THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL ADVANCED CERTIFICATE OF SECONDARY EDUCATION EXAMINATION
121/1 KISWAHILI 1
(Kwa Watahiniwa Walioko Shuleni na Wasiokuwa Shuleni)
Muda: Saa 3 Jumatano, 08 Februari 2012 asubuhi Maelekezo 1. Karatasi hii ina maswali kumi (10) katika sehemu A, B, C, D na E.
2. Jibu maswali saba (7) kwa kujibu maswali yote katika sehemu A, C na E; maswali mawili (2) kutoka sehemu B na swali moja (1) kutoka sehemu D.
3. Kila sehemu ina alama ishirini (20).
4. Simu za mkononi haziruhusiwi katika chumba cha mtihani.
5. Vikokotozi haviruhusiwi ndani ya chumba cha mtihani.
6. Andika Namba yako ya Mtihani katika kila ukurasa wa kijitabu chako cha kujibia.
SEHEMU A (alama 20) UFAHAMU
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata:
Waafrika ni binadamu ambao wamepitia mateso na shida nyingi sana. Baadhi ya mateso yalisababisha kumwaga damu na kutoa uhai na kibaya zaidi yalisababisha kupotea kwa tutu na asili ya mwafrika. Wengine walithubutu kusema kuwa waafrika wana laana na jitihada zozote za kujaribu kuwakomboa ni kama kufuru.
Waafrika walinyanyaswa ndani ya ardhi yao wenyewe, walifungwa minyororo na kuuzwa kama bidhaa sokoni. Walitumikishwa katika mashamba na migodi kwa ujira mdogo. Magonjwa yakawaandama na njaa ikawatafuna watu weusi bila huruma. Waliletewa silaha za kuuana wenyewe kwa wenyewe, madhehebu na makabila vikawa chanzo cha mapigano. Watu weusi wakabaki katika hali tete ambayo haikuchachusha tafakuri zenye kuleta maendeleo, kwa sababu taharaki ilitawala jamii.
Ndani ya uhuru wa bendera, wakapandikiziwa viongozi ambao hawakutofautiana na ile hadithi ya Kimbwangai nyani aliyetolewa mkia ili afanane na binadamu. Walipata fursa lakini hawakutenda ya kuwanufaisha wananchi wao. Hayo yalitendeka si kwa sababu kuwa watu weusi si viumbe razini la hasha! Yalitokana na shinikizo la mabepari waliotaka kupata malighafi ili kuneemesha kasri zao kiuchumi.
Katika enzi hizi za utandawazi, nchi za Afrika zimekuwa soko kubwa la bidhaa za nchi tajiri, zenye viwanda vinavyotegemea malighafi toka Afrika. Mitumba huletwa na kuuziwa wananchi kwa bei nafuu jambo linalohatarisha mazingira. Uwekezaji katika sekta ya madini umeshamiri na umekuwa tishio kubwa kwa ustawi wa jamii, twabakia na ardhi yenye mashimo.
Kwa ujumla waafrika wanakabiliwa na umaskini uliotopea kwa kipindi kirefu. Wakati umefika sasa wa kulipwa deni, hatuhitaji malipo ya fadhila, pesa wala maneno matamu. Malipo ya thamani yatakayokubalika na kizazi hiki na kizazi kijacho ni kuwaacha watu weusi kuwa huru katika nyanja zote za maisha, ili wajenge upya jamii zao:
Maswali (a) Toa maana za maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika habari uliyoisoma:
(i) Kufuru
(ii) Ujira
(iii) Tafakuri
(iv) Taharaki
(v) Fursa
(vi) Kasri
(vii) Mitumba
(viii) Uliotopea
(b) Mwandishi ana maana gani anaposema “hawakutofautiana na ile hadithi ya Kimbwangai nyani aliyetolewa mkia ili afanane na binadamu.”
(c) Unaelewa nini kuhusu uhuru wa bendera, toa maelezo yasiyozidi mistari mitatu.
(d) Kwa kurejea aya ya nne (4), mwandishi ana mtazamo gani kuhusu utandawazi kwa nchi za Afrika.
View Ans
2. Fupisha habari uliyoisoma kwa maneno mia moja (100).
View Ans
SEHEMU B (alama 20) MATUMIZI YA SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
Jibu maswali mawili (2) kutoka sehemu hii.
3. Katika kila tungo zifuatazo taja kielezi na fafanua aina ya kielezi hicho.
(a) Hospitali imefungwa kwa mara ya tatu.
(b) Amekaa juu ya nyumba.
(c) Anapigana kishujaa
(d) Nitaondoka asubuhi na mapema.
(e) Ameelekea upande wa kulia.
View Ans
4. Fafanua dhana zifuatazo kwa kutumia mifano:
(a) Kiunganishi
(b) Mzizi wa neno
(c) Sintaksia
(d) Kitenzi kisaidizi (e) O-rejeshi.
View Ans
5. “Kitenzi kikuu ni neno linalobebeshwa majukumu mengi katika tungo za Kiswahili.” Kwa kutumia mifano, toa hoja tano kuthibitisha kauli hiyo.
View Ans
6. “Matumizi ya rejesta huneemesha lugha ya Kiswahili.” Tumia hoja tano zenye mifano ili kufafanua hoja hiyo.
View Ans
SEHEMU C (Alama 20) UTUNGAJI
Jibu maswali la saba (7).
7. Jifanye wewe ni meneja wa kiwanda cha kutengeneza mazulia S.L.P 2011 Tanga, andika barua ya kumjibu kijana aitwaye Cheche Kirembwe ukimjulisha kuwa amepata nafasi ya kazi ya Afisa Biashara aliyoomba kiwandani hapo. Anwani yake ni S.L.P 2012 Tanga. Tumia namba ya kumbukumbu KCM/TANG/14/1. Jina lako liwe Pata Mafanikio.
View Ans
SEHEMU D (Alama 20) MAENDELEO YA KISWAHILI
Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.
8. Baada ya uhuru hadi leo, Tanzania imefanya juhudi mbalimbali zilizosaidia kuendeleza lugha ya Kiswahili nchini kupitia mfumo wa elimu. Fafanua dai hilo kwa kutumia hoja tano.
View Ans
9. “Ili lahaja yoyote iweze kusanifishwa ni lazima ikidhi masharti ya kitaalamu.” Elezea masharti matano ili kuthibitisha dai hilo.
SEHEMU E (Alama 20) TAFSIRI
Jibu swali la kumi (10).
View Ans
10. Nini maana ya tafsiri? Elezea dhima nne za tafsiri.
View Ans