Sura 01 : Lugha na mawasiliano
Utangulizi
Lugha ni chombo kikuu cha mawasiliano ya binadamu. Katika sura hii, utajifunza dhana na umuhimu wa lugha ya Kiswahili. Vilevile, utajifunza namna ya kuwasiliana kwa kutumia lugha fasaha na kutofautisha lugha fasaha na isiyo fasaha katika mazungumzo na maandishi. Utasoma matini za Kiswahili kwa kuzingatia matamshi, lafudhi, mkazo, na kiimbo sahihi. Pia, utafanya uchanganuzi wa vipengele vya sarufi ya Kiswahili kwa kuzingatia ufasaha wa lugha. Umahiri utakaoujenga utakuwezesha kuwasiliana kwa Kiswahili fasaha katika miktadha mbalimbali.
Dhana ya lugha
Kazi ya 1.1
Soma shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.
Nataka nena na wewe, upate kunielewa,
Wengi washikwa kiwewe, kwa kushindwa nielewa,
Yapaswa unielewe, nimekwishakubaliwa,
Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha.
Huwezi kuwazuia, waliokubaliana,
Mimi wananitumia, wapate kuelewana,
Kanuni wazingatia, ili kuwasiliana,
Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha.
Mfumo wangu makini, sauti kupangilia,
Maneno kuyatumia, yenye mpango sawia,
Sentensi kuzitumia, mawazo kupangilia,
Sauti zangu nasibu, hakuna wa kukanusha.
Maswali
1. Mwandishi anazungumzia nini katika shairi ulilosoma?
2. Ni nani waliokubaliana kuwasiliana kwa kutumia hicho alichokizungumzia mwandishi katika ubeti wa pili wa shairi?
3. Ni mambo gani matatu yaliyojumuishwa na mwandishi katika mfumo wa jambo alilozungumzia?
4. Unafikiri kwa nini mstari wa mwisho wa kila ubeti umerudiwarudiwa na mwandishi katika shairi hilo?
Kazi ya 1.2
Maneno yafuatayo yameandikwa kwa kuchanganya herufi. Chunguza maneno hayo, kisha jibu maswali yanayofuata.
1. luagh
2. anomasiwali
3. unabidam
4. ribaha
Maswali
1. Je, maneno hayo yana makosa gani?
2. Kuna changamoto gani katika kusoma maneno hayo?
3. Nini kifanyike ili maneno hayo yaweze kusomeka vizuri na kuleta maana?
4. Andika maneno hayo kwa usahihi.
5. Kutokana na uelewa ulioupata, lugha hufasiliwaje?
Zingatia
Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo zimebuniwa na kukubaliwa na jamii ya watu ili zitumike katika mawasiliano baina yao. Mfumo huo hujumuisha sauti, silabi, neno, na sentensi. Ili watu au jamii iweze kuwasiliana, sharti lugha inayotumika iwe inaeleweka vizuri kwa kuwa lugha ni chombo cha mawasiliano. Unapowasiliana kwa kutumia lugha ya Kiswahili ni muhimu kuzingatia kiimbo,
mkazo, matamshi na lafudhi sahihi.
Dhana ya mawasiliano
Kazi ya 1.3
Chunguza kielelezo cha mfumo wa mawasiliano, kisha jibu maswali yanayofuata.
Kielelezo namba 1.1: Mfumo wa mawasiliano |
Maswali
1. Kwa kutumia kielelezo cha mfumo wa mawasiliano, bainisha njia kuu mbili za mawasiliano unazoweza kutumia unapowasiliana kwa kutumia lugha.
2. Njia ulizozibainisha katika swali la 1 zinaweza kutumia vifaa gani vya mawasiliano kati ya vifaa vilivyobainishwa katika kipengele cha 3 katika kielelezo ulichopewa?
3. Bainisha vifaa vingine vya mawasiliano unavyoweza kutumia katika kuwasiliana.
4. Kwa kutumia kielelezo ulichopewa, eleza jinsi mchakato wa mawasiliano unavyofanyika.
5. Unafikiri ni mambo gani yanaweza kukwamisha mawasiliano unapotumia lugha?
Zingatia
Mawasiliano ni upashanaji habari au taarifa kwa njia mbalimbali. Mawasiliano hukamilika iwapo tu taarifa inayotolewa inaleta maana iliyokusudiwa. Binadamu huwasiliana kwa kutumia lugha. Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari. Katika mawasiliano lugha inaweza kuleta athari ama chanya au hasi. Lugha inaweza kumtambulisha mtumiaji wa lugha inayohusika, utamaduni wake na kubainisha hisia alizonazo. Pia, kwa kutumia lugha, mtu au jamii hupata maarifa kuhusu mambo mbalimbali. Maarifa hayo hupatikana ama kupitia lugha ya mazungumzo au lugha ya maandishi. Pamoja na hayo, lugha ikitumika vibaya,
inaweza kukwamisha mawasiliano au kuleta mgongano kwa watumiaji wake.
Ili mawasiliano yafanyike kwa ufanisi ni lazima pawe na mtoa ujumbe, ujumbe wenyewe, midia ambayo hubeba ujumbe, na mpokeaji wa ujumbe unaohusika. Aidha, ili mawasiliano yaweze kukamilika, sharti mpokeaji wa ujumbe atoe mrejesho kwa mtoa ujumbe.
Dhana ya lugha ya Kiswahili
Kazi ya 1.4
Soma habari ifuatayo, kisha jibu maswali yanayofuata.
Kiswahili ni lugha ya Kibantu inayozungumzwa kama lugha mama au lugha ya pili katika ukanda wa pwani ya Mashariki mwa Afrika. Pia, huzungumzwa kama lugha ya pili maeneo mengine ya Afrika Mashariki. “Kibantu” ni jina jumuishi linalotumika kutaja lugha zote zinazotumia maneno yanayoishia na –tu (au –ntu, -nthu, -nu, n.k) kurejelea mtu au watu. Kwa hiyo, hakuna lugha maalumu ijulikanayo kama Kibantu. Watu wanaozungumza Kiswahili kama lugha mama hujulikana kama Waswahili. Hata hivyo, jina hili linarejelea lugha yao tu na siyo kabila kwani hakuna kabila la Kiswahili wala Waswahili. Kiswahili kinatumika
Tanzania na Kenya kama lugha ya Taifa.
Nchini Tanzania, Kiswahili hutumika pia kama lugha ya kufundishia elimu ya msingi na vyuo vya ualimu elimu ya msingi. Aidha, lugha hii hufundishwa kama somo kuanzia ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu. Kwa upande wa Kenya na Uganda, Kiswahili ni lugha ya pili sanjari na Kiingereza. Nchini Kongo (Kinshasa), Kiswahili ni mojawapo ya lugha nne za utawala, lugha kuu ikiwa Kifaransa. Pamoja na kwamba Kiswahili ni lugha ya Kibantu, baadhi ya maneno katika lugha hii yamekopwa kutoka katika lugha mbalimbali kama vile, Kiarabu,
Kireno na Kiingereza. Inasemekana kwamba kuna lahaja kuu 15 za Kiswahili zinazotumika ingawa tafiti bado zinaendelea. Kwa upande wa Afrika Mashariki, lahaja zinazojulikana sana ni Kiunguja (kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Unguja) ambacho ndicho kilisanifishwa na kuwa Kiswahili Sanifu; Kipemba (kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Pemba); Kitumbatu (kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Tumbatu); Kimvita (kinachozungumzwa Mombasa); na Kiamu (kinachozungumzwa katika Kisiwa cha Lamu huko Kenya). Pamoja na lahaja zote hizo, Kiswahili Sanifu ndicho hufundishwa shuleni.
Maswali
1. Kwa nini Kiswahili kinazungumzwa kama lugha ya pili katika ukanda wa pwani ya Mashariki mwa Afrika?
2. Unaelewa nini kuhusu lugha mama?
3. Mwandishi ana maana gani anaposema, ‘‘... hakuna lugha maalumu inayojulikana kama Kibantu?’’
4. Ni nchi zipi zinatumia Kiswahili kama lugha ya taifa?
5. Je, ungepewa nafasi ya kupendekeza kuwa Kiswahili kitumike au kisitumike kama lugha ya kufundishia masomo ya ngazi ya sekondari hadi elimu ya juu ungependekeza nini na kwa sababu gani?
Kazi ya 1.5
Chunguza maneno ya Kiswahili, kisha andika maneno kumi (10) ambayo yamekopwa kutoka katika lugha mbalimbali.
Umuhimu wa kujifunza Kiswahili
Kazi ya 1.6
Soma sehemu ya mahojiano baina ya Mwandishi wa habari na Mwalimu, kisha jibu maswali yanayofuata.
Mwandishi: Baadhi ya watu hawaoni umuhimu wa kujifunza Kiswahili. Wewe una maoni gani?
Mwalimu: Kwa kweli, hayo ni mawazo potofu. Tuelewe kuwa lugha ya Kiswahili nchini Tanzania hutumika kufundishia masomo yote katika shule za msingi na vyuo vya ualimu elimu ya msingi vinavyotumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia. Hii inawasaidia wanafunzi wengi kuelewa masomo hayo kwa urahisi kwa kuwa wanafundishwa kwa lugha wanayoifahamu zaidi. Pia, Kiswahili hufundishwa kama somo katika elimu ya sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.
Mwandishi: Sawa. Je, kuna mahali kwingine ambako Kiswahili kinafundishwa?
Mwalimu: Ndiyo. Kiswahili kinafundishwa katika shule na vyuo vikuu vya nchi zingine za Afrika, na hata katika baadhi ya vyuo vikuu vya nchi mbalimbali za nje ya Afrika kama vile, Marekani, Uingereza,
Ufaransa, Ujerumani, China, Japani, na kadhalika.
Mwandishi: Mbali na umuhimu huo, kuna umuhimu mwingine?
Mwalimu: Ndiyo. Lugha ya Kiswahili inatumika kuwaunganisha Watanzania wote. Tanzania inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni hamsini wenye makabila tofauti lakini wanaunganishwa na lugha
ya Kiswahili kwa mawasiliano. Aidha, Kiswahili kinachangia katika kukuza uchumi, amani, na utulivu nchini na katika nchi jirani. Isitoshe, wakati wa kupigania uhuru, lugha ya Kiswahili ilitumika kama chombo muhimu cha umoja wa kimawasiliano.
Mwandishi: Kwa kweli, unanikumbusha mbali mwalimu. Naomba uendelee kunieleza zaidi.
Mwalimu: Lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi. Inatumika katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kiserikali kama vile katika mahakama, bunge na elimu. Vilevile, Kiswahili kama lugha ya taifa hutumika kama utambulisho wa taifa. Kwa hiyo, Kiswahili kina nafasi kubwa katika nyanja zote za maendeleo ya taifa.
Mwandishi: Kiswahili kina hadhi gani kimataifa?
Mwalimu: Kiswahili kimepata hadhi ya kutumika kimataifa. Hii ndiyo lugha pekee ya Kiafrika ambayo imesambaa zaidi kuliko lugha zingine. Hivyo, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuleta umoja barani Afrika. Ikumbukwe kwamba, Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika iliyopendekezwa kutumika pia katika vikao vya Umoja wa Afrika sanjari na lugha zingine. Aidha, Kiswahili kinatumika
kama lugha rasmi katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Mwandishi: Ni fursa zipi ambazo Watanzania wanafaidika nazo kutokana na kupanda hadhi kwa lugha ya Kiswahili?
Mwalimu: Kiswahili hutoa fursa za ajira. Kwa mfano, baadhi ya Watanzania wenye taaluma ya kufundisha Kiswahili hujipatia fedha kutokana na kufundisha Kiswahili. Vilevile, kutokana na umuhimu wa Kiswahili kutumika nje ya nchi, baadhi ya nchi kama vile Afrika Kusini zimekuwa zikihitaji wataalamu wa Kiswahili kwenda kukifundisha katika nchi hizo.
Mwandishi: Sasa turudi kwa wanafunzi. Je, wanafunzi wanapojifunza somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari wanapata manufaa gani?
Mwalimu: Mwanafunzi akijifunza kikamilifu somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari, ataweza kuwasiliana kwa Kiswahili fasaha
katika nyanja mbalimbali za maisha, na kukithamini Kiswahili kama sehemu muhimu ya utamaduni wa Mtanzania. Vilevile, husaidia kujenga tabia ya udadisi na ubunifu katika masuala ya
lugha na fasihi ya Kiswahili, kuelewa, kuthamini na kutumia kazi za fasihi katika maisha. Aidha, ataweza kutumia lugha hii katika miktadha mbalimbali; kukuza na kukieneza Kiswahili ili kiweze kutumika katika mawasiliano kitaifa na kimataifa, na kujenga uwezo wa kujisomea maandiko mbalimbali ya Kiswahili. Pia, atapata msingi bora na imara wa kujifunza na kujiendeleza katika
taaluma za Kiswahili na kukitumia kupata maarifa, mwelekeo, na stadi za kijamii, kitamaduni, kiteknolojia, na kitaaluma.
Mwandishi: Mwalimu, ninakupa nafasi ya kumalizia suala hili la umuhimu kama una lolote la kuongezea ili tuingie kwenye kipengele kingine.
Mwalimu: Ndugu mwandishi, ninapenda kumalizia kwa kueleza kwamba lugha ya Kiswahili, kama zilivyo lugha zingine, inaweza kutumika kutolea maarifa na ujuzi wa taaluma mbalimbali kama vile habari
na mawasiliano, historia, na sayansi na teknolojia.
Mwandishi: Asante sana mwalimu kwa maelezo yako ya kina kuhusu umuhimu wa kujifunza Kiswahili.
Mwalimu: Asante na karibu tena.
Mwandishi: Shukurani.
Maswali
1. Kuna faida gani ya kutumia Kiswahili kufundishia masomo yote ya elimu ya msingi?
2. Fafanua, kwa kutoa mifano, umuhimu wa kujifunza Kiswahili.
3. Mwanafunzi akijifunza kikamilifu somo la Kiswahili katika elimu ya sekondari atapata faida gani?
4. Kwa nini mwandishi alimshukuru mwalimu?
5. Eleza faida na changamoto za kutumia Kiswahili kama lugha ya kujifunzia na kufundishia masomo yote katika ngazi ya sekondari.
Matamshi na lafudhi ya Kiswahili
Kazi ya 1.7
Soma kisa kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.
Zukwe ni kijana aliyeishi katika Kijiji cha Misike kilichoko katika Wilaya ya Nduna mkoani Shobo. Kijana huyo alipenda sana kushiriki mazungumzo na vijana wenzake yaliyokuwa yakifanyika kijiweni wakati wa jioni baada ya kazi. Kijiwe hicho kiliitwa Bunguabongo kwa sababu vijana wengi waliopendelea kwenda mahali pale walikuwa wakiibua mazungumzo yaliyokuza fikra na
kuwafanya wapate mwelekeo sahihi wa maisha.
Siku moja Zukwe baada ya shughuli zake za ufugaji, alitembelea kijiweni kama ilivyokuwa ada yake. Alikwenda mahali pale kwa ajili ya kubadilishana mawazo na wenzake. Alipofika, aliwakuta vijana wenzake wakijadiliana kuhusu suala la ajira kwa vijana. Kwa kuwa Zukwe alikuwa anapenda sana mijadala, alisogea karibu na kuanza kusikiliza kwa makini ili aweze kuchangia mada.
Mazungumzo yao yalikuwa hivi:
Tongoa: Mimi ninaona ajira ziko za aina nyingi tu ila baadhi ya vijana wenzetu hawapendi kujituma; au unasemaje Benjo?
Benjo: Kweli bwana! Kwa mfano, mimi nimeamua kufuga kuku. Wakati ninaanza shughuli hii, vijana wengi mlinidhihaki. Sasa ninaona mnanimezea mate kwa jinsi ninavyopata pesa kutokana na kuuza
mayai, kuku, na mbolea inayotokana na kuku. Zukwe, si ndiyo?
Zukwe: Haswaaa! Mimi pia nilikuwa kama wewe. Ntoto wa ndugu yangu alinicheka sana na kunizarau nilipoanza kufuga mbuzi. Alisema nimekosa kazi ya kufanya. Benjo, fikiria ntoto kama yule ananicheka mimi. Ni zarau sana; ingawa sasa ninawauzia mbuzi wa nyama wafanyabiashara wa hapa kijijini na mjini.
Shehena: Mmmh! Zukwe, umesema ntoto! Ni nani huyo? Nani anaitwa ntoto hapa kijijini? Pia, umesema zarau. Mimi sikuelewi bwana.
Chachu: Shehena vipi? Ntoto si jina la mtu wa hapa kijijini bwana. Zukwe anamaanisha mtoto wa ndugu yake. Eti jamani .... si ndivyo? (Wote wanacheka).
Funko: Ndivyo ilivyo Chachu. Sasa tuendelee na mazungumzo yetu. Mimi ninafikiri ajira ni tatizo. Hata wenzetu waliosoma wanakwendaga mjini wanapata kazi lakini siku hizi wengi wanabaki hapahapa kijijini. Pia, hapa kijijini ninawaonapo watu wengi wanakaa tu. Ndugu zangu ajira hakuna kabisa.
Ajala: Funko! Wanakwendaga ... ninawaonapo ...! Sema vizuri bwana. Mimi ninakubaliana na Benjo na Zukwe. Kazi za kufanya zipo nyingi. Vijana wengi tunapenda kazi za ofisini hata kama hatuna ujuzi nazo. Mtu anaweza kuajiriwa au kujiajiri kama walivyofanya wenzetu Zukwe na Benjo. Si lazima kufuga kuku kwani unaweza kujishughulisha na kilimo au biashara. Shughuli zote hizi zinaweza
kutuletea maendeleo. Tufanye kazi bwana! Bila kufanya kazi maisha ni magumu kweli.
Shaburi: Kwa kweri nimejifunza jambo hapa. Kurara badara ya kutafuta kazi ya kufanya kunasababisha maisha kuwa magumu. Ama kweri erimu haina mwisho. Mazungumzo haya yamenifungua
macho kabisa. Kumbe! Ninaweza kufuga, kurima au kufanya biashara nikapata kipato badara ya kuenderea kuwategemea wazazi wangu. Nadhani ningekuwa mbari kama ningeanzisha kirimo cha mbogamboga. Nani yuko tayari, tuanzishe kirimo cha mbogamboga.
Egeli: Haaaa! Shaburi, unauliza au unaeleza? Umesahau tulivyofundishwa shule ya msingi? Kwenye swali sharti uweke kiulizo bwana.
Shaburi: Tatizo rako wewe ni mikwara tu. Kwani hujanierewa?
Egeli: Sema vizuri ueleweke. Mbogamboga zinalipa kweli? Sidhani. Fanya biashara ya duka Shaburi.
Shaburi: Tatizo rako Egeri hufikirii mbari na hupendi kujishughurisha kama mimi. Mbogamboga zitaturipa sana, hasa tukirima wenyewe. Hapa kijijini maduka ni mengi tu. Tufikirie shughuri tofauti na hiyo; au mnasemaje jamani?
Zukwe, Tongoa na Benjo: Kweli bwana.
Zukwe: Mimi ninaweza kushirikiana na mtu yeyote anayetaka kufuga mbuzi wa nyama. Tunaweza kuwa na mradi mkubwa tukasambaza nyama katika masoko mbalimbali na kujipatia fedha. Jamani, naona Dageta hafurahishwi na mazungumzo yetu. Vipi Dageta una neno?
Dageta: Nimekasirika kwa sababu nimepata ujumbe wa simu wenye taharifa mbaya kutoka kwa mjomba kwamba bibi aliyemzaa mama amelazwa hospitalini.
Zukwe: Dageta, pole sana. Ina maana umekasirika kwa sababu hiyo? Kwa nini ukasirike kama bibi yako amelazwa?
Dageta: Du! Nimepitiwa jamani. Mnajua bibi amenilea tangu nikiwa mdogo. Sijakasirika bwana.
Chachu: Kwa hiyo, Dageta “amehuzunika.” Sidhani kama unaweza kukasirika kwa sababu ya ugonjwa. Dageta, pole sana rafiki yangu.
Dageta: Asanteni.
Zukwe: Mazungumzo yetu yalikuwa matamu kweli lakini giza limeingia. Kila lenye mwanzo halikosi kuwa na mwisho. Kikubwa hapa ni kufanya kazi kwa bidii ndugu zangu. Tumsindikize rafiki yetu
Dageta kwenda hospitalini. Mnaonaje?
Wote: Sawa. (Wakaondoka na kwenda hospitalini.)
Wakiwa njiani kuelekea hospitalini, Zukwe aliendelea kutafakari maarifa aliyoyapata kupitia mazungumzo yao. Alidhamiria kuboresha biashara yake ya mbuzi wa nyama na kuongeza mradi wa kilimo cha mbogamboga ili kujiongezea kipato. Kutokana na mazungumzo yale, Zukwe alipata hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Maswali
1. Kwa kuzingatia kisa ulichosoma, kuwasiliana ni kufanya nini?
2. Katika kisa ulichosoma, lugha ina dhima gani?
3. Bainisha sentensi ambazo zimetumia lugha isiyo fasaha katika kisa ulichosoma.
4. Unafikiri kwa nini lugha hiyo siyo fasaha?
5. Andika kwa ufasaha sentensi ulizozibainisha katika swali la 3.
6. Kwa kuzingatia mjadala wa Zukwe na wenzake, wewe una maoni gani kuhusu mazungumzo yao?
7. Kipi kinafaa kuwa kichwa cha habari cha kisa ulichosoma?
Zoezi la 1.1
1. Kwa kuzingatia lafudhi na matamshi sahihi, bainisha maneno yenye makosa katika sentensi zifuatazo:
(a) Hata wenzetu waliosoma wanakwendaga mjini.
(b) Nimepata ujumbe wa simu wenye taharifa mbaya.
(c) Kurara badara ya kutafuta kazi ya kufanya kunasababisha maisha kuwa magumu.
(d) Ama kweri erimu haina mwisho.
(e) Rafiki yangu naja.
(f) Ntoto wangu aumwa.
2. Andika upya sentensi hizo kwa kusahihisha makosa uliyoyabaini.
3. Andika sentensi tano zenye makosa ya kisarufi yanayotokana na athari za lugha mama au mazingira.
Zingatia
Lafudhi ni jinsi mtu anavyotamka maneno. Aidha, lafudhi humpa mzungumzaji utambulisho ama wa jamii au eneo analotoka. Lafudhi ya mtu hutokana na athari za lugha mama, au eneo la kijiografia analotoka.
Kazi ya 1.8
1. Chunguza kwa makini mazungumzo kati ya Zukwe na wenzake, kisha bainisha maneno mengine yenye makosa na uyaandike kwa usahihi.
2. Kwa nini Shaburi ametumia maneno kweri, erimu, kurara, badara, na kirimo kwenye mazungumzo yake?
Zingatia
Matamshi ni jinsi ya kutamka maneno katika lugha yoyote ile. Matamshi sahihi ni utamkaji wa maneno kwa kuzingatia kanuni za sarufi ya lugha inayohusika. Mzungumzaji akikosea kutamka neno humfanya msikilizaji asimwelewe kabisa au aelewe tofauti na alichokikusudia mzungumzaji. Kwa mfano, mtu akitamka kura badala ya kula atawasilisha maana tofauti na iliyotegemewa; hivyo, hukwamisha mawasiliano.
Kazi ya 1.9
Chunguza sentensi zifuatazo, kisha bainisha tofauti zake.
1. Baraka analima.
2. Baraka analima?
3. Baraka analima!
4. Baraka, lima.
Zingatia
Kila lugha ina utaratibu wake maalumu wa upandaji na ushukaji wa mawimbi ya sauti wakati wa kuzungumza. Utaratibu huo huitwa kiimbo. Matumizi ya kiimbo yanasaidia kubainisha lengo la mzungumzaji; kwa mfano, kuuliza swali, kutoa maelezo, kutoa amri, au kushangaa.
Kazi ya 1.10
Tenganisha silabi za maneno yafuatayo:
1. Shusha
2. Ua
3. Pua
4. Gharama
5. Mpiganaji
6. Vilevile
7. Shangwe
8. Sikukuu
9. Kinanda
10. Kiswahili
Zingatia
Silabi ni sehemu ya neno inayoundwa na konsonanti na irabu au irabu peke yake na hutamkwa kwa pamoja na mara moja kama fungu moja la sauti. Lugha ya Kiswahili hutamkwa kwa utaratibu wa kufuata silabi. Kwa mfano, neno baba limeundwa na silabi mbili ambazo ni $ba$ $ba$. Muundo wa silabi za Kiswahili unajibainisha katika miundo ifuatayo:
(i) Irabu pekee: Kwa mfano, silabi $u$ na $a$ katika neno ua;
(ii) Konsonanti moja na irabu moja: Kwa mfano, silabi $la$ na $la$ katika neno lala;
(iii) Konsonanti mbili au zaidi na irabu moja: Kwa mfano, silabi $mba$ katika neno shamba;
(iv) Konsonanti moja, kiyeyusho kimoja na irabu moja: Kwa mfano, silabi $pya$ katika neno jipya; na
(v) Konsonanti mbili, kiyeyusho kimoja na irabu moja: Kwa mfano, silabi $mbwa$ katika neno pambwa. Irabu za Kiswahili ni a, e, i, o, na u. Konsonanti za Kiswahili ni b, ch, d, dh, f,
g, gh, h, j, k, l, m, n, ng’, ny, p, r, s, sh, t, th, v, na z.
Viyeyusho katika lugha ya Kiswahili ni w na y.
Silabi au mkusanyiko wa silabi unaotamkwa na kuleta maana fulani huitwa neno. Hata hivyo, silabi kama vile, $na$, $kwa$, na $la$ huweza kuwa neno pale ambapo zitatumika katika tungo. Aidha, neno au kifungu cha maneno kinachotoa taarifa kamili huitwa sentensi.
Kazi ya 1.11
Tamka kwa ufasaha maneno yafuatayo:
1. Muungano
2. Koo
3. Washirikishe
4. Bidhaa
5. Thamani
6. Shughuli
7. Ng´ombe
8. Nyanya
9. Ramani
10. Picha
Zingatia
Herufi za Kiswahili hutamkwa kwa kuhusisha herufi husika na irabu /e/ ambayo hupachikwa mbele ya herufi hiyo. Hata hivyo, herufi ambayo ni irabu hutamkwa kama inavyoandikwa. Rejea kielelezo namba 1.2 kinachoonesha herufi za Kiswahili na matamshi yake. Silabi za Kiswahili hutamkwa kutegemeana na irabu iliyopachikwa mbele ya konsonanti inayohusika; kwa mfano, $ba$, $be$, $bi$, $bo$, na $bu$.
Herufi za alfabeti | Matamshi ya herufi |
a b ch d dh e f g gh h i j k l m n ng' ny o p r s sh t th u v w y z | a be che de dhe e fe ge ghe he i je ke le me ne nye ng'e o pe re se she te the u ve we ye ze |
Kielelezo namba 1.2: Herufi na matamshi yake |
Kazi ya 1.12
Soma tena kisa chenye mazungumzo kati ya Zukwe na wenzake kwa kuzingatia usahihi wa matamshi, mkazo, kiimbo, na lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Zingatia
Sauti ni sehemu ndogo sana ya neno ambayo haiwezi kugawanyika zaidi. Kwa maneno mengine, sauti ni vitamkwa vinavyotamkwa na binadamu kwa kutumia ala za sauti ambazo ni mapafu, koo, midomo, ulimi, ufizi, meno, na kadhalika. Sauti zimegawanyika katika aina mbili ambazo ni irabu na konsonanti. Irabu ni aina ya sauti za lugha ambazo hutamkwa bila kuzuia mkondohewa ilhali konsonanti ni sauti ambazo hutamkwa kwa kuandamana na mzuio wa mkondohewa. Lugha ni chombo cha mawasiliano. Ili mawasiliano yafanikiwe, inabidi lugha iwe fasaha.
Hivyo, ni lazima kuepuka makosa mbalimbali ya kimatamshi katika mawasiliano. Makosa ya kimatamshi hujitokeza watu wanapozungumza kwa kushindwa kutamka baadhi ya sauti katika lugha kutokana na athari za lugha mama au mazingira aliyomo mzungumzaji; na hivyo, kukwamisha mawasiliano. Hali hii inaweza kupotosha maana. Aidha, ni vyema kuelewa kuwa kuna matamshi ya herufi za alfabeti ambazo huwakilisha pia sauti, hususani irabu. Aghalabu, katika Kiswahili sauti huandikwa kama zinavyotamkwa. Hata hivyo, kuna sauti chache ambazo herufi zake hutokana na muungano wa herufi mbili lakini ni sauti moja; kwa mfano, th, dh, ch, ng', ny, sh, na gh katika maneno kama thamani, dhahabu, chai, ng'ombe, nyanya, shamba, ghadhabu, n.k.
Kazi ya 1.13
Orodhesha makosa mbalimbali yasiyopungua sita (6) yanayofanywa na wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili, kisha rekebisha makosa hayo.
Kazi ya 1.14
Fuatilia taarifa ya habari kwa njia ya redio au televisheni kwa lengo la kubainisha makosa ya kimatamshi yanayojitokeza, kisha andika maneno hayo kwa matamshi sahihi.
Zoezi la 1.2
Andika sentensi zifuatazo kwa usahihi.
1. Zana ya neno ni mkusanyiko wa silabi wenye kuleta maana.
2. Alishiriki mazungumzo na wenzake aliyokuwa wakiyafanya kijiweni.
3. Nyumba na banda la kuku imebomolewa.
4. Baba alimkuta mama ameondoka.
5. Embe limeanguka kutoka juu ya mti.
Zoezi la 1.3
Chunguza sentensi zifuatazo, kisha jibu maswali yanayofuata.
1. Kaka alimpigia mpira mtoto wa jirani yetu.
2. Fatuma amechana kitabu cha rafiki yake Rose.
3. Binamu amenunua kanga.
Maswali
1. Sentensi ulizopewa zina maana zaidi ya moja. Eleza maana za sentensi hizo.
2. Unafikiri sentensi zenye maana zaidi ya moja zinawezaje kuathiri mawasiliano?
3. Nini kifanyike ili kuondoa utata katika sentensi hizo?
Zingatia
Kwa ujumla, lugha imegawanyika katika tanzu kuu mbili ambazo ni lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi. Lugha ya mazungumzo huwasilishwa kwa
mdomo ambapo chanzo ni mzungumzaji na kikomo ni msikilizaji. Lugha ya maandishi huwasilishwa kwa maandishi ambapo chanzo ni mwandishi na kikomo
ni msomaji. Mzungumzaji au mwandishi anapaswa kuwa makini ili kuwezesha mawasiliano. Usahihi wa maandishi au mazungumzo hutawaliwa na sarufi ya
lugha inayohusika. Sarufi imegawanywa katika matawi makuu manne ambayo ni sarufi matamshi (fonolojia), sarufi maumbo (mofolojia), sarufi miundo (sintaksia)
na sarufi maana (semantiki). Sarufi matamshi inashughulika na utamkaji wa sauti za lugha inayohusika ilhali sarufi maumbo inashughulika na maumbo ya maneno.
Aidha, sarufi miundo inashughulika na mpangilio wa maneno katika sentensi wakati sarufi maana inashughulika na maana za maneno na sentensi.
Zoezi la marudio la 1
1. Chagua jibu sahihi katika maswali yafuatayo:
(i) Dhima kuu ya lugha katika mawasiliano ni ipi kati ya hizi zifuatazo?
(a) Kutambulisha utamaduni
(b) Kutunza historia
(c) Kupashana habari
(d) Kuelimisha jamii
(e) Kuburudisha jamii
(ii) Kiimbo hufasiliwaje katika mazungumzo?
(a) Kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti.
(b) Kuzungumza na kuongea kwa sauti.
(c) Kuzungumza kwa kupandisha mawimbi ya sauti.
(d) Kuzungumza kwa kushusha mawimbi ya sauti.
(e) Kuzungumza na kushuka kwa mawimbi ya sauti.
(iii) Sentensi ipi kati ya hizi zifuatazo haina maana zaidi ya moja?
(a) Kaka amefua nguo.
(b) Nipe sahani ya kulia.
(c) Suedi amenunua mbuzi.
(d) Eva amenunua kanga.
(e) Joni amempigia mpira.
(iv) Dhana ipi kati ya zifuatazo huonesha utambulisho wa mzungumzaji?
(a) Matamshi
(b) Sauti
(c) Silabi
(d) Mkazo
(e) Lafudhi
(v) Neno shurutishwa limeundwa na silabi ngapi?
(a) Tano
(b) Nne
(c) Tatu
(d) Sita
(e) Kumi
2. Oanisha maana ya dhana katika orodha A na dhana zinazohusika kutoka orodha B kwa kuchagua herufi ya jibu sahihi.
Orodha A | Orodha B |
(i) Sehemu ya neno inayotamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la sauti. (ii) Utamkaji wa maneno unaozingatia kanuni za sarufi ya lugha. (iii) Nguvu inayotumika kutamka sehemu fulani ya neno. (iv) Vitamkwa vinavyotamkwa na binadamu kwa kutumia viungo sauti. (v) Jinsi mtu anavyotamka maneno ya lugha. |
|
3. Bainisha maneno yenye makosa katika sentensi zifuatazo kwa kuyapigia mstari, kisha andika sentensi hizo kwa usahihi.
(a) Mwanafunzi ayejitambua hawapendagi mzaha katika masomo.
(b) Shule yetu ina vifaa vya samani.
(c) Napenda kuchukua nafasi hii kuwajulisha kuwa wagonjwa wote wamepona.
(d) Mti uliokuwa karibu na bustani ya maua umedondoka.
(e) Mzee Kiza amedhuru mbuga za wanyama.
4. Matumizi ya kiimbo husaidia kubainisha lengo la mzungumzaji. Fafanua malengo ya mzungumzaji katika sentensi zifuatazo:
(a) Mwanafunzi anasoma kwa bidii.
(b) Mwanafunzi, soma kwa bidii.
(c) Mwanafunzi anasoma kwa bidii?
(d) Mwanafunzi anasoma kwa bidii!
5. Eleza maana ya msamiati ufuatao, kisha tunga sentensi moja kwa kila msamiati.
(a) baruapepe
(b) mitandao ya jamii
(c) tovuti
(d) faksi
(e) mawasiliano