Sura ya 01 : Ukoloni Mamboleo

Utangulizi

Hata baada ya uhuru na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Taifa la Tanzania bado limeendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ukiwamo ukoloni mamboleo. Katika sura hii, utajifunza kuhusu dhana na chimbuko la ukoloni mamboleo, athari zake, pamoja na mikakati ya Taifa letu katika kupambana nao. Umajiri utakaoujenga utakuwezesha kuthamini harakati za kupambana na ukoloni mamboleo na kulinda maliasili pamoja na maadili ya Kitanzania katika kipindi cha utandawazi.

Fikiri

Taifa katika ukoloni mamboleo

Dhana ya ukoloni mamboleo

Ukoloni mamboleo limechambuliwa kwa kina na wanazuoni wengi. Katika muktadha wa Afrika, wanazuoni hao wanaeleza kuwa kupata uhuru wa kisiasa pekee hakutoshi, iwapo nguvu za kigeni, mataifa tajiri, wawekezaji wa kimataifa na taasisi za kifedha bado zinaendelea kudhibiti nchi za Afrika kwa njia zisizo za moja kwa moja. Osagyefo Kwame Nkrumah, Rais wa kwanza wa Ghana, aliandika katika kitabu chake Neo-Colonialism: The Last Stage of Imperialism kwamba hata baada ya uhuru rasmi, mataifa ya Afrika yaliendelea kukabiliwa na vikwazo vingi vilivyotokana na utegemezi wa kiuchumi pamoja na ushawishi wa sera za nje kutoka kwa mataifa yaliyoendelea kiuchumi na yenye nguvu za kijeshi. Anasema: "Kiini cha ukoloni mamboleo ni kwamba serikali ambayo inaonekana kuwa huru kwa mujibu wa sheria na kwa kuonekana kuwa na bendera na sifa zote za uhuru wa kimataifa, kwa hakika mfumo wake wa uchumi, na hivyo sera zake za kisiasa, hudhibitiwa kutoka nje".

Aidha, Mwl. Julius K. Nyerere alibainisha kuwa hata baada ya uhuru, mataifa ya Afrika yaliendelea kuwa tegemezi kiuchumi, kijeshi na kisiasa. Hali hiyo ilikwamisha juhudi za ukombozi kamili wa Bara la Afrika, kwani liliendelea kutegemea mataifa mengine katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Kwa ujumla, ukoloni mamboleo ni hali ambayo mataifa ya kibeberu, pamoja na mashirika na taasisi za kimataifa, huingilia na kudhibiti mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya mataifa yaliyokuwa makoloni au mataifa maskini kwa madhumuni ya kuendelea kunyonya rasilimali za mataifa hayo. Ni hali inayojitokeza pale ambapo watawala wa kigeni huachia mamlaka rasmi ya utawala wa kikoloni kupitia uhuru wa bendera. Huku mfumo wa kiuchumi wa mamlaka hiyo ukiendelea kudhibitiwa kwa njia zisizo za moja kwa moja na zenye unyonyaji. Njia hizo ni pamoja na diplomasia, biashara, utamaduni, pamoja na ushawishi unaotokana na mashirika na taasisi za kimataifa. Mehakato huu hufanyika bila kuwepo kwa wakoloni moja kwa moja katika taifa husika, lakini athari zake huendelea kuonekana katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Sifa ya ukoloni mamboleo

Utegemezi wa kiuchumi: Nchi zilizokuwa makoloni pamoja na mataifa maskini mara nyingi huendelea kuwa tegemezi kiuchumi kwa kiasi kikubwa kwa mataifa yenye nguvu. Hali hii inatokana na muundo wa uchumi wa kikoloni uliowekwa kabla ya uhuru na kuendelea hata baada ya kupata uhuru wa kisiasa. Wakati wa ukoloni, nchi hizi zillazimika kuzalisha malighafi kwa ajili ya mataifa ya viwanda vya Ulaya Magharibi, huku zikiwa na uwezo mdogo wa kuzalisha bidhaa za viwandani kwa matumizi ya ndani. Baada ya kupata uhuru wa kisiasa, utegemezi huo haukuisha, kwani mataifa yaliyokuwa makoloni yaliendelea kuagiza bidhaa za viwandani, kutumia teknolojia na mitaji kutoka mataifa yenye nguvu ili kuendesha miradi mikubwa ya maendeleo. Kutokana na hali hiyo, nchi hizi zilizopata uhuru ziliendelea, na bado zinaendelea, kuwa na uchumi tegemezi unaokuza na kudumisha mfumo wa ukoloni mamboleo.

Misaada na mikopo: Ukoloni mamboleo hujitokeza pale ambapo nchi huendesha shughuli zake za kiuchumi kwa kutegemea misaada au mikopo kutoka mataifa tajiri au taasisi za kifedha za kimataifa, kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa. Mara nyingi, nchi hupokea misaada au mikopo hiyo kwa kukubali masharti magumu yanayolazimisha mabadiliko ya sera, muundo wa taaisi, pamoja na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma. Masharti hayo yanaweza kujumuisha kupunguza matumizi ya serikali, kupunguza idadi ya wafanyakazi wa umma, kurekebisha bajeti, kuanzisha au kuboresha sheria za ununuzi wa umma, pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa serikali. Nchi zinazotekeleza masharti haya hupoteza sehemu ya uhuru wao wa kiuchumi, kwani baadhi ya maamuzi ya kisera huamuliwa kutoka nje badala ya kuzingatia mahitaji ya ndani. Hivyo basi, ingawa mikopo yenye masharti magumu inaweza kuilazimisha nchi kufanya marekebisho muhimu na kuimarisha baadhi ya taasisi, kwa upande mwingine hudhoofisha uhuru wa kitaifa katika kutunga na kutekeleza sera. Aidha, hali hiyo inaweza kusababisha kupungua kwa upatikanaji na ubora wa huduma za jamii, pamoja na kuathiri uwajibikaji wa serikali kwa wananchi wake.

Wageni kudhibiti sekta muhimu: Katika uchumi wa mataifa mengi yanayoendelea, sekta muhimu kama vile mawasiliano, uchukuzi, madini na viwanda huwekwa chini ya udhibiti wa wawekezaji wa kigeni kupitia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi. Kwa mfano, kampuni za kimataifa ndizo humiliki na kuendesha shughuli kubwa za kiuchumi, kama uchimbaji wa madini, uendeshaji wa viwanda, pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii. Ingawa uwekezaji wa kigeni huchangia ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa miundombinu, kwa kiasi kikubwa mataifa husika huendelea kuwa tegemezi. Aidha, faida za uwekezaji huo mara nyingi sio endelevu, kwani wawekezaji wa kigeni huchukua sehemu kubwa ya mapato na kuyapeleka katika mataifa yao ya asili. Hali hii hudumisha utegemezi wa kiuchumi na kuendeleza mfumo wa ukoloni mamboleo.

Mwingiliano wa utamaduni: Kupitia elimu, vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, filamu na muziki, mataifa makubwa huendeleza utawala wa kiutamaduni dhidi ya nchi zinazoendelea. Nguvu ya mawasiliano husambaza maadili, tabia, hulka, mitindo na mitazamo ya maisha ya mataifa hayo, hali inayosababisha jamii za nchi zinazoendelea kuiga utamaduni wa kigeni na kuacha tamaduni zao za asili. Matokeo ya hali hii ni kudhoofika kwa maadili, lugha na desturi za ndani, pamoja na kuibuka kwa utegemezi wa kifikra na kiutamaduni. Utegemezi huo huchochea na kuendeleza mfumo wa ukoloni mamboleo katika mataifa yanayoendelea.

Kuingilia siasa: Mataifa ya kibeberu huingilia mifumo ya kisiasa ya nchi maskini kwa lengo la kulinda na kuendeleza maslahi yao. Uingiliaji huu hufanyika kwa kuunga mkono viongozi wa kisiasa wanaotetea maslahi ya mataifa hayo, na wakati mwingine kwa kuchochea mapinduzi ya kijeshi ili kuleta mabadiliko ya kiutawala katika mataifa husika. Kupitia mbinu hizo, mataifa makubwa huweza kuwaweka madarakani viongozi vibaraka katika nchi maskini na zisizo na nguvu, hali inayodhoofisha uhuru wa kisiasa na kuendeleza mfumo wa ukoloni mamboleo.

Ushirikiano wa kijeshi: Baadhi ya mataifa yanayoendelea hutegemea mataifa ya kibeberu katika shughuli mbalimbali za kijeshi, kama vile mafunzo ya kijeshi, ununuzi wa silaha na mifumo ya kiulinzi, pamoja na ulinzi wa mipaka na usalama wa taifa. Hali hii huwezesha mataifa ya kibeberu kuwa na ushawishi mkubwa katika masuala ya kiulinzi na kiusalama ya mataifa hayo. Aidha, katika baadhi ya nchi, mataifa yaliyoendelea huanzisha vituo vya kijeshi kwa lengo la kulinda maslahi yao maalum na ya kimkakati. Kwa mfano, Marekani ina vituo vya kijeshi katika nchi kama vile Niger, Kenya na Djibouti. Hali hii huendeleza utegemezi wa kijeshi na kuimarisha mfumo wa ukoloni mamboleo.

Kazi ya kufanya 1.1

Tumia mitandao na vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika kusoma matini zinazoeleza namna mifumo ya kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na kimaadili nchini inavyoathiri uwezo wa Tanzania kujitegemea. Baada ya hapo, chambua viashiria vya ukoloni mamboleo vinavyojitokeza katika maeneo hayo.

Chimbuko la ukoloni mamboleo

Chimbuko la ukoloni mamboleo linaweza kufafanuliwa kama matokeo ya mabadiliko ya mbinu ndani ya mfumo wa kibeberu kwa lengo la kuendeleza na kulinda maslahi yake. Mfumo huu ulihusisha kuachwa kwa utawala wa moja kwa moja wa kikoloni (ukoloni mkongwe) na kuanzishwa kwa udhibiti usio wa moja kwa moja kupitia sekta mbalimbali. Lengo lilikuwa ni kuimarisha maslahi ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni ya mataifa yaliyoendelea. Kwa hali hiyo, mfumo wa ukoloni mamboleo umeendelea kuwa kikwazo kwa nchi zinazoendelea, kwani hudhoofisha juhudi za kujitegemea na kufikia maendeleo endelevu. Sababu mbalimbali zilizosababisha kuibuka kwa ukoloni mamboleo duniani ni pamoja na athari za Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kupatikana kwa uhuru wa kisiasa, kuendelea kwa uchumi tegemezi, pamoja na utegemezi wa misaada na mikopo yenye masharti.

Vita Kuu ya Pili ya Dunia: Vita Kuu ya Pili ya Dunia ilikuwa na mchango mkubwa katika kuharakisha kuibuka kwa ukoloni mamboleo. Baada ya vita hiyo, nchi nyingi zilizokuwa makoloni zilianzisha harakati za kudai uhuru kutoka kwa watawala wao wa kikoloni. Hali hii ilitokana na mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yaliyosababishwa na vita hiyo. Baada ya vita, mataifa yaliyokuwa na makoloni, kama Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji na Italia, yalidhoofika sana kiuchumi. Udhaifu huo uliyafanya yashindwe kuendelea kuudumisha utawala wa moja kwa moja wa kikoloni katika maeneo yao. Kwa mfano, Uingereza iliona kuwa ni gharama kubwa kuendeleza himaya yake, hivyo ilianza mchakato wa kujiondoa katika makoloni yake.

Aidha, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, yaliibuka mataifa mawili yenye nguvu kubwa katika siasa za kimataifa, ambayo ni Marekani na Umoja wa Kisovieti. Mataifa haya yalikuwa na ushawishi mkubwa katika mwelekeo wa siasa za dunia. Marekani, kwa mfano, ilipinga mfumo wa ukoloni na iliunga mkono harakati za kupigania uhuru katika makoloni. Mwaka 1942, Marekani chini ya Rais Franklin D. Roosevelt iliingia mkataba na Uingereza chini ya Waziri Mkuu Winston Churchill uliofahamika kama *Mkataba wa Atlantic Charter*. Mkataba huo ulihimiza haki ya mataifa kujitawala, na uliitaka Uingereza kuyapa uhuru makoloni yake kama sehemu ya masharti ya msaada wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Ujerumani chini ya Adolf Hitler.

Hatua hizi zilichangia kuharakisha kuvunjika kwa mfumo wa ukoloni wa moja kwa moja, lakini wakati huohuo ziliandaa mazingira ya kuibuka kwa ukoloni mamboleo. Vilevile, kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa baada ya vita kulisaidia kuhamasisha na kusimamia michakato wa kuondoa ukoloni. Kati ya miaka ya 1940 na 1970, makoloni mengi ya Ulaya barani Afrika na kwingineko yalipata uhuru wa kisiasa kutokana na shinikizo la mataifa makubwa na Umoja wa Mataifa uliosisitiza haki ya kila taifa kujitawala. Hata hivyo, mataifa hayo makubwa yaliendelea kupata maslahi yao ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kupitia mfumo wa ukoloni mamboleo.

Kupatikana kwa uhuru wa kisiasa: Kupatikana kwa uhuru wa kisiasa katika miaka ya 1950 hadi 1970 kwa nchi nyingi za Afrika, Asia na Karibiani pia kulichangia kuibuka kwa ukoloni mamboleo. Ingawa nchi hizi zilipata uhuru rasmi na kukomesha utawala wa moja kwa moja wa kikoloni, zilibaki na miundo ya kiuchumi na kisiasa iliyokuwa imejengwa awali kwa manufaa ya mataifa ya Ulaya.

Miundo hiyo iliendelea kudhibitiwa kupitia makampuni ya kimataifa, wawekezaji wa zamani wa kikoloni, pamoja na mikataba ya biashara yenye masharti magumu. Kwa hali hiyo, mataifa yaliyokuwa watawala wa kikoloni yaliendelea kuwa na ushawishi mkubwa, japokuwa bila kuwepo moja kwa moja katika tawala hizo. Aidha, ushindani wa kisiasa uliotokana na Vita Baridi uliifanya Marekani na Umoja wa Kisovieti kutumia misaada, mikopo na usaidizi wa kiusalama kama nyenzo za kushawishi nchi changa zilizopata uhuru. Mara nyingi, misaada hiyo ilikuwa na masharti yaliyolenga kulinda maslahi ya mataifa hayo makubwa. Matokeo yake, nchi nyingi zilizopata uhuru wa kisiasa hazikuweza kufikia uhuru kamili wa kiuchumi wala kisera. Udhibiti wa nje uliendelea kupitia mikopo, misaada, masharti ya kifedha na mifumo ya biashara ya kimataifa. Hali hii ilipunguza uwezo wa nchi hizo kufanya maamuzi huru na kujitegemea kikamilifu. Hivyo kuendeleza mfumo wa ukoloni mamboleo.

Kutegemea uchumi wa kikoloni: Kutegemea uchumi wa kikoloni kulikuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya chimbuko la ukoloni mamboleo. Wakati wa utawala wa kikoloni, watawala waliunda mifumo ya kiuchumi iliyojikita katika uzalishaji na usafirishaji wa malighafi kutoka makoloni kwenda mataifa ya viwanda. Baada ya kupata uhuru wa kisiasa, nchi nyingi zilirithi mifumo hiyo bila kufanya mabadiliko makubwa, hali iliyozifanya ziendelee kutegemea masoko, teknolojia na mitaji kutoka nchi za Magharibi. Utegemezi huu uliimarishwa zaidi kupitia mikataba ya biashara yenye masharti magumu, pamoja na ushawishi wa mataifa yaliyoendelea katika sera za kiuchumi za nchi changa. Kutokana na hali hiyo, mataifa mengi yalishindwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kama vile uanzishaji wa viwanda vya ndani, ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme, pamoja na miundombinu ya barabara na bandari, bila misaada kutoka nje. Hivyo, yalilazimika kutegemea mikopo na misaada ya kigeni ambayo mara nyingi ilifuatana na masharti yanayodhoofisha uhuru wa kiuchumi.

Aidha, katika mfumo wa biashara ya kimataifa, kushuka kwa bei ya bidhaa ghafi kulinganisha na bei ya bidhaa zilizosindikwa kutoka mataifa ya Magharibi kuliendeleza pengo la kiuchumi na kuongeza utegemezi. Kwa sababu hiyo, licha ya kupata uhuru wa kisiasa, nchi nyingi hazikuweza kufikia uhuru kamili wa kiuchumi, bali zilibaki chini ya ushawishi wa nguvu za nje katika kupanga na kutekeleza sera za maendeleo.

Kwa mfano, baadhi ya nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Kifaransa katika Afrika Magharibi ziliendelea kuitegemea Ufaransa kiuchumi na kijeshi, hususan katika kudhibiti machafuko na kukabiliana na changamoto za kiusalama. Aidha, nchi hizo ziliendelea kutegemea ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wakoloni wao wa zamani katika kutekeleza mipango ya maendeleo baada ya uhuru. Vilevile, biashara za kuagiza na kusafirisha bidhaa ziliendelea kudhibitiwa na makampuni ya Ulaya Magharibi, huku mabenki ya nje yakiendelea kutoa mikopo kwa makampuni makubwa ya uchimbaji wa madini, mafuta na gesi katika nchi mbalimbali za Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.

Masharti ya kifedha na mikopo: Mikopo pamoja na masharti ya kifedha yaliyowekwa na Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia yamekuwa nyenzo muhimu za udhibiti wa kiuchumi, zilizoyafanya mataifa mengi yaliyopata uhuru kuendelea kuwa tegemezi kwa mataifa tajiri. Udhibiti huo umejidhihirisha kupitia masharti magumu, kama vile kupunguza matumizi ya serikali katika huduma za jamii, kuongeza au kurekebisha mifumo ya kodi, kuondoa vikwazo vya kibiashara, pamoja na kufungua milango kwa wawekezaji wa kigeni bila kuweka masharti madhubuti ya kulinda uchumi wa taifa.

Matokeo yake, serikali nyingi zilizilazimika kutekeleza sera ambazo hazikuwa chaguo lao la msingi, bali ziliathiriwa au kuamuliwa na taasisi za kifedha za kimataifa kwa lengo la kulinda maslahi yao. Hali hii ilisababisha utegemezi wa kudumu wa kifedha, ambapo mataifa yalilazimika kulipa riba kubwa na kuendelea kukopa ili kulipa madeni ya awali, na hivyo kuingia katika mzunguko wa madeni usio na mwisho.

Mzunguko huo ulipunguza uwekezaji katika maendeleo ya ndani, ukadhoofisha uhuru wa kutunga sera, na kuzuia serikali kuandaa sera zinazojibu mahitaji halisi ya wananchi. Badala yake, serikali zilizilazimika kufuata masharti ya mataifa na taasisi zenye nguvu za kiuchumi, hali iliyodumisha na kuendeleza mfumo wa ukoloni mamboleo.

Kazi ya kufanya 1.2

Tumia mitandao na vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika kusoma matini kuhusu chimbuko la ukoloni mamboleo. Kisha, chambua kwa kina namna ambavyo masharti ya kifedha na mikopo kutoka taasisi za kifedha za kimataifa yamechangia kuendeleza au kuimarisha ukoloni mamboleo katika nchi zinazoendelea, hususan barani Afrika.

Athari za ukoloni mamboleo

Ukoloni mamboleo unaendelea kuathiri maendeleo ya mataifa kwa namna mbalimbali kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kimaadili. Baadhi ya athari hizo ni:

Kiuchumi

Uchumi ni suala mtambuka katika maendeleo ya nchi, kwani ndio unaowezesha taifa kupanga na kutekeleza mipango bora ya maendeleo, pamoja na kutoa huduma muhimu kwa wananchi wake. Hata hivyo, ukoloni mamboleo una athari mbalimbali za kiuchumi, zikiwamo zifuatazo:

Utegemezi toka nje: Nchi nyingi zinazoendelea zimeendelea kuuza bidhaa ghafi badala ya kuendeleza viwanda vya kuchakata bidhaa hizo ndani ya nchi. Hali hii husababisha sehemu kubwa ya faida kwenda nje ya nchi badala ya kubaki ndani, na hivyo kuongeza utegemezi wa masoko ya kimataifa. Kutokana na hali hiyo, nchi huzalisha bidhaa ambazo hazitumii moja kwa moja na kutumia bidhaa ambazo haizalishi, jambo linaloimarisha utegemezi wa kiuchumi. Kadiri nchi inavyozidi kuwa tegemezi, ndivyo uwezo wake wa kudhibiti bei za bidhaa inazouza pamoja na mapato ya fedha za kigeni unavyopungua. Hivyo, nchi hulazimika kutegemea mikopo, misaada na wawekezaji wa kigeni ili kufadhili viwanda vya msingi, miundombinu na huduma za jamii. Mara nyingi, masharti ya mikopo na misaada hiyo hupendelea mataifa yaliyoendelea, na hivyo kuathiri uhuru wa nchi zinazoendelea katika kufanya maamuzi ya sera za ndani.

Athari za ukoloni mamboleo hujitokeza wazi pale ambapo mauzo ya nje yanategemea mazao machache ya kilimo, kama vile mikonge, kahawa, chai, korosho na pamba. Kwa kuwa nchi huuza zaidi bidhaa ghafi badala ya bidhaa zilizosindikwa na kuongezewa thamani, mapato yanayopatikana hubadilika kulingana na bei za soko la dunia na sera za wanunuzi wakubwa. Hali hii huwafanya wananchi washindwe kunufaika ipasavyo na rasilimali za nchi yao.

Aidha, hata baada ya kupata uhuru wa kisiasa, njia kuu za uzalishaji, kama vile biashara, viwanda na sekta ya benki, zilibaki kwa kiasi kikubwa mikononi mwa wawekezaji wa kigeni. Kwa mfano, benki kama Barclays Bank na Baroda Bank zilitawala sekta ya kifedha wakati wa awamu za mwanzo za uhuru. Vilevile, makampuni kama Tanganyika Planting Company (TPC), yanayomiliki mashamba ya miwa na kiwanda cha sukari eneo la Moshi, pamoja na Tanganyika Packers, kiwanda cha kuchinja na kusandika nyama kilichojengwa enzi za ukoloni katika miaka ya 1940, yaliendelea kuwa chini ya udhibiti wa kigeni. Pia nchi hizi ziliendelea kuwategemea wataalamu wa kifedha, viwanda, walimu, madaktari wa tiba na mpango toka nchi za nje katika kupanga mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii hasa katika elimu na afya. Serikali zilichukua hatua ya kuwandaa wataalamu ili kuachana na utegemezi wa wataalamu kutoka nchi za Ulaya Magharibi na Marekani, Urusi na Uchina.

Kikwazo cha sera za fedha: Hadi mwaka 1966, masuala yote ya kifedha katika nchi za Afrika Mashariki yalikuwa chini ya chombo kimoja kilichojulikana kama East African Currency Board (EACB), ambacho kilianzishwa na wakoloni. Bodi hii iliendelea kufanya kazi hata baada ya kupatukana kwa uhuru wa kisiasa, huku ikiendesha shughuli zake kwa kuzingatia zaidi matakwa ya serikali za kikoloni. Kutokana na hali hiyo, Tanzania haikuweza kuandaa na kutekeleza sera za fedha zinazozingatia mahitaji halisi ya uchumi wa ndani. Ni baada ya kujitoa katika bodi hiyo na kuanzisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 ndipo nchi ilipata uhuru wa kupanga na kusimamia sera za fedha kulingana na hali ya kiuchumi ya taifa.

Madeni na mikopo mikubwa kutoka nje: Serikali nyingi za nchi zinazoendelea hukopa fedha kutoka taasisi za kifedha za kimataifa kwa masharti magumu ambayo mara nyingi hayazingatii mazingira halisi ya uchumi ya wakopaji. Hali hii huzilazimisha serikali kutumia muda na rasilimali nyingi kulipa madeni, jambo linaloathiri utekelezi wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Aidha, taasisi za kifedha za kimataifa na mataifa tajiri mara nyingi hazitoi kipaumbele katika kufadhili miradi mikubwa ya kimkakati, kama vile ujenzi wa reli, uanzishaji wa viwanda vya uzalishaji au miradi ya uzalishaji wa umeme, ambayo ina mchango mkubwa katika mabadiliko ya kiuchumi ya muda mrefu. Badala yake, huwekeza zaidi katika huduma za kijamii ambazo, ingawa ni muhimu, mchango wake kwa ukuaji wa uchumi ni mdogo na hauathiri moja kwa moja miundombinu ya msingi au sekta ya viwanda. Masharti hayo huwalazimisha serikali kushirikiana na wawekezaji wa kigeni, kuongeza uhuru wa biashara, na kupunguza matumizi katika huduma za jamii. Hali hii huongeza pengo kati ya matarajio ya wananchi na uwezo halisi wa serikali kusimamia maendeleo kwa uhuru, bila kuathiriwa na nguvu za nje.

Usawa usio sawa katika biashara ya kimataifa: Athari nyingine ya ukoloni mamboleo ni kukosekana kwa usawa katika biashara ya kimataifa, hususan pale bei za bidhaa ghafi zinaposhuka ikilinganishwa na bei za bidhaa zilizotengenezwa viwandani. Hali hii husababisha nchi zinazotegemea kuuza malighafi kupata hasara kubwa katika biashara ya kimataifa. Matokeo yake ni kwamba nchi hizo hupunguza kiasi cha bidhaa au huduma wanazoweza kununua kwa kila kiasi cha malighafi wanachouza. Aidha, mapato ya fedha za kigeni hupungua, hasa pale bei za malighafi zinaposhuka katika soko la dunia au mataifa tajiri yanapodhibiti bei za bidhaa wanazouza. Udhaifu huu huathiri uwezo wa nchi kuwekeza katika viwanda vya ndani, kuendeleza teknolojia, na kujenga uchumi imara, na hivyo kuendeleza utegemezi wa kiuchumi kutoka nje.

Kudumaa kwa ukuaji wa viwanda: Mdororo wa viwanda ni mojawapo ya athari kuu za ukoloni mamboleo, kwani hupunguza uwezo wa uchumi wa ndani kukua na kujiimarisha. Mataifa mengi yaliyopata uhuru wa kisiasa yameendelea kutegemea kuuza rasilimali ghafi, kama vile madini, mafuta, gesi na mazao ya kilimo, bila kuzisindika au kuziongezea thamani. Hali hii husababisha bidhaa zao kuwa na thamani ndogo, huku wanunuzi wa nje wakipata faida kubwa zaidi. Viwanda vya ndani hushindwa kukua kwa kasi kutokana na ukosefu wa mitaji, teknolojia ya kisasa na masoko ya uhakika. Kutokana na hali hiyo, wananchi wengi huendelea kujishughulisha na kilimo cha kujikimu au biashara ndogo badala ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji viwandani.

Hatua hii hudhoofisha ukuaji wa uchumi wa ndani, huku mashirika ya kigeni yakiendelea kudhibiti bei za bidhaa. Matokeo yake ni kudumaa kwa sekta ya viwanda, hali inayosababisha ukosefu wa ajira za viwandani na kiufundi, pamoja na kuathiri maendeleo endelevu ya taifa.

Kazi ya kufanya 1.3

Tumia mitandao na vyanzo mbalimbali vya taarifa vya kuaminika, soma kuhusu athari za ukoloni mamboleo katika maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla. Kisha chambua athari zingine za kiuchumi zinazoletwa na ukoloni mamboleo.

Kisasa

Siasa ni nyenzo muhimu inayotumika kuongoza na kusimamia jamii. Baada ya ukoloni, nchi nyingi za Afrika, ikiwamo Tanzania, zilitarajia kujitawala kwa uhuru kamili. Hata hivyo, zimekabiliwa na changamoto mbalimbali za ukoloni mamboleo katika nyanja ya kisiasa, zikiwamo zifuatazo:

Utegemezi wa kisiasa: Nchi nyingi zilizopata uhuru wa kisiasa huonekana kuwa huru kisheria, lakini kwa uhalisia bado huathiriwa na kudhibitiwa na nguvu za nje. Sera za kifedha, kiuchumi, kiutawala na kijamii huendelea kuathiriwa na mataifa tajiri, wawekezaji wa kimataifa, pamoja na taasisi za kifedha za kimataifa. Udhibiti huu hutekelezwa kupitia mikopo, misaada na usaidizi wa kiusalama. Mara nyingi, mataifa makubwa na taasisi za kifedha za kimataifa huingilia mipango ya maendeleo ya nchi changa, hata katika hatua za utekelezi. Mfano halisi wa utegemezi huu ni tukio la uasi wa Jeshi la Tanganyika Rifles mwaka 1964, ambapo vikosi vya kijeshi kutoka Uingereza, taifa la zamani la kikoloni, vilitumika kurejesha amani na nidhamu jeshini. Aidha, utegemezi wa kisiasa huifanya nchi maskini kushindwa kuwa huru katika maamuzi muhimu yanayohusu masuala ya kitaifa. Kwa mfano, nchi nyingi za Afrika zilirejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa katika miaka ya 1990, kwa kiasi kikubwa kutokana na shinikizo la taasisi za kifedha za kimataifa na mataifa ya Magharibi.

Utawala wa kijeshi na mapinduzi ya mara kwa mara: Mifumo dhaifu ya kisiasa, ukosefu wa uwajibikaji, pamoja na ushawishi wa nje, vimechangia kudorora kwa utawala katika mataifa mengi ya Afrika. Hali hii imesababisha kutokea kwa mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara au kuundwa kwa serikali zisizo imara. Wakati mwingine, mapinduzi hayo hupangwa au kuungwa mkono na mataifa ya kibeberu kwa lengo la kuwaweka madarakani viongozi wanaolinda maslahi yao. Vilevile, mapinduzi huibuka pale serikali zinapotekeleza sera zinazolenga zaidi maslahi ya mataifa ya kibeberu na kupuuza mahitaji na matarajio ya wananchi. Hali hii hudhoofisha utawala wa kidemokrasia na kuendeleza ukoloni mamboleo katika nyanja ya kisiasa.

Mwendelezo wa mifumo ya utawala: Baada ya uhuru, nchi nyingi za Afrika ziliendelea kutumia mifumo ya utawala wa kikoloni, ikiwamo urasimu na matumizi ya lugha za kigeni zilizorithiwa kutoka kwa wakoloni. Mifumo hiyo mara nyingi haikulingana na mazingira, historia na utamaduni wa jamii husika, jambo lililosababisha maamuzi kufanywa kwa mtazamo wa kikoloni badala ya mtazamo wa kijamii au kitaifa. Hata hivyo, baadhi ya nchi zilichukua hatua za kubadili mifumo hiyo. Kwa mfano, nchi nyingi za Afrika ziliondoa Katiba za uhuru na kutunga Katiba za jamhuri, ambapo nafasi ya waziri mkuu au rais asiye mtendaji iliondolewa na kuanzishwa urais mtendaji wa jamhuri, akiwa mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu. Pamoja na mabadiliko hayo, mifumo ya kisheria, hususan mahakama na vyombo vya usalama, iliendelea kutumia sheria na taratibu nyingi zilizorithiwa kutoka kwa wakoloni.

Kugawanyika kwa kisiasa, kiitikadi na kikabila: Wakoloni waliweka mipaka ya kisiasa bila kuzingatia makabila, lugha, mila na desturi zilizokuwapo kabla ya ukoloni. Hali hii ilisababisha kuvunjika kwa umoja wa kijamii na kuchochea migogoro ya kisiasa baada ya kupatikana kwa uhuru. Aidha, wakati wa ukoloni, baadhi ya maeneo yalipata huduma muhimu kama elimu, afya na dini, ilhali maeneo mengine yalibaki nyuma, jambo lililoleta tofauti za maendeleo na kuongeza mgawanyiko na chuki miongoni mwa makundi ya kijamii. Baada ya uhuru, nchi nyingi za Afrika ziligawanyika kwa misingi ya tawala za kikoloni zilizowatawala awali. Hivyo, baadhi ziliingia katika makundi ya nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Kiingereza (Anglophone), Kifaransa (Francophone) au Kireno (Lusophone). Mgawanyiko huu ulisababisha nchi nyingi za Afrika kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na mataifa ya Ulaya kuliko baina yao wenyewe. Tofauti za lugha, utamaduni na mifumo ya utawala ziliendelea kusababisha migogoro ya kisiasa, jambo lililodhoofisha umoja wa kisiasa wa Bara la Afrika.

Uwepo wa viongozi vibaraka: Ukoloni mamboleo umezalisha tabaka la viongozi wasiokuwa wazalendo wa kweli, ambao hutanguliza maslahi binafsi na ya mataifa makubwa badala ya maslahi ya umma. Viongozi wa aina hii mara nyingi huingia madarakani kwa msaada wa mataifa ya kibeberu au kupitia mapinduzi ya kijeshi yanayoandaliwa au kuungwa mkono kutoka nje. Viongozi hao hushirikiana na wawekezaji wa kigeni wasio waaminifu katika uporaji wa rasilimali za taifa, huku wakipuuza misingi ya haki, usawa, utu na uwajibikaji kwa wananchi. Matokeo yake ni kudhoofika kwa utawala bora na kuendelezwa kwa ukoloni mamboleo katika nyanja ya kisiasa.

Rushwa na ufisadi: Athari nyingine ya ukoloni mamboleo ni kuenea kwa rushwa na ufisadi unaochochewa na ushawishi wa makampuni makubwa yanayonufaika na unyonyaji wa rasilimali za nchi maskini. Makampuni ya kibeberu yanayowekeza katika migodi, viwanda na mashamba makubwa hutumia nguvu ya kifedha kuwashawishi viongozi wachache wasio waadilifu ili walinde maslahi yao. Rushwa ya aina hii huwaacha wananchi wengi wakiendelea kuishi katika umasikini, huku faida kubwa zikiwanufaisha wachache. Aidha, rushwa ya kimfumo huharibu misingi ya utawala bora, hudhoofisha maadili ya jamii, na kuzuia utekelezi wa maendeleo endelevu katika mataifa husika.

Kazi ya kufanya 1.4

Tumia vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, ikiwemo mtandao, kusoma matini kuhusu ukoloni mamboleo. Kisha, husianisha migogoro ya kisiasa inayoendelea barani Afrika na athari za ukoloni mamboleo.

Kijamii

Katika muktadha wa kijamii, ukoloni mamboleo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, hususan katika maadili, familia, lugha, mavazi, elimu na mtazamo wa maendeleo. Mabadiliko hayo yamevuruga misingi ya utu, mila na mshikamano wa kijamii. Athari za kijamii za ukoloni mamboleo katika nchi zinazoendelea ni pamoja na zifuatazo:

Mfumo wa elimu wenye mtazamo wa kikoloni: Ukoloni mamboleo umefanya nchi nyingi za Afrika kuendeleza mitaala na lugha za kufundishia zilizorithiwa kutoka enzi za ukoloni. Kwa mfano, katika ngazi za juu za elimu, lugha za kufundishia zimeendelea kuwa Kiingereza, Kifaransa au Kireno. Hali hii imeendeleza utegemezi wa maarifa kutoka nje na kujenga mtazamo kwamba ufaulu wa kitaaluma na kazi za ofisini ndizo alama za mafanikio, badala ya elimu inayohimiza ubunifu na utoaji wa suluhu kwa changamoto halisi za jamii.

Huduma hafifu za kijamii: Kuongezeka kwa utegemezi wa bidhaa za nje bila kuimarisha uzalishaji wa ndani kumesababisha kupungua kwa mapato ya serikali. Hali hii imeathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa serikali kutoa huduma muhimu za kijamii, kama vile maji safi, huduma za afya na makazi bora kwa wananchi.

Kuvurugika kwa familia na mabadiliko ya majukumu ya kijinsia: Ukoloni mamboleo umechambia kudhoofisha misingi ya kifamilia katika jamii nyingi za Kitanzania. Kiasili, familia ilikuwa taasisi ya msingi katika kumjenga mtoto, kutoa elimu ya maadili, kukuza mila na desturi, na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za maisha. Hata hivyo, kupitia mifumo ya elimu, afya na dini, ukoloni mamboleo uliingiza misingi ya kibepari na propaganda zilizodharau mifumo ya familia ya asili kwa kudai kuwa duni na isiyoenda na ustaarabu wa kimagharibi. Aidha, mfumo wa elimu uliorithiwa kutoka kipindi cha ukoloni uliwatenganisha watoto na shughuli za kifamilia, mafunzo ya kijamii na utamaduni wa jamii zao. Hali hii imechangia kudhoofika kwa mahusiano ya kifamilia na kubadilika kwa majukumu ya kijinsia ndani ya familia. Ingawa familia bado ni taasisi muhimu katika jamii ya Tanzania, nafasi yake kama msingi wa utamaduni na elimu ya makuzi katika jamii imeanza kupungua kutokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni yanayotokana na ukoloni mamboleo.

Kukua kwa umasikini: Ukoloni mamboleo pia umechambia kuongezeka kwa umasikini katika nchi zinazoendelea. Kupitia mikopo yenye riba kubwa, misaada yenye masharti magumu, pamoja na nafasi dhaifu katika soko la dunia, Tanzania na mataifa mengi ya Afrika yamejikuta yakiendesha shughuli za uzalishaji kwa manufaa ya mataifa makubwa badala ya kunufaisha wananchi wao. Hali hii imeendelea kuzifanya nchi hizo kubaki katika mzunguko wa umasikini na utegemezi wa kiuchumi.

Kazi ya kufanya 1.5

Kwa kutumia maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania na matini mbalimbali ya kitaaluma, fanya uchambuzi kuhusu namna ambavyo ukoloni mamboleo umeathiri juhudi serikali katika kujenga taasisi imara za kijamii.

Kiutamaduni

Utamaduni ni mfumo unaongoza jamii katika taratibu na mwenendo wa maisha, ikiwemo maadili, lugha, mila, desturi na mitindo ya maisha. Mfumo huu wa utamaduni umeathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukoloni mamboleo kupitia nyanja mbalimbali, zikiwemo elimu, dini, lugha na vyombo vya habari. Athari za ukoloni mamboleo katika utamaduni ni kama ifuatavyo:

Kudhoofika kwa utambulisho wa kitamaduni: Athari hii imejidhihirisha tangu kuanzishwa kwa mfumo wa elimu ya kikoloni, ambao ulilenga kuuenzi na kuutukuza utamaduni wa kigeni huku ukipuuza na kudunisha utamaduni wa Kiafrika. Wanafunzi walifundishwa mitaala iliyosisitiza historia na ustaarabu wa wakoloni, huku tamaduni za Kiafrika zikionekana kuwa duni.

Aidha, katika mavazi na mitindo ya maisha, Watanzania wengi walianza kuiga mitindo ya kimagharibi na kudharau mavazi ya asili. Mfumo huu wa elimu umeendelea hata katika kipindi cha ukoloni mamboleo, na umeendelea kuleta athari hasi katika jamii za Kitanzania hadi leo.

Kukua kwa dini za kigeni: Wakoloni walianzisha dini za kigeni ambazo mara nyingi zilipinga au kudharau dini za asili za Kiafrika. Kabla ya ukoloni, jamii za Kitanzania zilikuwa na mifumo ya imani ya asili iliyosaidia katika masuala mbalimbali ya kijamii, kama vile ibada za kuomba mvua, kuondoa mikosi na balaa, pamoja na kuimarisha heshima kwa mizimu na miungu. Baada ya uhuru, athari hizi ziliendelea, ambapo dini za asili zilipoteza heshima na kuanza kutoweka taratibu, huku jamii zikizidi kutegemea dini zilizoletwa na wakoloni. Ukoloni mamboleo umeendeleza hali hii kupitia matumizi ya vyombo vya habari na taasisi za kidini, jambo linalopunguza imani na thamani ya mila na desturi za Kiafrika.

Kuporomoka kwa matumizi ya lugha za asili: Lugha ni kiini cha utamaduni wa jamii. Katika mfumo wa ukoloni mamboleo, lugha za kigeni zilitukuzwa na kuonekana kuwa ishara ya ustaarabu, elimu na hadhi ya kijamii. Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, elimu ya Magharibi iliendelea kuthaminiwa zaidi, hali iliyowafanya vijana wengi kuona aibu kuzungumza lugha zao za asili hadharani. Shuleni, wanafunzi walihimizwa kujifunza na kutumia lugha za kigeni, huku lugha za asili zikipewa umuhimu mdogo. Matokeo yake ni kupungua kwa matumizi na ujuzi wa lugha za asili katika jamii nyingi, jambo linalohatarisha urithi wa kitamaduni na utambulisho wa kitaifa. Kwa njia hii, ukoloni mamboleo huendelea kudhibiti fikra na mawasiliano, kwani lugha za kigeni zinatawala sekta za elimu, biashara na siasa.

Kimaadili

Maadili ni malezi yanayotolewa na wazazi, wakuu wa familia, jamii au taasisi kwa watoto na wanajamii kwa lengo la kuwaongoza kuishi kwa kutenda mema. Katika muktadha wa Tanzania, maadili hurejelea kanuni, misingi na viwango vinavyobainisha mema na mabaya na kuongoza mwenendo wa watu katika jamii. Chanzo cha maadili haya ni mila na desturi za Kiafrika, mafundisho ya dini, malezi ya kifamilia, pamoja na misingi ya taifa iliyoimarishwa tangu kupatika kwa uhuru. Maadili husaidia kudumisha umoja, heshima na mshikamano wa kijamii, hasa katika taifa lenye makabila zaidi ya 150 kama Tanzania. Hata hivyo, ukoloni mamboleo umeathiri maadili ya jamii kwa njia mbalimbali, zikiwemo zifuatazo:

Urasimu katika utoaji wa huduma: Ukoloni mamboleo umeendeleza maadili ya kikoloni katika utumishi wa umma, ambapo viongozi na watumishi wa taasisi za serikali hujikita zaidi katika taratibu kuliko katika matokeo na huduma kwa wananchi. Aidha, kumejitokeza pengo kati ya watumishi wa umma na raia, hali inayosababisha serikali kuonekana kama chombo kinachojitegemea badala ya kuwa mali ya wananchi. Hata baada ya uhuru, kuzingatia maadili katika jamii kumeendelea kupungua kutokana na kasumba za kikoloni, ambapo watu huiga mitazamo ya kigeni badala ya kuongozwa na misingi ya utu, ukarimu na mshikamano wa Kiafrika.

Kushuka kwa maadili ya jadi: Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa maadili ya jadi, kama vile ukarimu, heshima kwa wazee na utu wa pamoja, yameanza kupungua. Watu wengi wameathiriwa na mitazamo ya kigeni inayotukuza mali, mwonekano wa nje na mafanikio ya kifedha kuliko heshima ya familia na jamii. Matokeo yake, baadhi ya maadili ya jadi, kama vile taratibu za mazishi, matambiko na matumizi ya lugha za asili, yamepuuzwa au kuachwa kabisa na baadhi ya jamii.

Mmomonyoko wa maadili: Ukoloni mamboleo umesababisha jamii kuiga kwa kiasi kikubwa mitindo ya maisha ya mataifa yaliyoendelea, ambayo baadhi yake yanakwenda kinyume na mila na desturi za Kitanzania. Hali hii imesababisha mmomonyoko wa maadili, unaojitokeza kupitia tabia kama ukahaba, matumizi ya dawa za kulevya, wizi na ufisadi. Aidha, kumekuwapo na ongezeko la vijana kukosa heshima, kuacha mila zao, pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya uhalifu, kuchochea vurugu au kuzua taharuki katika jamii.

Upotevu wa uzalendo na kujitegemea: Ukoloni mamboleo umechambia kudhoofisha uzalendo na uwezo wa kujitegemea katika jamii nyingi. Badala ya kuhimiza uzalishaji wa ndani, ujenzi wa viwanda na kukuza uchumi wa kitaifa, maendeleo yameendelea kuonekana kama jambo linalopaswa kuletwa kutoka nje kupitia misaada au taasisi za kimataifa. Hali hii imeambatana na mfumo wa uchumi tegemezi unaosimamiwa na mataifa ya Magharibi kupitia mikopo, misaada na mahusiano ya kibiashara, na umeendelea kuwa sehemu ya urithi wa utawala wa kikoloni katika jamii nyingi za Afrika.

Ufisadi na tamaa ya mali: Ukoloni mamboleo uliweka misingi ya mifumo ya kiutawala na kiuchumi iliyonufaisha wachache na kuwaacha wananchi wengi nyuma, hali iliyochochea ufisadi na tamaa ya mali katika tawala za baada ya uhuru. Mfano wa hali hii ni matumizi ya rushwa ili kupata fursa za kiuchumi, kama vile leseni za uchimbaji wa madini, miradi ya ujenzi na biashara za kimataifa. Tabia hii imeendelea kushamiri hata baada ya uhuru, ambapo baadhi ya viongozi na watumishi wa umma hutanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa. Matukio kama kashfa ya Richmond na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ni mifano inayonesha namna ufisadi unavyoathiri maendeleo ya taifa. Hali hii husababisha kiasi kikubwa cha rasilimali za kifedha kunufaisha wachache badala ya kutumika kutatua changamoto za msingi katika jamii.

Kazi ya kufanya 1.6

Tumia vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, ikiwemo mtandao, kusoma matini kuhusu athari za ukoloni mamboleo. Kisha, tathmini athari za ukoloni mamboleo katika utamaduni na maadili ya Kitanzania ndani ya jamii inayokuzunguka, na hatimaye andaa ripoti.

Zoezi

1. Tumia nadharia ya Kwame Nkrumah kueleza kwa mifano jinsi ukoloni mamboleo unavyoendelea kuathiri maendeleo ya nchi za Afrika.

2. Kupatikana kwa uhuru wa nchi mbalimbali barani Afrika ulikuwa msingi wa ukoloni mamboleo, jadili hoja hii kwa kutumia mifano.

3. Changanua chimbuko la ukoloni mamboleo na eleza sifa zake kuu, kwa kutoa mifano halisi kutoka Tanzania.

4. Changanua kwa kina mikopo ya nje yenye masharti magumu inavyoweza kudhoofisha uhuru wa kisiasa na kiuchumi wa taifa la Tanzania.

5. Tathmini ambavyo ukoloni mamboleo unaathiri utekelezaji wa kauli mbiu ya "Tanzania ya viwanda" kwa kurejea masuala ya uwekezaji wa kigeni, teknolojia, sera za uchumi na umiliki wa rasilimali.

6. Chambua jinsi ukoloni mamboleo ulivyoathiri maadili za Kitanzania kwa kuzingatia mabadiliko katika utamaduni, lugha na mfumo wa elimu.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

1. Tumia nadharia ya Kwame Nkrumah kueleza kwa mifano jinsi ukoloni mamboleo unavyoendelea kuathiri maendeleo ya nchi za Afrika.

2. Kupatikana kwa uhuru wa nchi mbalimbali barani Afrika ulikuwa msingi wa ukoloni mamboleo, jadili hoja hii kwa kutumia mifano.

3. Changanua chimbuko la ukoloni mamboleo na eleza sifa zake kuu, kwa kutoa mifano halisi kutoka Tanzania.

4. Changanua kwa kina mikopo ya nje yenye masharti magumu inavyoweza kudhoofisha uhuru wa kisiasa na kiuchumi wa taifa la Tanzania.

5. Tathmini ambavyo ukoloni mamboleo unaathiri utekelezaji wa kauli mbiu ya "Tanzania ya viwanda" kwa kurejea masuala ya uwekezaji wa kigeni, teknolojia, sera za uchumi na umiliki wa rasilimali.

6. Chambua jinsi ukoloni mamboleo ulivyoathiri maadili za Kitanzania kwa kuzingatia mabadiliko katika utamaduni, lugha na mfumo wa elimu.

Mikakati ya kupambana na ukoloni mamboleo

Kutokana na athari za ukoloni mamboleo, mara baada ya kupata uhuru, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilibuni mikakati mbalimbali ya kupambana na athari hizo kwa lengo la kulinda uhuru wa taifa na kuleta ustawi wa nchi na wananchi wake. Mikakati hiyo ililenga nyanja mbalimbali, zikiwamo uchumi, siasa, jamii, utamaduni na maadili.

Mikakati ya kiuchumi.

Moja ya mikakati ya kiuchumi ni pamoja na;

Azimio la Arusha: Moja ya mikakati muhimu ya kiuchumi iliyobuniwa na Serikali ya Tanzania kupambana na athari za ukoloni mamboleo ilikuwa ni Azimio la Arusha. Azimio hili lilianzishwa ili kukabiliana na urithi wa utawala wa kikoloni mamboleo, na lililenga kuweka njia kuu za uchumi mikononi mwa wananchi kwa kuimarisha umiliki wa pamoja, kujitegemea kiuchumi na usawa wa kijamii.

Miongoni mwa mageuzi makuu yaliyotekelezwa kupitia Azimio la Arusha ni kuanzishwa kwa Siasa ya Ujamaa, ambayo iliweka misingi wa ushirikiano wa kijamii na kiuchumi. Kupitia siasa hii, wananchi walipewa nafasi ya moja kwa moja katika uzalishaji, usambazaji na matumizi ya rasilimali za taifa. Aidha, Azimio lisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kwa kutegemea misaada au mikopo kutoka mataifa tajiri, bali yanapaswa kuanzia kwa wananchi wenyewe kupitia kazi, ujuzi, mtazamo chanya na matumizi bora ya ardhi na rasilimali za ndani.

Ingawa Azimio la Arusha lilipata mafanikio makubwa, ikiwamo kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kuanzisha viwanda na mashirika ya umma, pamoja na kulinda rasilimali za taifa, lilikumbwa pia na changamoto mbalimbali za kiutendaji. Changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa wataalamu, mitaji na rasilimali za uzalishaji, pamoja na vikwazo vya kiuchumi na kisiasa kutoka mataifa ya Magharibi.

Udhibiti wa rasilimali za taifa: Baada ya uhuru, serikali ilichukua hatua za kitaifa kuhakikisha kuwa rasilimali muhimu zinakuwa mali ya umma. Rasilimali kama madini, ardhi, mbuga za wanyama, misitu na vyanzo vya maji ziliwekwa chini ya usimamizi wa serikali kwa mujibu wa sera za ujamaa zilizoanzishwa katika Azimio la Arusha. Kisheria, ardhi ilitangazwa kuwa mali ya umma chini ya udhamini wa Rais kwa niaba ya wananchi, huku madini yakitangazwa kuwa mali ya taifa. Serikali iliunda mashirika na taasisi za umma kwa ajili ya kusimamia uchimbaji, ununuzi, usambazaji na uhifadhi wa rasilimali hizo. Hata hivyo, utekelezaji wa sera hizi ulikumbwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo ukosefu wa mitaji, utaalamu na rasilimali za kiutendaji.

Aidha, mabadiliko ya sera za ndani na za kimataifa, kama vile mabadiliko ya masoko na uwekezaji mdogo, yalifanya udhibiti wa umma wa rasilimali kutokuwa na tija kama ilivyotarajiwa. Kutokana na hali hiyo, kuanzia miongo ya 1980 na 1990, serikali ilianza kuweka mkazo katika ushirikiano na sekta binafsi kupitia uundaji wa sheria mpya, programu za ubinafsishaji na mikakati ya ubia, kwa lengo la kuvutia mitaji na ujuzi wa ndani na wa kigeni.

Sekta ya benki na fedha: Katika sekta ya benki na fedha, serikali ya Tanganyika, na baadaye ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilichukua hatua muhimu ya kujiondoa katika udhibiti wa pamoja wa taasisi ya sarafu ya Afrika Mashariki. Wakati wa utawala wa kikoloni, masuala ya sarafu na sera za fedha yalikuwa yakisimamiwa na East African Currency Board (EACB), taasisi iliyodhibiti fedha za Kenya, Uganda na Tanganyika kwa kuzingatia mahitaji ya tawala za kikoloni.

Mfumo huo haukuzingatia mahitaji halisi ya uchumi wa ndani wa nchi wanachama. Hali hii ilibadilika kati ya miaka ya 1965 na 1966, baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (Bank of Tanzania Act) mwaka 1965. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza rasmi kazi tarehe 14 Juni 1966. Lengo kuu la hatua hii lilikuwa kuipa Tanzania udhibiti kamili wa sera za fedha, sarafu na taasisi za kifedha, ikiwamo kuanzishwa kwa Shilingi ya Tanzania. Hatua hii ililenga kupunguza utegemezi wa mifumo ya kifedha ya kikoloni na kuimarisha kujitegemea kiuchumi na kifedha cha taifa.

Uanzishaji na upanuzi wa biashara: Baada ya uhuru, serikali ya Tanzania ilianzisha na kuimarisha mashirika ya umma kwa lengo la kukuza biashara ndani ya nchi. Mojawapo ya taasisi muhimu ilikuwa Shirika la Maendeleo ya Taifa (National Development Corporation - NDC), lililoanzishwa mwaka 1962 kama Tanganyika Development Corporation (TDC) na kurekebishwa rasmi mwaka 1965. Kupitia NDC na mashirika mengine ya umma, serikali ilianzisha viwanda mbalimbali, vikiwamo vya nguo, usindikaji wa vyakula, viwanda vya msingi, usambazaji wa mafuta, pamoja na biashara ya jumla.

Lengo kuu la juhudi hizi lilikuwa kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kukuza uzalishaji wa ndani. Serikali ilihakikisha kuwa uzalishaji, usindikaji na usambazaji wa bidhaa unafanyika ndani ya nchi. Mfumo huu ulihusisha pia uanzishwaji wa bodi za masoko ya mazao ili kudhibiti bei na usambazaji, na kuhakikisha wakulima na wafanyakazi wanashughulika ipasavyo. Hata hivyo, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, sekta ya viwanda ilikumbwa na changamoto mbalimbali, zikiwamo kuingia kwa mfumo wa soko huria, ukosefu wa mitaji, upungufu wa wataalamu na mazingira magumu ya kiuchumi, hali iliyosababisha baadhi ya viwanda kushindwa kustawi.

Uchukuzi na mawasiliano: Baada ya uhuru, serikali ya Tanzania ilichukua hatua mbalimbali za kuimarisha miundombinu ya uchukuzi na mawasiliano kwa lengo la kukuza uchumi na kuimarisha mshikamano wa kitaifa. Serikali ilifanya ukarabati wa reli na kuongeza njia za reli ili kuunganisha Reli ya Kati na reli ya Tanga, hatua iliyosaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara kama pamba na mkonge. Aidha, serikali ilipanua umiliki wake katika reli za Tanzania na shirika la ndege, ambazo hapo awali zilikuwa zikimilikiwa kwa ushirikiano na Kenya na Uganda.

Vilevile, serikali ilichukua usimamizi wa Bandari ya Dar es Salaam na kuimarisha Bandari ya Zanzibar ili kuongeza ufanisi wa biashara ya baharini. Huduma za posta na simu nazo ziliimarishwa; kufikia mwaka 1966, Tanzania iliweza kuunganisha jiji la Dar es Salaam na miji ya Nairobi na Kampala kupitia huduma za simu, hatua iliyoboresha mawasiliano ya ndani na ya kikanda. Katika sekta ya mawasiliano ya habari, Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ilianzishwa mwaka 1965, huku Radio Zanzibar iliyoanzishwa mwaka 1964 ikiboreshwa. Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Radio Zanzibar ilibadilishwa jina na kuitwa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ). Vyombo hivi vya habari vilichangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuwawezesha wananchi kupata taarifa za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Umiliki wa ardhi: Mwaka 1963, Serikali ya Tanganyika ilipitisha Sheria ya Ardhi kwa lengo la kukomesha mfumo wa umiliki huria wa ardhi (freehold ownership) uliorithiwa kutoka kwa utawala wa kikoloni kupitia Sheria ya Ardhi ya mwaka 1919. Kwa mujibu wa sheria hiyo ya mwaka 1963, ardhi yote ya Tanzania ilitangazwa kuwa mali ya wananchi, huku Rais akiteuliwa kuwa mdhamini kwa niaba yao. Lengo kuu la sheria hii lilikuwa kuzuia umiliki wa ardhi kubwa na yenye rutuba na watu wachache, hususan wageni, na kuhakikisha ardhi inatumika kwa manufaa ya wananchi wote.

Vyama vya ushirika: Vyama vya ushirika vilianzishwa kwa lengo la kuwaimarisha wakulima wa ndani kiuchumi na kijamii. Kupitia vyama hivi, wakulima waliwezeshwa kupata bei bora za mazao yao, pembejeo za kilimo na huduma za masoko, badala ya kutegemea makampuni ya ununuzi au wafanyabiashara wa nje. Mfumo wa vyama vya ushirika ulianza hata kabla ya uhuru, kama ilivyokuwa vyama vya mauzo ya kahawa na tumbaku. Baada ya uhuru, serikali iliendelea kuvitumia vyama vya ushirika kama nyenzo za kiuchumi na kisiasa katika kuhamasisha umoja wa wananchi na ushiriki wao katika shughuli za maendeleo. Vyama hivi viliwapa wanachama nafasi ya kushiriki katika maamuzi kuhusu bei, takwimu za mauzo na mbinu za uuzaji wa mazao, hivyo kupunguza unyonyaji wa wafanyabiashara wa kigeni.

Hata hivyo, pamoja na manufaa yake, vyama vya ushirika vilikumbwa na changamoto kadhaa, zikiwamo ukosefu wa elimu na uelewa wa kanuni za ushirika miongoni mwa wanachama na viongozi, ukosefu wa mitaji na rasilimali, pamoja na udhaifu wa uongozi. Aidha, kukosekana kwa uwajibikaji na uwazi kuliibua rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali na kushuka kwa imani ya wanachama kwa vyama vyao.

Uanzishaji na upanuzi wa viwanda: Tanzania, kama taifa huru, ilijikita katika kuanzisha na kupanua viwanda kwa lengo la kupunguza utegemezi wa kiuchumi kwa mataifa tajiri. Kutokana na mkakati huo, viwanda vingi vilianzishwa na vingine kupanuliwa. Miongoni mwa viwanda hivyo ni viwanda vya nguo kama Urafiki na Sungura, viwanda vya saruji kama Wazo Hill na Mbeya Cement, pamoja na viwanda vya sukari kama Mtibwa, Kilombero na Kagera Sugar.

Aidha, vilianzishwa viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo, kama vile pamba, kahawa, korosho na chai, pamoja na viwanda vya chuma, vinywaji, sigara na bidhaa za ngozi. Viwanda hivi vililenga kuongeza ajira kwa wananchi, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuimarisha uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kazi ya kufanya 1.7

Umealikwa kuwa mshiriki katika mhadhara wa kitaaluma kuhusu madhara ya ukoloni mamboleo kwa vijana wa Kitanzania. Andaa wasilisho utakalotumia katika mhadhara huo, kisha uliwasilishe kwa wenzako kwa ajili ya majadiliaino.

Zoezi

1. Tathmini jinsi sera ya kutofungamana na upande wowote ilivyotekelezwa na Tanzania katika kupambana na ukoloni mamboleo?

2. Chambua mafanikio na changamoto za mikakati ya kupunguza utegemezi wa kigeni na kuimarisha maendeleo ya uchumi wa nchini, ukitolea mifano halisi kutoka sera, miradi ya kitaifa na juhudi za serikali.

3. Pendekeza ni kwa namna gani miradi ya kimkakati (mfano reli ya TAZARA na SGR) inaweza kusaidia mapambano dhidi ya mfumo wa ukoloni mamboleo.

MAJIBU YA ZOEZI

1. Tathmini jinsi sera ya kutofungamana na upande wowote ilivyotekelezwa na Tanzania katika kupambana na ukoloni mamboleo.

Jibu

Sera ya kutofungamana na upande wowote (Non-Aligned Policy) ni sera iliyofuatwa na Tanzania baada ya uhuru ambapo haikujiunga rasmi na kambi ya nchi za Magharibi zilizoongozwa na Marekani wala kambi ya Mashariki iliyoongozwa na Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi. Lengo lilikuwa kulinda uhuru wa maamuzi ya taifa na kupambana na ukoloni mamboleo.

Jinsi sera hiyo ilivyotekelezwa

(a) Kushiriki katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana (NAM)

Tanzania ilikuwa mwanachama hai wa NAM na ilitetea uhuru wa mataifa yanayoendelea bila kuathiriwa na siasa za kambi mbili.

(b) Kusaidia harakati za ukombozi wa Afrika

Tanzania ilitoa:

  • Mafunzo ya kijeshi.

  • Hifadhi kwa wapigania uhuru.

  • Misaada ya kifedha na kidiplomasia.

Mifano:

  • ANC (Afrika Kusini)

  • FRELIMO (Msumbiji)

  • MPLA (Angola)

  • ZANU na ZAPU (Zimbabwe)

  • SWAPO (Namibia)

(c) Kukataa tawala za kibaguzi

Serikali ya Tanzania ilipinga sera ya Apartheid nchini Afrika Kusini na ukoloni wa Wareno katika nchi za Kusini mwa Afrika.

(d) Kukuza sera ya Ujamaa na Kujitegemea

Kupitia Azimio la Arusha (1967), Tanzania ilihamasisha uchumi unaotegemea rasilimali za ndani badala ya misaada ya kigeni.

(e) Kudumisha mahusiano na mataifa mbalimbali

Tanzania ilishirikiana na nchi za Mashariki na Magharibi bila kuwa tegemezi kwa upande mmoja.

(f) Kushiriki katika diplomasia ya kimataifa

Kupitia Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (OAU/AU) na Jumuiya ya Madola, Tanzania ilitetea haki ya kujitawala kwa mataifa yaliyokuwa chini ya ukoloni.

Mafanikio ya sera

  • Kuimarisha hadhi ya Tanzania kimataifa.

  • Kuchangia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika.

  • Kulinda uhuru wa kufanya maamuzi ya kitaifa.

  • Kuimarisha mshikamano wa Afrika.

  • Kupunguza utegemezi wa kisiasa kwa mataifa makubwa.

Changamoto

  • Kutegemea misaada ya nje katika baadhi ya sekta.

  • Shinikizo kutoka mataifa makubwa.

  • Udhaifu wa uchumi wa ndani.

  • Migogoro ya kimataifa iliyopunguza uhuru wa maamuzi.

Hitimisho

Kwa kiwango kikubwa, sera ya kutofungamana na upande wowote ilitekelezwa kwa mafanikio. Iliiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa Afrika huku ikidumisha uhuru wa kisiasa na kidiplomasia, ingawa changamoto za utegemezi wa kiuchumi ziliendelea kujitokeza.

2. Chambua mafanikio na changamoto za mikakati ya kupunguza utegemezi wa kigeni na kuimarisha maendeleo ya uchumi wa nchini, ukitolea mifano halisi kutoka sera, miradi ya kitaifa na juhudi za serikali.

Jibu

Baada ya uhuru, Tanzania imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kupunguza utegemezi wa nje na kujenga uchumi unaojitegemea.

Mafanikio

(a) Utekelezaji wa Azimio la Arusha (1967)

Lilisisitiza:

  • Kujitegemea

  • Uzalishaji wa ndani

  • Umiliki wa rasilimali na wananchi

(b) Uwekezaji katika miundombinu

Miradi mikubwa imeboresha uchumi.

Mifano:

  • Reli ya Kisasa (SGR)

  • Daraja la Kigongo–Busisi

  • Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP)

  • Upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam

(c) Kuimarisha sekta ya viwanda

Kupitia sera za maendeleo ya viwanda, uzalishaji wa bidhaa mbalimbali umeongezeka na kupunguza uagizaji kutoka nje.

(d) Kuongeza uzalishaji wa umeme

Mradi wa Julius Nyerere Hydropower Project umeongeza uwezo wa kuzalisha umeme kwa maendeleo ya viwanda.

(e) Kuimarisha ukusanyaji wa mapato

Serikali imeongeza ukusanyaji wa kodi kupitia mifumo ya kidijitali na kuboresha usimamizi wa mapato.

(f) Kuimarisha sekta ya madini

Kuanzishwa kwa vituo vya biashara ya madini na usimamizi bora umeongeza mapato ya taifa.

(g) Kuimarisha usafirishaji

Miradi ya reli, barabara na bandari imepunguza gharama za usafirishaji na kuongeza biashara.

Changamoto

(a) Kuendelea kutegemea mikopo ya nje

Miradi mingi ya maendeleo bado inategemea mikopo kutoka taasisi za kimataifa.

(b) Teknolojia kutoka nje

Vifaa na teknolojia nyingi bado vinaagizwa kutoka mataifa mengine.

(c) Mtaji mdogo wa ndani

Wawekezaji wa ndani bado wana uwezo mdogo wa kufadhili miradi mikubwa.

(d) Mabadiliko ya uchumi wa dunia

Kupanda kwa bei za mafuta, vita na majanga ya kimataifa huathiri uchumi wa Tanzania.

(e) Upungufu wa wataalamu

Baadhi ya sekta bado zinategemea wataalamu kutoka nje.

(f) Mabadiliko ya tabianchi

Ukame na mafuriko huathiri uzalishaji wa kilimo na maendeleo ya uchumi.

Hitimisho

Ingawa Tanzania imepata mafanikio makubwa kupitia sera za kujitegemea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, bado kuna changamoto zinazohitaji kuimarishwa kwa uwekezaji wa ndani, maendeleo ya teknolojia na matumizi bora ya rasilimali za taifa.

3. Pendekeza ni kwa namna gani miradi ya kimkakati (mfano reli ya TAZARA na SGR) inaweza kusaidia mapambano dhidi ya mfumo wa ukoloni mamboleo.

Jibu

Miradi ya kimkakati ni uwekezaji mkubwa unaolenga kuimarisha uchumi na kupunguza utegemezi wa mataifa ya nje.

(a) Kupunguza utegemezi wa miundombinu ya mataifa ya nje

Reli ya TAZARA ilijengwa ili kutoa njia mbadala ya kusafirisha bidhaa bila kutegemea nchi zilizokuwa chini ya tawala za kibaguzi.

(b) Kuimarisha biashara ya ndani na kikanda

SGR inaunganisha mikoa mbalimbali ya Tanzania na nchi jirani, hivyo kuongeza biashara na mapato.

(c) Kupunguza gharama za usafirishaji

Usafirishaji wa bidhaa kwa reli ni nafuu kuliko barabara, hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.

(d) Kuvutia uwekezaji

Miundombinu bora huvutia wawekezaji wa ndani na wa nje kuanzisha viwanda na biashara.

(e) Kuongeza ajira

Miradi ya TAZARA na SGR imezalisha ajira wakati wa ujenzi na itaendelea kutoa ajira katika uendeshaji na matengenezo.

(f) Kuongeza mapato ya serikali

Kuongezeka kwa biashara na shughuli za uchumi huongeza ukusanyaji wa kodi na mapato ya taifa.

(g) Kuimarisha ushirikiano wa kikanda

Reli hizi huunganisha Tanzania na nchi jirani kama Zambia, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hivyo kuimarisha biashara ya Afrika.

(h) Kuongeza uwezo wa viwanda

Usafirishaji wa malighafi na bidhaa kwa gharama nafuu huongeza uzalishaji wa viwandani.

(i) Kuimarisha uhuru wa kiuchumi

Miundombinu ya kisasa huwezesha Tanzania kufanya maamuzi ya maendeleo kwa kujitegemea zaidi na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.

Hitimisho

Miradi ya kimkakati kama TAZARA na SGR ni nyenzo muhimu katika kupambana na ukoloni mamboleo kwa sababu huimarisha uchumi wa taifa, huongeza biashara, hujenga uwezo wa uzalishaji, huongeza ajira na mapato, na kupunguza utegemezi wa miundombinu na misaada ya mataifa ya nje. Serikali inapaswa kuendelea kuwekeza katika miradi hiyo pamoja na kuimarisha usimamizi wake ili kuhakikisha inaleta manufaa ya muda mrefu kwa maendeleo ya Tanzania.

Mikakati ya kisiasa

Pamoja na harakati za kiuchumi, Serikali ya Tanzania ilitumia mbinu mbalimbali za kisiasa ili kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake bila kuingiliwa na nguvu za nje. Miongoni mwa mbinu hizo ni kama ifuatavyo:

Kuachana na Katiba ya kikoloni (Mfumo wa Westminster): Uamuzi wa Tanganyika, na baadaye Tanzania, wa kuachana na Katiba ya kikoloni ya mfumo wa Westminster ulitokana na msukumo wa kisiasa wa kujitegemea na kajitawala kikamilifu. Baada ya kupata uhuru, Tanganyika ilirithi Katiba kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza, ambayo iliendelea kuiweka nchi chini ya utawala wa Malkia Elizabeth II kama Mkuu wa Nchi. Hivyo, licha ya kupata uhuru wa kisiasa, nchi haikuwa na mamlaka kamili ya kuamua mambo yake ya ndani.

Katiba ya mwaka 1961 iliifanya Tanganyika kuwa huru kwa jina tu, kwani iliendelea kuwa na muundo wa kikoloni uliomhusisha Malkia, Gavana, Waziri Mkuu na Bunge. Hali hii ilisababisha kutungwa kwa Katiba ya mwaka 1962, iliyoifanya Tanganyika kuwa Jamhuri yenye mfumo wa serikali unaongozwa na Rais Mtendaji. Kupitia mabadiliko hayo, Tanganyika iliondoa mfumo wa utawala wa kikoloni na kuanzisha mfumo wa kikatiba uliolenga kukidhi malengo ya taifa ya kujitegemea, kuondoa utegemezi wa kisiasa kwa wakoloni, na kuweka msingi wa namuzi wa ndani pamoja na jitihada za maendeleo zinazoongozwa na wananchi wenyewe. Kielelezo 1.1 kinaonesha picha ya Mwl. Julius K. Nyerere, Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika huru, mara baada ya kupata uhuru tarehe 9 Desemba 1961.

Kielelezo 1.1: Mwl. Julius Nyerere Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Mnamo tarehe 26 Aprili 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na malengo mengine, lengo kuu la Muungano lilikuwa kudumisha umoja wa kihistoria uliokuwapo kwa vizazi na vizazi kati ya wananchi wa Tanganyika na Zanzibar. Aidha, Muungano ulilenga kuzinganisha nchi hizo mbili na kuunda taifa moja lenye nguvu zaidi, fursa pana na uwezo wa kujitegemea, ili kuzuia kuingiliwa kisiasa na mataifa ya kigeni. Vilevile, Muungano ulikusudia kuvunja mipaka na mifumo ya migawanyiko iliyowekwa na utawala wa kikoloni kwa muda mrefu.

Sera ya kutofungamana na upande wowote: Sera ya kutofungamana na upande wowote ilikuwa msingi wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania. Tanganyika ilijiunga na Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote miezi mitatu kabla ya kupata uhuru, katika mkutano wa kilele uliofanyika Belgrade, Yugoslavia, mwaka 1961, ambapo umoja huo ulianzishwa. Juhudi hizi zilijiri ziliongozwa na viongozi mashuhuri kama Rais wa Yugoslavia Josip Broz Tito, Rais wa Misri Gamal Abdel Nasser na Waziri Mkuu wa India Jawaharlal Nehru. Baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi iliendelea kuwa mwanachama wa umoja huo.

Lengo kuu la kujiunga lilikuwa kulinda uhuru na hadhi ya kisiasa ya taifa, na kuhakikisha kuwa Tanzania haiegemei moja kwa moja upande wa nchi za Magharibi wala Mashariki wakati wa Vita Baridi, kipindi ambacho dunia iligawanyika katika kambi mbili zenye nguvu za kisiasa na kijeshi. Kupitia sera hii, Tanzania iliweza kudumisha uhuru wake wa kisiasa na kukataa mikataba iliyokuwa haina manufaa kwa taifa kutokana na shinikizo la kambi yoyote.

Uungaji mkono wa harakati za ukombozi: Tanzania ilijitambulisha kama kitovu muhimu cha harakati za ukombozi barani Afrika kwa kupinga utawala wa kikoloni na athari zake, ikiwemo ukoloni mamboleo. Baada ya kuzuiwa kufanya shughuli zake nchini Afrika Kusini, Chama cha African National Congress (ANC) kilifungua ofisi yake ya kwanza nchini Tanzania mwaka 1962. Hatua hii ilidhihirisha wazi msimamo wa Tanzania katika kusaidia harakati za kisiasa, kijamii na kiuchumi za mataifa yaliyokuwa yakipigania uhuru na kujitegemea. Vilevile, wapigania uhuru wa Namibia kupitia chama cha South West Africa People's Organisation (SWAPO) waliratibu shughuli zao nchini Tanzania.

Kupinga mikataba yenye viashiria vya ukoloni mamboleo: Katika nyakati tofauti, serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mwl. Julius K. Nyerere ilikataa kuingia katika mikataba iliyokuwa na viashiria vya kuingilia uhuru wa taifa, hata pale mikataba hiyo ilipoonekana kuwa na manufaa ya kiuchumi. Kwa mfano, Tanzania ilikataa misaada kutoka Ujerumani Magharibi baada ya nchi hiyo kuitaka Tanzania isitishe uhusiano wake na Ujerumani Mashariki. Msimamo huo ulitokana na sera ya kutofungamana na upande wowote wakati wa Vita Baridi. Aidha, baada ya uhuru, baadhi ya nchi za Magharibi na Benki ya Dunia ziliishauri Tanganyika kukubali uwekezaji mkubwa katika kilimo cha mazao ya biashara, kama ilivyokuwa kwa nchi jirani. Mwl. Julius K. Nyerere alikataa pendekezo hilo kwa kuamini kuwa hatua hiyo ingewafanya wananchi wa Tanzania kuendelea kuwa vibarua katika mashamba ya wageni, badala ya kuwa wamiliki wa uzalishaji wao wenyewe.

Kuvunjwa kwa utawala wa kichifu .Kuvunjwa kwa tawala za kichifu kulikuwa mkakati muhimu wa kupambana na ukoloni mamboleo. Hatua hii ililenga kuondoa mfumo wa utawala usio wa moja kwa moja (*indirect rule*) ambao wakoloni walikuwa wakitumia kudhibiti siasa na uchumi kupitia viongozi wa jadi. Badala yake, mamlaka yalihamishwa kwa vyombo vya kitaifa vilivyochaguliwa kwa misingi ya utawala wa kisasa, ili kuimarisha umoja wa taifa na kujitegemea. Hatua hii ilitekelezwa mapema baada ya uhuru kwa kufutwa kwa Mamlaka za Asili (*Native Authorities*) na kuondolewa rasmi kwa cheo cha chifu kupitia Sheria ya Machifu wa Kiafrika *African Chiefs Ordinance (Repeal) Act* ya mwaka 1963. Serikali iliunda serikali za mitaa kwa lengo la kuongeza uwajibikaji kwa wananchi badala ya kulinda maslahi ya wakoloni.

Kufutwa kwa mfumo wa vyama vingi na kuanzishwa kwa mfumo wa chama kimoja: Kwa lengo la kujenga taifa lenye umoja na mshikamano, Tanzania iliamua kufuta mfumo wa vyama vingi na kuanzisha mfumo wa chama kimoja mwaka 1965. Mwl. Julius K. Nyerere aliamini kuwa vyama vingine, tofauti na TANU, vilikuwa na misingi na misukumo iliyoweza kuligawa taifa changa. Kwa mfano, All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT) kilikuwa chama chenye mwelekeo wa kidini, ANC kilikuwa na misingi ya ubaguzi wa kiafrika (Africa for Africans), na UTP kilikuwa na uhusiano wa karibu na viongozi wa kimila pamoja na watu wa asili ya Ulaya. Hatua ya kuanzisha mfumo wa chama kimoja ililenga kuimarisha umoja wa kitaifa na kulinda uhuru wa kisiasa dhidi ya athari za ukoloni mamboleo.

Kazi ya kufanya 1.8

Tumia vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, ikiwemo mtandao, kusoma matini zinazohusu mikakati ya kisiasa ya kukabiliana na ukoloni mamboleo. Kisha, eleza mafanikio na changamoto ambazo Tanzania imezipata katika kupinga ukoloni mamboleo.

Mikakati ya kijamii

Katika kujenga jamii yenye mtazamo chanya kuhusu maendeleo, taifa huwekeza katika elimu ili kukuza mawazo, fikra na mitazamo mipya miongoni mwa wananchi. Hali hii ilisisitizwa na Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere, mara baada ya kupata uhuru mwaka 1961. Katika muktadha huo, mikakati ya kijamii ya kupambana na ukoloni mamboleo ililenga zaidi sekta ya elimu, kama ifuatavyo:

Elimu

Kati ya mwaka 1961 na 1966, Tanzania iliendeleza mapambano dhidi ya ukoloni mamboleo kupitia upanuzi na mageuzi ya sekta ya elimu ili iendane na mahitaji ya Watanzania baada ya uhuru. Katika kipindi hiki, elimu ya Tanzania ilikuwa na malengo yafuatayo:

(a) Kuandaa mitaala yenye mtazamo wa Kiafrika badala ya mitaala ya kikoloni iliyokuwa na mwelekeo wa Kimagharibi.

(b) Kusisitiza umuhimu wa elimu kama nyenzo ya kuwawezesha wananchi kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa lao, badala ya kuitazama elimu kama njia ya kuajiriwa tu katika ofisi na kupata mishahara.

(c) Kuhakikisha elimu inawafikia wananchi wengi zaidi, badala ya kuhodhiwa na wachache.

(d) Kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uendeshaji wa shughuli za umma kupitia sera ya Uafrikashaji (Africanisation). Kupitia sera hii, serikali ilitoa mafunzo kwa Watanzania ili waweze kutoa huduma za umma kwa ufanisi. Hatua hii ililenga kuziba nafasi za kiutawala zilizokuwa zikishikiliwa na wazungu na kupunguza utegemezi wa wataalamu wa kigeni.

Makazi

Mara baada ya kupata uhuru, Tanzania iliweka mkazo mkubwa katika kuboresha makazi ya wananchi kama sehemu ya juhudi za kuinua maisha ya watu na kujenga taifa linalojitegemea. Serikali iliaandaa na kutekeleza mipango mbalimbali ya uboreshaji wa makazi kama mkakati muhimu wa maendeleo ya kijamii. Ili kufikia malengo hayo, hatua zifuatazo zilichukuliwa:

Ujenzi wa makazi ya bei nafuu: Serikali ilianzisha miradi ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini na cha kati, hususan katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Mwanza, Unguja na Arusha. Makazi hayo yalitolewa kwa wananchi wote bila ubaguzi wa rangi, kabila au dini. Ujenzi wake ulizingatia ufanisi, usalama na upatikanaji rahisi wa huduma za kijamii, kama vile shule, hospitali na masoko.

Kuimarisha umiliki wa ardhi na nyumba: Serikali ilitekeleza sera za kuondoa mfumo wa kikoloni wa umiliki wa ardhi, uliowezesha watu wachache, hasa wageni, kumiliki ardhi kubwa. Kupitia sera za zakumilikisha ardhi kwa wananchi, familia nyingi ziliweza kujenga makazi na kupata uhuru wa kiuchumi na kiutawala.

Upangaji wa makazi wa kisasa: Serikali ilitekeleza mipango ya upangaji makazi wa kisasa uliolenga kuimarisha miundombinu ya miji, ikiwamo barabara, mitaro ya maji taka, usafi wa mazingira, maeneo ya michezo na huduma nyingine za jamii. Lengo lilikuwa kuhakikisha makazi yanakidhi mahitaji ya wananchi, kupunguza makazi holela na kujenga miji yenye maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Kuendeleza ushirikishwaji wa wananchi: Wananchi waliwezeshwa kushiriki kikamilifu katika mipango ya makazi ya maeneo yao kwa kutoa maoni na mapendekezo, pamoja na kushiriki katika ujenzi wa miundombinu ya makazi. Ushirikishwaji huu ulisaidia kupunguza utegemezi wa makampuni ya kigeni na kutumia maarifa ya ndani katika maendeleo ya makazi.

Maji

Uboreshaji wa miundombinu ya maji safi: Serikali ilitekeleza miradi ya mabomba ya maji mijini na visima vijijini ili kuhakikisha wananchi wengi wananufaika na maji safi.

Elimu ya usafi wa mazingira: Kampeni za elimu kuhusu matumizi ya maji safi, uhifadhi wa vyanzo vya maji, na usafi wa mazingira ziliimarisha afya ya jamii na kupunguza magonjwa yanayohusiana na maji machafu.

Ushirikishwaji wa wananchi: Wananchi waliwezeshwa kushiriki katika kudumisha vyanzo vya maji na ujenzi wa mitaro ya maji machafu katika jamii, jambo lililosaidia kupunguza utegemezi wa wataalamu wa kigeni na kuimarisha uendeshaji wa sekta ya maji.

Umeme

Upanuzi wa mtandao wa umeme: Serikali ilipanua mtandao wa umeme katika miji mikubwa, maeneo yenye viwanda na vijijini ili kusaidia maendeleo ya uchumi wa ndani na kupunguza utofauti miongoni mwa jamii.

Uanzishaji wa miradi ya nishati mbadala: Miradi ya nishati kama umeme wa maji, nishati ya bayogesi, nishati ya jua na jenereta ndogo ndogo ziliwekwa ili kuleta nishati endelevu na kupunguza utegemezi kutoka nchi za Magharibi.

Mafunzo kwa wananchi na wataalamu wa ndani: Ilianzishwa elimu na mafunzo kwa wananchi na wahandisi wa ndani ili kuhakikisha wanaweza kudumisha na kuendesha miradi ya umeme kwa ufanisi, jambo lililosaidia kujenga uwezo wa kitaifa na kupambana na ukoloni mamboleo.

Kazi ya kufanya 1.9

Kwa kutumia mtandao na vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, soma matini kuhusu mikakati ya kijamii katika kupambana na ukoloni mamboleo, kisha eleza changamoto katika utekelezaji wa mikakati hiyo.

Mikakati ya kiutamaduni

Utamaduni ni alama kuu ya utambulisho wa taifa lolote duniani. Kupitia lugha, mila na desturi, vyakula na tabia za wananchi, utamaduni huakisi historia, maadili na mwenendo wa jamii husika. Hata hivyo, uwepo wa ukoloni mamboleo umerudisha nyuma jitihada za kujenga na kuimarisha utamaduni wa Taifa la Tanzania. Kutokana na hali hiyo, serikali, kupitia taasisi zake mbalimbali, ilichukua hatua za makusudi kulinda na kukuza utamaduni wa taifa. Zifuatazo ni baadhi ya jitihada zilizochukuliwa:

Kukuza lugha ya Kiswahili na tunu za taifa: Serikali iliweka mkazo mkubwa katika kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili na tunu nyingine za taifa badala ya lugha ya Kiingereza na utamaduni wa kikoloni. Tofauti na mataifa mengi barani Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zilizochagua kukuza lugha ya asili ya wananchi wake kama lugha ya taifa na rasmi, huku Kiingereza kikipewa nafasi ndogo. Hatua hii ililenga kuimarisha utambulisho wa kitaifa na kupunguza utegemezi wa kiutamaduni kutoka nje.

Uanzishaji wa taasisi za kiutamaduni: Serikali ilianzisha na kuimarisha taasisi mbalimbali za kiutamaduni kwa lengo la kufikisha ujumbe wa kupinga ukoloni mamboleo kwa jamii. Mfano wa taasisi hizo ni Radio Tanzania na Sauti ya Tanzania Zanzibar, ambazo ziliwezesha wananchi kupata elimu kupitia vipindi mbalimbali, kusikiliza hotuba za kisiasa zilizolaani ukoloni mamboleo, pamoja na kutangaza na kuenzi utamaduni wa Mtanzania. Aidha, kuanzishwa kwa Wizara ya Utamaduni na Vijana kulilenga kusimamia na kushirikiana na wasanii na wadau wa sanaa katika kukuza utamaduni wa taifa, sambamba na kupinga athari za ukoloni mamboleo.

Mikakati ya kimaadili

Kabla ya ukoloni, jamii zetu ziliishi kwa kuzingatia maadili waliyorithi kutoka kwa wazee wao. Hata hivyo, katika kipindi cha ukoloni na baada ya kupata uhuru, mwingiliano wa jamii za Kitanzania na jamii nyingine za dunia ulisababisha kudhoofika kwa baadhi ya maadili ya asili. Kutokana na hali hiyo, kati ya mwaka 1961 na 1966, serikali ya Tanzania ilitumia mbinu mbalimbali za kimaadili kupambana na athari za maadili ya ukoloni mamboleo. Baadhi ya mbinu hizo ni kama zifuatazo:

Kukuza itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea: Mwl. Julius K. Nyerere alianza kuitumia falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea hata kabla ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967. Misingi mikuu ya itikadi hii ni utu, usawa wa binadamu na uwajibikaji. Kupitia misingi hiyo, Ujamaa ulipinga aina zote za unyonyaji na utegemezi unaotokana na mifumo ya kibepari, na hivyo kuwajengea wananchi misingi ya kimaadili ya kupinga ukoloni mamboleo.

Kusititiza maadili kwa viongozi wa kisiasa: Mwl. Julius K. Nyerere aliweka mkazo mkubwa kwa viongozi wa kisiasa kuishi kwa uadilifu na kutotumia madaraka yao kwa manufaa binafsi. Viongozi hawaruhusiwa kujilimbikizia mali wala kushiriki katika vitendo vya rushwa, kwani tabia hizo zingechochea kujipenyeza kwa mifumo ya kibepari na kudhoofisha maadili ya taifa.

Kuthamini utu na usawa wa binadamu: Mara baada ya uhuru, Tanzania ilisisitiza heshima kwa misingi ya utu na usawa wa binadamu, ikiamini kwamba binadamu wote ni sawa bila kujali rangi, kabila au asili yao. Aidha, taifa lilipinga ubaguzi wa rangi uliorithiwa kutoka katika utawala wa kikoloni. Kupitia msimamo huu, wananchi waliwezeshwa kupinga mifumo ya ukoloni mamboleo ambayo mara nyingi hutumia mgawanyiko wa kijamii kama nyenzo ya kuendeleza unyonyaji na utegemezi.

Kazi ya kufanya 1.10

Kupitia maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) soma matini mbalimbali kisha, andaa ripoti inayoonesha changamoto ambazo Tanzania inazipitia katika kupambana na athari za ukoloni mamboleo kwenye nyanja ya utamaduni.

Zoezi

1. Tathmini mikakati iliyotendeka katika nyanja ya elimu nchini Tanzania kupambana na athari za ukoloni mamboleo.

2. Jadili mafanikio na changamoto za mikakati ya kijamii nchini Tanzania katika kuimarisha utoaji wa huduma za jamii ili kupambana na athari za ukoloni mamboleo.

 3. Changanua mikakati iliyotekelezwa na Tanzania katika kuhifadhi na kuendeleza utamaduni na maadili ya Kitanzania ili kupambana na athari za ukoloni mamboleo, ukitolea mifano katika, sanaa, lugha, na mila za asili.

4. Tathmini mafanikio na changamoto za mikakati ya kiutamaduni na kimaadili ya Tanzania katika kupambana na athari za ukoloni mamboleo, ukitolea mifano halisi kutoka katika nyanja za elimu, sanaa, mitindo ya maisha, na jamii kwa ujumla.

www.learninghubtz.co.tz

Tamrini

1. Kwa kutumia mifano halisi, tathmini umuhimu wa kujenga jamii yenye uwajibikaji, uzalendo na uhuru wa kisiasa katika kukabiliana na ukoloni mamboleo.

2. Ainisha athari za kimaadili zinazotokana na ukoloni mamboleo kwa viongozi wa sasa wa kisiasa na kisha pendekeza njia za kupambana na athari hizo.

3. Jadili ni kwa namna gani Jumuiya za Kikanda barani Afrika zinaweza kusaidia mapambano dhidi ya ukoloni mamboleo.

4. Onesha uhusiano uliopo kati ya rushwa na ukoloni mamboleo.

5. Uhuru wa kiuchumi ni msingi wa kupambana na ukoloni mamboleo kwa nchi zinazoendelea. Jadili hoja hii kwa kutumia mifano halisi.

6. Kwa kutumia mifano halisi, chambua mchango wa viongozi wa nchi za Afrika katika kupambana na ukoloni mamboleo.

7. Pamoja na Tanzania kupata uhuru mwaka 1961, bado inakabiliwa na changamoto za ukoloni mamboleo. Tathmini hoja hii kwa kutoa mifano halisi kutoka katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kijamii au kiutamaduni.

8. Tathmini kwa kina jinsi rushwa inavyoweza kuathiri harakati na mikakati ya Tanzania ya kupambana na athari za ukoloni mamboleo, ukitolea mifano halisi kutoka katika sekta za umma.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256