Sura Ya 01 : Rasilimali asilia za Tanzania
| Utangulizi Tanzania ni nchi iliyojaliwa rasilimali asilia mbalimbali ambazo ni muhimu kwa uchumi wa wananchi na taifa kwa tafsiri hii ni pamoja na ardhi, misitu, maziwa, mito, madini, na wanyamapori mbalimbali, ambazo zote kwa pamoja zinachangia maendeleo ya nchi. Katika sura hii, tutajifunza namna ya rasilimali, rasilimali asilia zinazopatikana Tanzania, matumizi ya rasilimali asilia za Tanzania, na uhusiano kati ya rasilimali asilia na maendeleo. Uhalifu utakaojitokeza utakaoweza kutumia rasilimali asilia za Tanzania kwa maendeleo binafsi na ya taifa. |
| Fikiri Shughuli mbalimbali zinazowaingizia vipato watu wa jamii unayoishi. |
Maana ya rasilimali
Rasilimali ni vitu vinavyosaidia kufanikisha malengo yetu au kutimiza mahitaji yetu. Rasilimali zinaweza kutumika katika shughuli mbalimbali za kila siku, kama shughuli za uzalishaji au kufuriza. Rasilimali husaidia kufanyia maisha yetu kuwa rahisi na bora.
Aina za rasilimali
Kazi ya kufanya namba 1
Chukulia kwamba unatoka kuanzisha mradi wa kilimo cha mgomboga. Andaa jedwali kubainisha rasilimali muhimu ambazo utazitaji na onesha matumizi ya kila rasilimali utakayobainisha katika kufanikisha mradi huo.
Rasilimali zinaweza kuwa za aina mbalimbali, ikiwaemo rasilimali asilia kama ardhi, maji, misitu, wanyama na madini; rasilimali za kibinadamu kama ujuzi na nguvu kazi; na rasilimali mtaji kama pesa, mashine, majengo na miundombinu mingine. Kila aina ya rasilimali husaidia kwa njia tofauti kufikia malengo na kuboresha maisha yetu. Katika maktaba ya kijiografia, utajifunza kuhusu rasilimali asilia.
Rasilimali asilia
Rasilimali asilia ni vitu na malighafi za asili zinazopatikana katika mazingira na zinazumiwa na binadamu kwa matumizi mbalimbali. Mfano wa rasilimali asilia ni hewa, gesi asilia, maji, mwanga wa jua, ardhi, madini, mafuta, misitu, na wanyamapori. Kwa ujumla, rasilimali asilia zinaweza kugawanywa katika makundi makuu mawili, ambayo ni rasilimali jadidi na rasilimali zisizojadidi.
Rasilimali jadidi
Hizi ni rasilimali ambazo zinaweza kujirejesha au kuzalishwa ndani ya muda mfupi bila kuagi kiwango cha matumizi yake. Kwa mfano, mwanga wa jua, nishati ya upepo, maji na misitu.
Rasilimali zisizojadidi
Hizi ni rasilimali ambazo haziwezi kujirejesha au zinazukua muda mrefu kukundwa tena hivyo zinaisha kadri zinavyotumiwa kutumika. Mfano wa rasilimali hizi ni nishati ya mafuta, madini, na gesi asilia.
Rasilimali asilia zinazopatikana Tanzania
| Kazi ya kufanya namba 2 Chunguza maeneo mbalimbali yanayozunguka, kisha bainisha rasilimali asilia zinazopatikana katika maeneo hayo. |
Tanzania ina rasilimali asilia zenye thamani kubwa ambazo zinachangia uchumi na maendeleo ya taifa. Rasilimali hizi zinapaswa kubainishwa, kutunzwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye. Zifuatazo ni baadhi ya rasilimali asilia zinazopatikana Tanzania.
Madini
Tanzania ina rasilimali nyingi za madini, ikiwemo dhahabu, tanzanite, almasi, makaa ya mawe, shaba, chumvi, bati, nikeli, urani na vito vya thamani. Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika, ikiwa na akiba kubwa katika maeneo mbalimbali. Tanzanite ni madini ya thamani yanayopatikana
Tanzania pekee. Sekta ya madini ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania, ikivutia uwekezaji wa kigeni na kuzalisha mapato kupitia mauzo ya nje. Kielelezo namba 1 kinaonesha baadhi ya madini yanayopatikana Tanzania.
|
Kielelezo namba 1: Baadhi ya madini yanayopatikana Tanzania |
Ardhi
Tanzania ina utajiri wa rasilimali ardhi, ikiwemo maeneo ya ardhi yenye rutuba na maeneo makubwa ya malisho. Ardhi ya Tanzania ina udongo wenye rutuba unaofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama vile kahawa, chai, tumbaku, mahindi, maharage, mpunga, alizeti na mazao mengineyo. Aidha, Tanzania ina maeneo makubwa na muhimu kwa ufugaji wa mifugo mbalimbali kama vile ng’ombe, kondoo na mbuzi. Baadhi ya maeneo ya ardhi ya Tanzania ni mbuga na hifadhi za wanyamapori, misitu na vilima vya hifadhi. Pia, maeneo mengine ya ardhi hutumika kwa ajili ya makazi ya watu, viwanda na biashara. Hivyo, ardhi ni rasilimali muhimu ambayo huchochea maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania, hususani kwa kilimo na maendeleo ya mtu mmoja mmoja.
Maji
Maji ni rasilimali muhimu sana kwa uumbe hai wote wakiwemo binadamu, wanyama na mimea. Tanzania ina rasilimali nyingi za maji zinazopatikana katika vyanzo na maeneo tofauti ya nchi, ikiwemo mabwawa, mito, maziwa, bahari na maji ya chini ya ardhi. Rasilimali maji zina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na maisha ya kila siku. Baadhi ya rasilimali kubwa na muhimu za maji ni Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, na Ziwa Nyasa. Pia, kuna mito kama vile; Mto Rufiji, Ruvuma, Malagarasi, Ruvu, Wami, Kagera na Pangani na mabwawa makubwa kama vile; Julius Nyerere, Mtera, Nyumba ya Mungu na Kidatu. Watu na viumbe wengine hutegemea maji ili kuishi.
Vilevile, rasilimali maji zinasaidia kukuza kwa sekta za uchumi wa buluu. Tanzania, uchumi wa buluu unahusisha sekta mbalimbali za kiuchumi zinazotilia katika matumizi ya bahari, pwani na maji baridi kama vile; mito, maziwa na mabwawa. Sekta za uchumi wa buluu ni pamoja na uvuvi, usafirishaji, utalii, kilimo, na nishati hasa umeme unaozalishwa kutokana na maji, gesi asilia na mafuta. Aidha, uchumi wa buluu unasaidia kuboresha maisha ya watu na kutoa ajira huku ukisisitiza utunzaji wa bayonanuai na matumizi bora ya rasilimali maji.
Misitu
Misitu ni eneo lenye msusanyiko wa miti mingi mikubwa na midogo, vichaka na nyasi. Tanzania ina aina mbalimbali za misitu inayochukua takribani asilimia 40 ya ardhi ya nchi. Aina hizo ni pamoja na misitu ya milimani, misitu ya miombo, na mikoko. Misitu ni muhimu sana kwa wanyamapori na viumbe wengine kwa kuwa inatoa makazi ya wanyama na mimea mbalimbali. Misitu husaidia upatikanaji wa mbao za kujengea, kuni za kupikia, na mimea ya dawa inayotumika kutibu magonjwa. Pia, misitu husaidia kusafisha hewa na maji, pamoja na kudhibiti hali ya hewa kwa kunyonya kabonidayoksaidi kutoka angani. Aidha, misitu ya Tanzania ni chanzo cha kipato kwa watu wengi wanaofanya shughuli kama vile; ufugaji wa nyuki, kuvuna matunda pori, na kukusanya bidhaa nyingine za msitu. Hivyo, misitu ina mchango mkubwa katika kutunza mazingira na kusaidia jamii za maeneo hayo.
Wanyamapori
Wanyamapori ni rasilimali zinazohusisha wanyama wote pamoja na ndege wanaopatikana porini. Mfano wa wanyamapori ni kama vile; tembo, simba, faru, nyati, chui, swala, pundamilia, twiga, mbuni na wengine wengi. Tanzania ni makazi ya wanyamapori mbalimbali maarufu wa Afrika, ikiwa ni pamoja na wanyama wanaojulikana kama “The big five”, ambao ni simba, tembo, kifaru, nyati, na chui, kama wanavyoonekana katika Kielelezo namba 2. Wanyamapori hawa hupatikana kwa wingi katika hifadhi za taifa, maeneo ya uhifadhi, na mapori tengefu yanayochukua takribani asilimia 38 ya eneo lote la ardhi ya Tanzania. Baadhi ya maeneo ya wanyamapori yamewekwa kuwa maeneo muhimu ya urithi wa dunia ya UNESCO. Mfano wa maeneo hayo ni pamoja na eneo la uhifadhi la Ngorongoro pamoja na hifadhi za taifa za Serengeti, Nyerere na Kilimanjaro.
Aidha, Tanzania ina mamlaka mbalimbali zinazohusika na usimamizi wa maeneo ya wanyamapori. Mfano; Mamlaka ya hifadhi za taifa Tanzania (TANAPA)inasimamia hifadhi za taifa zote, eneo la uhifadhi la Ngorongoro linasimamiwa na Mamlaka ya eneo la uhifadhi la Ngorongoro (NCAA). Mapori tengefu kama vile; Ugalla, Moyowosi, Rungwa, Biharamulo, Ibanda, na Selous yanasimamiwa na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA). Wanyamapori ni rasilimali muhimu kwa taifa kwani wanachangia maendeleo ya nchi kwa njia mbalimbali kama vile; utalii, elimu ya wanyama, utamaduni na urithi wa taifa pamoja na uvuaji wa wanyama.
|
Kielelezo namba 2: Wanyama wajulikanao kama “The big five” |
Nishati
Tanzania ina rasilimali mbalimbali za nishati, zile jadidifu na zisizo jadidifu. Nchi inategemea zaidi nishati za maji, gesi asilia, na biomasi katika uzalishaji wa nishati. Nishati za maji zinachangia sehemu kubwa ya umeme unaozalishwa, ingawa uzalishaji wake unaweza kuathiriwa na ukame. Hifadhi za gesi asilia hasa maeneo ya mwambao wa pwani zimekuwa chanzo kikubwa cha nishati kwa uzalishaji wa umeme na matumizi ya viwandani. Biomasi hasa itokanayo na miti na mabaki ya kilimo hutumika sana kwa kupikia hasa katika maeneo ya vijijini. Aidha, Tanzania ina vyanzo vya nishati jadidifu kama vile upepo na jua ambavyo zinasidia kupunguza utegemezi wa mafuta, gesi asilia na umeme wa maji.
Kwa ujumla, rasilimali asilia za Tanzania zina mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania kupitia sekta za kilimo, madini, utalii, na viwanda. Serikali inaendelea kutekeleza mikakati ya kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali hizi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Zoezi La 01
1. Ni vyanzo gani vya nishati ya kupikia vinatumika na watu wa jamii unayoishi?
2. Je, vyanzo ulivyotaja katika swali la 1 vinatokana na rasilimali asilia zipi?
3. Fikiria, shule yako inataka kuzalisha umeme. Kuna vyanzo viwili, upepo na makaa ya mawe. Utashauri chanzo kipi kitumike? Toa sababu za jibu lako.
4. Eleza faida za rasilimali wanyamapori kwa Tanzania.
5. Eleza matumizi ya rasilimali ardhi katika jamii unayoishi.
6. Eleza namna utakavyotumia kwa ufanisi rasilimali asilia zilizopo katika eneo unaloishi kujiendelezea kipato.
Mtawanyiko wa rasilimali asilia za Tanzania
Rasilimali asilia nchini Tanzania hazipatikani kwa usawa katika kila sehemu ya nchi. Baadhi ya maeneo yana utajiri mkubwa wa rasilimali fulani wakati maeneo mengine rasilimali hiyo inapátikana kwa kiasi kidogo, au haipo kabisa, au rasilimali iliyo tofauti. Hali hii huitwa mtawanyiko wa rasilimali asilia. Ufuatao ni mtawanyiko wa rasilimali asilia za Tanzania.
Mtawanyiko wa rasilimali madini
Tanzania ni nchi tajiri katika rasilimali za madini, ikiwa na amana kubwa zilizotapakaa kote nchini. Madini ya dhahabu yanapatikana zaidi katika wilaya za Bukombe, Nyang’hwale na Bhomve mkoa wa Geita, wilaya za Bunda, Tarime na Butiama mkoa wa Mara na Bulyanhulu iliyopo halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga. Pia, madini ya dhahabu yanapatikana katika wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, eneo la Amani lililopo katikati ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa pamoja na eneo la Sekenke wilaya ya Iramba mkoani Singida na Chunya mkoani Mbeya. Hivyo, kufanyia dhahabu kuwa ni moja ya bidhaa kuu na muhimu za Tanzania zinazouzwa nje ya nchi.
Pia, kuna madini ya tanzanite, ambayo yanapatikana Tanzania pekee katika eneo la Mererani, wilaya ya Simanjiro mkoa wa Manyara. Madini haya ni sehemu ya utambulisho wa nchi ya Tanzania kwani hayapatikani mahali popote duniani zaidi ya Tanzania pekee. Aidha, kuna hifadhi kubwa ya makaa ya mawe yanayopatikana katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya kusini na magharibi mwa Tanzania. Maeneo haya ni kama vile; Muchuchuma iliyopo wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Kiwira iliyopo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Tunduma iliyopo wilaya ya Momba mkoani Songwe, na Ngaka iliyopo wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. Makaa ya mawe yanachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Tanzania kupitia matumizi yake viwandani pamoja na kuuza nje ya nchi. Kielelezo namba 3 kinaonesha uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe.
|
|
Madini ya almasi nchini Tanzania yanapatikana hasa katika eneo la Mwadui wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga. Eneo hili linaendelea kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya uzalishaji wa almasi nchini.
Madini ya urani yanapatikana hasa katika wilaya za Manyoni mkoani Singida, Bahi mkoani Dodoma na Namtumbo mkoani Ruvuma. Mpaka sasa madini ya urani yanachunguzwa kwa matumizi ya uzalishaji wa nishati, ingawa uchimbaji wake bado uko katika hatua za maendeleo.
Madini ya chuma yanapatikana katika eneo la Liganga wilaya ya Ludewa katika mkoa wa Njombe. Eneo hili linajulikana kwa kuwa na hifadhi kubwa ya madini ya chuma. Liganga inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika sekta ya viwanda nchini.
Pia, Tanzania inajulikana kwa madini ya vito mbalimbali, ikiwemo rubi na samafi (sapphires). Madini ya rubi hupatikana katika wilaya za Tunduru na Songea mkoa wa Ruvuma na wilaya za Ngorongoro mjini na Ulanga mkoa wa Morogoro. Madini ya samafi (sapphires) hupatikana katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma. Madini ya rubi na samafi ni maarufu sana katika masoko ya kimataifa.
Madini mengine yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini Tanzania ni pamoja na madini ya chumvi yanayopatikana wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani. Mikindani mkoa wa Mtwara, wilaya za Kilwa na Lindi, mkoa wa Lindi; na wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma. Madini ya fosfeti ambayo hutumika kutengeneza mbolea yanapatikana katika mikoa ya Tanga na Lindi, kalsiamu salfeti (Gypsum) inapatikana katika mikoa ya Mbeya na Rukwa na madini ya chokaa yanapatikana katika mikoa ya Tanga, Mbeya, na Arusha.
| Kazi ya kufanya namba 3 Chora ramani ya Tanzania, kisha tumia rangi mbalimbali kuonesha mtawanyiko wa madini ya dhahabu, almasi, tanzanite, makaa ya mawe, urani na madini ya chumvi. |
Mtawanyiko wa rasilimali maji
Rasilimali maji zilizopo Tanzania ni pamoja na maji ya chini ya ardhi, mito, mabwawa, maziwa, na bahari. Ufutao ni mtawanyiko wa rasilimali maji zilizopo nchini Tanzania.
Mabwawa
Tanzania imejaliwa mabwawa mengi makubwa na madogo yaliyopo katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mabwawa haya yanasadia katika kilimo cha umwagiliaji, uhifadhi wa ardhi, uzalishaji wa nishati, pamoja na matumizi mengine ya binadamu. Baadhi ya mabwawa muhimu yanayopatik ana nchini ni:
Bwawa la Mwalimu Nyerere
Bwawa la Mwalimu Nyerere ni bwawa kubwa la kuzalisha umeme nchini Tanzania. Bwawa hili limejengwa kwa madhumuni ya kupunguza uhaba wa nishati ya umeme nchini. Bwawa hili linapatikana eneo la Stiegler’s Gorge katika Mto Rufiji na lina uwezo wa kuhifadhi maji takribani mita za ujazo bilioni 34. Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere lina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2115. Bwawa hili pia linasaidia kuzuia mafuriko. Kielelezo namba 4 kinaonesha sehemu ya Bwawa la Mwalimu Nyerere.
|
Chanzo: https://www.ippmedia.com |
Bwawa la Mtera
Bwawa hili linapatikana katika wilaya za Chamwino na Mpwapwa mkoani Dodoma na wilaya ya Iringa mkoani Iringa. Chanzo cha maji ya Bwawa la Mtera ni Mto Ruaha Mkuu. Bwawa la Mtera lina ukubwa wa kilomita za mraba 660 na ni miongoni mwa mabwawa makubwa yanayotumika kwa uzalishaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme wa Mtera. Pia, linasaidia katika kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo ya karibu. Kielelezo namba 5 kinaonesha sehemu ya Bwawa la Mtera.
|
Kielelezo namba 5: Sehemu ya Bwawa la Mtera |
Bwawa la Nyumba ya Mungu
Bwawa la Nyumba ya Mungu lipo katika wilaya ya Mwanga mkoa wa Kilimanjaro. Chanzo cha maji ya Bwawa la Nyumba ya Mungu ni mito Kikuletwa na Mto Lumi. Bwawa la Nyumba ya Mungu lina ukubwa wa Kilometa za mraba 180. Bwawa hili ni mojawapo ya mabwawa makubwa yanayotumika kuzalisha umeme. Pia, hutumika katika kilimo cha umwagiliaji na shughuli za uvuvi hasa katika maeneo ya mikoa ya Kilimanjaro na Tanga. Kielelezo namba 6 kinaonesha sehemu ya Bwawa la Nyumba ya Mungu.
|
Kielelezo namba 6: Sehemu ya Bwawa la Nyumba ya Mungu |
Bwawa la Kidatu
Bwawa la Kidatu lipo katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro. Chanzo cha maji ya Bwawa la Kidatu ni Mto Ruaha Mkuu. Bwawa hili lina ukubwa wa kilometa za mraba 10, na linatoa maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kupitia kituo cha umeme cha Kidatu. Aidha, bwawa hili linachangia katika uhifadhi na matumizi usambazaji wa maji kwa ajili ya kilimo. Kielelezo namba 7 kinaonesha sehemu ya Bwawa la Kidatu.
|
Kielelezo namba 7: Sehemu ya bwawa la Kufulia |
Bwawa la Homboilo lipo katika eneo la jip la Urafiki, Mkoa wa Dodoma. Chanzo cha maji ya Bwawa la Homboilo ni Mto Mkungsushi. Bwawa hili ni muhimu kwa ajili ya shughuli za kilimo cha umwagiliaji, kunywesha mifugo, uvuvi na matumizi ya nyumbani katika eneo hili lenye hali ya ukame. Kielelezo namba 8 kinaonesha sehemu ya Bwawa la Homboilo.
|
Kielelezo namba 8: Sehemu ya Bwawa la Homboilo |
Mito
Tanzania ina mito mingi muhimu ambayo hutoa huduma ya maji kwa binadamu, wanyama, mimea na viwanda. Mito hii inapita katika mikoa mbalimbali hapa nchini. Ifuatayo ni baadhi ya mito muhimu nchini Tanzania na mahali inapoonzia, inapopita na inaposhia.
Mto Rufiji
Huu ni mto mrefu zaidi nchini Tanzania, unaanzia kwenye safu za milima ya Udzungwa iliyopo mikoa ya Iringa na Morogoro. Mto Rufiji unaungwa na matawi mito ya Mto Kilombero, Luwegu na Ruaha Mkuu na unapita katika mikoa mbalimbali ikiwemo mikoa ya Morogoro na Pwani. Mto huu unamwaga maji yake katika Bahari ya Hindi, kupitia Delta ya Rufiji iliyopo mkoa wa Pwani. Mto Rufiji ni muhimu sana kwa kilimo cha umwagiliaji katika maeneo unayopita, hasa katika bonde la Kilombero na Rufiji ambavyo yanajulikana kwa kilimo cha mpunga. Pia, bonde la Mto Rufiji ni makazi ya aina mbalimbali za wanyama, na unasadia mifumo ya ikolojia. Aidha, Mto Rufiji unasadia mito mbalimbali ya uzalishaji wa umeme wa maji, kama vile; mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere.
Mto Ruvuma
Mto huu unaanza kama kijito kidogo katika milima ya Matogoro Kusini mwa Tanzania karibu na mji wa Songea kuelekea njia ya Namtumbo na nchi jirani ya Msumbiji. Mto Ruvuma unamwaga maji yake katika Bahari ya Hindi kwa upande wa nchi ya Msumbiji. Mto huu ni muhimu nchini Tanzania na ni sehemu ya mpaka wa asili kati ya Tanzania na nchi ya Msumbiji katika upande wa kusini mwa nchi ya Tanzania. Aidha, ni mto muhimu kwa shughuli za kilimo cha umwagiliaji, usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, na mifumo ya ikolojia.
Mto Wami
Mto huu unaanzia maeneo ya milima ya Uguru iliyopo Mkoa wa Morogoro, ambapo mlima hii hutoa vyanzo vya matawimito inayoungana kuwa mto mmoja na kutiririsha maji yake kuelekea kusini-mashariki, kupitia mikoa ya Morogoro na Pwani. Katika mkoa wa Pwani, mto huu unapita vijiji za Chalinze na Bagamoyo. Mto Wami unamwaga maji yake katika Bahari ya Hindi kupitia Delta ya Wami, eneo lilio karibu na mji wa Bagamoyo. Mto huu ni muhimu kwa shughuli za kilimo, ufugaji, usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya viwandani na majumbani na mifumo ya ikolojia.
Mto Ruvu
Mto huu unaanzia kwenye milima ya Uluguru Mkoa wa Morogoro. Mto Ruvu umepita katika maeneo ya mkoa wa Morogoro, kuelekea maeneo ya mkoa wa Pwani. Aidha, unamwaga maji yake katika Bahari ya Hindi karibu na jiji la Dar es Salaam, kupitia Delta ya Ruvu. Mto huu ni muhimu kwa shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi, usambazaji wa maji kwa ajili ya matumizi ya viwandani na majumbani na mifumo ya ikolojia.
Mto Pangani
Mto huu unaoundwa na vyanzo au matawimito mawili. Chanzo cha kwanza kinatokea katika miteremko ya mlima Kilimanjaro ambapo maji yanatiririka chini ya mlima na kutengeneza mto Lumi. Chanzo cha pili kinatokea katika miteremko ya mlima Meru ambapo maji yanatiririka chini ya mlima na kutengeneza mto Kikuletwa. Mito yote miwili hukutana kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu. Kuanzia hapa, maji yanatengeneza mto Pangani ambao unatiririka kuelekea kusini-mashariki katika mkoa wa Kilimanjaro na kumwaga maji yake katika Bahari ya Hindi karibu na mji wa Pangani mkoa wa Tanga. Mto huu ni muhimu kwa shughuli za kilimo, ufugaji, na mradi wa uzalishaji wa umeme wa maji kupitia kituo cha umeme wa maji cha Hale.
Mto Ruaha Mkuu
Mto Ruaha Mkuu umezia katika safu za milima ya Kipengere kuelekea maeneo ya bonde la Usangu, hifadhi za Taifa za Ruaha, na Nyerere kabla ya kuungana na Mto Rufiji. Huu ni miongoni mwa mito muhimu nchini Tanzania, unachangia kwa kiasi kikubwa katika mfumo wa ikolojia na uchumi wa nchi.
Mito mingine inayopatikana nchini Tanzania ni kama vile; Mto Kagera uliopo mkoa wa Kagera, ambao unamwaga maji yake Ziwa Viktoria. Mto Malagarasi uliopo mikoa ya Kigoma, ambao unamwaga maji yake katika Ziwa Tanganyika na Mto Mara uliopo mkoa wa Mara ambao unamwaga maji yake katika Ziwa Viktoria.
Maziwa yaliyopo nchini Tanzania
Ziwa Viktoria
Hili ni ziwa kubwa zaidi la maji baridi barani Afrika na ziwa la pili kwa ukubwa duniani. Ziwa hili linapatikana katika nchi tatu ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda. Tanzania inachukua asilimia 49 ya ziwa lote ikifuatiwa na Uganda asilimia 45 na Kenya asilimia 6. Ziwa hili lina ukubwa wa Kilometa za mraba zipatazo 68,800. Kwa upande wa Tanzania, Ziwa Viktoria linapatikana katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Geita na Simiyu. Pia, Ziwa Viktoria lina visiwa kadhaa muhimu kama vile; kisiwa cha Ukerewe ambacho ni kisiwa kikubwa zaidi katika Ziwa Viktoria na Tanzania bara kwa ujumla. Kisiwa hiki kina kilometa za mraba zipatazo 530 na ni miongoni mwa wilaya zilizopo mkoa wa Mwanza. Pia kuna mto wa Saanane ambao ni hifadhi ya Taifa. Aidha, ziwa hili ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mto Nile ambao unapita nchi ya Sudan ya kusini, Sudan, Ethiopia na Misri kabla ya kumwaga maji yake katika bahari ya Mediterania.
Ziwa Tanganyika
Hili ni ziwa linalopatikana katika bonde la ufa la Afrika Mashariki, Magharibi mwa nchi ya Tanzania katika mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi. Pia, linapatikana katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi, na Zambia. Tanzania inachukua asilimia 46 ya eneo la ziwa takribani kilometa za mraba 32,900, sehemu kubwa zaidi ukilinganisha na nchi nyingine. Ziwa Tanganyika ndio ziwa la maji baridi lenye urefu mkubwa zaidi duniani ikiwa na km 673 kutoka kaskazini hadi kusini. Pia, ni ziwa la pili kwa kuwa na kina kirefu duniani na la kwanza barani Afrika kwa kina cheye urefu wa mita 1,470.
Ziwa Nyasa
Ziwa Nyasa ni miongoni mwa maziwa makubwa barani Afrika lililopo kwenye bonde la ufa la Afrika Mashariki. Katika muktadha wa Tanzania, ziwa hili huunda sehemu ya mpaka wa kusini mwa nchi na Malawi. Tanzania inachukua takribani asilimia 50 ya ziwa. Mkoa inayopakana na Ziwa Nyasa ni pamoja na Ruvuma katika wilaya ya Nyasa, Mbeya katika wilaya ya Kyela, na Njombe katika wilaya ya Ludewa. Ziwa hili lina ukubwa wa takribani kilometa za mraba 29,600 na kufinywa kuwa ziwa la tatu kwa ukubwa barani Afrika na la pili kwa kina baada ya Ziwa Tanganyika.
Ziwa Rukwa
Hili ni ziwa linalopatikana kwenye bonde la ufa la Afrika Mashariki ambalo lipo Kusini-magharibi mwa Tanzania. Ziwa hili linapatikana mikoa ya Rukwa, Songwe, na Katavi na ni ziwa lenye maji ya chumvi na Magadi. Nusu ya ziwa iko ndani ya sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Maziwa mengine muhimu yanayopatikana Tanzania ni pamoja na Ziwa Manyara, Eyasi na Natron. Ziwa Manyara ni ziwa lenye maji chumvi na magadi lililopo kwenye bonde la ufa la Afrika Mashariki katika mikoa ya Manyara na Arusha karibu na mji wa Mto wa Mbu na Karatu. Ziwa hili linajulikana kwa mfumo wake wa ikolojia na ni makazi ya aina mbalimbali za ndege wakiwemo flamingo. Aidha, ziwa hili linaunda hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Pia, kuna Ziwa Eyasi ambalo ni la maji chumvi lililopo katika Wilaya ya Karatu, mkoa wa Arusha kaskazini mwa Tanzania. Ziwa hili lipo ndani ya Bonde la Ufa Kusini-magharibi mwa Hifadhi ya Ngorongoro. Ziwa Natroni ni ziwa lenye chumvi na magadi kwa kiasi kikubwa, linapatikana Kaskazini mwa Tanzania, katika mkoa wa Arusha, wilaya ya Ngorongoro likipakana na nchi ya Kenya. Liko ndani ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki, jirani na mlima wa volkano wa Oldoinyo Lengai. Ziwa hili linajulikana kwa kuwa na maji yenye rangi nyekundu au pinki kwa sababu lina vimbe vidogo kama vile; cyanobacteria vinavyopenda mazingira yenye chumvi na joto kali. Viumbe hawa hutengeneza rangi maalumu zinazoonekana nyekundu au pinki, hasa wakati maji yanapopungua na chumvi kuongezeka.
Maziwa haya yote ni muhimu katika kukuza sekta ya uchumi wa bulu. Kwa mfano; uvuvi ambao ni chanzo cha kipato cha jamii za meneo yanayozunguka na taifa kwa ujumla. Pia, husaidia kurahisisha huduma za usafirishaji na utalii kwa mfano, katika eneo la Mamba Bay mkoani Ruvuma maji safi na ufufuko wa mchanga wa ziwa huvutia watalii. Kielelezo namba 9, kinaonesha mtawanyiko wa mito na maziwa yaliyopo Tanzania.
|
Kielelezo namba 9: Mtawanyiko wa Mito na Maziwa yanayopatikana nchini Tanzania |
Kwa ujumla Tanzania ni nchi yenye rasilimali maji nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangia maendeleo ya nchi hasa katika sekta ya kilimo, nishati, biashara, uvuvi, viwanda, utalii na usafirishaji.
Kazi ya kufanya namba 4
Tumia atlas au vyanzo vya mtandaoni vya kuaminika kusoma kuhusu rasilimali za maji zilizopo katika mkoa unaoishi. Kisha, orodhesha na bainisha mtawanyiko wake ndani ya mkoa.
Bahari ya Hindi
Bahari ya Hindi ni rasilimali maji muhimu inayopatikana upande wa Mashariki mwa nchi ya Tanzania. Inapakana na mikoa mitano ya Tanzania bara ambayo ni Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, na Mtwara, pamoja na kuzunguka visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 9. Fukwe za Bahari ya Hindi zina mvuto wa asili unaojumuisha fukwe za mchanga, misitu ya mikoko, na matumbawe. Bahari ya Hindi ina bandari kubwa na muhimu kama vile bandari za Dar es Salaam, Tanga, na Mtwara. Bahari ya Hindi inachochea sekta ya uchumi wa buluu kama vile: usafirishaji, uvuvi, biashara na utalii.
Mtawanyiko wa rasilimali wanyamapori Tanzania
Wanyamapori hupatikana zaidi kwenye maeneo maalumu ambayo yana maji, malazi, chakula na usalama. Nchini Tanzania, wanyamapori wanapatikana hasa katika hifadhi za taifa, maeneo ya uhifadhi na mapori tengefu. Maeneo haya yametengwa kwa ajili ya kulinda wanyamapori, mimea, vyanzo vya maji na mazingira asilia dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na shughuli za kibinadamu. Kutokana na upekee wa maeneo haya, yamekuwa vivutio vikubwa vya utalii nchini. Jedwali namba 1, 2 na 3 yanaonesha baadhi ya hifadhi za taifa na eneo la uhifadhi, mapori tengefu na hifadhi za bahari zilizopo Tanzania na vivutio vya utalii vilivyopo. Pia Kielelezo namba 10 kinaonesha mtawanyiko wa hifadhi za taifa, maeneo ya uhifadhi, na mapori tengefu.
Jedwali namba 1: Baadhi ya hifadhi za taifa na eneo la uhifadhi nchini Tanzania
| Hifadhi za Taifa na eneo la uhifadhi | Mahali | Ukubwa kwa kilomita za mraba | Vivutio | Upekee |
| Serengeti | Kaskazini Magharibi (Mara, Arusha na Simiyu) | 14,763 | Uhamaji wa makundi makubwa ya wanyamapori wakiwemo nyumbu na uwepo wa big five na wanyamapori wa aina mbalimbali | Sehemu ya mfumo mkubwa wa ikolojia, eneo kubwa la mbuga ya wazi yenye ardhi tambarare, Eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO, upatikanaji wa wanyama kwa mwaka mzima |
| Eneo la uhifadhi la Ngorongoro | Kaskazini (Arusha) | 8,292 | Kreta ya Ngorongoro, Empakaai na Olmoti, utamaduni wa Maasai, uwepo wa "big five" na wanyamapori wengine | Eneo la urithi wa Dunia la UNESCO, kreta kubwa na maarufu zaidi duniani, mchanganyiko wa wanyamapori, wanyama wafugwao na makazi ya wafugaji (wamasai, wasonjo na wahadzabe) |
| Kilimanjaro | Kaskazini (Kilimanjaro) | 1,688 | Mlima Kilimanjaro na ndege | Mlima mrefu Afrika (5,895m), mazingira ya aina mbalimbali, eneo la urithi wa dunia la UNESCO |
| Tarangire | Kaskazini (Manyara, Arusha na Dodoma) | 2,850 | Tembo wengi zaidi na wanyamapori wa aina mbalimbali, mibuyu mingi na ya kipekee, na aina mbalimbali za ndege | makundi makubwa ya tembo kuliko hifadhi yoyote, miti ya mibuyu |
| Ziwa Manyara | Kaskazini (Arusha na Manyara) | 649 | Ndege jamii ya flamingo, simba wanaopanda juu ya miti, ziwa manyara, viboko, chemchem ya maji moto, na msitu wa maji ya ardhini | Ziwa la maji chumvi, daraja la kamba na simba wanaopanda juu ya miti |
| Ruaha | Kusini-magharibi (Iringa na Mbeya) | 20,226 | Makundi makubwa ya Tembo na Nyati, na wanyamapori wengineo, Mto Ruaha Mkuu, samaki aina ya Tiger na maeneo ya kiutamaduni (nyumba ya Mfaw Mkwawa na Isimila) | Hifadhi ya pili kwa ukubwa Tanzania |
| Milima ya Mahale | Magharibi (Kigoma) | 1,613 | Sokwe, misitu , ziwa Tanganyika , na safu za Milima ya Mahale, | Makazi ya sokwe, ufukwe wa Ziwa Tanganyika |
| Gombe | Magharibi (Kigoma) | 56.2 | Sokwe, ziwa Tanganyika | Utafiti wa sokwe |
| Mikumi | Mashariki (Morogoro) | 3,230 | Wanyamapori mbalimbali kama vile; Twiga, pundamilia, simba, swala na pofu na Bwawa la viboko | Mazingira ya savana na maeneo tambarare |
| Nyerere | Kusini-Mashariki (Morogoro, Pwani, Lindi na Ruvuma) | 30,893 | Safari za boti kwenye mto Rufiji, bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na aina nyingi za wanyamapori | Hifadhi kubwa zaidi ya wanyamapori Tanzania na barani Afrika, eneo la urithi wa dunia la UNESCO |
| Saadani | Mashariki (Pwani na Tanga) | 1,100 | Fukwe, delta ya Mto Wami, aina mbalimbali za wanyamapori, na kasa wa kijani | Hifadhi pekee yenye bahari na nyika |
| Milima ya Udzungwa | Kusini-Mashariki (Morogoro na Iringa) | 1,990 | Misitu minene, kima wa kipekee aitwae Kipunji na maporomoko ya maji | Hakuna Barabara za magari ndani ya hifadhi, kuna njia za watembea kwa miguu kwa ajili ya kupanda mlima pekee |
| Katavi | Kusini -Magharibi (Katavi) | 4,471 | Viboko, mamba, simba, wanyama jamii ya swala (kongoni, Korongo na palahala) | Wanyama wengi, eneo la mbali |
| Kisiwa cha Rubondo | Ziwa Viktoria | 457 | Wanyamapori kama vile; Sokwe, Sitatunga, na tembo Ndege adimu kama vile; hondohondo, kasuku wa kijivu, na tai wa majini, pamoja na utalii wa kutumia mitumbwi, na kuendesha boti | Spishi adimu kama sitatunga |
| Kisiwa cha Saanane | Ziwa Viktoria (Mwanza jiji) | 2.18 | Safari za boti, wanyamapori kama vile; mbuzimawe, simba, pimbi, mamba na sato | Hifadhi pekee ndani ya mipaka ya jiji |
| Kitulo | Nyanda za Juu Kusini (mkoa wa Njombe na Mbeya) | 465 | Uwepo wa maua ya aina mbalimbali, ndege na maporomoko ya maji | "Bustani ya Mungu" yenye aina nyingi za maua |
| Mkomazi | Kaskazini Mashariki (Kilimanjaro na Tanga) | 3,245 | Faru weusi, mbwa mwitu na swala adimu kama vile; swalatwiga, choroa na tandala wadogo | Makazi ya spishi zilizo hatarini |
| Arusha | Kaskazini (Arusha) | 552 | Mlima Meru, Ziwa Momela, mbega weupe na weusi | Mandhari ya savana na misitu |
| Burigi-Chato | Kaskazini Magharibi (Geita) | 4,707 | Viboko, ndege | Hifadhi mpya Tanzania |
| Ibanda-Kyerwa | Magharibi (Kagera) | 294 | Mto Kagera na Wanyamapori mbalimbali kama vile chui, simba, viboko na nyati | Eneo la mbali lenye mandhari tulivu na la kipekee |
| Rumanyika-Karagwe | Magharibi (Kagera) | 247.5 | Wanyamapori, mabwawa mengi, na milima | Mandhari tulivu karibu na mpaka wa Uganda |
| Mto Ugalla | Magharibi (Tabora) | 3,865 | Viboko, mamba, simba, tembo, mbwamwitu, nyamera, korongo, palahala, tandala, kongoni, nyati, funo, pofu, oribi, tohe na nzohe | Mto na mbuga za maji (ardhi oevu) zenye wanyama wengi kama viboko na mamba wakubwa zaidi barani Afrika |
| Kigosi | Kaskazini Magharibi (mikoa ya Geita, Kagera, Shinyanga, Tabora) | 8,265 | Wanyamapori kama vile; fisi maji, kongoni, mbawala, kuro, mamba, na viboko Ndege adimu kama vile korongo-nyangumi, korongo-ndevu na bata bukini mbilikimo na misitu ya miombo | Mbuga za maji (yenye ardhi oevu) kubwa zaidi Afrika Mashariki na spishi za ndege adimu kama Korongo |
| Ghuba ya Jozani-Chwaka | Unguja (Zanzibar Kusini) | 50 | Mbega wekundu, misitu, ndege na vipepeo | Eneo la Urithi wa Dunia la UNESCO, hifadhi pekee Zanzibar |
Jedwali namba 2: Baadhi ya mapori tengefu Tanzania
| Pori tengefu | Mahali | Ukubwa kwa kilomita za mraba |
| Ikorongo na Grumet | Mara | 5,000 |
| Selous | Lindi na Pwani | 18,020 |
| Maswa | Simiyu | 2,200 |
| Mpanga Kipengere | Njombe na Mbeya | 1,574.3 |
| Kijereshi | Simiyu | 82 |
| Lukwati na Piti | Songwe | 6,118.9 |
| Moyowosi | Kigoma | 6,000 |
| Mkungunero | Dodoma na Manyara | 743.9 |
| Swagaswaga | Dodoma na Manyara | 871 |
| Luganzo -Tongwe | Katavi, Tabora na Kigoma | 5,746.2 |
| Rungwa | Singida na Mbeya | 9,000 |
| Muhesi | Singida | 2,000 |
| Kizigo | Singida | 4,000 |
| Liparamba | Ruvuma | 570 |
| Lwafi | Rukwa | 2,228 |
| Lukwika Lumesule | Mtwara | 444 |
| Msanjesi | Mtwara | 210 |
| Pande | Dar es Salaam | 15 |
| Rukwa | Katavi | 4,000 |
| Ugalla | Tabora | 7,577.4 |
| Uwanda | Rukwa | 5,000 |
| Wamimbiki | Morogoro na Pwani | 2,466.6 |
| Inyonga | Katavi | 6,569.9 |
| Wembere | Tabora na Singida | 5,385.8 |
| Igombe | Tabora | 1,367.1 |
Hifadhi za Taifa, Mapori Tengefu na Eneo la Uhifadhi Tanzania
|
Kielelezo namba 10:Hifadhi za taifa, mapori tengefu na eneo la uhifadhi Tanzania |
Kazi ya kufanya namba 5
Tumia vyanzo vya mitandaoni vya kuaminika, soma kuhusu sababu na umuhimu wa eneo la uhifadhi la Ngorongoro na hifadhi ya taifa ya Serengeti kuwa maeneo ya urithi wa dunia ya UNESCO.
Aidha, Tanzania ina mfumo mzuri wa hifadhi za bahari zinazolinda bayoanuai ya bahari na kutoa fursa za utalii wa kipekee. Hifadhi hizi zinasimamiwa na Kitengo cha Hifadhi za Bahari (MPRU). Jedwali namba 3 linaonesha baadhi ya hifadhi za bahari zilizopo Tanzania.
Jedwali namba 3: Baadhi ya hifadhi za bahari za Tanzania
| Jina la hifadhi | Mahali | Vivutio | Upekee |
| Kisiwa cha Mafia | Kusini (Pwani) | Mikoko, nyasi za bahari, matumbawe, visiwa (Shungimbili, Nyororo) | Uwepo wa viumbe adimu kama kiboko wa bahari na samaki wa rangi |
| Ghuba ya Mnazi (Mnazi Bay). | Kusini (Mtwara) | Mikoko, maji ya chumvi | Mazingira ya bahari yenye viboko na samaki wa maji ya chumvi |
| Tanga Silikanti | Kaskazini (Tanga) | Matumbawe, samaki wa rangi | Mandhari ya kuvutia kwa wapiga mbizi |
| Hifadhi ya bahari Dar es Salaam (DMRS) | Dar es Salaam | Visiwa (Bongoyo, Mbudya), ndege wa kijeshi, matumbawe, kamba wa kokoni | Kamba wa kokoni – mdudu mkubwa zaidi baharini |
Zoezi la 02
1. Tumia mifano kueleza tofauti kati ya hifadhi za taifa, eneo la uhifadhi na mapori tengefu.
2. Ni hifadhi ipi yenye uhamaji wa makundi makubwa ya wanyama kama vile nyumbu kila mwaka?
3. Ni sifa ipi ya kipekee inayoitofautisha hifadhi ya taifa ya Ziwa Manyara na hifadhi nyinginezo?
4. Utafiti juu ya Sokwe unafanyika katika hifadhi gani?
5. Ni sifa zipi zimetumika kuwabainisha wanyama wanaotambulika kama The big five?
Mtawanyiko wa rasilimali za nishati
Tanzania ina rasilimali mbalimbali za nishati ambazo zinachangia maendeleo ya kiuchumi na kushughulikia mahitaji ya umeme. Zifuatazo ni baadhi ya nishati muhimu zinazopatikana Tanzania.
Nishati ya gesi asilia
Tanzania ina gesi asilia kwa wingi hasa katika Mkoa ya Lindi na Mtwara. Ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia ulifanyika mwaka 1974 kwenye kisiwa cha Songo Songo (Lindi) na mwaka 1982 kwenye eneo la Ghuba ya Mnazi (Mtwara). Kwa sasa, hifadhi nyingi zaidi zimegunduliwa kwenye maeneo ya kina kirefu cha Bahari ya Hindi katika mikoa hii miwili. Gesi asilia ni muhimu kwa uchumi wa taifa kwani hutumika kuzalisha asilimia 50 ya umeme nchini kupitia mitambo ya kuchakata gesi kama vile; ile ya Madimba (Mtwara). Gesi hutumika katika viwanda, vyombo vya usafiri kama vile; bajaji na magari, na matumizi mengine kama nishati ya kupikia. Gesi asilia huongezeka pato la taifa kwa kuuza nchi za jirani kama Burundi, Malawi na Uganda. Pia, Tanzania inatarajia kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya na Zambia.
Nishati ya mafutaShughuli za utafiti wa mafuta nchini zimeanza tangu mwaka 1952. Hadi sasa Tanzania imegija mikataba na kampuni mbalimbali kwa ajili ya tafiti za mafuta. Hata hivyo, Tanzania imedhamiria kutumia katika mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Uganda (Hoima) hadi mkoa wa Tanga nchini Tanzania ujulikanao kama East African Crude Oil Pipeline (EACOP). Utekelezaji wa ujenzi wa mradi huu ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka 2026. Mradi huu wa mafuta ukikamilika utachangia uchumi na nishati nchini Tanzania.
Nishati ya maji, jua na upepo
Miradi ya maji, jua na upepo ni muhimu katika kukuza sekta ya nishati nchini Tanzania. Mfano, mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia upepo uliopo mkoani Singida. Pia, kuna mradi wa Julius Nyerere Stiegler’s Gorge uliogengwa kwenye Mto Rufiji. Aidha, umeme unaozalishwa kwa kiasi kikubwa katika mabwawa ya Mtera, Nyumba ya Mungu na Kidatu.
Uhusiano kati ya rasilimali asilia za Tanzania na shughuli za maendeleo
Rasilimali asilia za Tanzania zina mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo ya nchi. Ardhi yenye rutuba, madini, maji, misitu na wanyamapori vinatoa msingi imara kwa ukuaji wa sekta mbalimbali. Baadhi ya sekta zinazotegemea rasilimali asilia katika ukuaji wake ni pamoja na kilimo, uvuvi, ujenzi, nishati, utalii na viwanda. Ufanisi wa matumizi ya rasilimali hizi unachochea ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii, na uendelevu wa mazingira. Yafuatayo ni baadhi ya maendeleo ya sekta mbalimbali yatokanayo na rasilimali asilia zilizopo nchini.
Maendeleo katika sekta ya uvuvi
Rasilimali asilia nchini Tanzania zina jukumu muhimu katika maendeleo na uendelevu wa sekta ya uvuvi. Rasilimali maji ndio msingi wa sekta hii pamoja na sekta zinginezo za uchumi wa buluu. Maziwa makubwa kama Ziwa Viktoria, Tanganyika na Nyasa ni makazi ya aina mbalimbali za samaki kama vile sangara, sato, kambale, mbonge, mbasa, kampango, na migebuka. Mito kama Rufiji, Ruvuma, Wami , Ruva na Pangani pia huchangia uvuvi wa samaki kama vile; kamba, perege, ngege, kaa, kambale, kigoga, perege na kamongo. Pia, Bahari ya Hindi hutoa fursa za kuvua samaki kama vile; jodari, changu, kambale, kolekole, pweza, kaa na kasa. Rasilimali hizi za maji hufanya kazi kama sehemu za kuzaliana na kuzalisha samaki, na kuhakikisha kuwa sekta ya uvuvi inaendelea kwa muda mrefu. Samaki hawa hutumika kama chakula kwa jamii, lakini pia huuzwa ndani na nje ya nchi na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Maendeleo katika sekta ya uvuvi pamoja na uchumi wa buluu yanategemea sana usimamizi bora wa rasilimali maji.
Maendeleo katika sekta ya kilimo
Uwepo wa udongo wenye rutuba na hali ya hewa inayofaa (nzuri) imechangia kufanikisha kilimo cha mazao mbalimbali kama vile; mahindi, mpunga, viazi, mihogo, kahawa, chai, tumbaku, alizeti, miherage, mbogamboga na matunda. Pia, Tanzania ina rasilimali za maji kutoka kwenye mito, maziwa, na visima vya chini ya ardhi, ambavyo hutumika kwa umwagiliaji, hasa katika maeneo yenye mvua kidogo. Rasilimali hizi za asili zinazidia kilimo cha kujikimu na cha kibiashara, na kutoa ajira kwa sehemu kubwa ya wakazi. Usimamizi bora na uwekezaji katika rasilimali hizi ni muhimu ili kufungua fursa nyingi katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Maendeleo katika sekta ya uchimbaji madini
Uwepo wa hifadhi nyingi za madini nchini Tanzania unatoa msingi imara kwa ukuaji wa sekta ya uchimbaji madini nchini. Sekta ya uchimbaji madini ni moja ya sekta kuu zinazochangia maendeleo ya uchumi. Dhahabu, imekuwa ni mchango mkubwa katika mapato ya nchi kwa kutoa fedha za kigeni na kuvutia uwekezaji mkubwa wa kigeni. Uchimbaji wa tanzanite, jive la thamani linalopatikana Tanzania pekee, umeiweka nchi katika ramani ya kimataifa kwa kuongeza mapato ya taifa kupitia mauzo yake nje ya nchi. Sekta ya uchimbaji madini pia inafaidika na akiba kubwa ya makaa ya mawe, ambayo yanatumika kwa uzalishaji wa nishati ya umeme viwandani na pia kwa ajili ya kuuza nje. Upatikanaji wa madini ya viwandani kama vile chokaa na fosfeti pia umesaidia kukuza viwanda kama vile utengenezaji wa saruji na uzalishaji wa mbolea na kufanya sekta ya uchimbaji madini kukua zaidi. Hivyo, kwa usimamizi mzuri, na uwekezaji katika rasilimali za madini za Tanzania kunaweza kuleta maendeleo ya uchumi wa nchi, ajira, na kupunguza umasikini.
Maendeleo katika sekta ya nishati
Rasilimali za nishati ikiwa ni pamoja na mafuta, gesi asilia na makaa ya mawe zinachukua nafasi muhimu katika kudhiti mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini. Gesi asilia imekuwa chanzo kikuu cha nishati kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, kwani matumizi yake yamekuwa ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi, kutoa mbadala safi na bora zaidi kuliko vyanzo vya nishati vya jadi kama vile; biomasi, mkaa na kuni. Mbali na gesi asilia, Tanzania pia ina akiba kubwa ya makaa ya mawe ambayo yanatumiwa kuzalisha nishati inayotumika viwandani na pia kwa ajili ya kuuza nje. Rasilimali hizi ni muhimu katika kupanua gridi ya taifa, kuongeza upatikanaji wa umeme, na kuboresha usalama wa nishati nchini.
Zaidi ya hayo, Tanzania pia imejaa rasilimali za nishati jadidifu, ikiwa ni pamoja na jua na upepo. Chanzo kingine cha nishati jadidifu ni biogesi ambayo inatokana na uzo wa mabaki ya viumbe hai kama vile; kinyesi cha wanyama, mabaki ya chakula, majani na takataka za kilimo. Pia, biogesi ina uwezo wa kuzalisha umeme. Nchi ina uwezo mkubwa wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji, kutokana na uwepo wa mito mingi, mabwawa na mazalia ya umeme ya kutumia nguvu za maji nchini. Pia, upepo wa nishati ya jua na upepo kunaweza kusaidia maendeleo ya nishati safi na endelevu. Uwepo wa rasilimali asilia hizi unatoa fursa kwa Tanzania kupunguza utegemezi wa nishati inayotokana na mafuta ya nje, na kukuza maendeleo ya uchumi kupitia upatikanaji wa umeme wa bei nafuu na unaotegemewa.
Maendeleo katika sekta ya viwanda
Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi za asili ambazo zina mchango mkubwa katika kukuza maendeleo ya sekta ya viwanda. Uwepo wa madini mbalimbali kama vile; dhahabu, almasi, tanzanite, makaa ya mawe na madini ya viwandani kama vile; chokaa, fosfeti, na chumvi hutumika kama malighafi kwa ajili ya viwanda mbalimbali. Kwa mfano, dhahabu na vito vya thamani vinachangia katika maendeleo ya viwanda vya mapambo wakati chokaa hutumika katika viwanda vya saruji. Aidha, uwepo wa madini ya chumvi na fosfeti husaidia katika uzalishaji wa kemikali na mbolea viwandani ambazo ni muhimu kwa kilimo.
Zaidi ya hayo, rasilimali nyingi za maji nchini hutoa msaada muhimu kwa viwanda vinavyotegemea maji kwa ajili ya kupoza, usindikaji, na utengenezaji wa bidhaa kama vile vinywaji na vyakula vya kusindika. Uwepo wa misitu pia hutoa malighafi kwa viwanda vya mbao na karatasi. Vilevile, uwepo wa ardhi kubwa ya kilimo unasadia viwanda vya usindikaji wa mazao, vinavyohusiana na usindikaji wa chakula, utengenezaji wa nguo na bidhaa nyingine za kilimo. Mfano wa viwanda hivyo ni kama vile, kiwanda cha kusindika viyoyozi baridi cha Bakhresa Food Products kilichopo Mwanagwe wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani, kiwanda cha kusindika Kahawa cha TANICA kilichopo manispaa ya Bukoba mkoa wa Kagera na viwanda vya sukari, Mtibwa kilichopo wilaya ya Mvomero na Kilombero kilichopo wilaya ya Kilombero, mkoa wa Morogoro.
Maendeleo katika sekta ya utalii na usimamizi wa wanyamapori
Maendeleo ya viwanda hivi yanachangia katika kutoa ajira, kukuza uchumi na sekta ya biashara ya ndani na nje ya nchi. Usimamizi mzuri na uwekezaji katika rasilimali hizi ni muhimu ili kufungua uwezo kamili wa sekta ya viwanda nchini Tanzania.
Maendeleo katika sekta ya utalii na usimamizi wa wanyamapori baharini. Mazingira ya nchi kavu yanajumuisha savanna, misitu, na maeneo ya misitu. Mazingira ya bahari yanahusisha bahari pamoja na fukwe zake. Mazingira haya yote yanachangia uwepo wa sehemu muhimu za utalii wa wanyamapori na mazingira. Viumbe hai waliopo katika mazingira ya nchi kavu ikiwa ni pamoja na wanyama maarufu kama tembo, simba, twiga, mbogo na faru, ni vivutio vya utalii wa wanyamapori. Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ruaha, Nyerere, Tarangire na eneo la uhifadhi la Ngorongoro ni baadhi ya maeneo ambayo huvutia watalii na kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato kwa nchi.
Mbali na wanyamapori wa nchi kavu, maeneo ya pwani ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na visiwa vya Zanzibar vinatoa fukwe nzuri, maisha ya baharini, na miamba ya matumbawe ambayo inachangia katika kuvutia watalii zaidi. Rasilimali za asili kama misitu ya maji baridi, kama vile; Ziwa Tanganyika, Nyasa na Victoria, zinaboresha uwezekano wa utalii unaohusiana na maji, ikiwa ni pamoja na uvuvi, safari za meli, na hoteli za kando ya fukwe.
Aidha, misitu na hifadhi za taifa za Tanzania ni muhimu kwa uhifadhi wa bianuwai, na kusaidia kuhifadhi spishi zilizo hatarini. Pia, husaidia kudumisha usawa wa kimazingira, jambo ambalo linaisaidia kuimarisha sekta ya utalii.
Kwa ujumla, rasilimali asilia za Tanzania zinastahili kusimamiwa kwa ufanisi ili kuhakikisha kuwa zinawanufaisha wananchi wote. Pia, zinatoa fursa kubwa za ajira, kukuza uchumi na kulinda urithi wa asili wa nchi. Usimamizi bora na matumizi endelevu ya rasilimali hizi ni muhimu kwa mafanikio ya muda mrefu ya sekta ya utalii nchini Tanzania.
Maendeleo ya sekta ya ujenzi na miundombinu
Rasilimali asilia zina mchango mkubwa katika sekta ya ujenzi na miundombinu. Tanzania ina rasilimali kama chokaa, udongo na mchanga, zinazotumika kutengeneza saruji, matofali, na vifaa vingine vya ujenzi. Chokaa hutumika katika ujenzi wa barabara, nyumba, na majengo ya kibiashara, huku mchanga na udongo ukiwa malighafi muhimu kwa matofali. Pia, misitu ya Tanzania hutoa mbao zinazotumika kwenye ujenzi na utengenezaji wa samani na bidhaa nyingine za mbao. Hii inaonesha jinsi rasilimali za asili zinavyosaidia kuboresha miundombinu na maendeleo katika sekta ya ujenzi nchini.
Maendeleo katika sekta ya biashara
Rasilimali asilia zinachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya biashara nchini. Madini na vito vya thamani vimeleta fursa za uwekezaji wa ndani na wa nje, huku zikichochea biashara kama bidhaa za uchakataji, usafirishaji, na masoko. Upatikanaji wa mazao ya kilimo kutokana na uwepo wa ardhi yenye rutuba na hali ya hewa nzuri, unasaidia kukuji wa biashara za usindikaji wa chakula na vinywaji, upakiaji, na usambazaji ndani na nje ya nchi. Rasilimali hizi pia zinawezesha ujasiriamali na ajira, na kusaidia kukuza uchumi wa mtu binafsi. Kwa kutumia rasilimali zake kwa ufanisi, Tanzania inaweza kuvutia zaidi uwekezaji, kuimarisha biashara za ndani, na kuleta maendeleo endelevu.
Maendeleo katika sekta ya usafirishaji
Rasilimali za maji kama maziwa na mito zina mchango mkubwa katika sekta ya usafirishaji, ikiwemo kusafirisha abiria na bidhaa, hasa maeneo ambayo ni magumu kufikika kwa barabara. Mfano, maendeleo ya bandari ya Kigoma katika Ziwa Tanganyika yamewezesha usafirishaji wa abiria na mizigo kuelekea nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia na Burundi. Bandari ya Mwanza katika Ziwa Victoria inatumika kwa usafiri kuelekea mikoa inayozunguka ziwa Victoria, kwa upande wa kusini mwa Tanzania, bandari ya Mbamba Bay iliyopo katika Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma inachangia kurahisisha usafiri wa majini kuelekea nchi ya Malawi. Pia, katika pwani ya Tanzania, kuna bandari ya Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zinazotoa fursa ya usafiri wa baharini na kusaidia biashara ya ndani na ya kimataifa kwa kuunganisha nchi na masoko ya dunia. Rasilimali ardhi pia zina mchango mkubwa katika sekta ya usafirishaji wa njia ya nchi kavu. Rasilimali ardhi zimechangia sekta ya usafiri wa nchi kavu kwa kujenga barabara, reli na viwanja vya ndege, na hivyo kuimarisha miundombinu ya usafiri nchini kama inavyoonekana katika Kielelezo namba 11, 12 na 13.
|
Kielelezo namba 11: Daraja la Mlalakuwa, Dar es Salaam |
|
Kielelezo namba 12: Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam |
|
Kielelezo namba 13: Reli ya kisasa Tanzania |
Kwa ujumla, rasilimali asilia za Tanzania zinafanya msingi mkubwa wa maendeleo ya sekta za kiuchumi na kuboresha maisha ya watu. Usimamizi mzuri na uwekezaji wa kimkakati katika rasilimali hizi ni muhimu ili kufikia maendeleo ya kiuchumi nchini.
Zoezi La 03
1. Ikiwa utapewa jukumu la kupanga miradi ya maendeleo kwa kutumia rasilimali za maji zilizopo katika mkoa wako, elezea miradi utakayopendekeza ianzishwe?
2. Ni mbinu zipi zinaweza kutumika kuhakikisha uendelevu wa rasilimali maji zilizopo nchini?
3. Eleza kwa mifano fursa zitokanazo na rasilimali misitu.
4. Katika aya moja, eleza kuhusu uchumi wa buluu. Tumia vidoezo vifuatavyo;
| Msamiati
|
www.learninghubtz.co.tz
Zoezi la marudio
Sehemu A: Chagua herufi ya jibu sahihi
1. Ipi kati ya zifuatazo ni rasilimali isiyo jadidifu?
2. Madini ya tanzanite yanapatikana katika eneo gani la Tanzania?
3. Mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere umeanzishwa katika mto upi nchini Tanzania?
4. Ili kukuza sekta ya uchumi wa buluu tunapaswa kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali gani?
5. Maendeleo ya sekta ya kilimo hutegemea uwepo wa rasilimali asilia zipi?
Sehemu B: Maswali ya kuoanisha
6. Oanisha rasilimali maji za Tanzania zilizopo safu A na nchi zinazo pakana nazo kutoka safu B.
| Safu A | Safu B |
|
|
Sehemu C: Maswali ya majibu mafupi
7. Ni kwa namna gani rasilimali madini zinachangia maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania?
Eleza kwa mifano rasilimali asilia zinazopatikana katika mkoa wa Ruvuma na Mtwara.
8. Je, ni sifa zipi muhimu zinazotofautisha eneo la hifadhi ya Ngorongoro na hifadhi ya taifa ya Serengeti?
9. Eleza kwa mifano namna ambavyo uchumi wa buluu unachangia maendeleo ya nchi ya Tanzania.