FORM SIX KISWAHILI NECTA 2016

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL
ADVANCED CERTIFICATE OF SECONDARY EDUCATION
EXAMINATION

121/1 KISWAHILI 1

(Kwa Watahiniwa Walioko Shuleni na Wasiokuwa Shuleni)

Muda: Saa 3 Jumatatu, 02 Mei 2016 asubuhi

Maelekezo

  1. Karatasi hii ina maswali kumi (10) katika sehemu A, B, C, D na E.
  2. Jibu maswali saba (7) kwa kuzingatia maelekezo kutoka katika kila sehemu.
  3. Kila sehemu ina alama ishirini (20).
  4. Simu za mkononi haziruhusiwi katika chumba cha mtihani.
  5. Vikokotozi haviruhusiwi ndani ya chumba cha mtihani.
  6. Andika Namba yako ya Mtihani katika kila ukurasa wa kijitabu chako cha kujibia.


SEHEMU A (Alama 20)
UFAHAMU

Jibu maswali yote katika sehemu hii.

1. Soma kwa makini kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata.

Ustaarabu ni jambo jema ambalo hupendwa na kila mtu mwenye utashi mwema. Kila jamii yenye ustaarabu, mambo yake huendeshwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu zinazoeleweka. Maamuzi na maafikiano mbalimbali miongoni mwa wanajamii hutolewa bila hamaki wala uzandiki. Kanuni na taratibu hizo huiongoza jamii kufikia upeo wake kimaendeleo kuanzia ngazi ya chini kabisa ambayo ni familia mpaka ngazi ya juu kabisa ambayo ni Taifa. Kanuni na taratibu hizo huwekwa katika chombo maalum kiitwacho katiba. Taifa bila katiba ni sawa na behewa la gari moshi bila injini.

Katika nchi zenye utamaduni wa kidemokrasia, katiba huundwa kutokana na maoni ya wananchi wake kwa utaratibu maalum uliowekwa na serikali ya nchi husika. Aghalabu, maoni na mawazo yaliyotolewa na wananchi huwa chimbuko la katiba ya nchi hiyo na huwa sehemu ya utawala. Kinyume na hilo, nchi zenye utaratibu wa kiimla, katiba hutayarishwa na watawala kwa maslahi yao wenyewe. Katiba hutumiwa kama buruji la maslahi ya watawala. Maoni na fikra za wananchi si msingi wa katiba. Watawala katika jamii hii huonekana ni miungu itegemewayo sana katika ulimwengu. Wananchi huwa watwana katika nchi yao wenyewe.

Umuhimu wa katiba huonekana na hujidhihirisha waziwazi katika maisha ya kila siku ya nchi yoyote ile. Katiba huelekeza wajibu wa kila mwanajamii kwa taifa lake na wajibu wa viongozi kwa raia wake. Haki anazostahili raia na taratibu mbalimbali anazotakiwa kufuata ni msingi wa katiba. Licha ya kutoa utaratibu wa mchakato wa uongozi wa kisiasa na kijamii, uhuru wa mtu binafsi hulindwa na katiba ya nchi. Hata hivyo, nchi yenye katiba isiyokidhi matarajio ya wananchi wake ni sawa na debe tupu.

Wananchi hawana budi kuelewa maana ya katiba iii waweze kutoa maoni na mapendekezo ya kuunda katiba mpya au kuimarisha katiba iliyopo. Ni muhali kwa mtu asiyejua maana ya katiba kutoa maoni kuhusu katiba. Wananchi waelimishwe kupitia semina, warsha na makongamano iii kuiboresha au kuunda katiba mpya. Hivyo, ni vema kwa wananchi kutambua, kuheshimu na kuthamini uwepo wa katiba kama njia muafaka ya kujiletea maendeleo kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Pia watawala wasiwe kama wateule wa Maulana bali waheshimu katiba.

Maswali

(a) Andika kichwa cha habari uliyosoma kisichozidi maneno matano.

(b) Toa maana za maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika habari uliyosoma:

(i) Uzandiki

(ii) Katiba

(iii) Kiimla

(iv) Buruji

(v) Watwana

(vi) Muhali

(c) Kwa kuzingatia habari uliyosoma, taja faida nne zinazotokana na kuwepo kwa katiba katika taifa lolote.

(d) Mwandishi anamaanisha nini anaposema, "Taifa bila katiba ni sawa na behewa la gari moshi bila injini"?

(e) Kwa kutumia sentensi mbili eleza mtazamo wa mwandishi kuhusu jamii iliyostaarabika.

(f) Wazo kuu la mwandishi katika aya ya mwisho ni lipi.

View Ans


2. Fupisha habari uliyosoma kwa maneno mia moja na ishirini.

View Ans


SEHEMU B (Mama 20)

MATUMIZI YA SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

Jibu maswali mawili (2) kutoka sehemu hii.

3. Fafanua kuhusu dhana ya uainishaji wa ngeli za nomino kwa kigezo cha kisintaksia, kisha tumia mifano kutoa hoja nne zinazoonesha umuhimu wake katika lugha ya Kiswahili.

View Ans


4. Nini maana ya vivumishi na viwakilishi. Tumia hoja nne kuonesha kufanana na hoja nne kuonesha kutofautiana kati ya vivumishi na viwakilishi.

View Ans


5. Taja na fafanua kwa mifano vipashio vitano vya kiarifu katika tungo za Kiswahili.

View Ans


6. Eleza faida tano na hasara tano za kutumia misimu katika Kiswahili.

View Ans


SEHEMU C (Alama 20)

UTUNGAJI

Jibu swali la saba (7).

7. Andika insha ya maneno yasiyopungua mia tatu na hamsini na yasiyozidi mia nne kuhusu mchango wa vijana katika maendeleo ya taifa.

View Ans


SEHEMU D (Alama 20)

MAENDELEO YA KISWAHILI
Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.

8. Elezea matukio saba muhimu yaliyofanywa na serikali za Tanganyika na Zanzibar katika harakati za kusanifisha lugha ya Kiswahili kabla ya miaka ya 1960.

View Ans


9. Kwa kutumia mifano, elezea hoja tano ukionesha jinsi serikali ya Tanzania inavyojizatiti kukinusuru Kiswahili dhidi ya kasumba zinazokikabili katika ukuaji wake.

View Ans


SEHEMU E (Alama 20)
TAFSIRI
Jibu swali la kumi (10).

10. "Utoshelevu wa tafsiri hutokana na mfasiri mwenyewe." Thibitisha kauli hii kwa kutoa sababu nne zinazomfanya mfasiri kupata tafsiri toshelevu.

View Ans


Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256