Sura Ya 01 : Kuwasiliana kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi
| Utangulizi Upatanisho wa kisarufi ni hali ambayo nomino au kiwakilishi hukubaliana na maneno mengine hasa vitenzi na vivumishi katika tungo. Katika sura hii, utajifunza dhana ya upatanisho wa kisarufi na uainishaji wa ngeli za nomino kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi. Aidha, utajifunza kutumia urejeshi kwa kuzingatia ngeli za nomino. Kadhalika, utajifunza namna ya kuandika vifungu vya habari kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi. Umahir utakaoujenga utakuwezesha kuwasiliana kwa usahihi na ufasaha katika miktadha mbalimbali kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi. |
| Fikiri Mawasiliano bila kuzingatia upatanisho wa kisarufi |
Dhana ya ngeli za nomino na upatanisho wa kisarufi
Ghani shairi lifuatalo, kisha jibu maswali yanayofuata.
Najitanua kwa lugha, zilo tamu za Kibantu,
Kwenye kila fani nipo, sayansi na insia,
Mwenzangu nimesikia, watu wakiulizana,
Kuhusu jina la ngeli, mabishano hayakomi,
Hunikuti kwa wageni, ni kwa Wabantu wenzangu tu.
Wauliza ngeli? Hilo nimetoa kwa wenzangu,
Wenzangu gani? Nimetoa kwa Wahaya,
Ndege wafananao, huruka pamoja,
Nomino, kama ndege, huruka pamoja pia,
Hunikuti kwa wageni, ni kwa Wabantu wenzangu tu.
Ngeli za nomino zifananazo, muungano hudumu,
Viumbe hai na visivyo hai, ngelize haziungani,
Ngeli sikai kiholela, mpango nazingatia,
Upatanisho wa kisarufi, viambishi awali nazingatia,
Hunikuti kwa wageni, ni kwa Wabantu wenzangu tu.
Ukitaka kunielewa, kiambishi usikosee,
Ukikosea dhahiri, upatanisho tauharibu,
Utachepua maana, kwa watumiaji wa lugha,
Ukitaka tuendane, vitu na watu sichanganye,
Hunikuti kwa wageni, ni kwa Wabantu wenzangu tu.
Kupatanisha kisarufi, uhusiano wa viambishi ndio mpango,
Viambishi hupendana, upatanisho ni mshenga,
Ukinipanga kiholela, maana taiharibu,
Anisikilizaye na kunisoma, kamwe hatonielewa,
Hunikuti kwa wageni, ni kwa Wabantu wenzangu tu.
Kiswahili najidai, sifa zangu mzomzo,
Wauliza urejeshi, bila ngeli hujinadi,
Uhusiano murua, wa vipashio zingatia,
Ukisahau urafiki wa ngeli, urejeshi kupotoa,
Hunikuti kwa wageni, ni kwa Wabantu wenzangu tu.
Maswali
Zingatia
"Ngeli" asili yake ni neno la lugha ya Kihaya "engeli" lenye maana ya "aina". Hivyo, ngeli za nomino ni aina au makundi ya majina ya watu, wanyama, vitu, hali na mahali kulingana na sifa za kisarufi. Upatanisho wa ngeli za kisarufi ni hali ya nomino au viwakilishi kukubaliana na vitenzi na vivumishi kwenye tungo. Kwa mfano:
| Umoja | Wingi |
| (i) Mti ule umeanguka | Miti ile imeanguka |
| (ii) Mtoto yule anacheza vizuri. | Watoto wale wanacheza vizuri. |
| (iii) Kiti kizuri kimevunjika. | Viti vizuri vimevunjika. |
Kwa hiyo, katika mfano wa kwanza, kiambishi cha umoja cha upatanisho wa kisarufi ni U- na cha wingi ni I-. Hivyo, viambishi hivyo vinaunda ngeli inayoitwa U-I. Katika mfano wa pili, kiambishi cha umoja cha upatanisho wa kisarufi ni YU-/A- na cha wingi ni WA-. Viambishi hivi vinaunda ngeli ya YU/A-WA. Katika mfano wa tatu kiambishi cha umoja cha upatanisho wa kisarufi ni KI- na cha wingi ni VI-. Viambishi hivi vinaunda ngeli ya KI-VI.
Kiambishi ni kipande cha neno ambacho hutokea kabla au baada ya mzizi wa neno. Kwa mfano, neno anaimba [a-na-imb-a] lina viambishi a-, -na-, na -a. Viambishi a- na -na- ni vya awali na -a ni kiambishi tamati.
Mzizi ni sehemu ya neno ambayo haibadiliki. Hivyo, mzizi ni kiini cha neno. Kwa mfano, katika neno anaimba [a-na-imb-a], mzizi ni -imb-.
Kuainisha ngeli za nomino kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi
| Shughuli ya 1.1 Chunguza picha hizi, kisha fanya yanayofuata:
(i) Tunga sentensi mbili katika umoja kwa kila picha. (ii) Andika wingi wa sentensi ulizozitunga katika kipengele cha (i) (iii) Bainisha viambishi vinavyoonesha upatanisho wa kisarufi unaojitokeza katika kila sentensi uliyotunga. |
Zingatia
Ngeli za nomino huainishwa kwa kutumia vigezo mbalimbali vikiwamo umbo (viambishi vya umoja na wingi katika nomino), maana, na viambishi vya upatanisho wa kisarufi. Kigezo cha upatanisho wa kisarufi huainisha ngeli kwa kuangalia kupatana kwa nomino na maneno mengine katika tungo. Jina la ngeli husika hutokana hasa na viambishi vya upatanisho wa nomino na vitenzi. Kwa mfano:
(a) Shamba limelimwa - Mashamba yamelimwa. Nomino shamba ipo katika ngeli ya LI-YA.
(b) Uzi umekatika - Nyuzi zimekatika. Nomino uzi ipo katika ngeli ya U-ZI.
Katika mfano (a), kiambishi cha umoja cha upatanisho wa kisarufi baina ya nomino na kitenzi ni [LI-] na wingi ni [YA-].
Katika mfano (b), kiambishi cha umoja cha upatanisho wa kisarufi baina ya nomino na kitenzi ni [U-] na wingi ni [ZI-]. Hivyo, ngeli za upatanisho wa kisarufi za nomino katika mifano hiyo ni LI-YA na U-ZI.
Kwa kuzingatia kigezo cha upatanisho wa kisarufi, nomino za Kiswahili hugawanywa katika ngeli tisa kama zinavyooneshwa katika Jedwali la 1.1.
Jedwali la 1.1: Ngeli za nomino kwa kigezo cha upatanisho wa kisarufi
| Na. | Aina ya ngeli | Viambishi | Mifano | |
| Umoja | Wingi | |||
| 1. | YU-/A-WA- | YU-} umoja A-} WA- wingi | Mgeni yumo ndani. Mgeni amekuja. Ng'ombe amechinjwa asubuhi. | Wageni wamo ndani. Wageni wamekuja. Ng'ombe wamechinjwa asubuhi. |
| 2. | U-I- | U- umoja I -wingi | Mkutano umeanza mchana. Mgomba umekatika. | Mikutano imeanza mchana. Migomba imekatika. |
| 3. | LI-YA- | LI - umoja YA - wingi | Jembe limepotea. Papai limeiva. | Majembe yamepotea. Mapapai yameiva. |
| 4. | KI-VI- | KI - umoja VI - wingi | Kijiko kinang'aa. Kitabu hiki kinasomwa. | Vijiko vinang'aa. Vitabu hivi vinasomwa. |
| 5. | I-ZI- | I - umoja ZI - wingi | Kazi hii inatosha. Suruali itashonwa kesho. | Kazi hizi zinatosha. Suruali zitashonwa kesho. |
| 6. | U-ZI- | U - umoja ZI - wingi | Uzi umekatika. Ukuta umebomoka. | Nyuzi zimekatika. Kuta zimebomoka. |
| 7. | U-YA- | U - umoja YA -wingi | Uovu umezidi nchini. Ugonjwa umeenea. | Maovu yamezidi nchini. Magonjwa yameenea. |
| 8. | KU- | KU- | Kusoma kuna manufaa. Kucheza kunafurahisha. | Kusoma kuna manufaa. Kucheza kunafurahisha. |
| 9. | PA-MU-KU- | PA-MU-KU- | Hapa petu pamejaa. Humu ndani mna giza. Kule kunaonekana vizuri. | Hapa petu pamejaa. Humu ndani mna giza. Kule kunaonekana vizuri. |
Shughuli ya 1.2
Chunguza kifungu cha habari kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.
Mwaka huwa na majira mbalimbali yakiwamo masika, kiangazi, vuli na kipupwe. Masika ni kipindi ambacho mvua nyingi hunyesha sehemu kubwa. Kipindi hiki huwa ni liwazo kwa wanyama na wakulima. Wakulima hupiga vigelegele, vifijo na nderemo. Katika kipindi hiki pia wakulima huwa na hekaheka na ari kubwa ya kulima mashamba kwa kutumia jembe la mkono, plau au trekta. Baada ya kulima, wakulima hupanda mbegu bora ili kupata mazao kwa wingi. Wahenga hawakukosea waliposema "Jembe halimtupi mkulima". Kwa hakika, kila mkulima huvuna mazao kulingana na bidii yake. Hivyo, wakulima huona fahari kutekeleza kauli mbiu isemayo "Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu". Mavuno hutumika kwa chakula na mengine huuzwa ili kununua mahitaji muhimu. Licha ya vigelegele na furaha inayotokana na mvua, pia zipo hasara kwani kwa baadhi ya wakulima mambo huwaendea mrama. Hali hii inatokana na madhara yanayosababishwa na mvua kama vile mafuriko, ambayo huharibu mazao yao.
|
|
Siku moja usiku mwezi uliopita, Juma akiwa usingizini, ghafla alishtushwa na kelele za watu waliokuwa wanapiga mayowe wakisema "Maji! Maji! Maji! Nakufaaa! Uwiii! Nisaidieeee! Baada ya kuamka, aliona maji mengi yamejaa ndani ya chumba alichokuwa amelala. Nje, watu walitapatapa na kukimbia huku na huko. Maji yaliyochanganyika na matope na mabaki ya mimea yalijaa kijijini na kufunika baadhi nyumba. Wakazi wa eneo hilo hawakuamini macho yao jinsi mto uliokuwa jirani ulivyojaa na kufurika. Usiku huo ulikuwa wa patashika nguo kuchanika. Kila mmoja alipambana kunusuru maisha yake. Kijiji chao na vijiji vya jirani vilikuwa vimekumbwa na mafuriko yaliyoharibu mashamba, mazao, na kuua mifugo, hivyo kusababisha njaa. Methali isemayo "Jembe halimtupi mkulima" haikufua dafu tena kwani jembe liliwatupa wakulima kutokana na mafuriko yalisomba mazao yao. Mafuriko yaliharibu pia makazi na miundombinu kama vile barabara na madaraja. Kutokana na kuharibika kwa miundombinu hiyo, mawasiliano baina ya vijiji yalikatika.
Serikali na watu binafsi walifanya jitihada za kuokoa waathirika wa mafuriko. Vijana na wapigambizi walisaidia kuokoa watu na mali zao. Waathirika walibebwa mgongoni, mabegani, na wengine kwenye chombo maalumu. Mimea iliyokuwa ikinesanesa usiku na mchana kwa shukurani, ilionekana kupoteza matumaini kwani yote ilikuwa imemezwa na maji.
Shughuli za kiuchumi zilizorota. Maji machafu yaliyotuama kwenye madimbwi yalitengeneza mazalia ya mbu na vimelea vingine, hivyo yalisababisha mlipuko wa magonjwa.
Haya yote yalisababishwa na baadhi ya wananchi kukiuka sheria ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa kujenga makazi karibu na vyanzo vya maji, hasa mito. Kile walichokipuuza sasa kimetokea. Walikumbuka maneno ya wahenga yasemayo "Mdharau mwiba, mguu huota tende" na "Sikio la kufa halisikii dawa". Pamoja na juhudi zilizofanyika kuokoa maisha ya wananchi, serikali ilifanya kazi bega kwa bega na wananchi kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko ili kurudisha hali ya kawaida ya wananchi.
Maswali
Zoezi la 1.1
1. Kwa kila neno lililopo katika kisanduku, tunga sentensi mbili (2) moja katika umoja na nyingine katika wingi, kisha yapange maneno yaliyomo kwenye kisanduku katika ngeli za upatanisho wa kisarufi.
| sahani ubani jiko kuku meno ufa ng’ombe tunda debe sufuria mtoto Mungu kikombe karai uzi kalamu dirisha nyumba pembe gari |
2. Badili sentensi zifuatazo katika wingi, kisha bainisha viambishi vya upatanisho wa kisarufi kwa kupigia mstari.
3. Bainisha makosa ya upatanisho wa kisarufi katika sentensi zifuatazo, kisha rekebisha makosa hayo kwa kuandika sentensi hizo kwa usahihi.
4. Andika kifungu cha habari kwa kutumia ngeli mbalimbali za nomino, kisha bainisha nomino zinazoingia katika ngeli zifuatazo:
5. Ni mambo gani ya msingi huzingatiwa wakati wa kubainisha ngeli za nomino kwa kigezo cha upatanisho wa kisarufi?
| Shughuli ya 1.3 Tembelea maeneo mbalimbali yanayokuzunguka, kisha fanya yafuatayo: (a) Orodhesha nomino tano (5) kwa kila kundi la nomino zifuatazo: watu, vitu, wanyama, matunda, mimea, mbogamboga, hali na mahali. (b) Panga nomino hizo katika ngeli kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi, kisha weka kazi yako katika mkoba wa kazi. |
Kutumia urejeshi kwa kuzingatia ngeli za nomino
Soma kifungu cha habari kifuatacho, kisha jibu maswali yanayofuata.
Mwagito ni kijana ambaye anaishi na wazazi wake katika Kijiji cha Ipulilo Mkoani Njombe. Baada ya kuhitimu kidato cha nne, aliazimia kuanzisha kilimo cha maparachichi kijijini kwao. Alijisemea kimoyomoyo “Ili niwe mkulima stadi wa kilimo hiki, ninahitaji kupata ushauri kutoka kwa wataalamu”. Siku moja alimtembelea mzee maarufu pale kijijini aitwaye Likoko, aliyekuwa mkulima mzoefu wa maparachichi. Mzee Likoko alimkaribisha mgeni wake kwa bashasha. Mzee Likoko alianza kwa kusema, “Ninakupongeza sana kijana kwa kuamua kujiajiri katika kilimo hiki. Ni vijana wachache ambao wana uthubutu kama wako. Kwa hakika, utapata manufaa makubwa utakapozingatia yote nikuelezayo”. Ili upate mavuno mengi, zao la maparachichi linahitaji udongo unaopitisha maji vizuri na wenye rutuba ya kutosha. Baada ya kumweleza mengi kuhusu kilimo cha maparachichi, Mzee Likoko alimtembeza Mwagito katika mashamba yake ya miparachichi ili kushuhudia dhahabu hiyo ya kijani, kama wenyeji walivyosema. Mwagito alistaajabu kuona miparachichi yenye vimo tofautitofauti na iliyostawi mithili ya mitiki. Mwagito alihamasika kuanza kilimo hicho bila kuelehea. Alihakikisha anamuuliza maswali mwenyeji wake ili kuondoa madukuduku aliyokuwa nayo. Mwisho, alimshukuru Mzee Likoko kwa elimu aliyompa. Mzee Likoko aliitikia na kusema, "Udongo upate ungali maji". Kijana nenda kaanzishe kilimo hiki mapema iwezekanavyo. Niko tayari kukutembelea ili kuendelea kukusaidia zaidi". Mwagito alimuaga Mzee Likoko na kuondoka.
Mwagito aliporudi nyumbani kwake alikuwa na shauku kubwa ya kuandaa shamba ambalo alipewa na baba yake, Mzee Kimuli. Alitayarisha shamba lake kwa kuchimba mashimo yenye umbali wa kutosha kati ya shimo moja na lingine ili miparachichi ikue vizuri. Pia, aliandaa miundombinu ya umwagiliaji kipindi cha kiangazi na kuzuia mafuriko kipindi cha masika. Mara baada ya kuandaa shamba, aliagiza miche bora ya miparachichi kutoka kwa mtaalamu wa kilimo kama alivyoelekezwa na Mzee Likoko. Kabla ya kupanda, aliweka mbolea ya samadi ili kuongeza virutubisho kwenye udongo. Aliendelea kumwagilia maji ya kutosha hadi mvua iliponyesha. Miche ilipokua kiasi, aliongeza mbolea tena. Magugu yalipoota, Mwagito alipalilia shamba lake na alipulizia dawa ya kuua wadudu waharibifu walioshambulia miparachichi.
Baada ya miaka mitatu, miparachichi ilianza kutoa maua. Mwagito alipulizia viuatilifu na mbolea ya maji ili miparachichi istawi vizuri. Miezi michache iliyofuata, maparachichi yalikomaa na yalikuwa matamu sana. Wateja wengi waliyapenda na walimiminika kwa wingi kununua matunda hayo. Wateja hao waliuza matunda hayo ndani na nje ya nchi. Mwagito alifurahi kuona juhudi zake zikizaa matunda. Alisema, "Baada ya dhiki ni faraja; hakika utajiri unaanza kuninukia punde si punde". Fedha alizozipata kutokana na mauzo ya maparachichi alizitumia kwa kujikimu. Fedha zilizosalia alinunua mashamba katika vijiji vya jirani pamoja na kuhudumia shamba lake la awali. Kadiri siku zilivyosonga mbele, ndivyo Mwagito alivyopata mafanikio makubwa. Mwagito hakuwa mchoyo wa fadhila. Siku moja alimtembelea Mzee Likoko kwa ajili ya kumshukuru zaidi.
|
|
Mbali na faida za kiuchumi, Mwagito aliona fahari kwa kuwa mtunzaji mzuri wa mazingira. Pia, miparachichi ilitoa hewa safi pamoja na kivuli ambacho kiliwavutia wanyama na ndege kujisitiri mitini. Vilevile, kilimo hiki kilizuia mmomonyoko wa udongo na kuongeza rutuba kutokana na mboji ya majani ya miparachichi. Baada ya Mwagito kupata mafanikio, vijana wengine wa kijijini kwao walifuata nyayo zake kwa kuanzisha mashamba ya miparachichi. Mwagito alifurahi kuona kijiji chao kinastawi kutokana na vijana wengi kuwa na maisha mazuri.
Maswali
Zingatia
Urejeshi ni dhana ya kisarufi inayoonyesha tendo la kurejeshwa kwa nomino tajwa katika sentensi. Katika lugha ya Kiswahili, urejeshi huoneshwa kwa kutumia viambishi patanishi vya urejeshi. Viambishi hivi huweza kupachikwa ndani ya kitenzi (kabla ya mzizi) au mwishoni mwa kitenzi. Vilevile, viambishi vya urejeshi huweza kupachikwa katika umbo amba-.
Kwa mfano:
(a) Kiambishi rejeshi kabla ya mzizi:
(i) Vifaranga walioletwa wana afya nzuri.
(ii) Humo ulimoingia mnatisha.
(iii) Tabibu anayekuja atakuhudumia kwa umakini.
(iv) Mwanafunzi anayesoma kwa bidii hufaulu mtihani.
(b) Kiambishi rejeshi mwishoni mwa kitenzi
(i) Jambo lisemwalo linasikitisha wengi.
(ii) Nyumba ijengwayo ni ya babu.
(iii) Mtu aishiye hapa ni mjomba wangu.
(iv) Mwanafunzi apigaye kelele, ataadhibiwa.
(c) Kiambishi rejeshi kwenye umbo amba-
(i) Kitabu ambacho nimenunua, kimepotea.
(ii) Shule ambayo nimesoma, iko mbali.
(iii) Kijana ambaye hana nidhamu hafanikiwi.
(iv) Kamba ambazo umenunua zimekatika.
Katika mifano hiyo, viambishi vilivyokolezwa wino ni viambishi rejeshi. Viambishi hivyo vinafanya tendo lirejeshwe kwa nomino tajwa.
Urejeshi hufuata mfumo wa ngeli za upatanisho wa kisarufi. Hivyo, viambishi rejeshi hupatana na nomino kulingana na mfumo wa ngeli za upatanisho wa kisarufi.
Urejeshi kulingana na ngeli za nomino unaoneshwa katika Jedwali la 1.2.
Jedwali la 1.2: Viambishi rejeshi kulingana na ngeli za nomino za upatanisho wa kisarufi
| Na. | Aina ya ngeli | Viambishi vya ngeli | Viambishi vya urejeshi | Mifano |
| 1. | YU-/A-WA | YU- A- WA- | -YE- -YE- -O- | Mbuzi aliyepotea yuaja zizini. Mbuzi aliyepotea yumo zizini. Mbuzi waliopotea wamo zizini. Mzazi aliyekuja ametoa zawadi. Wazazi waliokuja wametoa zawadi. |
| 2. | U - I | U- I- | -O- -YO- | Mti ulionipa umestawi. Miti uliyonipa imestawi. |
| 3. | LI-YA | LI- YA- | -LO- -YO- | Koti lililofuliwa limekauka. Makoti yaliyofuliwa yamekauka. |
| 4. | KI-VI | KI- VI- | -CHO- -VYO- | Kiazi ulichopanda kimeota. Viazi ulivyopanda vimeota. |
| 5. | I-ZI | I- ZI- | -YO- -ZO- | Kalamu iliyonunuliwa imepotea. Kalamu zilizonunuliwa zimepotea. |
| 6. | U-ZI | U- ZI- | - O- -ZO- | Uzi ulioshonea umekwisha. Nyuzi ulizoshonea zimekwisha. |
| 7. | U-YA | U- YA- | - O- -YO- | Uovu uliokithiri ukomeshwe Maovu yaliyokithiri yakomeshwe |
| 8. | KU- | KU- | -KO- | Kucheza kusikovutia kunachosha. Kuchora kwake kulikozoeleka kutazingatiwa. |
| 9. | PA-MU-KU- | PA- MU- KU- | -PO- -MO- -KO- | Hapo ulipokaa pamelowa. Humo ulimoingia mmejaa. Huko unakokwenda hakuna kitu. |
Shughuli ya 1.4
1. Tumia vyanzo kama vile maktaba au mtandao kusoma hadithi mbalimbali, kisha fanya yafuatayo:
2. Buni mada uipendayo, kisha andika kifungu cha habari chenye viambishi vya urejeshi kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi.
Zoezi la 1.2
1. Bainisha viambishi vya urejeshi katika sentensi zifuatazo:
2. Bainisha aina ya ngeli kwenye sentensi zilizopo katika swali la 1.
3. Unafikiri ni kwa namna gani urejeshi unahusiana na ngeli za nomino?
4. Tunga sentensi kumi (10) zenye urejeshi za ngeli tofauti.
Kuandika kifungu cha habari kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi
Shughuli ya 1.5
Chunguza picha ifuatayo, kisha andika kifungu cha habari kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi.
|
|
Zingatia
Kifungu cha habari huweza kubeba taarifa au ujumbe kuhusu mtu, vitu, hali, tukio au jambo fulani. Kifungu cha habari hupaswa kuandikwa kwa kuzingatia mtiririko mzuri, unaojumuisha mwanzo, kiini na mwisho. Mtiririko huo unapaswa kuwa na mantiki, yaani kuwa na ushikamani wa maana na kisarufi. Pia, uwasilishaji wa taarifa au ujumbe katika kifungu cha habari vinapaswa kuwa na maana kwa wasomaji, yaani kizingatie hadhira husika na muktadha wao. Aidha, kifungu cha habari kinachoandikwa kinapaswa kitoe taarifa sahihi na halisi. Hali hii humlazimu mwandishi kutafuta taarifa kutoka vyanzo sahihi kuhusu jambo analoliandikia. Vilevile, kifungu cha habari kinapaswa kutumia lugha rahisi, yenye mvuto, na inayoeleweka kwa walengwa. Kadhalika, uandishi wa kifungu cha habari unapaswa kuzingatia kanuni za kisarufi.
Zoezi la marudio
1. Jibu maswali yafuatayo kwa kuandika herufi ya jibu sahihi.
(i) Mende anapenda kula uchafu. Neno lililopigiwa mstari lipo katika ngeli ipi?
(ii) __________ mna watu wengi.
(iii) Neno "papai" linaingia katika ngeli ipi?
(iv) "Shangazi yuko shambani". Neno lililopigiwa mstari katika sentensi hiyo lipo katika ngeli gani ya upatanisho wa kisarufi?
(v) Uzi ulionunuliwa umekatika. Kiambishi rejeshi -o- kipo katika ngeli ipi?
2. Jaza nafasi zilizoachwa wazi kwa kutumia maneno sahihi.
3. Tofautisha dhana zifuatazo huku ukitoa mifano:
4. Kwa kutumia mifano, husianisha upatanisho wa kisarufi na urejeshi.
5. Kwa kutumia viambishi ngeli vya urejeshi, tunga sentensi kumi, kisha bainisha viambishi vya urejeshi ulivyovitumia.
6. Chagua mada moja kati ya hizi zifuatazo, kisha andika kifungu cha habari kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi.
www.learninghubtz.co.tz