THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL
CERTIFICATE OF SECONDARY EDUCATION EXAMINATION
021 KISWAHILI
(Kwa Watahiniwa Walioko Shuleni tu)
Muda: Saa 3 Jumanne, 9 Oktoba 2012 mchana
Maelekezo
-
Karatasi hii ina sehemu A, B, C, D na E.
-
Jibu maswali yote katika sehemu A, B na D, swali moja (1) kutoka sehemu C na maswali matatu (3) kutoka sehemu E. Swali la 15 ni la lazima.
-
Zingatia maagizo ya kila sehemu na ya kila swali.
-
Simu za mkononi haziruhusiwi katika chumba cha mtihani.
-
Andika Namba yako ya Mtihani katika kila ukurasa wa kijitabu chako cha kujibia.
SEHEMU A (Alama 10) UFAHAMU
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata:
Mtu hutembea njiani akajikwaa, ukucha ukang’oka au pengine hata kubwagwa chini vibaya na kisiki, kisha mtu huyu hugeuka na akakiangalia kisiki hicho, ambacho pengine huwa hata hakitazamiki.
Kama kisiki kimkwazavyo mtu atembeaye, pia mikasa mbalimbali, midogo kwa mikubwa, huwakwaza na pengine hata kuwabwaga chini binadamu katika maisha yao. Jinsi baadhi ya mikasa hii ilivyo adhimu, mtu anapokumbuka huweza kulia. Kwa upande mwingine mtu hujionea fahari alivyopambana na mikasa hiyo kwa ujasiri hadi akaishinda au kuikwepa. Tukio kama hili hufanya shajara la mambo bora ya kukumbukwa maishani.
Maisha ya shule ni mazuri, lakini mara nyingi huwa magumu na hasa lile wingu jeusi la mitihani likaribiapo. Wanafunzi hupuuza sheria kama vile kwenda madarasani, michezoni na pengine hata kula, wakajibanza mahali pa faragha wakajisomea. Nyakati zipendwazo ni usiku wa manane, kwa kujua kuwa kila mtu amelala na kuwa hayupo mwalimu wa zamu awezayo kuzuru shule wakati huo. Wanafunzi wenye bahati hunufaika sana kwa mpango huo wala hawagunduliwi. Wengine mara hugunduliwa wakapewa adhabu ambayo huridhika kuifanya kwani nzi kufa kwenye kidonda si hasara.
Siku hiyo ilikuwa Jumapili, nami nikajiunga katika ngoma ya kusoma na wenzangu wanne, wawili wao walikuwa viranja wa madarasa. Ilipata saa nane za usiku nasi tukaingia katika chumba cha kuoneshea picha, tukafunga mlango kwa funguo na komeo. Baada ya kuhakikisha kuwa hapana hata mwonzi mdogo wa taa uliotambaa nje, tulitoa ala zetu, kila mtu akashughulika na hamsini zake.
Hapakupita saa moja, mara tunasikia mlango unabishwa hodi, “fungua mlango! tokeni sasa hivi.” Sauti hiyo ilikuwa ya mmoja wa wanafunzi wa shule yetu. Mwanafunzi huyu aliandamana na mtu ambaye tulimtambua kwa sauti kuwa alikuwa Tatu, dada mkuu wa shule. Mioyo ilianza kutudunda kwa hofu, damu zetu zikawa karibu kuganda. Mara nilipata fahamu nikazima taa, lakini kwa bahati mbaya chumba hicho hakikuwa na madirisha ambayo kwayo tungeliweza kutoka. Kumbe mwanafunzi huyo naye alipata maarifa, alipanga viti kimoja juu ya kingine, akapanda juu na kuchungulia ndani katika mwanya uliokuwa karibu na dari. Kumulika ndani akamtambua Dora. Dora! Dora! fungueni mlango na tokeni sasa hivi!” akang’aka, lakini tukapiga kimya humo ndani.
Mwanafunzi huyo alipoona ameshindwa kututoa, alifanya hila ya kumwita mwalimu mkuu. Naam, sauti ya simba huweza kumdondosha chini panya aliyejificha darini. “Dora fungua mlango sasa hivi!” alinguruma, sote tulibaki tumeduwaa. Dora akafungua mlango, “ ushikwapo shikamana” wahenga walisema, mlango ulipofunguliwa mimi nilibana nyuma yake bila mtu kufahamu. Mwalimu mkuu aliwasha taa akachungulia ndani. Kuona hakuna mtu alizima taa akaondoka zake kwenda kuwadadisi wenzangu. Moyo ulishuka pwaa! nikatoka huku nagwaya mwili mzima, nikakimbia kwa mashaka makubwa hadi benini kwangu. Kwa vyovyote vile nilijua nilikuwa ndani.
Hazikupita hata datika tano tokea nijitupe kitandani nikashtukia taa zinawashwa mabwenini. Kumbe mwalimu mkuu, mwalimu wa zamu na Tatu, wakisaidiana na akina dada kadhaa walikata shari wafanye uchunguzi wa shule nzima, ili kuona iwapo wanafunzi wote walikuwepo. Ama kweli “ siku za mwizi arobaini,” wanafunzi wapatao kumi na watano walikuwa mjini ambako kulipigwa muziki na bendi mashuhuri kutoka Dar es Salaam. Asubuhi niliamka kichwa kizito nikauhisi mwili sio wangu. Masomo kuanza tu likapitishwa tangazo likiwaita wale wenzangu niliokuwa nao usiku na wale waliotoroka. Ilipofika saa nne, tukakuta wote wanafunga virago, nikaanza kuwa na matumaini kuwa ama kweli niliponea chupuchupu.
Maswali
(a) Fafanua maana za misemo ifuatayo kama ilivyotumika katika habari uliyosoma:
-
Nzi kufa kwenye kidonda si hasara.
-
Kila mtu akashughulika na hamsini zake.
-
Ushikwapo shikamana.
-
Siku za mwizi arobaini.
View Ans
(b) Unafikiri kwanini uongozi wa shule aliyokuwa anasoma mwandishi ilipiga vita tabia ya wanafunzi kusoma wakati wa usiku wa manane.
View Ans
(c) Una mawazo gani kuhusu kitendo cha Tatu kufuatilia mienendo ya wanafunzi wenzake hasa kwa usiku ule wa manane.
View Ans
(d) Andika kichwa cha habari kinachofaa kwa habari uliyosoma kisichozidi maneno matano (5).
View Ans
2. Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha andika ufupisho wa maneno arobaini (40).
Kamati imeundwa ikihusisha kikundi maalum cha wataalamu ambao watavalia miwani na kuandika upya historia ya Bara la Afrika. Mpango huu ni mahususi na tunaunga mkono wananchi wote. Ni mpango wa jinsi hii ambao utatokomeza maandishi yaliyoandikwa na wakoloni, waliopotosha ukweli wa maisha, mila na utamaduni wetu.
Vitabu vingi vya historia ya bara letu vinavyotumiwa na vijana shuleni, viliandikwa na watu waliokuja kutawala na kujitafutia mali. Katika maandishi yao walidiriki kutufanya tuamini kwamba lugha zao, lia na maisha yao vilikuwa na vitu azizi kuliko vyetu. Mpaka leo hii ni watu wachache wanaoamini kuwa tunao ustaarabu na utamaduni ulio imara tangu zama za wahenga. Tunaamini kuwa miaka michache ijayo upeo utageuka kabisa katika nadharia zilizo vichwani mwa watu wengi waliolishwa kasumba ya ukoloni.
View Ans
SEHEMU B (Alama 25) SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA
Jibu maswali yote katika sehemu hii.
3. Kwa kutumia mifano dhahiri, fafanua dhana zifuatazo:
-
Kiima
-
Chagizo
-
Shamirisho
-
Utohoaji
-
Urudufishaji
View Ans
4. “Maneno huweza kubadilika kutoka aina moja na kuwa aina nyingine.” Dhihirisha kauli hii kwa kubadili maneno yafuatayo kwa kuzingatia maelekezo yaliyo katika mabano.
(a) Mkono (badili kuwa kielezi)
(b) Kwenda (badili kuwa nomino)
(c) Bora (badili kuwa kitenzi)
(d) Ogopa (badili kuwa kivumishi)
(e) Mzazi (badili kuwa kitenzi)
(f) Bisha (badili kuwa kivumishi)
(g) Refu (badili kuwa kitenzi)
(h) Linda (badili kuwa nomino)
(i) Kabati (badili kuwa kielezi)
(j) Uguza (badili kuwa nomino)
View Ans
5. Kamusi ni muhimu kwa mtumiaji yeyote wa lugha. Taja hoja tano zinazothibitisha umuhimu huo.
View Ans
6. Kwa kutumia mifano ya lugha ya Kiswahili, taja sababu tano za utata katika mawasiliano.
View Ans
7. Kwa kutumia mifano, taja miundo mitano ya kirai nomino.
View Ans
SEHEMU C (Alama 10) UANDISHI
Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.
8. Jifanye kuwa umepata barua ya mwaliko wa sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa rafiki yako aitwaye Faraja Matata, itakayofanyika siku ya tarehe 10/10/2012. Kwa bahati mbaya siku tatu kabla ya sherehe umepata safari ya kikazi kuelekea mkoani Singida. Andika barua kumtaarifu rafiki yako kuwa hutaweza kuhudhuria sherehe hiyo. Jina lako liwe Tumaini Baraka.
View Ans
9. Andika insha yenye maneno yasiyopungua mia mbili na hamsini (250) na yasiyozidi mia tatu (300) kuhusu umuhimu wa huduma za simu ya mkononi.
View Ans
SEHEMU D (Alama 10) MAENDELEO YA KISWAHILI
Jibu swali la kumi (10)
10. Kwa kutumia mifano, onesha jinsi shughuli za dini, utawala, biashara na elimu zinavyokuza na kueneza lugha ya Kiswahili nchini Tanzania.
View Ans
SEHEMU E (Alama 45) FASIHI KWA UJUMLA
Jibu maswali matatu (3) kutoka katika sehemu hii. Swali la 15 ni la lazima.
11. “Maana ya methali inafungamana na muktadha, hivyo ikitumiwa vibaya inaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.” Dhihirisha dai hilo kwa kutumia methali sita za Kiswahili.
View Ans
12. “Washairi ni wataalamu wazuri na waliobobea katika kutumia taswira zinazotoa ujumbe kwa jamii.” Tumia taswira tatu kwa kila diwani kati ya diwani mbili zilizoorodheshwa kuthibitisha kauli hiyo.
View Ans
13. Tumia vitabu viwili vya riwaya kati ya vilivyoorodheshwa, kutoa hoja tatu kwa kila kitabu, zinazothibitisha dai kuwa mwanaume ni kikwazo cha mafanikio katika jamii.
View Ans
14. Tumia vitabu viwili vya tamthiliya kati ya vilivyoorodheshwa, kujadili madhara ya ukosefu wa elimu katika jamii. Toa hoja tatu kwa kila tamthiliya.
View Ans
15. Umeteuliwa kuwa mmoja kati ya waandaaji wa shindano la sanaa za maonesho litakalofanyika wakati wa kusherehekea siku ya walimu duniani mwaka 2013. Andika majigambo yenye beti nne ya mhusika ambaye ni mwalimu.
ORODHA YA VITABU
Ushairi
Wasakatonge - M.S. Khatibu (DUP)
Malenga wapya - TAKILUKI (DUP)
Mashairi ya Chekacheka - T.A Mvungi (EP& D.LTD)
Riwaya
Takadini - Ben Hanson (MBS)
Watoto wa Maman’tilie - E. Mbogo (H.P)
Joka la Mdimu - A.J. Safari (H.P)
Tamthiliya
Orodha - Steve Raynolds (MA) Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe - E. Semzaba (ESC)
Kilio Chetu - Medical Aid Foundation (TPH)
View Ans