UHAKIKI WA FANI KATIKA FASIHI ANDISHI
UHAKIKI WA FANI KATIKA RIWAYA YA TAKADINI
MWANDISHI: BEN J. HANSON
WACHAPISHAJI: MATHEWS BOOKSTORE AND STATIONARIES
MWAKA: 2004
JINA LA KITABU
Jina la kitabu TAKADINI lina maana ya “Sisi tumefanya nini”. Hili ni jina ambalo Sekai alimpa mwanae mara baada ya kumzaa. Jina hili lilitokana na majonzi aliyokuwa nayo juu ya kutaka kuuawa kwa mwanae na yeye ilihali hawakuwa na hatia, ila tu kwa sababu ya mila za jamii yake zilivyotaka. Jina hili la kitabu ni sadifu kwani linasawiri vyema maudhui yaliyomo katika kitabu hiki. “Sisi tumefanya nini?’ ni swali ambalo linatokana na ukosefu wa haki ya kuishi, kubaguliwa kutopendwa, na hata kutengwa kwa watu wenye matatizo katika jamii. Swali hili linawaelekea wanajamii ambao bado wanashikilia mila potofu zinazowakandamiza na kuwanyanyasa watu wenye matatizo mfano, ulemavu wa ngozi, wagonjwa nk. Jina hili pia ni sadifu kwa maisha ya jamii yetu ya watanzania kwani watu bado wanashikilia mila potofu ambazo si nzuri. Mwandishi ametumia jina hili makusudi ili kutaka kuionesha jamii hali halisi ya vilio vya albino, wasichana wadogo wanaolazimishwa kuolewa nk. Kuwa huu sasa ni muda mwafaka wa jamii kuyaacha na kutupilia mbali mambo hayo.
MUUNDO
Muundo alioutumia mwandishi wa riwaya hii ni muundo wa msago au kwa jina lingine muundo wa moja kwa moja. Ameyapanga matukio katika mtiririko sahili kwani ameanza kutuonesha toka mwanzo mpaka mwisho wa maisha ya kijana Takadini “Msope”.Toka kutungwa kwa mimba yake, kuzaliwa kwake na kuishi kwake, matatizo na changamoto zinazomkumba na jinsi anavyokabiliana nazo na hatma ya maisha yake.
Mgawanyo wa visa na mtukio umepangwa katika sura ambapo visa vimejengwa kwa ufundi na kuvifanya vijengane na kukamilishana kuelekea kilele cha masimulizi. Matukio haya yamewekwa katika sura kumi na tatu.
- Sura ya Kwanza:Sura hii inaanza kutuelezea kuhusu mwanamke Sekai anavotunga mimba, pia tunaelezwa kuhusu mtazamo mbaya wa wake wenzie juu ya mimba hiyo baada ya Sekai kukaa kwa muda mrefu bila ya kujaliwa mtoto.
- Sura ya Pili:Hapa tunasimuliwa jinsi Sekai anavyofanikiwa kujifungua salama. Lakini kwa bahati mbaya kwa kawaida ya jamii yao anajifungua mtoto Zeruzeru ambaye kwa mila zao mtoto huyo ni laana. Hivyo alipaswa kutupwa mara moja ama kuuawa. Hakuna ambaye alikuwa tayari kumpokea mtoto yule kwani si baba yake wala jamii yake ila mama yake pekee.
- Sura ya Tatu:Jamii bado haipo tayari kumpokea mtoto Sope, wanawake wenza wa Sekai wanasubiri kwa hamu kuona tukio la kutupwa kwa Takadini litakavokuwa, kwani ndio jinsi mila na taratibu za mababu zilivyotaka. Kutokana na hali hii ndipo Sekai anapata wazo la kutoroka. Anaamua kuondoka kwenda mbali ili kukinusuru kichanga kisicho na hatia kwani alisubiri kwa hamu na uchu wa muda mrefu kupata mtoto.
- Sura ya Nne:Sekai anafanikiwa kutoroka na mwanae Takadini ili kumuepusha na kifo, jamii na Mtemi wanapata habari ya kutoroka kwake. Upelelezi unafanyika lakini juhudi hazikuzaa matunda kumpata Sekai na mwanae mchanga waliotakiwa kuuawa. Sekai anasafiri mbali na kufikia kijiji kingine na kupokelewa na mzee Chivero.
- Sura ya Tano:Sekai anapokelewa katika kijiji cha mzee Chivero, jamii na wazee wanashitushwa sana na ujio huo lakini wanalazimika kumpokea tu baada ya malumbano ya muda mrefu. Kwani mila ziliwataka kutowatelekeza wageni katika kijiji chao, na hiyo ndiyo inakuwa mwanzo wa matumaini ya Sekai kuhusu kuishi kwa mwanae ambaye alionekana kuwa ni laana ya mababu na hakupaswa kuishi.
- Sura ya sita:Baada ya Sekai kupokelewa katika kijiji cha mtemi Masasa, habari za ujio wake zinaenea kwa wanakijiji wote na wanaonekana kushtushwa sana, si hivo tu bali pia wanajiapiza katu kutomsogelea Sope kwani waliamini amelaaniwa. Lakini kwa juhudi za mzee Chivero baba mpya mlezi wa Takadini Sekai anapata rafiki. Tendai mke wa mtemi Masasa. Anajengewa kibanda cha kuishi yeye na mwanae na maisha yanaanza.
- Sura ya saba:Sekai anaanza kujishughulisha na shughuli za kawaida kama mama na mwanamke, analima bustani na kufanya kazi ndogo za nyumbani. Siku moja katika safari ya kurudi nyumbani kwa bahati mbaya wanavamiwa na nyuki na kujeruhiwa vibaya yeye na mwanae, anaamua kumtupia mwanae kichakani ili kumuokoa na yeye kujitumbukiza mtoni. Wote wawili wanafanikiwa kutibiwa na kupona majeraha.
- Sura ya nane:Taratibu Takadini anaanza kukua lakini anagundulika kuwa hawezi kutembea vyema kwa mguu mmoja, hii ilitokana na kuvunjika Mguu baada ya kurushwa kichakani na mamaye kama juhudi za kumwokoa. Hali hii inamhuzunisha zaidi Sekai na Chivero kwani walimpenda sana. Hapa ndipo mapenzi ya Chivero yalianza kudhihirika rasmi kwa Takadini kwani alijenga urafiki naye na kumpenda kama mwanae. Alimfundisha utabibu wa dawa za kienyeji na mambo mengine mengi. Pia tunaona watoto jinsi walivyombagua Takadini kutokana na hali yake, kwani waliambiwa na wazazi wao wasicheze naye amelaaniwa hivo hawakuthubutu.
- Sura ya tisa:Katika sura hii, Mzee Masasi anafariki dunia na kumuacha mzee Chivero katika majonzi makuu. Hali ya mzee Chivero nayo inaanza kuzorota kwa uzee. Anampa Takadini usia mbalimbali na kumfunza. Pia tunaelezwa juu ya fikra mpya za Takadini za kupiga “mbira” kifaa cha muziki cha kijadi, hii baada ya kuvutiwa na sanaa hiyo aliposhiriki sherehe za mavuno za mwaka. Jamii bado ilimtenga Takadini na kumbagua, walimwona si binadamu bali mzuka tu! Na kwa bahati mbaya mzee Chivero naye aliaga dunia na kuacha simanzi kuu kwa Sekai na Takadini mbao alikuwa ni tegemeo na faraja kwao.
- Sura ya kumi:Baada ya kifo cha mzee Chivero, Takadini anapata mwalimu maarufu mpiga mbira mzee Kutukwa, anamfundisha kupiga mbira, Takadini anaonesha juhudi kuu na kufanikiwa. Pia anmsaidia kifaa cha kumsaidia kutembea kutokana na mguu wake mbovu, hii inakuwa ni faraja kubwa kwa Takadini na mamaye.
- Sura ya kumi na moja:Hapa tunaelezwa juu ya kijana Nhamo adui mkuu wa Takadini kwani hakumpenda na alimdhihaki na kumdhalilisha mara kwa mara. Kijana huyu anaonekana kuwa ni shujaa katika jamii yake kwa kitendo cha kumuua simba mla mifugo. Hiyo inamletea sifa kubwa na majivuno mengi hivo wasichana wengi kumtamani awaoe, hali ni tofauti kwa Shingai ambaye anaonesha hisia za mapenzi kwa Takadini pamoja na hali yake ya “Usope”. Chemchemi za mapenzi ya Takadini kwa Sekai zinaanza kumea jambo ambalo linamkera sana Nhamo na kuzidisha chuki kwa Takadini kwani pia alitamani kuwa na Shengai binti mrembo. Jamii inafanya kikao kujadili suala la Shengai kumpenda Takadini na wanalipinga vikali suala hilo.
- Sura ya kumi na mbili:Nhamo anakata shauri na kwenda kumposa Shengai, wazazi wa pande zote mbili wanaliunga suala hilo mkono asilimia zote. Kwani hilo lingewanusuru aibu ya mwanao kuolewa na Sope, kwani walijua fika Shingai alimpenda Takadini na hakumtaka Nhamo. Nhamo anamuonya vikali Takadini kuwa asiendelee na lolote kwa Shengai. Pia hapa zinafanyika sherehe ya kijadi ya kumkaribisha hayati mzee Chivero tena nyumbani.
- Sura ya kumi na Tatu:Wakati wa sherehe ya mavuno, binti Shengai anashindwa kuvumilia na kuamua kumfuata Takadini kibandani kwake. Anaamua kuvunja mila za kwao kwani alimpenda kwa dhati Takadini, pamoja na dharau, kejeli, kubaguliwa, ulemavu wake na kuonekana kuwa ni mtu aliyelaaniwa. Wazazi wake wanamtenga na kutomtambua kama ni mtoto wao tena. Suala hilo linatikisa jamii ya watu wa kijiji kile na hata kutaka kuwafukuza Sekai na mwanae lakini wanaokolewa na maamuzi ya busara ya wazee kwa kuwacha Shengai na mpenziwe Takadini waishi hali wakisubiri matokeo! Kuwa je mtoto atazaliwa sope? Na kuongeza ukoo wa masope na kijiji chao kuwa cha masope? Hapa ndio inapojulikana hatma ya Takadini na mkewe kwani anapata ujauzito na kufanikiwa kujifungua mtoto salama asiye Sope. Ilikuwa furaha kuu kwa mama na mtoto na wote pia. Wanaamua kurudi kijijini kwao walikotoroka ili kwenda kuwadhihirishia kuwa hata sope anaweza kuishi hapaswi kubaguliwa na kutengwa
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo kadha wa kadha ili kuipamba kazi yake na kuifanya ivutie wasomaji; mfano matumizi ya nafsi mbalimbali, matumizi ya nyimbo nk.
Matumizi ya nafsi
Kwa kiasi kikubwa yametawala matumizi ya nafsi ya tatu umoja na wingi katika sura zote.Mfano.uk. 30. “ aliingia ndani na kuanza kazi.”Piauk.3 “ Sekai alikoka moto nje ya kibanda, akaketi na kuzungumza na Pindai”.
Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia
Mfano uk 29 - 30. Mazungumzo kati ya Chivero na Sekai:“je umelala salama?“je umelala salama?Sijambo mwanangu, sijui wewe?Sijambo Sekuru,Na mwanao je?Naye hajambo.”
Matumizi ya nafsi ya kwanza. Mfano uk. 82 na 83
“lakini ghafla nilipata nguvu mpya”;“nilikuwa na nguvu kama kijana….”
Pia mwandishi ametumia nyimbo katika baadhi ya sura ili kuwaburudisha na kuliwaza wasomaji. Mfano uk. 2 wimbo aliouimba mke mwenza wa Sekai Rumbdzai.
“Mashamba yetu yamelimwa mbegu nazo zimepandwa zimechipua na kumea, sisi watatu tumepanda mavuno yetu; mheshimiwa wetu amemiliki mavuno kwa mikono yake halisi kutoka mashamba yetu yote lakini ni kipi alichoambulia kutoka ardhi ile isiyomea kitu?”pia ametumia wimbo uk. 34, 57, 85.
Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi pia ni mtindo mwingine wa usimulizi alioutumia mwandishi.Mfano uk 82 Kutukwa alisimulia vijana hadithi enzi ya ujana wake na jinsi alivopambana na maadui vitani.
Matumizi ya Lugha
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi inayoeleweka kwa wasomaji wake. Ametumia pia lugha nyinginezo kama vile lugha za kikabila.Maneno kama vile“Amai”,lenye maana ya mama, “Sope” lenye maana yazeruzeru, “shumba”- simba, “mbira” – chombo cha asili cha muziki, “gudza” – blanketi lililotengenezwa kwa nyuzi za magome ya miti.nk.Hivyo mwandishi ametumia lugha hii ili kuwaleta wasomaji kwenye mazingira halisi ya kiutamaduni ya jamii ile.
Matumizi ya tamathali za Semi
- Tashibiha:Mfano uk. 6 “ muda huenda polepole mithili ya mwendo wa kakakuona Uk.15 “ habari njema huchechemea kwa mguu mmoja lakina mbaya hukimbia kama Sungura”Uk.16 “….. alibaki kama kinyago cha mpingo”.Uk.28 “ sio kufurika kama Chura”Uk.33 “aligeuza shingo yake sawa na Mbuni”Uk.42 “ nywele kama vinyweleo vya mahindi yaliyokaribia kukomaa”Uk.82 “muziki ulikuwa kama chemchemi ya maji mwilini mwake”
- Tashihisi:Mfano uk. 5 “ndege mbalimbali wakiimba kuikaribisha siku mpya” Uk. 7 “vivuli vya jioni viliongezeka urefu” Uk. 18 “maneno yananila mifupa yangu”Uk 25 “kifo kilinukia”
- Tafsida:Mfano, uk. 83 “sehemu zake za siri”
- Sitiari:Mfano, uk. 88 “Tapfumaneyi aligeuka mbogo” Uk.97“mwana Mbwa hakuiba mfupa”, Tawanda mfupa ulikwenda wenyewe kuchezanaye.” Hapa mfupa umefananishwa na Shingai na Takadini ndio mwana mbwa
Matumizi ya Semi
- Methali:Uk. 45 “ kipofu huwa hachagui shimo la kutegea wanyama”uk.33 “ moyo mwema utakufanya uuwawe”
- Misemo:Mfano.Uk. 12 “kufikiri katika siri ni sawa na safari ya mbwa”Uk. 100 “kanga hawezi kutua juu ya bua la mtama”Uk.101 “kibuyu kikubwa hakikosi mbegu ndani”Uk. 125 “fuvu la nyani limekuwa kijiko kwa mlo wa mahindi”
- Nahau:uk. 27 “ penzi langu kwake halikufua dafu”Uk. 88 “kutiana moyo wa ari”
Matumizi ya mbinu nyinginezo za kisanaa
- Nidaa:Mfano,Uk.4 “Ha!” , “Ha! Atimuliwe tena? Mchawi?” Uk.16 “Mai, Wee!” Uk.39. “Ha! Iwe! Ha!”
- Mdokezo:MfanoUk.3 “ndiyo Pindai, ninaogopa……….” Uk.42 “mtu mzima kama watu wenine ameamua………”
- Takriri:Mfano,uk 57 “ mwanangu, mwanangu, mwanangu, wamekufanya nini?”
Wahusika
Sekai
- Ni mke wa Makwati wa kwanza.
- Ni mwanamke jasiri.
- Anapinga mila potofu na mbaya za jamii yake.
- Ni mvumilivu.
- Ni mchapakazi mzuri.
- Anajifungua mtoto zeruzeru ambaye ni laana kwa jamii yake.
- Ni mtiifu na mwenye adabu.
- Ana huruma na mnyenyekevu.
- Ana mapenzi ya dhati.
- Anafaaa kuigwa na jamii.
Takadini
- Ni mtoto anayezaliwa na ulemavu wa ngozi( albino)
- Anasadikika kuwa ni laana kwa jamii yake hivyo kupaswa kuuawa au kutupwa mbali.
- Anaokolewa na mama yake kwa kutoroshewa katika kijiji kingine.
- Anapokua anakua kijana jasiri.
- Hapendwi na jamii.
- Anabaguliwa na jamii, hana rafiki.
- Ni mvumilivu na msikivu mwenye heshima.
- Alimpenda Chivero sana.
- Alikuwa mpiga mbira (chombo cha muziki cha kijadi) maarufu.
- Alimuoa Shingai na kupata mtoto asiye Sope.
Makwati
- Mume wa Sekai.
- Ameoa ndoa ya mitara ana wake wanne.
- Anashikilia mila na desturi potofu.
- Hana mapenzi ya dhati kwa mwanae.
- Hafai kuigwa na jamii.
Dadirai na Rumbidzai
- Wake wengine wa mzee Makwati.
- Wana wivu.
- Hawampendi Sekai.
- Wana roho mbaya kwani wanamwombea Sekai mabaya.
- Ni katili kwani wanashinikiza Sekai na mwanae wauawe bila huruma.
- Wasengenyaji.
- Hawafai kuigwa na jamiii.
Pindai
- Mke wa pili wa Makwati.
- Ana upendo wa dhati kwa Sekai.
- Ni mkweli.
- Hana wivu.
- Ni mshauri mzuri.
- Anafaa kuigwa na jamii.
Chivero
- Ni mzee wa kijiji cha mzee Masasa.
- Anawapokea Sekai na mwanae baada ya kutoroka kwao kwa ukarimu mkubwa.
- Ni mwenye roho nzuri.
- Ana huruma sana.
- Ni mganga wa tiba za asili.
- Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini na Sekai.
- Anamrithisha Takadini uganga.
- Ana busara na hekima.
- Ni mshauri mkuu wa Mtemi Masasa.
- Anafaa kuigwa na jamii.
Mtemi Masasa
- Ana busara na hekima.
- Ana huruma.
- Anafuata mila na desturi ya jamii yake.
- Ni msikivu.
- Ni rafiki mkubwa wa Chivero.
- Ni kiongozi bora.
- Anafaa kuigwa na jamii
Nhamo
- Ni kijana katika kijiji cha mtemi Masasa.
- Ana majivuno na jeuri.
- Hampendi Takadini kwani alimbagua kumpiga na hata kumdhalilisha.
- Hafai kuigwa n ajamii.
Tendai
- Mke mdogo wa mwisho wa mtemi Masasa.
- Aliolewa bila kupenda, hakumpenda mtemi Masasa kwani alimzidi umri.
- Alikuwa rafiki mzuri wa Sekai.
- Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini.
- Ana bidii na mvumilivu.
- Anafaa kuigwa na jamii
Nhariswa na mkewe
- Ni wazazi wa Shingai
- Wanashikilia mila desturi potofu
- Hawakupenda kabisa kitendo cha mtoto wao kumpenda Takadini
- Walimlazimisha kuolewa na Nhamo kwani walitaka sifa na maujiko
- Walimtenga Shingai baada ya kutoroka na kuolewa na Takadini
- Si wazazi wazuri
- Hawafai kuigwa na jamii
Kutukwa
- Ni mzee katika kijiji cha mtemi Masasa
- Ni mpigaji mbira maarufu
- Alimfundisha Takadini kupiga mbira
- Alitoa mtazamo mbaya kwa wanakijiji wenzake kwa kuwaeleza sifa nzuri za Takadini
- Alimpenda Takadini. Anafaa kuigwa na jamii
Mandhari
Mandhari aliyotumia Ben J Hanson ni mandhari ya kijijini kwani maisha ya watu na mazingira yanayoelezwa ni ya kijijini, masuala kama ya kilimo, ufugaji, sherehe za mavuno, makazi ya watu kukaa katika jumuiya ya pamoja kijamaa inayoongozwa na mtemi mmoja. Mfano mtemi Masasa, yote haya ni viashiria kuwa mandhari ni ya kijini. Mandahari ambayo mwandishi ameijengea mawazo yake na kuyaibua ni sadifu na halisi. Kwani maeneo ya vijijini ndiko kulikokithiri mambo ya imani potofu na za kishirikina kama vile kuwaua watoto Sope au albino.
UHAKIKI WA MAUDHUI KATIKA KAZI ZA FASIHI ANDISHI - Maudhui katika riwaya ya Takadini
DHAMIRA
Dhamira kuu
- Suala la imani potofu na ushirikina:Wanakijiji wa kijiji cha Sekai na wanakijiji wa kijiji cha Mtemi Makwati, wana imani potofu juu ya binadamu aliye na ulemavu wa ngozi yaani albino “sope” wanaamini kuwa kuzaliwa kwa mtoto wa aina hiyo ni laana na hapaswi kabisa kuishi. Hawaamini kuwa ni binadamu wa kawaida. Mfano uk.8Ambuya Shungu anasema“mtoto ni Musope.Ni wajibu wetu kumuharibu”.Mwandishi amelionesha suala hili makusudi ili jamii iweze kupinga na kuacha mila hizi potofu mara moja! Anaiasa jamii kuwapenda, kuwajali na kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi na si hivyo tu bali pia anaona upo umuhimu wa jamii kuwapa nafasi watu wa aina hiyo kwani wanaweza kuwa na umuhimu mkubwa na mchango katika jamii.
Dhamira ndogo ndogo
- Ubaguzi kwa watu wenye ulemavu:Hii ni dhamira nyingine ambayo imejadiliwa ndani ya riwaya hii. Mwandishi anaonesha kuwa ubaguzi si mzuri kwani huwafanya watu wenye ulemavu wa ngozi wajisikie vibaya na kujiona si sehemu ya jamii wanayoishi. Tunaona jinsi Nhamoalivyombagua nakumtenga Takadini, uk. 62 “huwezi kukimbia na huwezi kupigana…..tena hata huoni vizuri. Ha! Wala hufanani hata na mmoja kati yetu, watu wanasema una laana, sitaki kuwa rafiki yako....anaendeleakumwambia“wewe ni sope, sope, sope!”kumbe tunapaswa kuwapenda na kuwajali watu wote bila ubaguzi.
- Ndoa za mitara:Wanaume wa kijiji cha Sekai wana desturi ya kuoa mke zaidi ya mmoja. Mfano Makwati alikuwa na wake wanne ambao ni Sekai, Pindai, Dadirai na Rumbdzai. Wake hawa si wote walipendana bali walijitenga na kuoneana wivu mfano Dadirai na Rumbdzai hawakumpenda kabisa Sekai walimsimanga na kumsengenya. Mfano uk.15 Dadirai alisema kwa chuki “lazima atimuliwe hapa…. arudi kwao” “Ha! Atimuliwe tena? Ni mchawi!”hivyotunaona kuwa ndoa za mitara ni tatizo katika jamii kwani huweza kusababisha migogoro na ugomvi tena huweza kusababisha hata kuambukizana magonjwa hatari hasa katika kizazi cha leo ambapo magonjwa ni mengi ya hatari.
- Mapenzi ya dhati na huruma:Mzee Chivero ni mzee aliyeonesha mapenzi ya dhati kwa Sekai na mwanae kwani aliwapokea na kuishi nao, pamoja na hali waliyokuwa nayo bila kuwabagua. Alimhurumia Takadini akampenda, kumsaidia na kumshauri vyema siku zote. Pia tunaona Sekai alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mwanae Takadini kwani aliweza kumkinga na kumuokoa asiuawe. Mfano uk.10 Sekai anasema“hapana Ambuya mtoto lazima aishi. Hapana Ambuya mtoto ni wangu na sitamwachia mtu”…… sitamwachia mtu yeyote mwanangu”.
Nafasi ya mwanamke
Mwanamke amechorwa katika nafasi mbalimbali katika riwaya hii kukamilisha ujumbe wa mwandishi kwa jamii kuhusu wanawake.
- Mwanamke amechorwa kama kiumbe jasiri: Sekai ameonekana kuwa na ujasiri wa hali ya juu kwani aliamua kupingana na mila za jamii yake na kuamua kutoroka na kitoto bila kujua alipoelekea ili tu kumuokoa mwanae. Hivo anapaswa kuigwa na jamii.
- Amechorwa kama mwanamapinduzi:Sekai na Shingai wamechorwa kama wanawake wanamapinduzi kwa kuubadilisha mtazamo wa wanajamii wenzao kuhusu baadhi ya mila potofu. Mfano Shingai aliamua kuolewa na Takadini bila kujali ulemavu wake. Hakuogopa wazazi wake wala hakuogopwa kutengwa na ndipo badae jamii ilimkubali. Pia Sekai ni mwanamapinduzi kwa kuzikataa mila potofu ya kuwaua albino, alimtunza mwanae na kumlea mapaka akakua.
- Amechorwa kama chombo cha starehe: Mwanamke katika jamii hizi alionekana kama chombo cha starehe tu kwani waliolewa wanawake wengi kwa mwanaume mmoja na lengo nikumburudisha tu na kumzalia watoto.
- Amechorwa kama kiumbe dhaifu asiyeweza kusema chochote wala haki yoyote: Wazazi wa Shingai hawakumpa kabisa Shingai uhuru wa kuchagua mwanaume aliyempenda. Walimlazimisha kuolewa na mwanaume waliyemtaka. Mfano uk.118 Shingai anasema“huyu ndiye mtu ninayeteka anioe. Hakuna aliyeniuliza kama nampenda Nhamo. Wewe na baba mlikuwa na hamu ya kuniozesha katika familia ya Manyamombe hata matakwa yangu hayakusikilizwa. Sasa nimechagua”.
- Amechorwa kama mtu mwenye mapenzi ya dhati: Sekai alikuwa na mapenzi ya dhati kwa mwanae Takadini. Pia Shingai alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Takadini na hata kuamua kuolewa naye.
- Amechorwa kama mtu mvumilivu: Mfano mzuri ni Sekai alivumilia kwa muda mrefu bila kukata tamaa kukosa uzazi, masimango ya wake wenzake na hatimaye alipata mtoto. Pia alivumilia kumlea Takadini wala hakuthubutu kumtenga hata mara moja bali alimvumilia mpaka alipokua.
MIGOGORO
- Mgogoro kati ya Sekai na Rumbdzai na Dadirai: Sababu ya mgogoro huu ni kwamba, wanawake hawa wawili hawakumpenda kabisa Sekai na walimuonea wivu kwa kitendo cha kupendwa sana mumewe. Walimsimanga na kumsengenya muda mwingi na hasa kutokana na tatizo la Sekai la kukosa mtoto kwa muda mrefu. Walimwita mchawi.
- Mgogoro kati ya Sekai na Makwati mumewe:Sababu ya mgogoro huu ni Sekai kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi ambapo katika jamii yao ni laana. Mumewe hakumwamini alimgombeza na kumtishia kumuua akidhani Sekai ni mchawi. Sekai na mwanae anaamua kutoroka ili kuondokana adha ile.
- Mgogoro kati ya Nhamo na Takadini:Sababuni kuwa Nhamo alimpiga na kumdhalilisha Takadini mara kwa mara mbele ya vijana wengine kwakuwa ni Sope. Alimkejeli na kumdhihaki mfanouk.62 “wewe ni sope umelaaniwa”Nhamo alimwambia Takadini. Pia sababu nyingine ni kutokana na Shingai mchumba wa Nhamo kuwa na mapenzi ya dhati kwa Takadini na kumkataa yeye. Takadini alivumilia na kutolipiza kisasi na baadae alifanikiwa kumuoa Shingai na kuzaa naye mtoto wa kiume.
- Mgogoro kati ya Nhariswa na mkewe:Nhariswa alimpiga na kumgombeza mkewe kwa kitendo cha kutomfuatilia binti yao na kumwacha aanzishe uhusiano na kijana aliyeaminiwa kuwa amelaaniwa.
- Mgogoro kati ya Shingai na mama yake:Mgogoro huu ulitokana na Shingai kuamua kuolewa na Takadini jambo ambalo hawakulitaka kabisa kutokana na hali ya Takadini. Mama yake anaamua kumkana Shingai hadharani kuwa si mtoto wake tena.
- Mgogoro kati ya Nhamo na Tapfumaneyi.Vijana hawa walipigana ili kumtafuta mshindi na shujaa bingwa wa mapigano. Vijana walipigana sawia na walitoka sawia.
- Mgogoro wa nafsi kwa Sekai.Sekai alisumbuliwa na mgogoro wa nafsi kwa muda mrefu juu ya mwanae ambaye alitengwa na kubezwa kutokana na hali yake. Alilia na kuhuzunika mara nyingi akiilaumu Miungu yao kuwa “Sisi tumefanya nini” hatimaye mgogoro wake uliisha baada ya Takadini kujenga heshima yake upya mara alipomuoa Shingai na kubahatika kupata mtoto wa kiume tena asiye Sope. Na hapo ndipo ilirejea faraja na furaha mpya.
- Mgogoro wa nafsi kwa Takadini:Huu ulisababishwa na hali yake ya ulemavu wa ngozi iliyopelekea yeye kutengwa na kubaguliwa na wanajamii na mara kadhaa kutishiwa kuuawa. Hali hii ilimtesa ka muda mrefu kwani alitengwa na hakuwa na rafiki toka utotoni hadi ujana wake. Lakini mgogoro huu unaisha baada ya kupata mke aliyempenda kwa dhati na kumzalia mtoto wa kiume. Hii inampa faraja na kujiona mwanaume halisi na kuithibitishia jamii kuwa alikuwa sawa na wanajamii wengine.
- FALSAFA:Falsafa ya mwandishi Ben Hanson, anaamini kwamba watu wenye ulemavu wa ngozi wana haki ya kuishi kama binadamu wengine kwani wana akili, utashi, uwezo wa kufanya kazi kama binadamu wengine na ni sawa na binadamu wengine.Wao kuwa na ulemavu wa ngozi si kigezo cha kuwaua na kuwabagua. Hana imani juu ya mila potofu kwani katika masimulizi yake anaonesha kushindwa kwa mila potofu kama vile kuamini kuwa albino ni viumbe waliolaaniwa na hawatakiwi kuishi. Anaamini kuwa wakipewa nafasi ya kuishi na kushirikishwa katika shughuli za kijamii, kupewa elimu na mahitaji yote wanaweza kuwa ni watu muhimu sana katika jamii na hili analidhihirisha kupitia Takadini.
- MTAZAMO:Mtazamo wa mwandishi ni wa kiyakinifu. Tunaweza kusema hivyo kwa sababu ya mambo ambayo mwandishi anayamulika katika kazi yake. Mambo kama vile kuzaliwa kwa albino haoni kuwa ni laana bali ni kawaida tukutokana na masuala tu ya kimaumbile. Haoni kuwa kuna haja ya kuwatenga au kuwabagua albino kwakuwa ni binadamu sawa na sisi.
- MSIMAMO:Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani analenga kuyapindua mawazo na imani potofu za baadhi ya jamii kuwa albino hafai kuishi. Anakemea suala la kuwatenga na kuwabagua albino, anakemea pia suala la ndoa za lazima na mila zingine potofu. Anataka jamii ibadilike na kuendana na wakati kuwapa usawa watu walio na ulemavu wa ngozi, anatetea haki za wanawake anataka wapewe nafasi sawa katika jamii wasibaguliwe. Hivyo msimamo wa mwandishi ni mzuri na unatakiwa kufanyiwa kazi katika jamii.
FALSAFA
Kupitia Takadini, Mwandishi amwonyesha falsafa zifatazo
- Mwandishi anaamini hata mtu mwenye ulemavu wowote wanaweza kupata nafasi katika jamii kwa kumtumia muhusika mkuu takadini
- Mwandishi anaanimi wapo wanawake ambapao bado hawana maamuzi kuhusu ndoa zao,kwa sababu wanachaguliwa wachumba/ wanaumw kwa mtumia
- Mwanadishi anaamini kuwa mila mbaya za kiafrika zinabidi ziondolewe.
- Mwandishi anaamini elimu ndio chanzo kizuri cha waelewano katika jamiii,kwa sababu wapo watu wanafanya wafanya mambo kwa sababu ya kukosa elimu.
MTAZAMO:Mtazamo wa mwandishi ni wa kiyakinifu kwa kutumia kitabu hiki tumepata mitazamo mbalimbali kama ifatavyo,
- Mwandishi anaona kuwa hata mtu mwenye ulemavu wowoteanaweza kupata nafsi katika jamii,kwa kumtummia muhusika mkuu takadini
- Mwandishi anaona kuwa mila mbaya za kiafrika zinabidi ziondolewe
- Mwandishi anaona elimu kuwa ndio chanzo kizuri cha maelewano katika jamii husukia
MSIMAMO:Msimamo wa mwandishi ni wa kimapinduzi kwani analenga kuyapindua mawazo na imani potofu za baadhi ya jamii kuwa albino hafai kuishi. Anakemea suala la kuwatenga na kuwabagua albino, anakemea pia suala la ndoa za lazima na mila zingine potofu. Anataka jamii ibadilike na kuendana na wakati kuwapa usawa watu walio na ulemavu wa ngozi, anatetea haki za wanawake anataka wapewe nafasi sawa katika jamii wasibaguliwe. Hivyo msimamo wa mwandishi ni mzuri na unatakiwa kufanyiwa kazi katika jamii.
UJUMBE
- Albino au watu wenye ulemavu wa ngozi wanatakiwa kupewa haki ya kuishi, kupendwa kusaidiwa na kulindwa.
- Mila na desturi potofu si budi kupigwa vita katika jamii.
- Upendo na huruma ni mambo ya msingi katika jamii.
- Wanawake wapewe uhuru wa kuchagua wanaume wanaowapenda kuishi nao katika ndoa.
- Wanawake wapewe nafasi na kushirikishwa katika masuala ya jamii.
- Malezi bora ni msingi wa jamii na taifa kwa ujumla