SURA YA 01 : Dhana ya Historia ya Tanzania na Maadili


UTANGULIZI

Katika sura hii utajifunza kuhusu dhana ya Historia ya Tanzania na Maadili. Pia, utajifunza kuhusu vitendo vya kimaadili. Vilevile, utajifunza umuhimu wa Historia ya Tanzania na Maadili nchini. Umahiri utakaoupata katika sura hii utakuwezesha kuthamini Historia ya Tanzania, Maadili ya Tanzania na kutenda vitendo vya maadili.

Fikiri

Dhana ya Historia ya Tanzania na Maadili

Kazi ya kufanya namba 1

Fanya uchunguzi mdogo kuhusu tukio mojawapo unalolikumbuka katika maisha yako, kisha wasilisha darasani.

Matukio tuliyoyaandika yanaonesha mfululizo wa mambo yaliyotokea katika maisha yetu katika vipindi tofauti. Mfululizo huu wa matukio ni sehemu ya historia ya maisha yetu. Ni historia kwa sababu matukio haya yanajenga kumbukumbu katika maisha yetu. Historia inaweza kuhusu maisha yetu binafsi, familia, shule, jamii inayokuzunguka, nchi au dunia.

Kazi ya kufanya namba 2

Andika matukio yaliyotokea na kuacha kumbukumbu katika shule yako.

Matukio tuliyoorodhesha ni sehemu ya historia katika shule yetu. Matukio haya ni sehemu ya historia ya shule yetu kwa kuwa yameacha alama ya kumbukumbu katika shule. Dhana ya Historia ya Tanzania na Maadili imeundwa na dhana ya historia ya Tanzania na dhana ya maadili. Dhana ya historia ya Tanzania imebeba maana, matukio ya kihistoria Tanzania na umuhimu wa historia ya Tanzania. Dhana ya pili inahusu maadili, ambayo imebeba maana, vitendo vya maadili na umuhimu wa maadili nchini. Tunapojifunza dhana hizi kwa pamoja, tunapata nafasi ya kubaini maadili yetu na misingi ya ujenzi wa maadili katika historia ya jamii za Kitanzania. Hivyo, kuiwezesha jamii ya sasa kukuza na kulinda maadili ya Watanzania kwa sasa.

Maana ya historia ya Tanzania

Inawezekana umewahi kusikia kuhusu Historia ya Tanzania au maeneo yenye historia ya Tanzania. Historia ya Tanzania ni nini?

Kazi ya kufanya namba 3

Soma matini kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwemo mtandao, kuhusu maana ya historia ya Tanzania.

Historia ya Tanzania ni elimu kuhusu matukio yaliyotokea nchini Tanzania tangu mwanzo wa maisha ya watu mpaka leo. Pia, inahusu namna matukio hayo yalivyotokea. Kwa ujumla, historia ya Tanzania ina mfululizo wa matukio yaliyotokea katika nchi na jinsi yalivyotokea. Mfululizo huo ndio uliounda uthibitisho wa historia ya Taifa la Tanzania tulilonalo kwa sasa. Mfululizo na muunganiko wa matukio haya ndio historia ya Tanzania. Tutajifunza kuhusu matukio ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yenye kumbukumbu za historia ya Tanzania. Je, unafikiri kuna umuhimu gani wa kujifunza historia ya Tanzania?

Umuhimu wa kujifunza Historia ya Tanzania

Kazi ya kufanya namba 4

Fanya uchunguzi kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa kusoma matini na maktaba mtandao na eleza umuhimu wa kujifunza historia ya Tanzania.

Mara nyingi tunashindwa kuanza jambo jipya kwa kukosa taarifa za awali. Mambo tunayoyaona sasa yanaweza kuwa yamewahi kutokea zamani. Taarifa za kihistoria ni muhimu kwetu, kwa jamii na Taifa. Hivyo, kujifunza historia ya Tanzania ni muhimu kwa sababu inatupa:

  1. Taarifa za matukio yaliyotokea zamani na jinsi yalivyotokea;
  2. Funzo la kutuwezesha kuendeleza mambo mazuri;
  3. Elimu ya kuboresha mipango ya sasa na kupata matokeo mazuri;
  4. Elimu ya kukabili changamoto tunazokutana nazo kwa sasa;
  5. Dira ya kutatua mambo ya sasa;
  6. Sababu ya kufanya maamuzi sahihi kwa sasa;
  7. Kukuza na kulinda uzalendo kwa sasa;
  8. Kuthamini historia kama sehemu ya urithi wa Taifa; na
  9. Kukuza na kulinda mila na desturi kama sehemu ya maadili yetu.

Vyanzo vya Historia ya Tanzania

Tunaweza kupata taarifa za historia ya Tanzania kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo kusikiliza masimulizi au kusoma vitabu. Pia, katika makumbusho ya Taifa na binafsi na maeneo yenye hifadhi za nyaraka kuna taarifa za kihistoria. Tunaweza kupata taarifa za historia kutoka kwenye taarifa za kianthropolojia, akiolojia na isimu historia.

Vilevile, tunaweza kuuliza watu waliotangulia ili kupata taarifa hizi. Vyombo vya habari na tovuti vinaweza pia kuwa ni vyanzo vya kupata taarifa hizo. Vyanzo hivi vinawezesha kujifunza historia ya Tanzania ya nyakati tofauti kama vile kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni.

Dhana ya maadili

Kazi ya kufanya namba 5

Soma vyanzo mbalimbali, ikiwemo maktaba mtandao, kuhusu maana ya maadili.

Maadili ni mwenendo au utendaji uliokubalika katika jamii. Maadili hueleza matendo yanayofaa na matendo yasiyofaa katika jamii husika. Maadili yanaweza kulenga katika tabia au matendo ya kufuata katika familia, shule, dini, jamii au Taifa. Maadili huwezesha watu kuishi kwa kuzingatia utu, upendo na tabia njema. Ujenzi wa maadili si jambo la muda mfupi, bali hufanyika kwa kipindi fulani na kukubaliwa na

jamii nzima kuwa ndizo tabia, kanuni na sheria za kikundi au jamii husika.

Soma matendo yanayofaa na yasiyofaa katika sehemu A, kisha fanya zoezi linalofuata.

A


B


C


Matendo yanayofaa na yasiyofaa


Matendo yanayofaa Matendo yasiyofaa
kufanya kazi, kutoroka nyumbani, kucheza, kuwaheshimu watu waliokuzidi umri, kuchelewa kurudi nyumbani, kufanya kazi za nyumbani, kuwasalimia watu wengine, kuwatukana watu wengine, kuwafinya wenzako, kusema ukweli, kupigana na wenzako, kuiba, kutokupenda kufanya kazi, kuwahi shuleni, kuwatembelea wagonjwa, kuacha kuwasalimia wenzako, kuacha kuwasalimia watu waliokuzidi umri, kuacha vyombo mezani baada ya kula, kukataa kula chakula, kuosha chombo chako baada ya kula, kuacha kufanya usafi, kuwanyanyasa na kuwadhalilisha

wenzako, kuwasaidia wasiojiweza, kutoroka shuleni, kusema uongo, kutokumaliza mazoezi ya darasani



Zoezi la 1

  1. Andika matendo yanayofaa katika sehemu B na yasiyofaa katika sehemu C.
  2. Eleza ni kwa nini matendo yaliyoorodheshwa katika sehemu B ni matendo yanayofaa.
  3. Eleza ni kwa nini matendo yaliyoorodheshwa katika sehemu C ni matendo yasiyofaa.


Matendo yanayozingatia kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa katika familia, shule au jamii ni matendo yanayofaa. Matendo hayo ni nguzo ya kujenga maadili na kuondoa ugomvi katika mazingira yanayotuzunguka. Maadili ya jamii zetu husisitiza uzingatiaji wa kanuni, miongozo, mila na desturi za jamii husika. Tabia zisizozingatia maadili ya familia, shule au jamii ni matendo yasiyofaa. Maadili katika jamii husisitiza matendo yanayofaa. Lengo ni kuiwezesha jamii kuishi katika misingi ya utu, uadilifu, umoja, upendo, usawa na amani.

Vitendo vya kimaadili

Kazi ya kufanya namba 6

Chunguza na andika vitendo vya kimaadili vinavyofanywa shuleni au nyumbani.

Vitendo vya kimaadili vinahusisha tabia na vitendo ambavyo vinakubalika katika jamii. Vitendo vya kimaadili hutofautiana kulingana na tamaduni za kila jamii.

Kusaidia wazee na watu waliotuzidi umri

Kusaidia wazee na watu waliotuzidi umri ni mojawapo ya matendo ya kimaadili. Vijana au watoto wanawajibika kuwasaidia mizigo na kazi mbalimbali watu waliowazidi umri, nyumbani na shuleni. Kitendo cha kijana au mtoto kumsaidia mzee na mtu aliyemzidi umri huonesha upendo na heshima kama ilivyo katika Kielelezo namba 1.

Kielelezo namba 1: Mtoto akimsaidia mzigo mzee


Kuwatunza, kuwathamini na kuwalea wazee ni matendo ya kimaadili. Maadili yanasisitiza kutembelea wazee na kuwahudumia kwa kuwapa zawadi na chakula kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 2. Pia, tunasisitizwa kuwasaidia kazi mbalimbali.

Kielelezo namba 2: Kijana akimwandalia mzee chakula

Kuheshimu watu wazima

Kuwaheshimu wazee na watu waliokuzidi umri ni matendo ya kimaadili. Watu walio na umri mdogo wanawajibika kuwaheshimu watu waliowazidi umri. Tangu kale, watu wenye

umri mkubwa waliheshimika. Jamii iliamini kuwa watu wenye umri mkubwa wana maarifa, busara na ufahamu wa mambo zaidi ya wenye umri mdogo. Mfano, vijana walilazimika kuwapisha viti watu waliowazidi umri ili kuonesha heshima.

Ilikuwa ni jambo la aibu kwa kijana kukaa kwenye kiti wakati watu waliomzidi umri wamesimama kama ilivyo katika Kielelezo namba 3 (a).

Kielelezo namba 3 (a): Vijana wamekaa wakati mtu mzima amesimama

Vijana walitakiwa kuwapisha viti watu wenye umri mkubwa kama ilivyo katika Kielelezo namba 3 (b). Hii ilionesha heshima na adabu kwa watu wazima.

Kielelezo namba 3 (b): Kijana amesimama kumpisha mtu mzima kiti akae

Pia, wazazi waliitwa kwa majina ya watoto wao, kama vile mama Juma au baba Bahati. Hii ilifanyika ili kuwapa heshima kama wazazi. Vilevile, ilikuwa mwiko na jambo lisiloonesha heshima wazazi kuitwa kwa majina yao na watoto au vijana.

Kusalimiana

Kusalimiana ni mojawapo ya matendo ya maadili. Wadogo kwa umri walitakiwa kusalimia waliowazidi umri. Pia, watu wa rika moja walisalimiana ili kuonesha kujali na utu kwa watu wengine. Jamii zilisalimiana nyakati zote, asubuhi, mchana na jioni. Wanajamii walisalimiana kwa ama kushikana mikono, kupiga goti, kushika kichwa, kusimama, kukaa chini au kukumbatiana ili kuonesha heshima. Angalia mfano wa matendo ya kusalimiana katika Kielelezo namba 4.

Kielelezo namba 4: Vitendo vya maadili katika kusalimiana

Tofauti katika matendo ya kusalimiana hutegemea tamaduni za jamii husika. Mtoto alipaswa ama kusimama au kupiga goti anaposalimia watu waliomzidi umri. Kitendo cha kijana kukaa wakati anamsalimia mtu mzima si kitendo cha kimaadili ya Kitanzania.

Zoezi la 2

  1. Taja vitendo vya kimaadili vinavyoonesha heshima vinavyofanyika shuleni.
  2. Taja vitendo vya kimaadili vinavyoonesha heshima vinavyofanyika nyumbani.

Vitendo vya maadili katika malezi na ulinzi wa watoto

Malezi na ulinzi wa watoto ni sehemu ya matendo ya kimaadili. Tangu kale jamii zilisisitiza malezi ya watoto. Wazazi walitenga muda wa kukaa na watoto wao. Hii iliwasaidia wazazi na

watoto kukaa na kuongea pamoja mambo yanayohusu familia na kujua changamoto zao kama ilivyo katika Kielelezo namba 5.

Kielelezo namba 5: Wazazi na watoto wakiongea pamoja

Pia, wazazi wanawajibika kulinda usalama wa watoto wakati wote. Ulinzi na malezi ya watoto katika jamii ulifanyika kwa kushirikiana na lilikuwa jukumu la jamii nzima. Hata sasa jamii

inapaswa kulinda usalama wa watoto. Mfano, wazazi wana wajibu wa kuwapeleka watoto shuleni kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 6 na kuwafuata wakati wa kurudi nyumbani ili kuwalinda. Pia, ni muhimu kuweka mifumo imara katika jamii ili kulinda usalama wa watoto shuleni na nyumbani.

Kielelezo namba 6. Watoto wakipelekwa shuleni na mzazi

Vitendo vya maadili katika kazi

Kufanya kazi kwa bidii ni jambo lililosisitizwa katika maadili ya jamii. Tabia ya kupenda na kufanya kazi ni matendo ya kimaadili katika jamii. Hivyo, kila mtu anapaswa kupenda na kufanya kazi kwani kazi ni msingi wa maendeleo. Tangu kale, uvivu ulipingwa na jamii nzima. Watu katika jamii walithaminiwa kutokana na uwezo wao wa kufanya kazi. Mtu mvivu alipingwa kwa kukiuka maadili ya jamii. Viongozi walichaguliwa kwa kuzingatia uwezo wao wa kufanya kazi. Kielelezo namba 7 kinaonesha watoto wakifanya kazi mbalimbali nyumbani.

Kielelezo namba 7: Watoto wakifanya kazi mbalimbali nyumbani

Matendo ya maadili katika kusaidiana

Jamii zetu zinasisitiza matendo ya kuwasaidia watu wengine na kusaidiana. Kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu ni sehemu ya maadili ya jamii za Kitanzania. Kila mmoja anao wajibu wa kuwasaidia watu wanaohitaji msaada kama ilivyo katika Kielelezo namba 8. Kuwasaidia watu wengine kunasaidia watu kupendana, kusaidiana na kushikamana.

Kielelezo namba 8: Wanafunzi wakimsaidia mwanafunzi mwenzao

Kazi ya kufanya namba 7

Andika matendo mengine ya kimaadili katika kusaidiana shuleni na nyumbani.

Kuhusiana na watu wengine

Uhusiano mwema ni sehemu ya matendo ya kimaadili. Uhusiano mwema huzuia malumbano na ugomvi kati ya mtu na mtu. Uhusiano mwema kati yetu hujengwa kwa kuonesha upendo, kuheshimiana na kutosema uongo dhidi ya watu wengine. Pia, matendo kama kuwasiliana kwa lugha isiyo ya ukali na matusi na kuwasikiliza watu wengine yanaashiria uhusiano mwema. Vilevile, matendo ya kucheza na kusoma pamoja huonesha uhusiano mwema kati yetu na watu walio karibu nasi.

Chunguza matendo katika picha zifuatazo katika Kielelezo namba 9, kisha jibu zoezi linalofuata.

Kielelezo namba 9: Matendo ya kuhusiana shuleni

Zoezi la 3

1. Eleza matendo yanayofanyika katika Kielelezo namba 9.

2. Eleza faida za matendo yanayofanyika katika Kielelezo namba 9.

Kushirikiana

Kazi ya kufanya namba 8

Fanya uchunguzi katika maeneo yanayokuzunguka na eleza matendo ya maadili katika kushirikiana.

Ushirikiano katika kazi mbalimbali kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 10 ni miongoni mwa vitendo vya kimaadili.

Kielelezo namba 10: Wanafunzi wakishirikiana kazi shuleni

Ni wajibu wetu kushirikiana katika kazi za shuleni na nyumbani. Jamii za kale zilishirikiana katika kazi zilizofanyika katika maeneo yao, kama vile kufanya usafi, kuchimba visima na kutengeneza barabara. Watu wote katika jamii wanaume, wanawake na watoto, walitakiwa kufanya kazi hizi kwa pamoja. Pia, ushirikiano ulifanyika katika shughuli za sherehe, misiba

na mazishi kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 11.

Kielelezo namba 11: Watu wakishirikiana katika msiba

Hapo kale, mtu ambaye hakushiriki katika misiba alipewa adhabu. Pengine alitengwa na jamii yote na hata kutozwa faini. Kushiriki katika misiba ni mojawapo ya vitendo vya kimaadili kwa sababu huonesha hali ya kujali na kufariji watu wengine. Tunaposhiriki misiba, tunatakiwa kusaidia kazi kwa hali na mali. Ushiriki unaweza kuwa katika kuchimba kaburi, kupika chakula na kuchota maji. Pia, tunasisitizwa kwenda kwenye misiba na chakula, maji, mafuta, kuni, fedha na mahitaji mengine. Hii inasaidia kuwezesha kufanyika kwa shughuli za msiba kwa wafiwa. Hapo kale ilikuwa ni mwiko na aibu kwenda msibani mikono mitupu.

Vilevile, kushirikiana katika sherehe ni vitendo vya kimaadili. Tangu kale, jamii zilisisitiza kushirikiana katika sherehe kama vile harusi na sherehe za mavuno. Watu walishirikiana katika sherehe kwa kutoa mchango, zawadi na vitu mbalimbali ilikufanikisha sherehe. Ushirikiano ni jambo muhimu katika jamii.

Jamii kwa sasa inaweza kukuza ushirikiano kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii. Ushirikiano hujenga upendo na umoja katika jamii.

Kazi ya kufanya namba 9

Jadili namna runinga, radio, muziki wa kizazi kipya, tamthilia, simu janja, katuni na matangazo mbalimbali yanavyochangia katika kuharibu na kukuza maadili nchini Tanzania kwa sasa.

Vyombo vya habari na matangazo vina athari mbalimbali katika maadili ya jamii kwa sasa. Watoto wana wajibu wa kuacha kuiga tabia zisizofaa ili kujenga tabia njema katika jamii ya sasa. Matendo yasiyofaa yana athari kubwa kwa mtoto, familia na jamii kwa ujumla. Pia, sisi sote tuna wajibu wa kuwaeleza watoto wengine kuacha vitendo vilivyo kinyume na maadili ili kujenga maadili yanayofaa nchini.

Kukataa vitendo vya rushwa

Rushwa ni kitendo cha kutoa au kupokea fedha au kitu cha thamani ili kutenda kitendo kilicho kinyume na haki ya mtu mwingine. Pia, kuombwa fedha au kitu cha thamani na mtu mwingine ili kupata haki usiyostahili ni vitendo vya rushwa. Kukataa vitendo vya kutoa na kupokea rushwa ni matendo ya kimaadili. Vitendo vya kutoa na kupokea rushwa hufanyika kwa lengo la kufanya upendeleo kwa anayetoa rushwa na kwa lengo la kumnyima mtu mwingine haki yake. Vitendo hivyo vinaweza kufanyika shuleni, nyumbani na maeneo mengine yanayotuzunguka.

Kazi ya kufanya namba 10

Chunguza na orodhesha vitendo vinayoashiria rushwa nyumbani na shuleni.

Vitendo vinavyoashiria rushwa ni pamoja na:

(a) Kumpatia au kupokea kitu kutoka kwa mtu mwingine mfano pipi au biskuti, ili kufanya vitendo visivyostahili au vilivyo kinyume na maadili;

(b) Kupewa au kupokea kitu ili uandikiwe au umwandikie mwanafunzi mwenzako majibu ya kazi za darasani;

(c) Kudai zawadi au fedha ili kutekeleza jambo fulani; mfano, kukubali kutumwa;

(d) Kununuliwa kitu kama vile chakula au zawadi na mtu mwingine kwa ushawishi wa kufanya vitendo visivyofaa;

(e) Kupewa lifti katika vyombo vya usafiri mara kwa mara na mtu mwingine ili kufanya vitendo visivyo vya kimaadili;

(f) Walimu kuwapa wanafunzi majibu ya mtihani kwa malipo fulani;

(g) Kutoa fedha au zawadi ili kupata upendeleo wa ziada kutoka kwa walimu, viranja, wazazi au walezi;

(h) Kupokea fedha au zawadi ili kuwafanyia watu wengine vitendo vilivyo kinyume na maadili;

(i) Mwalimu au mwanafunzi ambaye ni kiranja kupokea fedha au zawadi ili kuruhusu mali za shule kama vile vitabu, redio au televisheni kuchukuliwa na kupelekwa nyumbani kwa matumizi binafsi;

(j) Mlinzi wa shule kupokea fedha au kuahidiwa kupewa fedha ili kuruhusu vifaa vya shule kama taa, madawati, au mbao na saruji za kujengea miradi ya shule kuchukuliwa shuleni;

(k) Kupewa zawadi ili kuacha kutoa taarifa za uhalifu kwa uongozi wa shule au kwa wazazi nyumbani;

(l) Mwanafunzi kutoa au kumpa zawadi mwalimu au kiranja ili asipewe adhabu kwa kosa alilolifanya; mfano, kuchelewa kufika shuleni au kupiga kelele darasani;

(m) Mwanafunzi au mzazi kutoa au kumpa zawadi mwalimu ili atoe alama za upendeleo kwa mwanafunzi; na

(n) Dada mlezi nyumbani kupokea fedha au mali kama simu kutoka kwa mtoto na kumruhusu aende kucheza wakati mzazi ameelekeza mtoto huyo abaki nyumbani na kukamilisha kwanza kazi za shuleni na za nyumbani kabla ya kwenda kucheza.

Vitendo vya kutoa na kupokea rushwa vina madhara kwetu na kwa jamii inayotuzunguka. Baadhi ya madhara yanayoweza kutokea unapotoa au kupokea rushwa ni pamoja na:

(a) Kushindwa kupata wanafunzi waliofaulu mitihani kwa akili zao;

(b) Miradi ya shule kama vile madarasa kushindwa kukamilika kwa wakati;

(c) Kukosa wataalamu wenye uwezo stahiki nchini kutokana na wanafunzi kupata alama za mitihani wasizostahili;

(d) Kusababisha watu wengine kukosa haki zao kwa sababu ya kukosekana kwa usawa katika jamii;

(e) Kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa sababu ya kulea uzembe shuleni na nyumbani; na

(f) Kukosekana kwa maendeleo katika familia au jamii kutokana na kukosa watu sahihi wa kuleta maendeleo.

Zoezi la 4

1. Taja madhara mengine matatu ya vitendo vya rushwa. Mwanafunzi ana wajibu wa kuzuia vitendo vya rushwa katika maeneo yanayomzunguka shuleni na nyumbani. Tunaweza kufanya mambo yafuatayo ili kuepuka na kuzuia vitendo vya rushwa:

(a) Kufuata na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za shule na familia;

(b) Kusoma kwa bidii ili kuweza kufaulu mitihani bila kutafuta upendeleo;

(c) Kutotoa zawadi au pesa ili kupata upendeleo wa aina yoyote;

(d) Kumjulisha mwalimu, mzazi au mtu mwingine unayemwamini kuhusu jambo baya alilofanya mwanafunzi, mwalimu, mfanyakazi wa shule au ndugu nyumbani;

(e) Kusema ukweli wakati wote bila upendeleo ili kuwa sehemu ya msaada wa watu kupata haki zao inavyostahili;

(f) Kuwatendea mema watu wengine bila kuwa na upendeleo;

(g) Kuwaheshimu na kuwapenda watu wengine;

(h) Kukemea vitendo vya rushwa;

(i) Kupenda shule na familia kwa kuthamini na kutunza mali za nyumbani na za shuleni; na

(j) Kufanya kazi kwa bidii ili kupata mahitaji yako bila upendeleo.

Kuepuka rushwa ni vitendo vya kimaadili. Mtu anayeshiriki vitendo vya rushwa hana maadili. Mtu mwenye maadili huepuka vitendo vya rushwa ambavyo vinaweza kuleta madhara kwake,

kwa watu wengine, jamii na Taifa kwa ujumla.

Umuhimu wa vitendo vya kimaadili

Vitendo vya kimaadili vinajenga tabia za malezi bora kwa watoto. Malezi hayo ni pamoja na kuwafundisha watoto matendo yanayofaa. Tunapaswa kuendeleza vitendo vya kimaadili shuleni na nyumbani.

Kazi ya kufanya namba 11

Chunguza na eleza umuhimu wa vitendo vya kimaadili vinavyofanyika shuleni na nyumbani.

Vitendo vya kimaadili ni muhimu katika maisha yetu. Vitendo hivi hujenga umoja katika jamii bila ya kujali tofauti za kijinsi, kiimani, kielimu au rangi. Vitendo vya kimaadili ni muhimu kwa sababu husaidia:

  1. Jamii kufanya na kuthamini kazi;
  2. Kuleta usawa katika jamii bila kujali hali ya mtu;
  3. Kujenga tabia ya kuheshimiana na kuhusiana;
  4. Kujenga malezi bora katika jamii;
  5. Kulinda na kuimarisha maadili katika jamii;
  6. Kujenga tabia ya mshikamano na moyo wa kusaidiana katika jamii; na
  7. Kujenga undugu na upendo katika jamii.

Kazi ya kufanya namba 12

Andika mambo uliyojifunza kuhusu vitendo vya maadili na jinsi ya kudumisha maadili hayo nyumbani na shuleni.

Kimsingi dhana ya Historia ya Tanzania na Maadili inajumuisha mfululizo wa matukio ya kihistoria yaliyotokea nchini na maadili yaliyojengwa tangu nyakati za kale hadi sasa. Tangu kale, jamii zetu zilikuwa zikisisitiza vitendo vya kimaadili vinavyosisitiza tabia za malezi bora kwa watoto na vijana, heshima, kuheshimiana, upendo, kujali watu wengine, ushirikiano, umoja na kupenda kufanya kazi kwa bidii.

Vitendo hivi vilisitizwa kama msingi wa maendeleo katika jamii. Hata sasa, vitendo hivi vya kimaadili vinasisitizwa ili kukuza na kulinda maadili yetu. Hivyo, ni wajibu wetu kwa sasa kuendeleza vitendo vya maadili shuleni na nyumbani. Kujifunza Historia ya Tanzania na Maadili kutaisaidia jamii kwa sasa kujenga maadili, kukuza utaifa na kulinda maslahi ya nchi na rasilimali za Taifa. Kwa kufanya hivyo, tutaishi katika misingi ya utu, uadilifu, usawa, umoja na upendo.

Zoezi la jumla

Jibu maswali yafuatayo:

1. Eleza maana ya historia ya Tanzania.

2. Eleza umuhimu wa kujifunza historia ya Tanzania.

3. Jiulize, kisha andika hatua utakazochukua ikiwa:

  1. Mwanafunzi mwenzako amejikwaa na kuanguka.
  2. Mdogo wako analia.
  3. Mtu mwenye ulemavu wa uoni yuko kandokando ya barabara akihitaji kuvuka.
  4. Mwanafunzi mwenzako hana kalamu wakati wewe una kalamu mbili.
  5. Mwanafunzi mwenzako anafanyiwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji au udhalilishaji na mwanafunzi mwenzako.
  6. Mwanafunzi mwenzako anafanyiwa vitendo vya ukatili, unyanyasaji au udhalilishaji na mtu aliyekuzidi umri.
  7. Umeamka asubuhi na kukutana na watu waliokuzidi umri.
  8. Umekutana na mwalimu amebeba daftari anaelekea darasani.

4. Andika NDIYO kwa sentensi inayoashiria kitendo cha rushwa na HAPANA kwa sentensi isiyoashiria kitendo cha rushwa.

  1. Mwanafunzi amepiga kelele darasani lakini kiranja wa darasa hajaandika jina lake kwa vile ni ndugu au rafiki yake.
  2. Mwalimu amempa alama za upendeleo mwanafunzi baada ya kupewa fedha na mzazi wa mwanafunzi huyo.
  3. Mwanafunzi amechelewa kufika shuleni lakini hakuadhibiwa kwa vile kiranja alinunuliwa andazi na mwanafunzi huyo.
  4. Mlinzi nyumbani amepewa fedha ili auze mabati na saruji za ujenzi wa nyumba.
  5. Mwalimu kutoa majibu ya mtihani kwa wanafunzi kwa sababu walimpa zawadi siku yake ya kuzaliwa.

5. Eleza manufaa ya mtoto kuonywa na jamii anapokosea.

6. Taja faida nne za mtoto kuwa na tabia njema.

7. Eleza hasara za kuwa na tabia mbaya katika jamii.

8. Eleza misingi ya matendo ya kimaadili katika jamii za Kitanzania.

9. Andika mambo uliyojifunza kuhusu vitendo vya kimaadili.

10. Taja vyanzo sita (6) vya kupata taarifa za historia ya Tanzania.

Msamiati

  • Akiolojia : taaluma ya uchunguzi wa kisayansi kuhusu masalia ya mambo ya kale na utamaduni wa mwanadamu
  • Anthropolojia :taaluma inayohusu kusoma utamaduni wa historia ya maisha na maendeleo ya binadamu
  • Isimu historia : hufafanunua taarifa za mabadiliko katika lugha kwa vipindi mbalimbali
  • Kuheshimiana : kuoneshana tabia za adabu, kujali kwako na kwa watu wengine bila ubaguzi
  • Kushirikiana: hali ya watu kuungana na kufanya jambo fulani kwa pamoja
  • Makumbusho : maeneo yanayotumiwa kuhifadhi vitu vyenye historia na urithi wa kiasili na kiutamaduni
  • Tabia : kitendo kinachofanyika mara kwa mara
  • Uhusiano : hali ya kuwa na fungamano na wengine
  • Vitendo : mambo yote yanayotendwa na binadamu


www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256