Sura Ya 01 :Ukoloni Katika Jamii Za Kitanzania
| Utangulizi Kipindi ukoloni unaingia, jamii nyingi za Kitanzania zilikuwa zimepiga hatua katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Katika sura hii, utajifunza kuhusu chimbuko, ukuaji. mifumo na mchango wa ukoloni katika uhusiano wa Tanzania na mataifa yaliyoitawala. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuthamini maendelea ya jamii za Kitanzania katika kipindi cha ukoloni. Pia. utaweza kushiriki nyema katika juhudi za kuleta maendeleo ya Tanzania |
| Fikiri Hali ya jamii ya kitanzania wakati ukoloni unaingia. |
Chimbuko na ukuaji wa ukoloni
Ukoloni ni hali ya nchi moja huitawala nchi nyingine katika nyanja zote za kiuchumi. kisiasa na kiutamaduni. Katika muktadha huu. uchumi. siasa na utamaduni wa nchi zinazotawaliwa hutumiwa kwa malengo ya wakoloni. Ukoloni ulitokana na kustawi kwa mfumo wa ubepari, ambao ulifikia hatua ya ubeberu huko Ulaya Magharibi. Ubeberu huu uliwalazimu wakoloni kuvuka mipaka ya nchi zao ili kutafuta rasilimali na masoko mapya ya bidhaa zao na sehemu za kuwekeza mitaji. Ukuaji wa ubepari katika robo ya mwisho ya karne ya 19 uliambatana na mapinduzi na maendeleo ya viwanda katika nchi za Ulaya Magharibi. Maendeleo hayo ya viwanda yalisababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya malighafi hasa za kilimo na madini kwa ajili ya uzalishaji viwandani. Katika kipindi hicho, malighali kutoka makoloni mengine kama vile Australia. Kanada na Bara la Asia hasa India ya Uingereza (British India) hazikutosheleza mahitaji ya viwanda. Baada ya nchi za Ulaya Magharibi kutuma wapelelezi miaka ya 1850 hadi 1870 waligundua kuwa Bara la Afrika lina uwezo wa kuzalisha malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda vya Ulaya Magharibi. Mataifa kama Uingereza, Ufarasa. Ujerumani. Ubelgiji na Ureno yalivutiwa na rasilimali hasa ardhi yenye rutuba, misitu, mito, wanyama pori na madini barani Afrika.
Wakati huo huo, mataifa haya yalihitaji masoko mapya kwa bidhaa zilizozalishwa na viwanda vyao na hivyo makoloni yalionekana kama masoko mapya ya bidhaa za viwandani. Pia, mataifa haya yalihitaji maeneo ya kuwekeza mitaji yao ili kupata faida kubwa. Hivyo, Bara la Afrika lilionekana kuwa suluhisho kwa uwekezaji huo wa kibiashara. Kulikuwa pia na ushindani wa kisiasa na kijeshi kati ya mataifa ya Ulaya Magharibi kutawala maeneo makubwa. Lengo lilikuwa ni kudhihirisha nguvu zao za kiuchumi na kijeshi na hasa kutawala sehemu muhimu za kimkakati. Sehemu hizo ni kama vile njia za bahari za Atlantiki na Mediterania kupitia Bahari ya Shamu hadi Bahari ya Hindi na mabonde muhimu kama Kongo. Naili, Niger na Zambezi.
Vilevile, kulikuwa na matamanio makubwa ya kueneza dini ya Kikristo, kwani wamisionari waliona ni wajibu wao kueneza maadili ya Kikristo katika maeneo mbalimbali, hasa barani Afrika. Wamisionari wa kwanza wa madhehebu ya Kikristo katika jamii za Kitanzania walikuwa Ludwig Krapf na Johan Rebman. Katika kupeleleza jamii za Kitanzania, wamisionari hawa walijifunza mila. desturi, maadili na mazingira ya Kitanzania. Walijifunza pia fikra za wananchi na viongozi wa jadi, ili kujua namna ya kuzitawala jamii hizo.
Ukoloni ulishamiri barani Afrika katika karne za 19 na 20. Wakoloni walitumia mbinu mbalimbali kuanzisha na kuimarisha tawala zao. Mbinu hizo ni pamoja na mikataba ya kilaghai, kutumia viongozi wa jadi ili angalau kupata ushawishi na hatimaye kuzitawala jamii hizo. Moja ya mikataba ya kilaghai iliyosainiwa ni We wa kati ya Chifu Mangungo wa Usagara na Karl Peters, mwakilishi wa Wajerumani mwaka 1885. Mkataba huo uliruhusu matumizi ya ardhi ya Usagara na uliweka msingi wa kukua na kuenea kwa ukoloni wa Kijerumani katika maeneo yaliyoitwa Afrika Mashariki ya Kijerumani. .
Mikataha iliyosainiwa kati ya viongozi wa jadi na mawakala wa wakoloni ilikuwa na masharti magumu na iliwanyima wenyeji haki ya kuihoji kabla ya kuisaini. Wakati mwingine ukoloni ulikuwa na kuenea kwa kutumia nguvu za kijeshi. Maeneo ambayo wenyeji walipinga uvamizi walishindwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ubora wa silaha za wakoloni ukilinganisha na silaha za jadi zilizotumiwa na jamii za Kitanzania. Njia hii ya matumizi ya nguvu za kivita ndiyo iliyotumiwa zaidi kwani jamii nyingi za Kitanzania hazikuwa tayari kuupoteza uhuru wao kirahisi.
Pia, wakoloni walitumia mbinu ya kuungana na baadhi ya jamii za Kitanzania dhidi ya jamii nyingine. Hii ilitokea katika maeneo yaliyokuwa na uhasama kati ya jamii za Kitanzania. Kwa mfano, Wajerumani waliungana na Chifu Merere wa Wasangu na baadhi ya viongozi wa Wabena kuwapiga Wahehe waliokuwa chini ya utawala wa Mtwa Mkwawa. Vilevile, Wajerumani waliungana na Mangi Mandara wa Moshi kumpiga Mangi Sina wa Kibosho. Mara nyingi. wakoloni waliungana na jamii dhaifu
Waingereza walitawala Tanganyika kuanzia mwaka 1919 hadi 1961. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Tanganyika iliwekwa chini ya udhamini wa Jumuiya ya Mataifa (League of Nations) na baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, chini ya Umoja wa Mataifa (United Nations Organisation). Hata hivyo, taasisi hizo ziliipa Uingereza mamlaka ya kuitawala Tanganyika na kuiandaa kujitawala yenyewe. Hivyo, kuanzia mwaka 1919, Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa Waingereza, ambapo Sir Horace Byatt alikuwa Gavana wa kwanza. Kielelezo 1.1 kinaonesha picha ya Gavana Sir Horace Byatt.
|
Kielelezo 1.1: Gavana Sr Horace Byatt. |
Kuanzia mwaka 1919 hadi 1925, Waingereza waliendeleza muundo wa utawala waliourithi kutoka kwa Wajerumani. Hata hivyo, kuanzia mwaka 1926, chini ya uongozi wa Gavana Sir Donald Cameron, Waingereza walibadilisha mfumo huo na kuanzisha utawala wa kiuwakala. Katika mfumo huu mpya, walitumia mamlaka za jadi kutekeleza sera za kikoloni. Tofauti na utawala wa Wajerumani, mfumo huu haukuwa na ukatili mkubwa. Mifumo na utawala wa Waarabu, Wajerumani na Waingereza imefafanuliwa kwa kina katika sehemu zinazofuata.
| Zoezi la 1.1 1. Kwa nini Waingereza walibadilisha mfumo wa utawala kutoka utawala wa moja kwa moja hadi mfumo wa uwakala? 2. Eleza jinsi mifumo ya utawala wa Waarabu, Wajerumani na Waingereza ilivyoyaathiri maendeleo ya jamii za Kitanzania. 3.Tofautisha mifumo ya utawala wa Waarabu, Wajerumani na Waingereza katika Tanzania. |
Utawala wa Waarabu
Waarabu kutoka Oman walifika Zanzibar na Tanganyika mwishoni mwa karne ya 18. Kwa madhumuni ya kutawala, walijenga makazi yao katika maeneo ya Unguja, Pemba na pwani ya Tanganyika, hususani katika miji ya Kilwa, Tanga na Bagamoyo, kama inavyoonyeshwa kwenye Kielelezo 1.2. ili kuzipiga jamii zenye nguvu na hivyo kujipenyeza na hatimaye kuimarisha tawala zao.
Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 — 1885, pamoja na mambo mengine, ulilenga kuligawanya bara la Afrika miongoni mwa mataifa ya Ulaya bila kujali mipaka ya asili ya Waafrika na hivyo kuharakisha ukuaji wa tawala za kikoloni. Hii ilileta madhara makubwa kwa jamii za Kiafrika zilizokuwa zimejengwa katika misingi ya utu, umoja, uzalendo na amani. Kukua na kuenea kwa ukoloni kulianza kusababisha kuporomoka kwa maadili ya jamii nyingi za Kitanzania. Tamaduni nyingi za asili zilianza kufifia kutokana na athari za ukoloni. Kwa mfano, lugha, mila na desturi za asili zilianza kupotea au kubadilika kutokana na kuingiliwa, kudumazwa na kubezwa na tamaduni za kikoloni.
| Kazi ya kufanya 1.1 Umeteuliwa kuwa miongoni mwa wanafunzi watakaoshiriki mdahalo wenye mada isemayo "ukoloni ulikuwa na manufaa katika maadili ya jamii za Kitanzania." Soma vitabu na matini mbalimbali kisha andaa dondoo utakazozitumia wakati wa mdahalo huo. |
Mifumo ya kikoloni ya mataifa yaliyozitawala jamii za Kitanzania
Mifumo ya utawala ya Waarabu, Wajerumani na Waingereza katika jamii za Kitanzania ilitofautiana kwa kiasi kikubwa, ingawa lengo kuu la mifumo hiyo lilikuwa kunyonya na kupora rasilimali watu na rasilimali asilia za jamii za Kitanzania. Waarabu wa mwanzo waliofika pwani ya Afrika Mashariki kabla ya kame ya 18, hawakuja kama wakoloni bali kama wafanyabiashara. Hata hivyo, Waarabu kupitia utawala wa Sultani wa Zanzibar kuanzia karne ya 18, walijikita zaidi katika biashara, hususani biashara ya pembe za ndovu, watumwa, karafuu na nazi. Mfumo huu wa utawala ulitengeneza tabaka la juu katika jamii, yaani tabaka la Waarabu na Wahindi waliojihusisha na kilimo cha mashamba makubwa na biashara, huku Waafrika wengi wakibaki katika hali duni ya kiuchumi, kisiasa na kijamiii
Wajerumani walitawala jamii za Kitanzania kuanzia mwaka 1885 hadi 1919 baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Katika utawala wao, Wajerumani walitumia mfumo wa utawala wa moja kwa moja, uliokuwa na matumizi ya nguvu za kijeshi na sheria kali dhidi ya watawaliwa. Jamii nyingi za Kitanzania ziliporwa ardhi na kulazimishwa kufanya kazi katika mashamba na miradi ya kikoloni kama vile ujenzi wa reli na miundombinu mingine kwa ujira mdogo. Wajerumani walitawala nyanja zote za maisha ya Waafrika huku wakiendeleza miundombinu kwa ajili ya masilahi yao.
|
Kielelezo 1.2: Maeneo ambayo Waarabu waliweka ngome za utawala wao |
Watawala wa Kiarabu waliotawala pwani ya Afrika Mashariki walifika nchini katika vipindi mbalimbali. Wengi wao walivutiwa na utajiri wa rasilimali uliokuwapo katika eneo hili. Utajiri huo ulijulikana kutokana na uhusiano wa kibiashara wa muda mrefu kati ya pwani ya Afrika Mashariki na nchi za bara la Asia kama vile Omani, Uhindi, Uchina na Uajemi.
Mtawala wa kwanza wa Kiarabu katika eneo hili alijulikana kama Sultani Seyyid Said bin Sultan. Sultani huyu alikuwa Mwarabu wa kwanza kutawala kwa pamoja dola za Omani na Zanzibar, kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1800 hadi alipofariki dunia mwaka 1856. Sultani alivutiwa sana na hali ya hewa ya Zanzibar, pamoja na kustawi kwa biashara katika ukanda huo, kina kirefu cha bandari ya Zanzibar na udongo wenye rutuba uliostawisha mazao mbalimbali, kama vile mikarafuu na minazi Hivyo, kiongozi huyu aliwahimiza matajiri wa Kiarabu kutoka Omani kuhamia Zanzibar na kuanzisha mashamba makubwa ya mikarafuu Mnamo mwaka 1840, Sultani Seyyid Said alihamisha rasmi makao yake kutoka Muscat, Omani hadi Zanzibar na kuifanya Zanzibar kuwa makao makuu ya utawala wake. Baada ya kifo chake mwaka 1856, urithi wa utawala ulifuata kwa watawala wengine, akiwemo Sultani Seyyid Majid, Sultani Barghash na hatimaye Sultani Jamshid bin Abdullah Al Said. Jamshid bin Abdullah Al Said alizaliwa tarehe 16 Septemba 1929 na kuwa Sultan wa Zanzibar baada ya kifo cha baba yake, Abdullah Bin Khalifa mwezi Julai 1963. Yeye alikuwa Sultan wa mwisho wa Zanzibar kutoka kwa familia ya al Busaid wa Oman waliotawala kwa miaka 91.
Mabadiliko ya kisiasa wakati wa utawala wa Waarabu
Jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilikuwa na mfumo madhubuti wa uongozi, utoaji wa uamuzi na umiliki wa ardhi kabla ya kuja kwa Waarabu wa Oman. Hivyo, ardhi katika jamii nyingi ilimilikiwa kwa pamoja na jamii nzima. Kila mwanajamii alikuwa na uhuru wa kuchagua sehemu za kulima, kukata miti au kufuga. Ardhi ambayo haikutumiwa kwa wakati huo ilikuwa ikihifadhiwa kwa matumizi ya baadaye ya jamii nzima. Hata hivyo, baada ya kuja kwa Waarabu, mabadiliko yalitokea. Kwa mfano, Waarabu walianzisha mtindo mpya wa kilimo cha mazao ya biashara, ambao ulisababisha baadhi ya jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar kuporwa ardhi yao yenye rutuba na kugawiwa kwa wakulima wa mazao ya biashara wa Kiarabu.
Kama ilivyokuwa kwa wakoloni wengine, Waarabu walitekeleza sera za kuchukua sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo cha mikarafuu na minazi. Ili kufanikisha mpango huo, Sultani Seyyid Said alihamasisha kwa kiasi kikubwa kilimo cha mikarafuu na minazi. Sehemu kubwa ya ardhi ya Zanzibar, ambayo awali ilitumiwa kwa kilimo cha mazao ya chakula, ilichukuliwa na mamwinyi wa Kiarabu na kuanzishwa mashamba makubwa ya mikarafuu na minazi. Mfumo huu mpya wa uongozi na siasa kwa ujumla, ulioruhusu ardhi yenye rutuba kumilikiwa na Waarabu, uliwafanya wananchi kuwa watumwa katika nchi yao. Katika mazingira haya, heshima, uwezo, haki na mali za Waranzibari zilinyakuliwa na utawala wa Sultani. Kielelezo 1.3 kinaonesha picha ya Sultani Seyyid Said.
|
Kielelezo 1.3: Sultani Seyyid Said |
Mtindo mpya wa ugawaji ardhi uliathiri mfumo wa kisiasa wa jadi wa umiliki wa ardhi kwa wanajamli wote, hali iliyosababisha kuibuka kwa matabaka katika jamli. Tabaka la kwanza lilikuwa la wanyonyaji, likiongozwa na viongozi wa serikali, wafanyabiashara wa kihindi na mamwinyi hasa wa Kiarabu. Tabaka la pili lilijumuisha wakulima wadogo wadogo, raia wa kawaida, huku tabaka la tatu likiwa la watwana na watumwa. Kuja kwa Waarabu kulibadilisha mfumo wa utawala wa kidemokrasia ya kijadi na umoja uliokuwa ukiendeshwa na tawala za kijadi. Mfumo huu mpya ulileta mgawanyiko katika jamii. Mfano wa mgawanyiko huo ni jamii za Kizanzibari zilipoteza mifumo yao ya kiuongozi ya kijadi na badala yake, mfumo wa kiutawala wa Kiarabu kushika hatamu visiwani humo. Hivyo, Waarabu walisababisha migogoro katika jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar.
Miongoni mwa mbinu walizozitumia na Waarabu ni kuwagawa watawala wa jadi kwa kumuunga mkono mtawala aliyeonekana kuwa na nguvu zaidi kuliko wenzake na wale walioonekana kuwa wasaliti. Kwa upande wa Zanzibar, watawala wa jadi kama Mwinyi Mkuu alifanywa kuwa mshirika mwenza katika utawala. Waarabu walitumia uongozi wa mabavu, unyanyasaji na ukandamizaji kwa wananchi. Kwa mfano, wananchi walifanyishwa kazi ngumu bila malipo. walinyang'anywa ardhi yenye rutuba na Waafrika wengi walichukuliwa na kupelekwa sehemu zingine kama watumwa.
| Kazi ya kufanya 1.2 Soma vitabu na matini mbalimbali kwenye mtandao, kisha fanya uchunguzi katika mfumo wa umiliki wa ardhi kabla na baada ya ujio wa Waarabu visiwani Zanzibar na Pemba. Uchunguzi wako ujikite katika maeneo yafuatayo: (a) Namna mfumo wa umiliki wa ardhi ulivyokuwa kabla ya ujio wa utawala wa Waarabu; (b) Mabadiliko yaliyoletwa na utawala wa Waarabu katika mfumo wa umiliki wa ardhi; na (c) Athari zilizoletwa na mabadiliko katika mfumo wa umiliki wa ardhi. |
Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Waarabu
Kuongezeka kwa mahitaji ya pembe za ndovu, karafuu, mafuta ya nazi na mpira katika viwanda vya Ulaya na Marekani kulimhamasisha sana Sultani wa Zanzibar pamoja na wafanyabiashara wa Kiarabu kuendeleza biashara ya bidhaa hizo. Hali kadhalika, mashamba makubwa ya mikarafuu na mpira yalianzishwa visiwani, jambo lililosababisha ongezeko la mahitaji ya nguvukazi hasa vibarua wa kupalilia, kuchuma karafuu na kuangua nazi.
Waarabu walifanya biashara na wenyeji wa pwani ya Tanganyika na Afrika Mashariki kwa ujumla. Katika biashara hiyo, walitafuta dhahabu, shaba, pembe za ndovu, magogo ya mikoko, nta na ngozi za wanyama pori kama vile chui na pundamilia. Vingine ni magamba ya konokono na kobe, pamoja na watumwa. Waarabu nao walileta bidhaa mbalimbali kama manukato, vyombo vya nyumbani viungo vya chakula kama vile karafuu, mdalasini na tangawizi. Bidhaa nyingine zilikuwa shanga, majambia, bunduki, vioo vya kujitazamia na nguo. Kutokana na ustawi wa biashara hiyo, Zanzibar illimarika na kuwa dola kuu ya kibiashara katika eneo la Afrika Mashariki likijumuisha pwani wa Bahari ya Hindi, mashariki mwa Kongo, Malawi and kaskazini mwa Msumbiji.
Biashara za masafa marefu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati zilifanyika kwa kutumia njia kuu tatu zilizoanzia pwani kuelekea bara, kama inavyooneshwa kwenye Kielelezo 1.4. Njia ya Kaskazini ilianzia Saadani kuelekea Pangani hadi Mlima Kilimanjaro, kisha kuingia nchini Kenya. Njia ya kati ilianzia Bagamoyo kupitia Morogoro hadi Tabora. llipofika Tabora, iligawanyika katika matawi mawili: tawi la kwanza lilianzia Tabora kuelekea kaskazini huko Karagwe, Buganda na Bunyoro. Tawi la pili lilianzia Tabora kuelekea magharibi huko Ujiji, Burundi, Rwanda, Katanga na Umanyema huko Kongo. Njia hii ilimilikiwa zaidi na Wanyamwezi na Wasumbwa.
|
Kielelezo 1.4. Njia kuu za biashara ya masafa marefu wakati wa utawala wa waarabu |
Mfanyabiashara maarufu wa Kiarabu katika njia hii ya kati alikuwa Hemed bin Muhammad bin Juma bin Rajab el Murjebi, maarufu kama "Tippu Tip". Njia kuu ya tatu ilikuwa ya Kusini. Njia hii ilianzia Kilwa Kivinje kuelekea Ziwa Nyasa, kaskazini mwa Msumbiji, Malawi na mashariki mwa Zambia. Njia hii ilitawaliwa na Wayao. Njia hizi zilitumika kupitisha bidhaa mbalimbali pamoja na misafara ya watumwa.
Ukuaji wa kilimo cha mazao ya biashara kama karafuu katika visiwa vya Pemba na Unguja na kilimo cha miwa huko Komoro, Ngazija, Mauritius na Retkion, ulisababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya watumwa kutoka maeneo hasa Tanganyika. Hii ilichangia kukua kwa biashara ya utumwa katika maeneo mengi ya eneo hili
Kwa ujumla, katika kipindi cha utawala wa Waarabu, uchumi ulikuwa wa kinyonyaji, kwani Waarabu walikuwa wanufaika wakuu wa mapato, huku Waafrika wengi wakinyonywa kwa kufanya kazi kwa ujira mdogo na wengine wakigeuzwa kuwa watumwa. Watumwa hawa waliuzwa na wengine kutumikishwa katika mashamba makubwa ya mikarafuu na minazi ya Waarabu huko visiwani Unguja na Pemba.
| Zoezi la 1.2 1. Fafanua namna ambavyo kushamiri kwa biashara kulivyoifanya Zanzibar kuwa dola kubwa na kitovu cha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki. 2. Eleza mabadiliko ya kiuchumi yaliyoletwa na Waarabu katika jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar. 3. Linganisha thamani ya bidhaa zilizobadilishwa kati ya wafanyabiashara wa Kiarabu na jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar. |
Mabadiliko kijamii wakati wa utawala wa Waarabu
Kabla ya kuwasili kwa Waarabu, jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilijengwa juu ya maadili yaliyotokana na dini zao za jadi, ambapo baadhi yao waliabudu Mungu kupitia miti mikubwa, majabali na mapango makubwa, mito, maziwa na bahari na walitoa kafara kwa malengo mbalimbali kulingana na imani zao. Aidha, jamii hizi zilijikita katika kutoa elimu ya jadi ambayo ililenga kumpatia kijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na mazingira yake. Hii ilimwezesha kuishi vyema kwa kufuata maadili na mila za jamii yake. Kuja kwa Waarabu kulileta mabadiliko makubwa katika masuala ya elimu, maadili na utamaduni katika jamii hizi.
Jamii za pwani ya Tanganyika na Zanzibar zilijifunza lugha ya Kiarabu ili kuimudu dini ya Kiislamu na kuendana na matakwa na tamaduni za Waarabu. Hali hii ilisababisha watu wengi kujiunga na madrasa kwa ajili ya kujifunza dini ya Kiislamu na lugha ya Kiarabu, huku lugha ya Kiswahili ikiendelea kutumika kama lugha ya biashara na mawasiliano ya kila siku.
Mwingiliano baina ya Waarabu na jamii za pwani ulisababisha mabadiliko makubwa ya kitamaduni. Kwa mfano, uvaaji wa mavazi kama vile kanzu, baibui, baraghashia na makubadhi ulienea sana. Lugha ya Kiswahili pia ilianza kupata maneno mapya baada ya kutohoa baadhi ya msamiati kutoka lugha ya Kiarabu ili kurahisisha mawasiliano. Mfano wa baadhi ya maneno hayo ni kama vile marhaba, shukrani, sheria, heshima, nzuri, labeka na hayati. Jamii zilizoathiriwa zaidi na tamaduni za Kiarabu ni pamoja na Wahadimu, Watumbatu, Wapemba,Wazaramo na Wakwere kutokana na mwingiliano wao wa karibu katika shughuli za kila siku.
| Kazi ya kufanya 1.3 Soma matini mbalimbali katika vitabu na mtandao kuhusu mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Waarabu kisha; tengeneza vibonzo vinavyoonyesha namna utamaduni, maadili na elimu vilivyobadilika baada ya ujio wa Waarabu. |
Utawala wa Wajerumani
Utawala wa Wajerumani katika Afrika Mashariki ya Kijerumani ulisukumwa na mabadiliko ya kiuchumi yaliyokuwa yakijitokeza barani Ulaya, ikiwemo nchini Ujerumani. Mabadiliko hayo yalitokana na kuongezeka kwa teknolojia iliyochochea mapinduzi ya viwanda yaliyoshika kasi kuanzia mwaka 1750 nchini Uingereza. Mapinduzi hayo yalisababisha uzalishaji mkubwa wa bidhaa na hivyo kuongeza mahitaji ya malighafi kwa ajili ya uzalishaji pamoja na masoko mapya na makubwa kwa ajili ya kuuza bidhaa hizo. Ili kukabiliana na changamoto hii, Wajerumani, pamoja na mataifa mengine ya Ulaya, walitafuta njia za kupata suluhisho kupitia nchi za nje.
Bara la Afrika lilionekana kuwa eneo muafaka kwa uwekezaji na utatuzi wa changamoto za upatikanaji wa malighafi na masoko Katika robo ya mwisho ya karne ya 19, Wajerumani walifika Afrika Mashariki ya Kijerumani baada ya kupata taarifa kuhusu uwapo wa malighafi na soko la bidhaa Taarifa hizo walizipata kutoka kwa wamisionari, wafanyabiashara na wapelelezi waliotumwa na makampuni ya Kijerumani hapa nchini. Hii iliwasaidia sana kuyatambua maeneo muhimu ya kuwekeza na kuanzisha mashamba makubwa ili kupata malighafi mbalimbali zilizohitajika katika viwanda vya Ujerumani.
Utawala wa Wajerumani katika eneo hili unaweza kugawanywa katika vipindi vifuatavyo: Kati ya mwaka 1886 hadi 1891. Kipindi hiki, Afrika Mashariki ya Kijerumani ilitawaliwa na Kampuni ya Kijerumani ya Afrika Mashariki chini ya uongozi wa mfanyabiashara Karl Peters. Kuanzia mwaka 1891 hadi 1918, serikali ya Ujerumani ilichukua rasmi mamlaka ya kutawala Afrika Mashariki ya Kijerumani. Wajerumani walikusudia kuimarisha utawala wao katika koloni hili kwa kuzitumia mbinu mbalimbali. Mbinu hizo zilijumuisha matumizi ya vyombo vya kiitikadi kama vile elimu na dini. Mbinu nyingine ilikuwa ni kuunda vyombo vya dola kama jeshi, magereza na mahakama za kikoloni ili kuhakikisha wananchi hawaupingi utawala wa kikoloni na wanazitii sheria zilizowekwa. Aidha, walitumia mbinu ya kuwapeleka watawala wazungu katika ngazi za uongozi na kuondoa tawala za jadi. Kwa ujumla, ujio wa Wajerumani ulileta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa na katika jamii za Kitanzania.
Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Wajerumani
Kama ilivyosemwa awali, lengo kuu la Wajerumani kuja katika Afrika Mashariki ya Kijerumani lilikuwa kutafuta suluhisho la changamoto za kiuchumi zilizotokana na mapinduzi ya viwanda, kama vile upungufu wa masoko na malighafi, kwa viwanda vyao barani Ulaya. Kwa hivyo, kupitia ukoloni, wakoloni waliweza kuzipunguza changamoto hizo kwa kuanzisha uchumi wa kikoloni ambao ulileta mabadiliko makubwa kwenye jamii za Kitanzania. Shughuli za uzalishaji mali zilitegemea sana uzalishaji wa mazao ya biashara kama vile kahawa, chai, mkonge, pamba, tumbaku na mpira. Mazao haya yalilimwa katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki ya Kijerumani. Kwa mfano, kahawa ililimwa Bukoba, Kilimanjaro, Arusha na Tukuyu; pamba ilianza kulimwa katika maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro, Bagamoyo, Rufiji na Lindi; katani ililimwa huko Tanga, Morogoro, Lushoto, Lindi, Dar es Salaam na Pwani; mpira ulilimwa maeneo ya pwani hasa katika bonde la mto Pangani huko Tanga na bonde la mto Rufiji hasa maeneo ya Mohoro. Walowezi wa Kijerumani walianzisha mashamba ya katani yenye ukubwa wa ekari zaidi ya 100,000 (hekta 40,000). Walowezi wengine walipanda zaidi ya miche milioni mbili ya kahawa, ekari 200,000 (hekta 81,000) za miti ya mipira na mashamba ya pamba. Maeneo ya Rukwa, Kigoma, Mtwara, Dodoma na Singida hayakuruhusiwa kuanzisha kilimo cha mashamba makubwa kwa sababu yalitengwa maalumu kwa ajili ya kutoa wafanyakan na vibarua (manamba) watakaofanya kazi katika mashamba makubwa ya walowezi na migodi ya madini hasa dhahabu huko Chunya, Sekenke na Mwanza.
Kwa upande wa viwanda, Wajerumani hawakuanzisha viwanda vikubwa bali walijenga viwanda vidogo, hasa vya kuchakata malighafi ili kupunguza uzito wake kabla ya kusafirishwa kwenda Ujerumani. Kwa mfano, walijenga vinu vya kukoboa kahawa, kuchambua pamba na kusindika mkonge. Wajerumani walijenga viwanda vidogovidogo vya kuzalisha viatu, viberiti, baruti na risasi. Wajerumani hawakujenga viwanda vikubwa vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za viwandani kama vile nguo, kamba na mazulia, bali walilenga kurahisisha usafirishaji wa malighafi tu.
Vilevile, Wajerumani waliendesha biashara ya kinyonyaji, kwani koloni hili lilitumika kama soko la kuuzia bidhaa za viwandani kutoka Ujerumani, kama vile nguo, baiskeli, mapanga, majembe, viatu na sigara. Bidhaa hizi zote ziliuzwa kwa bei kubwa, wakati malighafi zilizotumika kuzalisha bidhaa hizo zilinunuliwa kwa bei ndogo sana.
| Zoezi la 1.3 1. Fafanua sababu zilizowafanya Wajerumani kuanzisha utawala wa kikoloni katika jamii za Kitanzania. 2. Kwa nini Wajerumani walijenga viwanda vidogo badala ya viwanda vikubwa katika Afrika Mashariki ya Kijerumani? 3. Eleza athari ambazo zingetokea iwapo Wajerumani wangejenga viwanda vikubwa vya kuchakata malighafi katika Afrika Mashariki ya Kijerumani. |
Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Wajerumani
Wajerumani walilazimika kujenga na kutoa huduma kadhaa ili kufanikisha malengo yao katika Afrika Mashariki ya Kijerumani. Huduma hizi zilijumuisha elimu, afya, maji na umeme, pamoja na miundombinu ya mawasiliano.
Elimu
Elimu iliyotolewa na Wajerumani ililenga kukidhi mahitaji ya shughuli zao za kikoloni. Mfumo wa elimu uliundwa mahususi ili kuandaa wasaidizi watakaowasaidia Wajerumani katika shughuli hizo. Elimu hiyo ililenga zaidi wananchi wachache ambao wangeweza kuzalisha malighafi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya uchumi wa kikoloni. Malengo ya elimu hiyo yalikuwa yafuatayo:
(a) Kueneza utamaduni wa Kijerumani.
(b) Kuandaa watumishi wa ngazi za chini;
(c) Kufundisha uadilifu na maadili ya kazi; na
(d) Kuandaa wazalishaji mall kwa ajili ya uchumi wa Kijerumani.
Ili kutimiza malengo hayo, mtaala wa elimu ya Kijerumani ulifundisha stadi kama vile uashi, useremala, ukarani, upigaji picha, ufundi wa kushona na utengenezaji wa viatu. Shule mbalimbali zilianzishwa na kugawanywa katika makundi mawili: shule za Wamisionari na shule za serikali. Hata hivyo, mtaala wa shule za serikali ulipingwa na Wamisionari ambao walitaka utumike mtaala wa shule zao. Elimu ilitolewa kwa lugha ya Kiswahili, huku shule za serikali zikihudumia zaidi wavulana na wasichana wakibaguliwa. Mfumo huu wa elimu ya kikoloni ulikuwa na idadi ndogo ya wanafunzi wa Kiafrika.
Afya
Huduma za afya katika kipindi cha ukoloni zilitolewa kwa ubaguzi wa rangi, ambapo huduma hizo zilipatikana katika maeneo ambayo wakoloni walianzisha shughuli kubwa za uzalishaji mali kama vile mashamba na makazi yao. Wazawa walipata matibabu ya kiwango cha chini ukilinganisha na Wazungu na Wansia Matibabu haya yalilenga kuwawezesha Waafrika kuzalisha malighafi bila kusumbuliwa na magonjwa hasa ya kitropiki au kuumia wakiwa kazini. Aidha, huduma za afya zilitilia mkazo masibabu badala ya kinga dhidi ya magonjwa Madhumuni ya kueneza huduma hizi yalikuwa ni kuhakikisha kwamba wazalishaji mali katika maeneo hayo wanakuwa na afya njema ili waweze kufanikisha malengo ya kikoloni.
Athari hasi za huduma hizi zilikuwa ni kupotea kwa umaarufu kwa waganga na matabibu wa jadi, pamoja na dawa zao kushuka thamani. Hii ilisababishwa na ongezeko la vituo vya matibabu na matumizi ya dawa za kigeni. Hata hivyo, bado waganga wa jadi waliendelea kutoa matibabu, hasa katika maeneo ya vijijini
Huduma za maji na umeme
Katika kipindi cha ukoloni, huduma za maji na umeme zilitolewa kwa ubaguzi na upendeleo, kwani huduma hizi zilielekezwa zaidi katika maeneo yenye umuhimu wa kiuchumi. Kwa mfano, usambazaji wa huduma hizi ulifanyika katika migodi, viwandani, maeneo ya mijini, mashamba makubwa ya wakoloni na makazi ya walowezi wa Kizungu na Kiasia.
Miundombinu ya mawasiliano
Wakoloni walijenga njia za uchukuzi na mawasiliano kama vile barabara, reli na bandari. Miundombinu hii ilikuwa muhimu kwa usafirishaji wa malighafi, bidhaa na watu. Reli na barabara zilijengwa kutoka maeneo ya uzalishaji wa malighafi hadi bandarini. Malighafi kutoka makoloni ilisafirishwa kwenda Ulaya na bidhaa za viwandani kutoka Ulaya kama vile nguo, vyombo vya nyumbani na zana za chuma ziliingizwa kupitia bandari hizo na kuletwaAfrika Mashariki ya Kijerumani.
| Kati ya kalanya 1.4 Kwa kusoma matini katika vitabu na mtandaoni, fanya utafiti mdogo kuhusu tiba za jadi wakati wa ujio wa Wajerumani. Utafiti wako ujikite katika maeneo yafuatayo: (a) Namna tiba za jadi zilivyokuwa kabla ya ujio wa Wajerumani; (b) Magonjwa yaliyotibiwa kwa kutumia tiba za jadi; (c) Namna Wajerumani walivyoathiri tiba za jadi; na (d) Toa ushauri kuhusu umuhimu wa tiba za jadi kwa jamii za sasa za Kitanzartia. |
Jamii zilivyoathirika na utawala wa Wajerumani
Wajerumani walijenga himaya yao ya kikoloni katika Afrika Mashariki ya Kijerumani kuanzia mwaka 1885. ili kufanikisha malengo yao ya kiuchumi, Wajerumani walianza kutafuta njia mbalimbali za kiuchumi zilizoweza kuwaletea faida. Miongoni mwa njia hizo, walitafuta maeneo mapya ya kibiashara, ambapo walijipenyeza katika maeneo ya bara kwa kufuata njia za biashara ya masafa marefu zilizotumiwa na jamii za Kitanzania kabla ya ukoloni. Wakati huohuo, walijenga ngome za kijeshi na vituo vikubwa huku wakiwabadilisha au kuwaondoa kwa nguvu watawala wa jadi waliokuwepo. Walianzisha mfumo wa utawala uliokuwa chini ya liwali na maakida, ambao aghalabu walikuwa Waarabu na watu kutoka sehemu nyingine za Afrika, hususani Waswahili. Kwa ujunda, karibu jamii zote katika Afrika Mashariki ya Kijerumani ziliathiriwa na utawala wa Wajerumani. Kwa mfano, baadhi ya jamii zilizoathirika ni pamoja na Wanyamwezi, Wazigua, Wayao, Wangindo, Wamatumbi, Wambunga, Wahehe, Wachaga, Wameru na Waha.
Jamii za Kitanzania zilizokuwa zimezoea kujitawala, zilivurugwa na kuja kwa utawala wa Wajerumani. Wajerumani waliweka vibaraka waliotii sheria na matakwa yao. Katika maeneo fulani au wilaya, walianzisha utawala wa kijeshi na kuondoa kabisa utawala wa jadi, kama ilivyokuwa lringa na Mahenge. Hivyo, wazawa walipoteza nguvu yao ya kujitawala.
Wajerumani waliwataka wenyeji kulipa kodi, lakini wenyeji walikataa na hatimaye machafuko na vita kadhaa vilizuka. Kwa mfano, mwaka 1898, kulizuka Vita ya Maboga ambapo Wamatumbi walishindwa. Wamatumbi wa Kilwa na wa Liwale pia waliathirika kutokana na kulipwa ujira mdogo, kufanya kazi za sulubu, Wangindo kulipa kodi ya rupia tatu na kuadhibiwa vikali kwa makosa mbalimbali. Vilevile, utawala wa Kijerumani ulisababisha kutothaminiwa kwa utu wa wanajamii wengi. Wazazi au watu wazima walidhalilishwa mbele ya watoto wao, kwa mfano, kuchapwa viboko pale waliposhindwa kulipa kodi ya kichwa au walipotenda makosa madogo madogo.
Utawala wa Kijerumani ulisababisha utengano miongoni mwa jamii za Kitanzania. Kwa mfano, Mangi Marealle wa Wachaga wa Marangu aliungana na Wajerumani kumpiga Mangi Meli wa Moshi. Kwa ujumla, jamii za Kitanzania zilipata athari katika uchumi na hata kisiasa, kwani mfumo wao wa kujitawala ulibadilishwa. Hali hii iliwapa ujasiri wa kudai uhuru wao kwa njia na mbinu mbalimbali, ikiwemo vita.
| Zoezi la 1.4 1. Fafanua namna mabadiliko katika mfumo wa utawala wa jadi kufuatia kuja kwa Wajerumani yalivyoathiri jamii za Kitanzania 2. Kwa nini jamii za Kitanzania zilipinga ulipaji wa kodi ulioanzishwa na utawala wa Kijerumani? 3. Unajifunza nini kutoka kwa mababu na mabibi zetu waliopinga mfumo na utawala wa Kijerumani? |
Utawala wa Waingereza Tanganyika na Zanzibar
Afrika Mashariki ya Kijerumani ilikuwa sehemu ya koloni la Ujerumani hadi kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1918. Wakati wa vita hivyo, koloni la hili lilitekwa na majeshi ya Uingereza na Ubelgiji. Mkataba wa Amani wa Versailles wa mwaka 1919 uliamua kwamba makoloni yote yaliyokuwa ya Wajerumani yakabidhiwe mataifa yaliyoshinda vita hivyo. Hivyo, Afrika Mashariki ya Kijerumani ilikabidhiwa rasmi kwa Waingereza chini ya udhamini wa Jumuiya ya Kimataifa (League of Nations).
Kwa upande wa Zanzibar; utawala wa Waingereza ulianza baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa pili kati ya Wajenumani na Waingereza Mkataba huo ulisainiwa tarehe 1 Julai, 1890, unaojulikana kama Mkataba wa Heligoland. Kulingana na mkataba huo, Uingereza ilipewa mamlaka ya kuiweka Zanzibar chini ya himaya yake kwa makubaliano na mtawala wa wakati huo, Sayyid Ali bin Said.
Jamii za Tanganyika na Zanzibar wakati huo zilifuata mwelekeo wa kiuchumi, kisiasa na kijamii ulioanzishwa na Waingereza. Ili kuimarisha ukoloni, Waingereza walibadilisha mfumo wa utawala uliokuwapo na kuanzisha mfumo wa kiuwakala ambao ulibadilisha pia uchumi, siasa na utamaduni wa Tanganyika. Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba, ni utawala wa Kiingereza uliobadilisha jina la koloni hilo kutoka Afrika Mashariki ya Kijerumani na kuwa Tanganyika.
Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Waingereza
Mabadiliko ya kiuchumi wakati wa utawala wa Waingereza yalilenga kuendeleza kilimo, biashara na viwanda vidogovidogo. Kwa upande wa kilimo, utawala wa Waingereza ulihamasisha kilimo cha mazao ya biashara kama vile kahawa, pamba, mkonge, chai na pareto. Serikali hiyo pia iliwahimiza walowezi kufufua mazao ya biashara ambayo yalikuwa yameathiriwa na vita. Walowezi hawa walitoka mataifa mbalimbali kama Uingereza, Afrika Kusini, Ugiriki na India Lengo kubwa la kufufua mazao haya ya biashara lilikuwa kupata malighafi za kutosha kwa ajili ya viwanda nchini kwao Uingereza.
Hata hivyo, wakati Waingereza walipopewa idhini ya kutawala Tanganyika na Zanzibar, wananchi walikuwa tayari wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya biashara, kama vile buni iliyolimwa Moshi na Bukoba. Pamba nayo ilikuwa ikilimwa katika maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Morogoro na Pwani. Shughuli za biashara wakati wa utawala wa Waingereza zilifanywa na watu wa jamii ya Kiasia, hasa Waarabu na Wahindi. Jamii hii ilijihusisha na biashara ya kununua mazao kutoka kwa wakulima na kuyauza kwa makampuni ya kibepari ya Wazungu. Pia, walifanya biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali zilizoagizwa kutoka Ulaya magharibi na Marekani. Watanganyika na Wazanzibari hawakuruhusiwa kushiriki katika biashara wakati wa utawala huo. Waingereza, Wagiriki na Wahindi ndio waliofanya biashara ya kuagiza na kusafirisha nje ya koloni bidhaa mbalimbali. Waarabu na Wahindi walifanya biashara ya maduka ya rejareja maeneo ya mijini na vijijini
Kwa upande wa viwanda, Waingereza hawakuwekeza sana katika viwanda vikubwa ila walianzisha viwanda vidogo vidogo. Serikali ya Waingereza ilikusanya malighafi kama vile mazao ya kilimo, madini na miftigo na kuzisafirisha kwenda kwenye viwanda vyao huko Uingereza. Bidhaa zilizozalishwa huko zililetwa na kuuzwa kama bidhaa za viwandani hapa nchini. Viwanda vilivyokuwa hapa vilijikita zaidi katika kuchakata malighafi ili kupunguza uzito kabla ya kusafirishwa. Kwa mfano, viwanda vya kusindika buni, katani, karanga na pamba, pamoja na viwanda vya kukaushia tumbaku vilianzishwa. Waingereza pia waliendeleza uchimbaji wa madini kwa kupanua migodi iliyoachwa na Wajerumani na kuanzisha mingine mipya, kama migodi ya chumvi huko Uvinza na Ulanga na migodi ya dhahabu huko Chunya na Geita.
Usafirishaji na uchukuzi ni baadhi ya shughuli za kiuchumi zilizopewa kipaumbele na serikali ya Waingereza. Juhudi za kufufua miundombinu iliyoharibiwa na vita zilifanyika, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa reli katika baadhi ya maeneo kama vile reli kutoka Tabora hadi Mwanza na reli kutoka Moshi hadi Arusha. Pia, bandari na usafiri wa meli katika Ziwa Tanganyika na ziwa Viktoria uliimarishwa. Lengo la kuimarisha usafirishaji na uchukuzi lilikuwa kurahisisha usafirishaji wa malighafi kutoka maeneo ya uzalishaji hadi bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara tayari kwa kusafirishwa Ulaya. Vilevile, njia hizi za usafirishaji ziliwezesha bidhaa za viwandani kusafirishwa kutoka bandarini kuelekea masoko ya maeneo ya bara.
Kwa upande wa Zanzibar, Waingereza waliwatumia Waarabu na Wahindi kuendeleza masilahi yao ya kiuchumi. Waarabu walipewa ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo cha mikarafuu na minazi, wakati Wazanzibari wengi walipewa ardhi isiyo na rutuba. Wahindi walipewa jukumu la kusimamia biashara, hivyo walijenga shule ili kuendeleza uzoefu wao. Mnamo mwaka 1923, shule kwa ajili ya watoto wa Kihindi zilianzishwa.
| Kazi ya kufanya 1.5 Shule yako imealikwa kushiriki mdahalo katika shule ya jirani; andaa hoja utakazotumia katika mdahalo huo kuhusu mada inayosomeka "utawala wa Waingereza ulikuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi katika jamii za Tanganyika na Zanzibar" |
Mabadiliko ya kisiasa wakati wa utawala wa Waingereza
Baada ya Waingereza kukabidhiwa rasmi madaraka, serikali iliimarisha misingi ya utawala kwa kuweka taratibu na sheria ili kurejesha hali ya utulivu iliyotoweka wakati wa vita. Awali, Waingereza waliendelea kutumia mtindo wa utawala uliokuwa ukitumiwa na Wajerumani. Hata hivyo, baadaye walibadilisha Infunto wa utawala kwa kuanza kuwatumia viongozi wa jadi katika shughuli za utawala. Viongozi hawa walikuwa na majukumu ya kusimamia maagizo ya serikali, kukusanya kodi, kufanya sensa ya watu na mifugo, kuwa na daftati la walipa kodi na kuamua kesi zilizofikishwa katika mahakama zao. Majukumu haya yalitekelezwa chini ya usimamizi wa mabwana shauri wa Kingereza waliokuwa na jukumu la kufafanua sheria za kikoloni kwa wananchi.
Mtindo wa kisiasa wa kuwatumia machifu ulikuwa ni chombo cha kuendeleza mipango ya ukoloni ya kuwakandamiza na kuwanyonya wananchi. Waingereza walisisitiza sana ukabila katika mipango yao ili kuwagawa na kuwadhibiti wananchi. Kwa mfano, kwenye mashamba na migodi, vibarua walipangiwa mabweni ya kulala kwa misingi ya kikabila. Aidha, ubaguzi ulionekana katika shule na hata kwenye mashindano ya ngoma na michezo yajadi.
Ili kuimarisha utawala wa Waingereza, sheria na kanuni mbalimbali zilitungwa kwa lengo la kuwakandamiza wananchi. Sheria zote hizi zililenga kuwanufaisha Wazungu na Waasia. Wakoloni walitumia mbinu za kuwalaghai machifu kwakuunda shirikisho la machifu kwa kila kabila na kumteua chifu mmoja kuwa kiongozi mwandamizi wa wengine. Kwa mfano, Marealle aliteuliwa kuongoza machifu wa Kichaga, Fundikira aliteuliwa kuongoza machifu wa Kinyamw ezi, Makwaia aliteuliwa kuongoza machifu wa Kisukuma na Chifu Luther Kingu alichaguliwa kuongoza machifu wa Iramba.
Waingereza walitumia mtindo wa utawala uliokuwa ukijulikana kama utawala wa kiuwakala ulioanzishwa na Gavana Sir Donald Cameron mwaka 1926. Mtindo huu uliendeshwa kwa kutumia makamishna wa majimbo na wilaya. Makamishna wa wilaya ndio waliokuwa kiungo kati ya serikali ya kikoloni na serikali za mitaa zilizoongozwa na machifu wakisaidiwa na majumbe.
Baada ya Vita Kuu ya Pill ya Dunia, Waingereza walipanua Baraza la Kutunga Sheria. Baraza hili lilikuwa na kazi ya kumshauri Gavana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utawala. Jukumu jingine la baraza lilikuwa ni kutunga sheria ambazo zilihitaji idhini kutoka serikali ya Uingereza kabla ya kutumika. Wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria waliingia kwa kuteuliwa na Gavana mwenyewe, huku wengine wakiteuliwa kutokana na nyadhifa zao serikalini. Baraza hili kwa mara ya kwanza lilijumuisha machifu wa Kitanganyika, wakiwemo Chifu Abdieli Shangali na Chifu Kidaha Makwaia.
Zanzibar ilikuwa na uhusiano maalumu na Waingereza, lakini kwa hali halisi, siasa ya Waingereza iliifanya Zanzibar kuwa koloni. Ingawa Waingereza waliutumia utawala wa Sultani katika kuitawala Zanzibar, utawala wa Kisultani haukujitegemea hata mara moja. Mwanzoni mwa mwaka 1914, Baraza la Ushauri lilianzishwa kwa lengo la kumshauri Sultani na serikali yake kuhusu masuala ya serikali. Unguja na Pemba ziligawanywa katika wilaya, mudiria na shehia. Kila wilaya ilikuwa chini ya afisa wa serikali ambaye alikuwa Mwingereza, huku Mudir na Sheria wa Kiarabu wakisimamia mudiria na shehia. Hata hivyo, kulikuwa na Waafrika wachache waliokuwa wakisimamia shehia, lakini walipewa jukumu la kuwahimiza wenzao kuwatumikia Wazungu, Waarabu na Wahindi.
| Zoezi la 1.5 1. Tofautisha mfumo wa utawala wa Waingereza na ule wa Wajerumani katika kuzitawala jamii za Kitanzania. 2. Eleza kwa kifupi majukumu ya viongozi wa jadi katika serikali ya Kiingereza. 3. Linganisha majukumu ya viongozi wa sasa wa serikali za mitaa na yale ya viongozi wa jadi wakati wa utawala wa Waingereza Tanganyika. 4. Tofautisha utawala wa Waingereza Tanganyika na Zanzibar. |
Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Waingereza
Mabadiliko ya kijamii wakati wa utawala wa Waingereza yalijikita zaidi katika utoaji wa huduma za msingi kama elimu, afya, maji, umeme na miundombinu. Huduma hizi zilitolewa kwa madhumuni ya kuiwezesha serikali ya Waingereza kurahisisha utekelezaji wa malengo ya kikoloni, ikiwemo kupata nguvukazi ya kutosha miongoni mwa wananchi ili kuwezesha uzalishaji wa malighafi muhimu kwa viwanda vyao huko Ulaya. Kwa kiasi kikubwa, huduma za jamii zilizoanzishwa na serikali ya kikoloni hazikulenga kuwahudumia wananchi bali kutimiza masilahi ya wakoloni. Elimu: Shughuli za utoaji wa elimu ziliathirika sana wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Serikali ya Uingereza, kwa kushirikiana na mashirika ya dini, ilianza kutoa elimu kwa wananchi kwa kufuata mipango na mahitaji ya wakoloni. Sehemu zilizopewa kipaumbele ni zile zilizozalisha mazao ya biashara, hususani kahawa na pamba, pamoja na vituo vya wamisionari. Kwa mfano, shule nyingi katika Tanganyika zilijengwa katika maeneo ya Kilimanjaro na Bukoba.
Malengo ya elimu iliyotolewa na Waingereza yalikuwa kuwapatia wananchi maarifa yatakayowasaidia kuendeleza mipango na mikakati ya kikoloni. Hii ilifanywa kwa kuwapa wananchi elimu ya mbinu bora za kilimo na ufugaji na elimu ya afya. Pia, iliwaandaa mabwanyenye uchwara ambao walisaidia kuongoza na kufundisha utii na unyenyekevu ili kutekeleza maagizo na maelekezo ya serikali ya kikoloni. Elimu ilitolewa katika ngazi zifuatazo: elimu ya msingi (darasa la 1- 4), elimu ya kati (darasa la 5-8) na elimu ya sekondari (darasa la 9-12). Mtaala wa elimu ulijikita zaidi katika kufundisha mambo ya kigeni, hivyo maudhui yaliyofundishwa shuleni hayakuwasaidia wananchi kutatua matatizo yao ya kila siku. Kwa mfano, wanafunzi walifundishwa kuhusu mila, tamaduni na desturi za Kiingereza badala ya mila zao za asili.
Kwa upande wa Zanzibar, Waingereza walitoa elimu iliyoendeleza matabaka ya kijamii. Wazanzibari walifundishwa jinsi ya kuwa watiifu na waaminifu kwa Sultani na viongozi wao, ambao wengi walikuwa Waarabu. Waarabu walipewa elimu maalumu iliyowawezesha kuendelea kujiona kuwa bora kuliko Waafrika. Ubaguzi huu katika utoaji wa elimu ulikuwa kikwazo kikubwa kwa Watanganyika na Wazanzibari.
Aidha, ubaguzi wa kikanda na kimaeneo ulikuwa dhahiri katika mfumo wa elimu, ambapo shule nyingi zilijengwa katika maeneo ya uzalishaji mali kama Moshi, Bukoba, Mbeya na Mwanza. Maeneo ya Rukwa na Kigoma yalikuwa na shule chache kwa kuwa hayakuwa maeneo ya uzalishaji mali. Hivyo, wananchi wa maeneo haya walinyimwa fursa za elimu. Wananchi hawa waliendelea kwenda kufanya kazi za manamba katika mashamba na migodi ya kikoloni. Hivyo, elimu iliyotolewa iliwafaidisha wachache pekee kwani hata shule zilikuwa chache na zilitoa elimu kwa watoto wa machifu. Kwa mfano, Shule ya Wavulana Tabora ilikuwa maalumu kwa watoto wa machifu.
Afya: Huduma za afya wakati wa utawala wa Waingereza zilitolewa kwa lengo la kuziendeleza na kuzilinda afya za wananchi ili wawe na nguvu za kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuendeleza uchumi wa kikoloni. Pamoja na kwamba Waingereza walihitaji nguvu kazi yenye afya, bado huduma za afya zilikuwa chache na duni. Sehemu zilizopata huduma za afya ni zile zilizo kwenye maeneo ya uzalishaji mali, makazi ya walowezi na vituo vya wamisionari.
Kama ilivyokuwa katika elimu, huduma za afya pia zilitolewa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Huduma bora zaidi zilitolewa kwa Wazungu, wakifuatiwa na Waasia, huku Waafrika wakipewa huduma za kiwango cha chini. Waingereza hawakuwaandaa Waafrika kuwa matabibu wa ngazi za juu, bali walifundishwa kuwa matabibu wa ngazi za chini. Vilevile, hospitali na vituo vya afya vilifuata misingi hiyo ya ubaguzi, ambapo kulikuwa na hospitali maalumu kwa Wazungu na nyingine kwa ajili ya watu wenye rangi nyingine. Kwa mfano, Hospitali ya Ocean Road ilikuwa maalumu kwa Wazungu, kwa kuwa ilitoa huduma bora zaidi.
Miundombinu: Katika kutekeleza mpango wa ukoloni wa kupata malighafi muhimu kwa ajili ya viwanda vya Ulaya, Waingereza waliendelea kufufua na kuanzisha miundombinu kutoka maeneo ya pwani hadi maeneo ya uzalishaji mali kama migodi na mashamba ya pamba, mkonge na kahawa. Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na barabara, reli na bandari. Reli kutoka Tabora hadi Mwanza ilikamilishwa mwaka 1928. Pia, usafiri katika Ziwa Tanganyika na Viktoria uliimarishwa. Bandari za Tanga na Dar es Salaam, ambazo zilikuwa zimeathiriwa na vita, zilikarabatiwa. Waingereza pia walijenga bandari ya Mtwara. Aidha, miundombinu mingine ya reli iliongezwa kwa lengo la kusafirisha malighafi na vibarua kutoka sehemu mbalimbali za nchi, kama inavyoonekana kwenye Kielelezo 1.5.
|
Kielelezo 1.5: Miundombinu ya reli wakati wa utawala wa Waingereza |
Miundombinu ya barabara, reli na usafiri wa majini ililenga kuunganisha maeneo muhimu ya uzalishaji mali, kama vile mashamba ya mkonge, pamba, karanga na kahawa na yale maeneo waliyotokea manamba. Hivyo, miundombinu hiyo wakati wa utawala wa Waingereza ilisaidia katika kuwasafirisha manamba kwenda kufanya kazi kwenye mashamba na migodi. Pia, miundombinu ya barabara na reli ilitumika kusafirisha malighafi kutoka bara hadi bandarini, kusambaza bidhaa za viwandani kutoka bandarini hadi bara. Vilevile, kusafirisha askari kwenda maeneo yaliyokuwa na upinzani na hatimaye, kusafirisha watawala kwenda kusimamia shughuli katika maeneo mbalimbali. Huduma za usafirishaji wakati wa utawala wa Waingereza hazikulenga moja kwa moja kuwanufaisha Waafrika kama abiria, bali zililenga kurahisisha mipango na matakwa ya kikoloni ya unyonyaji na ukandamizaji wa wananchi, pamoja na kusafirisha malighafi kwenda Ulaya kwa ajili ya viwanda vyao.
Huduma za maji na umeme: Serikali ya Uingereza ilijitahidi kuwapa wananchi wa Tanganyika na Zanzibar huduma za maji na umeme ili kuwawezesha kuwa na afya bora ili kuendelea kuzalisha malighafi. Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, serikali ilipanua huduma hizi, upanuzi ambao ulifanyika zaidi katika maeneo ya mijini na ya uzalishaji. Maeneo hayo ni kama vile mashamba ya kikoloni, migodini na mahali walipoishi watawala wa kikoloni.
Ubaguzi wa rangi ulijitokeza katika utoaji wa buduma za maji na umeme. Ubaguzi huu ulidhihirika zaidi katika maeneo ya mijini. Huko huduma bora za maji na umeme walipatiwa kwanza Wazungu, wakifuatiwa na Waasia na hatimaye Waafrika. Kutokana na hali hii, baadhi ya maeneo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam na Mwanza yalijulikana kama Uzunguni na Uhindini. Maeneo ya mjini walipokaa Waafrika wengi yaliitwa maeneo ya Uswahilini. Maeneo ya yalipatiwa huduma duni zaidi ikilinganishwa na yale ya mijini, hali iliyosababisha watu wa vijijini kuhangaika kutafuta huduma za maji na umeme. Maeneo ya vijijini yaliendelea kutumia kuni, koroboi na taa za chemli kutoa mwanga wakati wa usiku.
Mchango wa ukoloni katika uhusiano wa Tanzania na mataifa yaliyoitawala
Kabla ya ujio wa wakoloni, jamii za Kitanzania zilikuwa na uhusiano wa kuheshimiana na kushirikiana na jamii nyingine za Afrika na kwingineko. Uhusiano huu ulijengwa kwa misingi ya biashara, ambapo jamii hizo zilibadilishana bidhaa kama vile dhahabu, pembe za ndovu na vyakula. Ushirikiano huu ulizingatia maadili ya kutegemeana, kusaidiana na kuaminiana. Biashara iliyofanyika kati ya jamii hizi ilichangia kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi
Hali hii ya ushirikiano ilianza kubadilika baada ya ujio wa wakoloni kutoka Ulaya Magharibi. Mataifa ya Ulaya, hususani Ujerumani na Uingereza, yalitawala maeneo mbalimbali kwa lengo la kunyonya rasilimali za jamii za Kitanzania. Wakoloni walivunja uhusiano wa asili uliokuwepo kwa kuanzisha mipaka mipya na kuleta maadili ya kikoloni. Pia, waliweka sera mpya zilizovuruga maadili ya kijamii ya Kitanzania, ambayo yalijengwa katika misingi ya utu, upendo, umoja, kusaidiana na kuheshimiana kama jamii huru.
Baada ya ukoloni kushamiri, uhusiano kati ya jamii za Kitanzania na wakoloni uliingia katika hali ya uhasama mkubwa. Mataifa ya kikoloni ya Ulaya Magharibi yalitumia mbinu za kijeshi na kisiasa kutawala jamii za Kitanzania. Hali hii ilileta migongano ya mara kwa mara Wazawa walilazimika kupigania na kulinda ardhi zao, utu na uhuru wao dhidi ya utawala wa kigeni. Hali hii lilisababisha uadui kati ya wakoloni na jamii mbalimbali za Kitanzania.
Ukoloni uliathiri kwa kiasi kikubwa uhusiano wa kijamii na kiuchumi wa jamii za Kitanzania. Uhusiano wa kibiashara uliokuwa na mafanikio zamani sasa ulibadilika na kuwa wa kiunyonyaji. Wakoloni walipora rasilimali kama vile ardhi na madini na kuwanyonya wafanyakazi wa Kitanzania katika mashamba na migodi yao. Hii ilisababisha kuongezeka kwa umasikini na ukosefu wa haki miongorti mwa Watanzania.
Mbali na uhasama, ukoloni pia ulileta athari kubwa kwenye utamaduni na mifumo ya kijamii. Utamaduni wa kigeni ulienea katika jamii za Kitanzania na kudhoofisha utamaduni na maadili ya asili. Hali hii ilichangia kuvunjika kwa mshikamano wa kijamii na kuendeleza uhusiano hasi kati ya jamii za Kitanzania na wakoloni.
Ingawa ukoloni ulisababisha uhusiano mbaya baina yake na jamii za Kitanzania, pia ulisababisha mwamko mpya wa utaifa wa kudai uhuru. Harakati za kudai uhuru na kujikomboa zilichochea umoja miongoni mwa jamii za Kitanzania. Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, uhusiano mpya ulijengwa kati ya Tanganyika huru na mataifa ya kigeni, yakiwemo mataifa yaliyokuwa yakiitawala. Uhusiano huu ulijengwa katika misingi ya kimaadili iliyolenga kuimarisha umoja wa kitaifa, kulinda uhuru, kujitegemea na kuheshimu haki za binadamu. Katika kipindi hicho cha uhuru wa Tanganyika na mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Tanzania ilijipambanua kama taifa lenye msimamo huru katika uhusiano wake na mataifa mengine.
Zoezi la marudio
1. Eleza sababu za wakoloni kutoanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa katika maeneo ya Tanzania wakati wa ukoloni.
2. Linganisha hali ya utoaji wa huduma za jamii wakati wa utawala wa Wajerumani na Waingereza katika jamii za Kitanzania.
3. Fafanua namna ambavyo sera za utawala wa Wajerumani na Waingereza zilivyokinzana na maadili ya jamii za Kitanzania.
4. Jamii za sasa za Tanzania zinaweza kujifunza nini kuhusu usimamizi wa rasilimali na utawala kutoka kwa Wajerumani na Waingereza?
5. Kwa kurejelea utoaji wa huduma za kijamii wakati wa ukoloni, pendekeza namna bora ya kuboresha utoaji wa huduma za kijamii katika Tanzania ya sasa.
6. Tofautisha utoaji wa huduma za jamii wakati wa sasa na ule wa utawala wa Wajerumani na Waingereza.
www.learninghubtz.co.tz