano wa besini yenye maji ni Ziwa Viktoria lililopo mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, na Geita. Ziwa Viktoria ni kubwa kuliko maziwa yote yanayopatikana Tanzania na Afrika kwa ujumla.

Zoezi la 2

1. Eleza tofauti zilizopo kati ya Ziwa Viktoria na Tanganyika.
2. Ni mikoa ipi ya Tanzania iliyopo katika uwanda wa juu kusini?
3. Ni katika umbo lipi la sura ya nchi utapendelea zaidi kujenga nyumba yako? Kwa nini?
4. Unafikiri nini kitatokea endapo watu watajenga nyumba jirani na maeneo yenye mabonde?

Zoezi la marudio

Chagua herufi ya jibu sahihi

1. Ni katika umbo gani la sura ya nchi kati ya yafuatayo linaweza kusababisha kutokea kwa aina mojawapo ya mvua?

(a) Tambarare
(b) Bonde
(c) Mlima
(d) Besini

2. Safu za milima ya Usambara zinapatikana katika mkoa gani?

(a) Kilimanjaro
(b) Morogoro
(c) Tanga
(d) Mbeya

3. Oanisha safu A na safu B ili kuleta maana.

Safu A Safu B
i. Mlima A. ardhi iliyoinuka kwa urefu wa wastani na haina miteremko mikali
ii. Mabonde B. hakuna milima, vilima, wala miinuko mikubwa
iii. Tambarare C. una kimo kirefu zaidi kilichoinuka juu ya uso wa dunia
iv. Vilima D. hutokea katikati ya milima au vilima

Maswali ya majibu mafupi

4. Ni vitu gani vinavyotofautisha sura ya nchi ya mahali?

5. Bainisha kwa mifano maumbo makuu ya sura ya nchi yanayopatikana katika mikoa ifuatayo:

(a) Iringa
(b) Morogoro
(c) Mwanza
(d) Kigoma
(e) Kilimanjaro
(f) Singida

6. Tumia mifano halisi kueleza umuhimu wa maumbo ya sura ya nchi ya Tanzania.

Msamiati

  • Makazi sehemu ambapo watu huishi na kujenga nyumba zao
  • Mwinuko sehemu ya ardhi iliyoinuka kuliko maeneo mengine
  • Uso wa dunia sehemu ya nje ya dunia inayojumuisha maeneo ya nchi kavu na maji
  • Utalii Matembezi yanayohusisha watu kwenda kutembelea maeneo nje ya mazingira yao ya kawaida kwa lengo la kupumzika, biashara au kujifunza
  • Ziwa sehemu kubwa ya maji ambayo kwa kawaida huzungukwa na nchi kavu

www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256