KISWAHILI KIDATO CHA PILI

MADA KUU: UUNDAJI WA MANENO:

Mada ndogo:

  • Dhana ya uundaji wa maneno
  • Mazingira yanayosababisha mahitaji ya maneno mapya.
  • Dhana ya mofimu

Kueleza dhana ya mofimu.

Kuunda maneno kwa kutumia:-

1. Uambishaji

  • Dhana ya uambishaji
  • Dhima ya uambishaji.

2. Unyambulishajij

  • Dhana ya unyambulishaji
  • Dhima ya unyambulishaji.

DHANA YA UUNDAJI WA MANENO

Uundaji wa maneno ni sanaa ambayo amekuwa nayo mwanadamu tangu alipopata na kuannza kutumia lugha. Uundaji wa maneno ni mbinu ya utengenezaji wa maneno mapya ambayo yatakidhi haja ya mawasiliano katika lugha.

Katika lugha ya kiswahili, uundaji wa maneno umekamilika kiumbo na umejitosheleza kimaana. Maneno huundwa kwa vipashio vijulikanavyo kama mofimu.

MAZINGIRA YANAYOSABABISHA MAHITAJI YA MANENO MAPYA:

Yapo mazingira mbalimbali yanayopelekea mahitaji ya maneno mapya. Yafuatayo ni baadhi ya mazingira hayo:-

(i) Kukidhi haja ya mawasiliano katika muktadha maalumu.

Hapa inamaanisha watumiaji wa lugha katika muktadha fulani wanasukumwa kuunda maneno mapya baada ya jambo/tukio fulani kufanyika. Mfano neno “chakachua” limeundwa baada ya tabia ya kuchanganya mafuta ya dizeli na aina nyingine za mafuta kama vila mafuta ya taa au petrol.

(ii) Maendeleo ya sayansi na teknolojia;

Ugunduzi wa mambo mapya ya kitaalam, kunasababisha uundaji wa maneno utakaotumika katika taaluma husika. Mfano, maneno kama vile kisimbusi, kidhibiti, mwendo, king’amuzi, ungo, simu ya mkononi na mtandao ni maneno yaliyopatikan baada ya ugunduzi wa teknolojia mpya.

(iii) Matukio mbalimbali.

Matukio mbalimbali husababisha uundwaji wa maneno mapya. Kwa mfano, vita vya kagera vimepelekea uundaji wa maneno kama vile nduli, dada, mtutu na fashisti.

(iv) Biashara mbalimbali.

Mazingira ya kibiashara husababisha uundwaji wa maneno mapya. Kwa mfano maneno kama vile machinga, ushuru, risiti, mama lishe na kodi yameingia kwenye msamiati rasmi wa kiswahili kutokana na maendeleo ya biashara.

(v) Siasa na utawala.

Siasa na utawala vimesababisha uundaji wa maneno mapya. Kwa mfano, maneno mpambe, bajeti, hotuba, bunge na upinzani yameingia katika msamiati rasmi wa kiswahili.

(vi) Hivyo basi, haya ni baadhi tu ya mazingira yanayopelekea uwepo wa lugha ya uundaji wa maneno mapya katika lugha ya kiswahili, kufanikisha maendeleo ya dhana mbalimbali.

MOFIMU:

Mofimu ni kipashio kidogo cha lugha chenye kubeba maana. Vipashio vingine vya lugha ni neno, kirai, kishazi na sentensi.

Vilevile, tunaweza kusema kwamba mofimu ni kipashio kidogo kabisa cha kimaumbo chenye maana ama ya kileksika ni hali ya mofimu kusimama kama kidahizo kwenye kamusi. Mfano: maneno kama baba, cheza, soma, vuta, shangazi, toto, baya, chafu, ni mofimu za kileksika kwani zinaweza kusimama peke yake kama vidahizo kwenye kamusi.

Mofimu kuwa na maana ya kisarufi ni hali ya mofimu kubainisha kategoria mbalimbali kama vile, nafsi, idadi, kauli, njeo na ngeli.

Kwa mfano:

-wa- = Idadi (wingi) nafsi ya tatu wingi

-li- = Njeo iliyopita

-ni- = Mtendwa, wingi

-pig- = Mzizi wa neno

-a- = Mofimu tamati.

AINA ZA MOFIMU:

  • Mofimu zimegawanyika katika aina kuu mbili, nazo ni:-

(i) Mofimu huru

(ii) Mofimu tegemezi.

I. MOFIMU HURU:

Mofimu huru ni mofimu ambazo husimama peke yake bila kutegemea mofimu nyingine.

Mfano wa mofimu huru ni kama vila toto, baya, shangazi, mama, simu, chama, chombo, kaka na saa.

Kitu cha msingi hapa mtumiaji na mjifunzaji wa lugha, anapaswa kuepuka kuchanganya dhana ya mofimu huru na mofimu za kileksika.

II. MOFIMU TEGEMEZI:

Mofimu tegemezi ni mofimu ambazo zinategemea mofimu nyingine kukamilisha muundo wa neno na kutoa maana. Mifano ya mofimu tegemezi ni hizi zifuatazo:-

Wanaimba – wa-na-imb-a, mofimu wa-,-na-,-imb- na –a ni mofimu tegemezi kwani zinategemeana katika muktadha wa neno wanaimba.

MZIZI, MASHINA NA VIAMBISHI:

I. MZIZI:

Mzizi ni umbo la msingo la neno ambalo hutumika katika kuundia maneno mengine. Pia tunaweza kueleza dhana ya mzizi kwamba ni sehemu inayobakia baada ya viambishi vyote awali na tamati kuondolewa.

Mfano:

Neno

Mzizi

Kiambishi tamati

  • Cheza

-chez-

a

  • Zama

-zam-

a

II. VIAMBISHI:

Kiambishi ni kipashiio / kipande cha neno ambayo hupachikwa kabla na baada ya mzizi wa neo ili kukamilisha muundo wa neno

Mfano:

Neno

Kiambishi awali

mzizi

Kiambishi tamati

Mtoto

Mzazi

-m-

-za-

-zi

Msomi

-m-

-som-

-i

Anacheza

A, na

-chez-

-a

Zipo aina mbili za viambishi navyo ni viambish awali na viambishi tamati.

III. MASHINA:

Shina ni sehemu ya neno yenye muunganiko wa mzizi na kiambishi anghalabu kiambishi tamati.

Mfano:

Neno

Kiambishi awali

mzizi

Kiambishi tamati

Shina

Walimu

wa

-alim

-

alimu

Mjuzi

m

-ju-

-zi

jua

Wakazi

wa

-ka-

-zi

kaa

Unakula

u, na, ku

-l-

-a

la

DHIMA ZA MOFIMU:

Mofimu ina dhima zifuatazo:

(i) Kuzalisha maneno mapya; mfano, kutokana na mzizi –lim-, tunapata maneno mbalimbali baada ya kupachika mofimu kabla na baada ya mzizi huo –lim-. Maneno hayo ni kama vile analima, unalima, mnalima, tutalima na kilimo.

(ii) Kuonesha idadi na ngeli, mfano,

Umoja

Wingi

Mtoto

Watoto

(A – wa)

Kijiji

Vijiji

(Ki – vi)

Mwalimu

walimu

(A – wa)

(iii) Kuonyesha njeo mbalimbali

Mfano:

a) Anafundisha

-na- = Njeo ya wakati uliopo

b) Tutafaulu

-ta- = Neo ya wakati ujao

c) Mlimuona

-li- = Njeo ya wakati uliopita.

(iv) Kubainisha kauli mbalimbali

Mfano:

a) Somea: -e- = Kauli ya kutendea

b) Onwa: –w- = Kauli ya kutendwa

c) Saidiana: -an- = Kauli ya kutendana.

(v) Kubainish hali mbalimbali

Mfano: Hali ya masharti.

a) Wakifaullu: -ki- = masharti yanayowezekana.

UAMBISHAJI:

Uambishaji ni upashikaji wa viambishi kwenye mzizi wa neno. Vipashio vinavyopachikwa kwenye mzizi wa neno huitwa viambishi. Katika dhana ya uambishaji, viambishi hupachikwa kabla na baada ya mzizi wa neno huitwa viambishi awali na viambishi vinavyopachikwa baada ya mzizi wa neno huitwa viambishi tamati.

Mfano:

(i) Analima – a – na – lim – a

Kwahiyo:

-a- = kiambishi awali

-na- = kiambish awali

-lim- = mzizi

-a- = kiambishi tamati.

(ii) Mkulima – m – ku – lim – a

Kwahiyo:

-m- = kiambishi awali

-ku- = kiambishi awali

-lim- = mzizi

-a- = kiambishi tamati.

DHIMA ZA UAMBISHAJI:

Uambishaji una dhima mbalimbali, zifuatazo ni baadhi ya dhima za uambishaji:-

(i) Kuonesha mtenda.

Mfano, anafagia

A - = Kiambishi awali, cha mtenda nafsi ya tatu umoja.

(ii) Kuonesha ngeli na idadi

Mfano, Mtoto – Watoto

M- = Kiambishi awali, ngeli ya kwanza umoja.

Wa- = kiambishi awali, ngeli ya kwanza wingi

(iii) Kuonyesha nafsi.

Mfano, umemaliza

U- Kiambishi awali cha nafsi ya pili umoja

Tulipanda

Tu- Kiambishi awali cha nafsi ya kwanza wingi

(iv) Kuonesha ukanushi

Mfano, Hachezi

Ha- Kiambishi awali cha ukanushi, nafsi ya tatu umoja

Huwezi.

Hu- Kiambishi awali cha ukanushi nafsi ya pili umoja.

(v) Kubainisha kauli mbalimbali.

Mifano:

Pigwa-

-w- Kiambishi tamati cha kauli ya kutendwa

Somesha –

-sh- Kiambishi tamati cha kauli ya kutendesha.

MIFANO YA UUNDAJI WA MANENO KWA UAMBISHAJI.

Unda maneno mapya kwa kutumia uambishaji wa mizizi ifuatayo:

Mzizi

Maneno mapya

-li-

Lala, lalika, lalia, lalisha

-fik-

Fika, fikia, fikwa, fikisha

-vun-

Vuna, vunwa, anavuna.

-f-

Amefariki, anakufa, wanakufa

-on-

Tumeonwa, ameniona, onesha

UNYUMBULISHAJI

Unyumbulishaji ni upashikaji wa mofimu baada ya mzizi wa neno ili kuunda neno jipya na kulirefusha.

Mfano:

Mzizi

Unyambulishaji

Viambishi nyambulishi.

-pig-

Pigwa, pigana

-w-, an-

-zim-

Zimwa, zimika

-w-, ik-

-shik-

Shikwa, shikana

-w-, -an-

Dhima ya unyambulisha

Dhima kuu ya unyambulisha ni kuunda maneno mapya. Maneno mapya huundwa kwa kubainishwa kauli mbalimbali.

Mfano: Maneno kama vile chezea, pakiwa, fundishwa, valisha na pigia yamenyambulishwa baada ya kupashikwa viambishi nyambulishi. –e-, iw, -w-, -lish- na –i-

www.learninghubtz.co.tz

MASWALI YA MADA. MADA YA KWANZA.

MADA: UONGEZAJI WA MSAMIATI:

A: CHAGUA HERUFI YA JIBU SAHIHI.

  1. Neno “Kizibo” limeundwa kutokana na njia ya uundaji wa maneno iittwayo:-
  1. Kuambatanisha maneno
  2. Kubadili mpangilio wa maneno
  3. Kuangalia kazi ya kitu.
  4. Kubadili mpangilio wa neno.
  1. Ipi orodha ya maneno ambayo yameundwa kwa njia ya utohoaji wa maneno?
  1. Bendera, meza, beseni na pesa.
  2. Shuka, saa, doti na kigoda.
  3. Bajia, leso, waya na ikulu.
  4. Namba, elimu, papaya na ng’atuka.
  1. Ipi kati ya njia zifuatazo za uundaji wa maneno si njia sahihi ya uundaji wa maneno.:-
  1. Uambishaji.
  2. Kutohoa.
  3. Kuambatanisha maneno.
  4. Kutafsiri.
  1. Lipi kati ya maneno yafuatayo limeundwa kwa njia ya kufananisha sauti?
  1. Malapa.
  2. Redio
  3. Kikunio.
  4. Shati.

B: JAZA NAFASI ZILIZO WAZI:

  1. Neno “Kikunio” limeundwa kutokana na njia ya uundaji wa maneno iitwayo__________
  2. Mfano wa neno lililoundwa kwa njia ya uambishaji ni ________________
  3. Maneno motomot, mbalimbali, sawasawa, yameundwa kwa njia ya______________
  4. Neno “Kipanya” limeundwa kutokana na njia ipi?_________________
  5. Njia mbili za uundaji wa maneno ni __________________ na ________________
  6. Mfano wa neno lililoundwa kwa kufupisha maneno ni ________________

C: MAJIBU YA MAELEZO MAREFU:

  1. Eleza namna maneno yaliyoundwa katika miktadha ya:

(i) Maendeleo ya kiuchumi

(ii) Maendeleo ya sayansi na teknolojia

(iii) Mabadiliko yo mfumo wa siasa

(iv) Maendeleo ya mfumo wa tiba

(v) Maendeleo ya kiutamaduni.

  1. Eleza umuhimu wa kuongeza msamiati katika lugha. Toa oja tano.

LEARNINGHUBTZ.CO.TZ Page 1

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256