JINA LA KITABU: NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE

MWANDISHI: EDWIN SEMZABA

WACHAPISHAJI: NYAMBARI NYANGWINE PUBLISHERS

MWAKA:2006

UHAKIKI WA FANI KATIKA TAMTHILIA

UTANGULIZI WA KITABU

Ngoswe penzi kitovu cha uzembe ni tamthiliya maarufu sana ambayo imewahi kuigizwa katika redio Tanzania na katika majukwaa mbalimbali hapa nchini. Ni tamthiliya ambayo imeundwa vyema katika vipengele vya fani na maudhui. Ameteua lugha nzuri na yenye mvuto kwa wasomaji yenye mbinu za kifasihi zilizosheheni, muundo wenye mtiririko mzuri, unaoakisi kuanza kuchipuka kwa matukio mpaka kilele cha matukio. Wahusika wamebeba vyema uhusika wao mfano Ngoswe.

Ameibua dhamira kuhusu mambo yanayoigusa jamii ya leo kama vile uzembe, madhara ya ulevi, uzembe kazini, suala la matabaka kati ya mjini na vijijini. Mtazamo, falsafa na msimamo wake ni kulenga kuibadilisha jamii na kuleta maendeleo.

JINA LA KITABU

Jina la kitabu “Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” ni jina ambalo limesawiri vyema yaliyomo ndani ya kitabu hicho, kwani Ngoswe ndio jina la mhusika mkuu anayebeba dhamira kuu ya tamthiliya. Pia penzi limeonekana kuwa ni kitovu cha uzembe kwani ndio yaliyopelekea kuteketezwa kwa karatasi za takwimu za sensa. Hivyo jina la kitabu si tu kwamba limesawiri yaliyomo katika kitabu bali pia katika jamii.

MTINDO

Mtindo alioutumia mwandishi ni dayalojia au majibizano. Mwandishi amepanga visa na masimulizi kwa kutumia majibizano ya wahusika.

  • Matumizi ya nafsi ya kwanza.Mwandishi ndiye ameyafafanua na kuelezea baadhi ya matukio. Katika karibu kurasa zote mwandishi ameonekana kuwa ndiye msimuliaji wa matukio.
  • Matumizi ya nafsi ya pili.Hapa watu wawili na zaidi wanajibizana. Tamthilya hii wahusika wanaojibizana kuibua dhamira na migogoro. Kuna majibizano baina ya mzee Mitomingi, Ngoswe na Mazoea nk.unaweza kupata mfano uk. wowote kwani ndio mtindo uliotawala.

MUUNDO

Muundo uliotumika ni muundo wa mojakwamoja au sahili. Kwani ameonesha tangu mwanzo wa mambo mpaka mwisho, anajenga visa vidogo mpaka visa vikuu au kileleni.Amepanga visa na matukio yake katika maonesho matano. Kila kichwa kina maelezo yaliyojadiliwa katika onesho hilo.

  • KIJITO:Hapa yanaeleza jinsi mambo yanavyoanza. Jinsi Ngoswe anavyoingia kijijini anavyopokelewa na kuanza kufahamiana na wenyeji wake.
  • VIJITO:Hapa Ngoswe anaanza kufanya kazi iliyompeleka kijijini na tunaanza kuoneshwa changamoto anazokumbana nazo.
  • MTO:Ni mwendelezo wa matukio ya mwanzo hapa visa vinazidi kukua.
  • JITO:Hapa Ngoswe anakumbana na changamoto nyingi zaidi katika kazi yake. Na hapa anazidi kuanguka kwani anajiingiza katika mapenzi na msichana Mazoea, anaendekeza ulevi na kuharibu kazi kabisa.
  • BAHARINI:Hapa inaoneshwa mwisho wa mambo jinsi yalivyokuwa. Yanaonekana mahojiano baina ya Serikali na Ngoswe na Mitomingi juu ya uzembe uliofanyika wa kupoteza takwimu na hapa ndipo suluhisho linapotolewa juu ya matatizo hayo.

WAHUSIKA

NGOSWE

  • Kijana wa kiume umri kati ya miaka 20-25
  • Ameelimika na amestaarabika
  • Anatumwa na serikali kufanya sensa kijijini
  • Anajihusisha na mapenzi na msichana mazoea
  • Ni mlevi
  • Hana umakini katika kazi
  • Aliharibu kazi ya serikali
  • Hafai kuigwa na jamii

MAZOEA

  • Ni msichana mwenye umri kati ya miaka 18-20
  • Ni binti wa Mzee Ngengemkeni Mitomingi
  • Hana elimu na hajastaarabika
  • Ana nidhamu ya woga
  • Ana tama
  • Hana msimamo alikubali kuchukuliwa na Ngoswe hali akijua alishatolewa mahari
  • Hafai kuigwa na jamii.

NGENGEMKENI MITOMINGI

  • Ni balozi katika kijiji chake
  • Ni baba mzazi wa Mazoea
  • Ameoa ndoa ya mitara, ana wake wawili
  • Hajaelimika
  • Anashikilia mila na desturi za kale
  • Mlevi
  • Mkali sana
  • Anateketeza karatasi za takwimu

MZEE JIMBI

  • Mwanakijiji
  • Hajaelimika kwani hajui hata umri wake
  • Ni mlevi
  • Ana wake wawili
  • Anashikilia ukale

MAMA MAZOEA

  • Mke mkubwa wa Mitomingi
  • Mama yake Mazoea
  • Mlezi wa familia
  • Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi katika familia

MAMA INDA

  • Mke wa pili Mzee Mitomingi
  • Mama yake Huzuni
  • Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi
  • Ni mlezi wa familia.

MANDHARI

Mandhari ya tamthiliya hii imechorwa katika mazingira ya kijijini. Mambo yanayoelezwa ni ya kijijini mfano kilimo, hali ya watu kimaisha, huduma duni sana za kijamii kama vile shule, umbali wa makazi toka nyumba moja hadi nyingine. Haya yanatudhihirishia vyema mandhari hiyo ambayo kwayo imeibua dhamira mbalimbali kama vile umaskini, ukosefu wa elimu, huduma duni za afya vijijini, masuala ya imani potofu nk.

MATUMIZI YA LUGHA

Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi kueleweka kwa wasomaji. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano uk. 1 “bell bottom”

Matumizi ya semi

  • Methali:Uk.22 “Penye nia pana njia”.Uk.27 “Waona vyaelea vyaundwa.”
  • Misemo:Uk.14 “Akuwaniae ujovu haji kweupe”
  • Nahau:Uk.11 “hebu keti tutupe mawe pangoni” –tule chakulaUk.7 “mbongo zimelala”-ana maarifa Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda”- anapenda pombe sana.

Matumizi ya tamathali za semi

  • Tafsida:Uk.21 “Wala hajarudi, kama ingekuwa ni kujisaidia si angekuwa amekwishamaliza?”
  • Tashbiha:Uk.1 “vumbi jekundu kama ugoro wa subiana”Uk.8 “sarawili yake miguuni kama kengele ya bomani”Uk.17 “wanaondoka huku wakitazamwa kama vile mizuka”
  • Sitiari:Uk.7 Mama Mazoea : “kiziwi mkubwa wee!”Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda!”Uk.26. “karatasi? za takwimu? Ndio wanyama gani hao?”
  • Mubaalagha:Uk.11 Mama Mazoea : “kupeleka chakula ndio umefanya makao!”Mama mazoea : “Kujibu swali ndio ukachukua mwaka mzima!”

Mbinu nyingine za kisanaa

  • Mdokezo:Uk.22 Mazoea : “sijui….. siwezi….. namuogopa baba”Uk.16 Ngoswe : “huyo mtoto wenu wa kwanza anaishi hapa au…..”
  • Takriri:Uk.9 “Mama Masikio! We Mama Masikio!”Uk.13. “Hodi! Hodi!”Uk.2 “karibu karibu”
  • Tashtiti:Uk.5 Ngoswe: “hivyo waitwa nani?”Mazoea: “mie?”Uk.22 Ngoswe: “mchumba? Kwani mchumba ni kitu gani?”Uk.26 Mitomingi: “karatasi? Za takwimu? Ndio wanyama gani hao?Hapa wahusika waliuliza maswali ambayo majibu yake waliyaelewa ila kutokana na kutaka kudhihirisha hasira, msisitizo nk. Ndio maana wametumia tashtiti.
  • Onomatopea/tanakali sauti:Uk.7 Kifaruhande anacheka “Ha! ha! ha!

Ujenzi wa taswira

Mwandishi ametumia taswira ya mto kuelezea visa vyake. Sehemu ya kwanza ni sehemu ya kijito, kijito ni kimto kidigo mwandishi hapa anaanza kueleza mambo yakiwa machanga kabisa ndio yanaanza.

Sehemu ya pili ni vijito. Huu ni muunganiko wa vijito vidogovidogo hapa mwandishi anaanza kueleza visa vidogovidogo. Sehemu inayofuata ni sehemu ya Mto. Hii inaashiria mambo yameanza kuwa mazito, visa vinakua zaidi na Ngoswe anazidi kuingia katika changamoto kubwa zaidi.

Pia Jito ni taswira ambayo mwandishi ameitumia kuashiria hatari zaidi mambo makubwa zaidi na hapa ndipo tunaona Ngoswe anaanguka kabisa katika kazi yake kwani Jito ni lenye maji mengi na yanayoenda kwa kasi hivyo huhitaji umakini mkubwa zaidi.

Mwisho sehemu ya Bahari ambapo hapa ndipo hatima ya mambo inaelezwa Ngoswe anazama na kupotea kabisa! Hafanikiwi kutoa takwimu kwani karatasi zilichomwa moto.

UHAKIKI WA MAUDHUI KATIKA TAMTHILIA

Maudhui katika Tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe

DHAMIRA

Dhamira kuu

  • Suala la kuchanganya kazi na mapenzi:Mhusika Ngoswe ambaye alitumwa na serikali kwenda kufanya zoezi la sensa la sensa kijijini anajiingiza katika mapenzi na binti Mazoea uk.5 na hivyo kusababisha kutokuwa makini na kazi yake. Anaamua kutoroka na Mazoea jambo ambalo linamfanya Mzee Mitomingi ateketeze karatasi za takwimu kwa kutoroshewa mwanae uk.28. hivyo tunaona jinsi mapenzi yallivyohaaribu kazi.Suala hili ni halisi katika jamii yeetu ya leo kwani watu wamekuwa wakijisahau na kuchanganya kazi na mapenzi, mwandishi ameliweka jambo hili wazi ili jamii iweze kubadilika na kuacha tabia hiyo mbaya inayodidimiza maendeleo ya jamii.

Dhamira ndogo ndogo

  • Hasara za ulevi:Suala la ulevi na hasara zake limejadiliwa na mwandishi akiwachora wahusika kama Ngoswe na Mzee Mitomingi na wanakijiji ambao ni walevi. Mfanouk.6 Mzee Mitomingi anasema “haya matatizo yote ni shauri ya pombe, sina shaka yuko kilabuni”.Ngoswe naye anapata hasara kutokana na ulevi kwani analewa sana na kuchoma karatasi za takwimu na kusababisha kuhesabu upya watu tena jamo ambalo lilipoteza mda zaidi.uk.18-19.Katika jamii yetu suala laulevilina hasara kubwa kama vile kurudisha nyuma suala zima la maendeleo, kusababisha vifo na ajali, migogoro ya kifamilia na matatizo mengine mengi. Jamii inaaswa kujirekebisha na kukemea suala hili kwani lina madhara makubwa katika koizazi cha sasa.
  • Umuhimu wa elimu:Wanakijiji wa kijiji cha Mzee Ngengemkeni hawana elimu na wala hawatilii maanani juhudi za kupata elimu. Huduma za kielimu ni mbovu kama vile shule iko mbali sana hazipo kijijini kwao. Familia nyingi na watoto wao hawasomi. Uk.16. zoezi la uhesabuji watu linakuwa gunu zaidi kuutokana na watu kutokuwa na elimu.Ili kupata maendeleo katika jamii yoyote ile si budi suala la elimu kupewa kipaumbele na wanaoelimika wanapaswa kutumia vyema elimu yao. Wanapaswa kurejesha mchango chanya katika jamii na sio kurudisha nyuma maendeleo.Mfano Ngoswe ambaye hakutumia vizuri elimu yake. Elimu lazima itumike kuibadilisha jamii na kusukuma mbele zaidi maendelo.
  • Suala la umaskini:Wanakijiji wanaelezwa kuwa na maisha duni sana ya hali ya chini, makazi duni. Mfano wanalala kwenye vibanda vibovu mfano Ngoswe anakaribishwa kulala katika moja ya kibanda kibovu kinaachovuja. Mwandishi amelionesha hilo makusudi kwani maeneo mengi ya mijini yamesahaulika na bado wapo nyuma kimaendeleo. Serikali iangazie maeneo ya vijijini na kutoa elimu ya namna ya kupambana na umaskini, kujenga makazi bora. Pia wanakijiji wanaaswa kuacha uvivu na kujishughulisha ili kumpinga adui maskini.
  • Suala la malezi na ndoa za mitara:Wanakijiji wa Balozi Mitomingi wana utamaaduni wa kuoa mke zadi ya mmoja. Pia suala la malezi si la baba bali la mama pekee. Mzee Mitomingi aliwaachia wakeze suala la kulea watoto na kuwa watazamaji wa familia, hali kadhalika Mzee Jimbi mda wote alishinda kilabuni kwenye pombe na hakuwa na mda wa kufanya kazi yoyote ya kimaendeleo wala kuangalia familia suala hilo aliwachia wake zake. Hili si jambo zuri.Kuhusu ndoa za mitara kwa jamii ya leo zina athari kwanikatika malezi ni vigumu kumudu ukubwa wa familia, usalama wa kiafya huwa ni mdogo kwani wanandoa wana hatari kubwa ya kuambukizana magonja hatari.
  • Imani potofu na ushirikina:Uk.14 tunaona wanawake wanakataa zoezi la kuhesabiwa kutokana na imani kuwa mtu anayehesabu watu ni mchawi. Kutokana na hili, zoezi la uhesabuji watu linakuwa gumu.Wanaamini kuwa mtu akifa basi amerogwa. Mfanouk.16 “wamemroga bure mume wangu. alikufa akiwa na nguvu zake”.Mambo mengine ya kimaendeleo hushindikana kutokana na imani potofu wanazoshikiliawanajamii. Mwandishi amelionesha ili jamii ijikomboe kutoka katika imani hizo potofu. Pia anaona upo umuhimu wa serikali kuelimisha jamii juu ya hili, kuacha kushikilia ukale na kuchangamkia maendeleo.

  • Utabaka kati ya mjini na vijijini:Katika tamthiliya hii suala la utabaka kati ya mjini na vijijini. Kuna tofauti kubwa kati ya mjini na vijijini katika masuala ya huduma za jamii kama vile elimu, afya na mengineyo. Uk.29 Ngoswe anasema:“Shurti vijiji kurekebishwa,Ujinga, magonjwa naUmaskini kupigwa vita,Na njia ni moja tu!Kuishi pamoja kijamaa.”Hivyo mwandishi amelionesha jambo hili ambalo linahalisika katika jamii yetu ya leo, hivyo si budi serikali kulitazama jambo hili kwa jicho pevu. Teknolojia na mawasiliano yaboreshwe kwani ni msingi wa maendeleo.

Nafasi ya mwanamke

Tamthiliya ya Ngoswe imemchora mwanamke katika sura zifuatazo:

  • Kama mlezi na muangalizi wa familia:Mama Mazoea na mama Inda na akina mama wengine ni waangalizi wa familia.
  • Kama chombo cha starehe:Wanaume wameonekana kuwatumia wanawake kwa ajili ya starehe. Hii inathibitishwa na tabia ya kuoa mitara.
  • Kama kiumbe duni asiyeweza kutoa maamuzi yoyote ndani ya jamii yake:Mfano Mitomingi anasemauk.26 “nyie wanawake akili zenu wote sawa si Mazoea si mama yake….”Jamii inashauriwa kumpa mwanamke nafasi na kumthamini hasa katika masuala ya uamuzi.
  • Kama mtu asiye na msimamo:Mfano ni Mazoea ambaye anaamua kutoroka na Ngoswe huku alijua ametolewa mahari.

MIGOGORO

  • Mgogoro kati ya Ngoswe na Mzee Mitomingi: Mgogoro huu unatokea baada ya Ngoswe kuamua kumtorosha binti wa Mitomingi. Mitomingi anaamua kuchoma moto karatasi za takwimu.
  • Mgogoro baina ya Mazoea na wazazi wake: Sababu ya mgogoro ni Mazoea kujihusisha na mapenzi na kutoroka na Ngoswe hali akijua alishatolewa mahari. Baba yake alimuadhibu kwa kumchapa.
  • Mgogoro kati ya Ngoswe na serikali: Sababu ya mgogoro ni kutokana na Ngoswe kushindwa kupeleka hesabu ya watu kama alivyoagizwa. Uk.28-29.
  • Mgogoro wa nafsi wa Ngoswe. Ngoswe alisononeka na kuwaza kuwa angejibu nini serikalini kwani karatasi za takwimu ziliteketea kutokana na uzembe wake.

FALSAFA:Imani ya mwandishi anaamini kuwa mabadiliko na maendeleo katika jamii yanawezekana kama watu watajishughlisha na pia kama serikali itagawanya vyanzo vya maendeleo bila ubaguzi nchini. Pia anaamini kuwa jamii inaweza kuingia matatizoni kama itachanganya mambo mawili kwa pamoja. Hivyo anashauri watu kuheshimu na kushikilia jambo moja ndipo utafanikiwa.

MTAZAMO:Mtazamo wa mwandishi ni wa kiyakinifu kwani anayaona mambo kiyakinifu, anaona kuwa kufanya kazi kwa bidii, kuheshimu kazi, kuwa na msimamo katika maisha ni suluhisho na chachuya maendeleo.

MSIMAMO:Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi kwani anapingana na mambo mabaya na kuyaweka wazi mfano uvivu, uzembe, kuchanganya kazi na mapenzi. Pia anapinga suala la ushirikina na imani potofu. Anaona kuwa ipo haja jamii kuwa na msimamo wa kimapinduzi kwa kupinga mambo yanayodidimiza maendeleo.

UJUMBE

  • Si vyema kuchanganya kazi na mapenzi kwani husababisha kazi kuharibika.
  • Ulevi huleta madhara na matatizo ndani ya jamii hivyo si budi jamii kupinga ulevi.
  • Elimu ni muhimu sana kwa jamii yoyote.
  • Kufanya kazi kwa bidii ni msingi wa maendeleo.
  • Wanawake wanapaswa kupewa nafasi ya kufanya maamuzi katika jamii.
  • Serikali na jamii vinapaswa kugawanya maendeleo sehemu zote za vijijini na mijini ili kuwa na maendeleo yasiyopishana sana ili kufifisha umaskini uliokithiri.
  • Wanaume wanaowavuruga wasichana kwa tamaa zao ipo siku watafikia tamati na kupata machungu ya ubaya wao.
  • Msimamo katika maamuzi ya mambo na kufikiri kabla ya kutenda ni jambo la msingi.
  • Nidhamu ya woga haijengi.

www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256