Sura ya 01 : Dhana ya Historia ya Tanzania na Maadili
Utangulizi Ni muhimu kuenzi, kudumisha na kuhifadhi historia ya Tanzania na maadil manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo. Katika sura hii, utajifunza maana ya historia ya Tanzania, maadili na uhusiano kati ya somo Historia na Maadili na masomo mengine. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuthamini historia ya Tanzania, maadili na uzalendo na kueleza uhusiano kati ya somo la Historia ya Tanzania na Maadili na masomo mengine. |
Fikiri kuhusu somo la Historia ya Tanzania na Maadili. |
Historia ya Tanzania na Maadili
Somo la Historia ya Tanzania na Maadili linaundwa na dhana kuu mbili. Dhana ya kwanza ni historia ya Tanzania na dhana ya pili ni maadili. Historia huhusu mambo au matukio yaliyopita yenye athari kubwa kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni katika jamii. Baadhi ya matukio hayo ni biashara ya watumwa, ukoloni na vita. Kwa mfano, ukoloni, si tu uliathiri utamaduni wa jamii pia ulileta utamaduni mpya katika jamii za Kitanzania. Kwa hiyo, historia ya Tanzania ni mfululizo wa matukio yaliyotokea nchini Tanzania yanayohusisha masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Historia hii inakumbusha mambo yaliyotokea katika jamii za Tanzania kwa lengo la kusaidia kuelewa tulikotoka, tulipo na kutafakari juu ya tunakokwenda. Historia ya Tanzania inazingatia mambo mbalimbali ambayo ni pamoja na:
(a) Makabila mbalimbali katika nchi hii yalivyoendeleza utamaduni wao na jinsi mwingiliano kati ya makabila ulivyojenga utamaduni wa kitaifa;
(b) Mabadiliko ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika jamii za Kitanzania, kama vile ya familia, elimu, na shughuli mbalimbali za kiuchumi katika jamii za Kitanzania;
(c) Umuhimu wa kujenga utambulisho na mshikamano wa kitaifa kwa kuunganisha tofauti za kikabila na kidini;
(d) Utambuzi wa umuhimu wa kuwa na umoja na ushirikiano kama taifa;
(e) Maendeleo ya kiuchumi kutokana na kilimo na biashara za kijadi hadi uchumi wa kisasa;
(f) Ukuaji na mabadiliko ya uchumi wa nchi katika vipindi mbalimbali na jinsi maendeleo hayo yalivyoathiri maisha ya jamii za Kitanzania; na
(g) Kudumisha utamaduni, amani na ushirikiano kati ya makabila na dini mbalimbali.
Kazi ya kufanya 1.1 Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali vya taarifa ikiwamo maktaba mtandao na bainisha mambo yanayoweza kufundishwa katika somo la Historia ya Tanzania na Maadili |
Zoezi la 1.1
1. Fafanua matukio mbalimbali ya kihistoria unayoyafahamu kuhusu Tanzania.
2. Kwa nini ni muhimu kujua historia yetu?
3. Eleza ni kwa namna gani historia ya Tanzania ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
4. Kwa nini kujifunza na kuelewa historia ya Tanzania na maadili kunawezesha kujenga uzalendo?
5. Kwa jinsi gani historia ya Tanzania na maadili inachangia katika kujenga utambulisho wa kitaifa?
Dhana ya maadili
Maadili ni miongozo inayotawala tabia na matendo ya mtu mmojammoja au jamii kwa ujumla. Ni miongozo au maelekezo ya mienendo na matendo mema au kuwa na tabia njema. Katika muktadha huu neno maadili pia huashiria jitihada za kujua vigezo vya matendo yanayofaa na yasiyofaa katika jamii inayohusika.
Neno maadili linapotumika huweza pia kuashiria au kumaanisha tunu za jamii au taifa. Kwa mfano, uhuru na amani ni tunu za taifa letu na mtu au kikundi cha watu kinapovunja amani au kubana uhuru na haki za binadamu, huwa tunasema wamevunja maadili au hawana maadili. Vilevile, maadili hujumuisha ushirikiano na mshikamano. Ushirikiano na mshikamano ni nyenzo muhimu katika jamii za Kitanzania kwani huimarisha jamii na kuboresha maisha ya watu.
Ushirikiano na mshikamano hujidhihirisha kupitia kusaidiana katika kazi mbalimbali, matukio ya kijamii, na kusaidia majirani wakati wa matatizo. Aidha, jamii za Kitanzania ni maarufu kwa ukarimu kwa wageni. Wageni hukaribishwa kwa furaha na kupewa heshima kubwa ikiwa pamoja na kukirimiwa kwa chakula na malazi. Hivyo, ukarimu ni sehemu muhimu ya maadili ya Kitanzania.
Umuhimu wa maadili kwa taifa unaweza kutazamwa katika mambo yafuatayo:
(a) Kutambulisha utu wetu;
(b) Kukuza na kuendeleza uhusiano wa karibu miongoni mwa watu;
(c) Kujenga heshima na uaminifu miongoni mwa watu;
(d) Kujenga uhusiano miongoni mwa watu na mazingira yao;
(e) Kuleta maendeleo;
(f) Kujenga amani;
(g) Kupunguza uhalifu na kuimarisha utii wa sheria; na
(h) Upatikanaji wa haki, usalama na furaha katika jamii.
Kazi ya kufanya 1.2 Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali ikiwamo maktaba mtandao na andika umuhimu mwingine wa historia ya Tanzania na maadili. |
Zoezi la 1.2
1. Ungepewa nafasi ya kuongoza klabu ya kusimamia maadili shuleni, ni mambo gani ungependa yajadiliwe kuhusu maadili?
2. Unadhani ni vitu gani vinachangia kujenga tabia njema?
3. Eleza uhusiano uliopo kati ya historia na maadili.
4. Una ushauri gani kuhusu ujenzi wa maadili kwa watoto na vijana?
5. Bainisha matendo ya kimaadili unayotenda au kutendewa na wenzako shuleni?
Kwa muktadha huu, dhana za historia na maadili zimetawala katika somo hilizikitambulisha matukio yaliyopita ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi; miongozo, taratibu na kanuni zilizotawala tabia na matendo ya jamii za Kitanzania. Pia, dhana hizi zitawezesha kutambua kutoka katika historia ya taifa letu, maelekezo na fikra za kutuwezesha kutenda matendo mema au kuwa na tabia nzuri. Kwa maneno mengine, dhana za historia na maadili zinaelekeza kutambua vigezo vya matendo mema na mabaya katika jamii za Kitanzania za zamani na sasa, hivyo kuwezesha kujifunza au kujua maadili ya jamii ya Kitanzania za kale na za sasa.
Umuhimu wa somo la Historia ya Tanzania na Maadili
Kuna umuhimu wa kusoma somo la Historia ya Tanzania na Maadili. Baadhi ya umuhimu huo ni kama ifuatavyo:
(a) Kuelewa tulikotoka na tulipo na kutafakari kuhusu tunakotaka kwenda kama taifa;
(b) Kubaini mila, desturi na maadili yaliyojengwa na jamii za asili za Tanzania ili kurithisha vizazi vya sasa na vijavyo;
(c) Kujenga moyo wa kuipenda, kuilinda na kuithamini nchi ya Tanzania na kujenga uhusiano mwema baina ya jamii mbalimbali;
(d) Kufahamu vyema asili na maadili ya jamii za Kitanzania;
(e) Kuchambua maendeleo ya jamii za Tanganyika na Zanzibar kabla, wakati na baada ya ukoloni;
(f) Kujenga utu, heshima, uaminifu na amani miongoni mwa Watanzania; na
(g) Kukuza maadili na utii wa sheria kwa kujiepusha na vitendo vya uhalifu kama vile rushwa.
Kazi ya kufanya 1.3 Andika insha kuhusu matendo yasiyo ya kimaadili katika jamii yako huku ukipendekeza mikakati ya kukabiliana na matendo hayo. |
Uhusiano kati ya somo la Historia ya Tanzania na Maadili na masomo mengine
Somo la Historia ya Tanzania na Maadili lina uhusiano na masomo mengine kwa kuwa matukio ya kihistoria na maadili ya jamii huenda sambamba na matukio mengine yahusuyo taaluma zingine. Baadhi ya masomo yenye uhusiano na somo la Historia ya Tanzania na Maadili ni kama ifuatavyo:
Jiografia: Somo la Historia ya Tanzania na Maadili linahusiana na somo la Jiografia hasa katika mazingira. Mazingira ya kijiografia yanaweza kuathiri shughuli za binadamu kama vile biashara, utamaduni, kilimo na uhamaji wa watu. Hivyo, jiografia hutusaidia kufafanua mazingira ambapo matukio ya kihistoria na maendeleo ya jamii yalitokea. Zaidi ya hayo, mazingira kama sehemu ya jiografia yanategemea maadili kwani bila maadili mazingira hayawezi kutunzwa vizuri na hatimaye yanaweza huharibika. Kwa mfano, kukata miti hovyo na kuchoma misitu ni uharibifu wa mazingira na ni ukiukaji wa maadili. Pia, uchimbaji madini bila kuzingatia athari za kimazingira ni ukiukaji wa maadili.
Hisabati: Somo la Historia ya Tanzania na Maadili linahusisha matumizi ya takwimu na tafsiri zake kuhusu matukio ya zamani. Hisabati inaweza kutumiwa kuchambua takwimu za kihistoria na maadili. Vilevile, takwimu lazima ziwe na faida kwa binadamu na zifuate maadili ya jamii inayohusika, kwa mfano, kutunza siri za watu wakati wa kukusanya takwimu hizo.
Kiswahili na Kiingereza: Lugha hizi ni muhimu katika kusoma na kuelewa vyanzo vya kihistoria maadili na maandiko mbalimbali yaliyoandikwa kuhusu historia ya Tanzania na maadili. Lugha hizi husaidia kueneza na kuhifadhi maarifa ya kihistoria na maadili ya jamii. Isitoshe lugha ndizo zinaeleza maadili ya jamii kwa sababu bila lugha mawasiliano hayawezekani.
Chakula na Lishe: Somo la Historia ya Tanzania na Maadili lina uhusiano wa karibu na chakula na lishe kwa sababu huchangia katika kuelewa asili ya vyakula, mabadiliko ya mitindo ya kula katika jamii, na jinsi tabia za kula zinavyoathiri afya ya binadamu na mazingira. Zaidi ya hayo chakula kisichotumiwa kwa kufuata maadili kinakuwa hatari kwa binadamu. Kwa mfano, ni kinyume cha maadili kupikia mafuta yaliyopita muda wake wa matumizi au kampuni kudanganya bidhaa yake ina vitamini na madini zaidi kuliko uhalisia ili kuwavutia wateja. Vilevile, kuvua, kuuza na kula samaki waliovuliwa kwa njia ya sumu ni kinyume cha maadili na huathiri afya na mustakabali wa jamii.
Sanaa na Michezo: Sanaa na michezo ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Tanzania na inaathiriwa na historia na maadili ya jamii katika zama mbalimbali. Kuelewa historia ya sanaa na michezo kunaweza kutusaidia kufahamu jinsi utamaduni wa Kitanzania ulivyokua na kubadilika kupitia sanaa na michezo katika vipindi tofauti. Pia, sanaa na michezo huongozwa na maadili, kama vile kutunza vifaa na viwanja vya michezo na ushindani wa haki. Mifano ya kukosa maadili katika sanaa na michezo ni pamoja na kutozingatia miiko na utamaduni wa jamii kama vile kutumia lugha isiyo na staha, kuvaa nguo zisizo na staha au kuvua nguo jukwaani na michezoni na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni.
Muziki: Muziki umekuwa sehemu ya historia tangu enzi ya mababu. Kupitia historia ya muziki, tunajifunza jinsi ambavyo muziki umekuwa chombo cha kuelimisha, kuburudisha, na kufahamisha kuhusu matukio mbalimbali ya kihistoria na maadili ya jamii. Kupitia muziki, maadili yamefundishwa na kujenga tabia za watu kama upendo, heshima na kujali wengine.
Kilimo: Somo la Historia ya Tanzania na Maadili lina uhusiano na kilimo kwa kuwa kilimo ni sehemu ya mila na desturi za jamii za asili za Kitanzania na za sasa. Kilimo kimekuwa sehemu muhimu ya utamaduni na mila za Kiafrika. Taarifa za kihistoria zinaonesha jinsi shughuli za kilimo zinavyoingiliana na mila na desturi za kijamii kutoka enzi za kale. Kilimo kisichofuata maadili huharibu mazingira na kutokuwa na faida kwa binadamu. Mfano wa kilimo kisichozingatia maadili ni kulima kwenye vyanzo vya maji na kuchoma misitu. Kwa ujumla, somo la Historia ya Tanzania na Maadili linahusiana na masomo mengine kwa kuwa hutoa ufahamu wa kina juu ya utamaduni, maadili, mazingira, na maendeleo ya jamii ya Tanzania katika nyakati tofauti za kihistoria.
Kazi ya kufanya 1.4 Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali na andika maelezo ya ziada kuhusu uhusiano wa somo la Historia ya Tanzania na Maadili na masomo mengine |
www.learninghubtz.co.tz
Zoezi la marudio
1. Eleza sababu za kujifunza historia ya Tanzania na maadili.
2. Fafanua uhusiano uliopo kati ya somo la Historia ya Tanzania na Maadili na masomo ya Kiswahili na Jiografia.
3. Nje ya sababu zilizotajwa katika sura hii, unafikiri ni sababu gani zingine za kujifunza somo hili?
4. Nini matarajio yako katika kujifunza somo hili?