KISWAHILI FORM ONE SUBJECT NOTES
CHAPTER : 1  MAWASILIANO

KIDATO CHA KWANZA

MADA YA KWANZA

MAWASILIANO:

Mawasiliano ni upashanaji habari baina ya watu wawili au zaidi kwa kutumia njia ya ana kwa ana, simu, barua na teleksi.

Hivyo basi, mawasiliano huunganisha watu katika nyanja mbalimbali za maisha. Hata hivyo, mawasiliano hayafanywi tu baina ya watu bali hata wanyama huweza kufanya mawasiliano kwa namna anuai.

NYANJA ZA MAWASILIANO:

Zipo nyanja kuu tatu za mawasiliano, ambazo ni:-

(i) Ishara

(ii) Miondoko ya mwili na ala za sauti.

(iii) Lugha.

(i) Ishara: Ishara ni alama yenye kuwakilisha jambo fulani.

Kwa mfano; Mtumiaji wa ishara, anapotaka kumpa ishara mwenzake ili akatae jambo fulani akiwa kwenye kundi la watu hufanya ishara ya kufinya jicho. Basi mtu huyo anapotekeleza agizo la huo mwenzake, basi watu hao wawili wanakuwa wamekuwa wamefanya mawasiliano kwa kupitia uwanja wa ishara.

Baadhi ya ishara ni hizi zifuatazo:

a) Kutoa sauti fulani, kama vile kunguruma.

b) Kutikisa kichwa chini na juu – maana yake ni kukubalianan na jambo fulani.

c) Kutikisa / ua kuzungusha kichwa kushoto na kulia – maana yake ni kutokubaliana na jambo fulani.

d) Kuinua juu na kushusha chini mabega – maana yake kukataa jambo fulani.

e) Mnyama kama vile mbwa, kuchezesha chezesha mkia wake – maana yake amefurahi kumwona mtu anayemfahamu na aliyemzoea.

Hivyo basi, njia hii ya mawasiliano kwa kutumia ishara hutumiwa na binadamu na wanyama. Wanyama na binadamu huweza kufanya mawasiliano kwa njia anuai. Mfano binadamu hupiga makofi ili kuashiria kupongeza na kusifu jambo fulani lililozungumziwa na mtu fulani. Mbwa hubweka kwa sauti kuu kuashiria uwepo wa hali isiyo ya kawaida katika mazingira ya nyumbani.

(ii) Ala za sauti na miondoko ya mwili ni uwanja mwingine wa mawasiliano.

Kwa mfano; Kupiga filimbi, kupiga ngoma, kupiga mbinja, kupiga kengele na baragumu ni aina ya mifano iliyomo kwenye uwanja huu. Askari hupiga filimbi wakati anapofukuza mwizi ili kuashiria watu weingine wasaidie katika zoezi hilo la kumkamata. Mwamuzi uwanjani hupuliza kipenga ili kuashiria madhambi yaliyofanywa na mchezaji fulani dhidi ya mchezaji mwingine.

Miondoko ya mwili kama vile kucheza cheza, kuinua mikono na kunyoosha mkono na kurukaruka ni mifano ya miondoko ya mwili.

Wanyama na binadamu hutumia uwanja huu wa mawasiliano kwa namna mbalimbali.

(iii) Lugha:

Lugha pia ni nyanja ya mawasilianao.

Lugha ni nini? Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu za kusemwa na binadamu zenye kubeba maana, zilizokubaliwa na jamii fulani ili zitumike katika mawasiliano.

MAMBO YA MSINGI YALIYOMO KWENYE DHANA YA LUGHA:

(i) Lugha ni mfumo wa sauti: yaani lugha hupangiliwa vizuri kwa kutumia sauti mbalimbali. Sauti za lugha zipangiliwe hovyo hovyo bila kuwa na utarabutu maalumu, hulinganishwa na kelele.

(ii) Lugha ni sauti za nasibu: Lugha ilizuka tu. Hakuna kikao chochote kilichokaliwa na binadamu katika kutengeneza lugha.

(iii) Lugha hutumiwa na binadamu: Lugha hutumiwa na binadamu, wanayama wengine hawatumii lugha katika mawasiliano miongoni mwao, bali hutumia nyanja nyingine za mawasiliano.

(iv) Lugha huwa na maana: Lugha huwa na maana, ni kwamba sauti za lugha na maneno mbalimbali yanayotolewa na binadamu huwa na maana. Sauti za lugha zinazotolewa pasipo kuleta maana, basi sauti hizo hazina sifa ya kuitwa lugha. Sauti zinazotolewa na wanyama mbalimbali hazina maana ambayo inaweza kueleweka na binadamu. Kwa hali hiyo, hazina sifa ya kuitwa lugha.

(v) Lugha ni chombo cha mawasiliano katika jamii. Lugha ni nyenzo ya mawasiliano. Watu hupashana habari mbalimbali miongoni mwao kwa kutumia lugha.

Hivyo basi, lugha hutumiwa na binadamu, katika mawasiliano. Wanyama hawana sifa ya kutumia lugha kwa sababu hawana uwezo wa kutengeneza sauti za lugha zenye mfumo maalum, hawatoi sauti zenye kubeba maana ambayo zinaeleweka kwa binadamu na pia wanyama siyo binadamu. Sauti za lugha husemwa na binadamu tu.

Lugha hujengwa kwa maneno. Maneno huungwa kwa vitamkwa vyenye mpangilio maalumu ambao hulipa neno maana. Maneno ya kipangwa kwa njia maalum hutoa kauli zenye kuleta mawasiliano baina ya wazungumzaji. Muundo wake huanzia vitamkwa, mofimu, maneno, virai, vishazi, sentensi ambazo hupangiliwa kwa njia maalumu.

SIFA ZA LUGHA

Lugha ina sifa zifuatazo:

(i) Huhusisha mzungumzaji na msikilizaji.

(ii) Huathiri na huathiriwa.

(iii) Hubadilika kulinganan na wakati na mazingira

(iv) Lugha zote ni bora. Hakuna lugha iliyo bora kuliko nyingine.

(v) Lugha ina utamaduni wake

(vi) Lugha huwa na maana.

DHIMA YA LUGHA KATIKA MAWASILIANO:

(i) Lugha ni chombo cha mawasiliano. Watu hupashana habari mbalimbali kwa kutumia lugha.

(ii) Lugha hutambulisha jamii. Wazungumzaji wa lugha hutambuliwa wanapotumia lugha fulani, mfano, waswahili huzungumza lugha ya kiswahili.

(iii) Lugha hujenga na kudumisha ushirikiano. Wazungumzaji wa lugha fulani, huwa wamoja wanapozungumza lugha moja.

(iv) Lugha hujenga na kudumisha utamaduni wa jamii. Kwa mfano, kusalimiana kwa kushikana mikono.

(v) Lugha hutumika katika kutolea elimu.

LUGHA FASAHA:


Lugha fasaha ni lugha inayozingatia taratibu za kusarufi na mantiki ya lugha husika.

SIFA ZA LUGHA FASAHA:

(i) Ni lugha sahihi inayokubalika kwa misingi ya kisarufi.

(ii) Huwa na utamaduni wake

(iii) Huwa na sarufi yake

(iv) Hukubaliwa na wazawa wa lugha

(v) Huwa na matamshi sahihi na lafudhi inayokubalika.

UMUHIMU WA KUTUMIA LUGHA FASAHA.

(i) Hudumisha taratibu za kisarufi za lugha. Lugha ya kiswahili kwa mfano, inakanuni zake ambazo husimamia lugha hiyo. Endapo kanuni na taratibu hizo zikipuuzwa, huweza kuondoa maana fasaha ya neno au sentensi.

(ii) Hudumisha kaida za lugha kutegemea na mila na desturi.

(iii) Hujenga na kukuza hadhi ya lugha.

(iv) Hufanikisha mawasiliano kwa watu mbalimbali.

(v) Huongeza msamiati wa lugha. Maneno yanayokubalika huwa ni sehemu ya msamiati wa lugha husika.

MADHARA YA KUTOTUMIA LUGHA FASAHA:

(i) Kuvunjiwa kwa kanuni za kisarufi.

(ii) Kukwamisha mawasiliano

(iii) Kudumishwa kwa lugha

(iv) Kudhoofisha kaida za lugha

(v) Kutoongezeka kwa msamiati wa lugha.

MATAMSHI NA LAFUDHI YA KISWAHILI.

Matamshi sahihi: Utumiaji wa matamshi sahihi ninamna ya kutamka maneno katika hali inayozingatia kanuni zote za kisarufi za maneno hayo. Neno linapotamkwa katika hali isiyo sahihi husababisha neno au sentensi, hutoa maana isiyoeleweka.

Mfano, kurara badala ya kulala.

Ili kutoa maana inayoeleweka, kuna mambo muhimu ya kuzingatia katika utoaji wa sauti, ambayo ni kiimbo na mkazo.

(i) Kiimbo

Kiimbo ni utaratiby maalumu wa kupanda na kushuka kwa mawimbi ya sauti wakati wa utamkaji wa sauti za lugha. Lugha ya kiswahili huwa na kiimbo ambapo sauti huwa juu, katikati na chini.

Mfano,

a) Mjomba amekuja. (maelezo)

………………………………………… (kiimbo cha katikati)

b) Mjomba amekuja? (swali)

………………………………………….(kiimbo cha juu)

c) Mjombo amekuja (mshangao)

………………………………………….(kiimbo cha chini)

(ii) Mkazo:
Mkazo ni nguvu ya ziada inayotumika kutamka silabi mojawapo ya neno kuliko silabi nyingine au zingine.

Silabi yenye mkazo huwa inatamkwa kwa nguvu nyingi kuliko ile isiyokuwa na mkazo. Ni muhimu kutumia mkazo ipasavyo wakati wa utumikaji wa lugha ili kuondoa mkanganyiko wa maana.

Matumizi mabaya ya mkazo huweza kusababisha matamshi yasiyo sahihi. Kwa kawaida mkazo katika lugha ya kiswahili huwekwa katika silabi ya pili kutoka mwisho.

Mfano;

  • Barabara – Njia pana ipitayo magari.
  • Barabara – sawasawa/maridhawa.

LAFUDHI:

Lafudhi ni namna ya mtu kutamka maneno ambayo hutambulisha mahali anakotokea. Lafudhi inaweza kutambulisha jamii au aneo analotokea mtu na anavyozungumza.

Mfano, Kizungu, kihindi, kiarabu, kichaga, kisukuma na kihaya.

Mfano: Mbusi badala ya mbuzi (wamasai)

TANZU ZA LUGHA

Neno tanzu lina maana ya matawi. Lugha ina tanzu kuu mbili, ambazo ni sarufi na fasihi.

(i) Sarufi:

Sarufi ni sheria/taratibu zinazosimamia lugha husika. Sheria na taratibu hizo zinapokiukwa huwa zinakuwa zimeharibu hiyo lugha husika.

Mfano: Mzungumzaji wa lugha ya kiswahili anaposema “nimeenda kwa John nimemkutaga hayupo”. Mzungumzaji huyu wa lugha amekiuka sarufi ya kiswahili. Mzungumzaji huyu alipaswa kusema, nimeenda kwa John lakin sikumkuta.

Tanzu za sarufi:

Sarufi ina tanzu kuu nne, nazo ni;

(i) Sarufi sauti/matamshi (fonolojia)

(ii) Sarufi maumbo (mofolojia)

(iii) Sarufi muundo (sintaksia)

(iv) Sarufi maana (semantiki)

(i) Sarufi sauti: Sarufi sauti hujihusisha na matamshi ya sauti za lugha. Sauti za lugha zisipotamkwa kwa usahihi, neno huleta maana tofauti au kupoteza maana kabisa.

Kwa mfano: Mtumiaji wa lugha anapotamka neno “tosa” badala ya neno “toza” atakuwa amepoteza maana ya neno la awali. Hii in maana kwamba,

Toza – Chukua vitu kama vile pesa kutoka kwa mtu kuwa ni ushuru, kodi au fidia.

Tosa – Tia kitu katika kiowevu kama vile mafuta au maji.

Hivyo basi, sauti “z” imetamkwa kama sauti ‘s’, hivyo maana ya neno ‘toza’ imebadilika na kubeba maana ya neno ‘tosa’

Aina za sauti za lugha.

Sauti za lugha zipo za aina kuu mbili, nazo ni:-

a) Irabu na

b) Konsonanti.

(a) Irabu: Ni sauti za lugha ambazo hutamkwa pasipo mzuio wa hewa itokayo mapafuni kupitia katika chembe ya kinywa na chembe ya pua. Katika kiswahili, irabu zipo tano. Nazo ni:-

(i), (e), (a), (o) na (u)

(b) Konsonanti: Ni sauti za lugha ambazo hutamkwa kwa kuzuia hewa itikayo mapafuni na kisha kuiachia. Katika lugha ya kiswahili, zipo konsonanti kumi na tisa (19). Nazo ni (b), (ch), (d)…………. (z). Katika alfabeti ishirini na sita (26), sauti (q) na sauti (x) hazimo kwenye sarufi ya lugha ya kiswahili.

(ii) Sarufi maumbo: Sarufi maumbo ni taaluma inayohusi na kushughulika na jinsi maneno yanavyoundwa na kazi yake katika sentensi. Kipashio cha msingi cha sarufi maumbo huitwa mofimu. Mofimu ni kipashio cha lugha chenye maana. Mfano neno analima, limeundwa na mofimu a – na – lim – a.

(iii) Sarufi muundo: Sarufi muundo ni taaluma inayoshughulikia mpangilio na mfuatano wa maneno katika sentensi.

Mfano:

  • Uchumi wetu umeanza kuimarika
  • Kuimarika uchumi umeanza wetu.

Sentensi ya kwanza in ampangilio unaokubalika katika sarufi ya kiswahili wakati sentensi ya pili ina mpangilio wa maneno ambao haukubaliki katika sarufi ya kiswahili.

Hivyo basi, manneo katika sentensi yakipangwa vizuri kwa mujibu wa sarufi ya lugha husika huleta maana lakini yasipopangwa vizuri hayaleti maana na huweza kupotosha maana.

(iv) Sarufi maana. Sarufi maana ni taaluma ambayo hushughulikia maana katika sentensi. Maanan katika sentensi isipozingatiwa huzuia mawasiliano au ujumbe husika.

Mfano:

Baba Nuru leo amenunua mbuzi. Sentensi hii ina maana mbili, kama ifuatavyo:-

(i) Baba yake Nuru amenunua kibao cha kukunia nazi

(ii) Baba yake Nuru amenunua mbuzi kwa ajili ya kufuga.

www.learninghubtz.co.tz

COMING
Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256