Sura Ya 01 : Fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili

Utangulizi

Fasihi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha katika kuwasilisha ujumbe kwa jamii. Katika sura hii, utajifunza kuhusu dhana ya fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili. Pia, utajifunza sifa na umuhimu wa fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili. Vilevile, utajifunza kuhusu mchango wa fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili katika maendeleo ya fasihi. Ujuzi utakaoujenga utakusaidia kuthamini umuhimu wa fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili katika kustawisha maisha ya Waswahili.

Umuhimu wa fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili

Shughuli ya 1.1

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa, ikiwamo mtandao, soma vitabu mbalimbali vya fasihi ya Kiswahili, kisha eleza maana, sifa na umuhimu wa fasihi ya Kiswahili.

Dhana ya fasihi ya Kiswahili

Dhana ya Fasihi ya Kiswahili ni pana. Wataalamu mbalimbali (kama vile Mlaga, 2017 na Mulokozi, 2017) wanaelezea kuwa fasihi ya Kiswahili ni ile iliyoaandikwa kwa Kiswahili, na inayozungumzia utamaduni wa Waswahili. Ponera (2014) anaeleza kuwa utamaduni ni jumla ya mambo yanayopambanua, kutambulisha, na kupa upekee jamii fulani. Hivyo, fasihi ya Kiswahili inaweza kufasiliwa kuwa ni kazi mbalimbali za fasihi zilizowamo hadithi, ushairi na semi kwa upande wa fasihi simulizi; na riwaya, tamthiliya, ushairi, na hadithi fupi kwa upande wa fasihi andishi.

Sifa za fasihi ya Kiswahili

Mbali na kuwa na sifa za jumla za fasihi, fasihi ya Kiswahili ina sifa mahsusi zinazoitambulisha na kuitofautisha na fasihi za jamii nyingine. Sifa mojawapo ya msingi ya fasihi ya Kiswahili nikutumia lugha ya Kiswahili katika kuwasilisha maudhui. Maudhui hayo huweza kuwasilishwa kwa maandishi au masimulizi ambapo mwandishi au msimulizi huchagua maneno kwa ustadi ili kuonesha ubunifu. Aidha, hutumia mbinu mbalimbali za kisanaa ili kubeba hisia, maana na ujumbe.

Vilevile, fasihi ya Kiswahili huakisi utamaduni wa Waswahili, kwani huzaliwa kutoka katika misingi na mazingira ya Waswahili na jamii husika. Vipengele vya kitamaduni vinavyoakisiwa hujumuisha lugha, desturi (kama vile mazoea, kaida au tajiriba), na mila (kama vile miiko au makatazo). Hivyo, kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili hufumba maudhui na uhai ya kitamaduni. Mtunzi au msimulizi huweza kusawiri vipengele hivyo vya kitamaduni kwa sababu ya kufundisha, kusifia, kuburudisha, kulemewa, au hata kurekebisha. Mifano ya masuala yanayoweza kusawiriwa na mtunzi au msimulizi ni: bidii ya kazi, tabia njema, usaliti, na ubadhirifu. Aidha, hadhira husoma au kusikiliza, kisha huweza kujifunza na, wakati mwingine, kujiburudisha kutokana na visa na matukio yaliyoangiliwa katika kazi mahsusi ya fasihi.

Aidha, fasihi ya Kiswahili huangazia historia ya Waswahili na jamii husiani. Kwa kuwa fasihi ya Kiswahili hutokana na jamii ya Waswahili na jamii husiani, fasihi hii hujichomoza kama zana muhimu ya kusawiri mapito mbalimbali ya jamii ya Waswahili na jamii husiani. Kwa mantiki hiyo, wapokezi wa kazi za fasihi ya Kiswahili hupata nafasi pana ya kutambua matukio mbalimbali ambayo jamii ilimepitia katika nyakati mbalimbali. Mathalani, fasihi ya Kiswahili humulika hali ya Waswahili iliyokuwa wakati wa utumwa. Kazi mbalimbali, kama vile riwaya ya Uhuru wa Watumwa, zinaonesha madhila ya kipindi hicho cha kihistoria. Pia, baadhi ya kazi zinatoa taarifa kuhusu maisha ya jamii au mataifa ya Waswahili katika miaka ya mwanzooni baada ya kupata uhuru. Mfano mzuri katika hoja hii ni tamthiliya za Kijiji Chetu na Giza Limeingia. Tukio lingine la kihistoria ambalo hadhira ya kazi za fasihi ya Kiswahili huweza kupata kupitia fasihi ya Kiswahili ni kuhusu ujio wa janga la UKIMWI katika jamii za Waswahili. Kazi mbalimbali, kama vile tamthiliya ya Ushuhuda wa Mifupa, Kilio Chetu na Orodha, zimesawiri vema kuhusu ujio wake, njia za kuambukiza, madhila yake, na jinsi ya kujiepusha na janga hili.

Fasihi ya Kiswahili pia husawiri falsafa na itikadi ya Waswahili na jamii husiani kwani kila jamii huwa na falsafa na itikadi yake. Falsafa ni mawazo yanayoaminiwa na watu katika kuongoza maisha yao; na itikadi ni imani inayotumiwa kama njia au nyenzo ya kutekelezea falsafa, yaani mawazo kuhusu maisha. Aghalabu, dhana hizi mbili, yaani falsafa na itikadi, huenda pamoja kwa sababu mawazo ya kila peke yake kuhusu maisha hayawezi jamii kuishi kwa mujibu wa mawazo hayo. Hivyo, huitajika njia au nyenzo ya kutekeleza namna ya kuishi kwa mujibu wa fikra husika. Falsafa na itikadi hujitokeza takribani katika kila nyanja ya maisha ya jamii, hususan katika utamaduni, siasa, mazingira, na uchumi.

Madumula (2009) anaeleza kuwa wapo wanandishi wanaocheka nje ya eneo la Afrika Mashariki na Kati lakini wanashababu Uswahili, yaani waandishi wa Kiswahili wenye asili ya Ulaya kama vile Harold E. Lambert, Graham Hyslop, na Richard Mabala ambao wameweza kutunga na kuandika kazi za kifasihi zinazotumia lugha ya Kiswahili na kuakisi vema utamaduni wa Mswahili. Hii inaamanisha kuwa kazi za fasihi ya Kiswahili huweza kuandikwa au kuwasilishwa na mzawa wa jamii za Waswahili au mtu yeyote aliyeishi na kustaarabu vipengele mbalimbali vya maisha ya Waswahili.

Umuhimu wa fasihi ya Kiswahili

Fasihi ya Kiswahili imekuwa na umuhimu mkubwa kwa Waswahili wenyewe na kwa jamii za Kiafrika na dunia kwa ujumla. Umuhimu huo umejidhihirisha katika kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili, hususan katika kukuza msamiati na matumizi sahihi ya lugha kwa wasikilizaji na wasomaji wa kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili. Kazi za fasihi ya Kiswahili zimewasaidia watu wa marika yote kuimarisha usomaji, usikilizaji, uandishi, na uelewa wa lugha ya Kiswahili. Zaidi ya hayo, zimesaidia kuimarisha vipengele mbalimbali vya lugha ya Kiswahili kama vile methali, misemo, na tamathali za semi za lugha ya Kiswahili. Hali kadhalika, kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili zimekuwa zikiendeleza na kuhifadhi vipengele mbalimbali vya utamaduni wa Mswahili na jamii husiani. Fasihi kwa ujumla hukuza na kuhifadhi vipengele vya utamaduni wa jamii, vikiwamo ushirikiano, adabu na miiko. Mfano mmoja wapo wa kazi ya fasihi ya Kiswahili ambayo inadumisha kipengele cha ushirikiano ni riwaya ya Mtu ni Utu (1971) na Mfadhili (2007) zilizoandikwa na George Mhina na Hussein Tuwa mtawalia. Kazi hizi zinaeleza umuhimu wa wanajamii kusaidiana bila kutarajia kupata kitu chochote kama ilivyo desturi ya Waswahili au Waafrika kwa ujumla.

Vilevile, kazi za fasihi ya Kiswahili hutoa elimu (maarifa na ujuzi) ambapo hadhira hunufaika na elimu hiyo kwa namna mbalimbali. Mathalani, hadhira hufundishwa kuhusu faida za mvuendo mwema. Pia, huonywa kuhusu madhara ya tabia na masuala mengine yanayorudisha nyuma maendeleo ya yanayoweza kuleta unyufivu wa amani katika jamii kama vile rushwa, ulevi, uzembe, wizi, ufisadi, na ubaguzi. Mfano mmoja wapo wa elimu inayotolewa kupitia semi mbalimbali ni methali ya Kiswahili isemayo, mwenda tezi na omo, marejeo ngoma. Kupitia methali hii, hadhira hupata maarifa kuhusu dhana ya utulivu na uvumilivu, hasa mtu anapokuwa katika tatizo au msukosuko unaochukua muda mrefu. Mtu huyo anaelimishwa kuwa, akiwa katika hali hiyo, bora atulie kuliko kuhangaila huku na huko, yaani asiende tezi (sehemu ya mbele ya mashua au meli) wala omo (sehemu ya nyuma ya mashua au meli), bali abakie katika sehemu sahihi ya kukaa (ngama) akitafakari kuhusu namna ya kukabiliana au kutatua tatizo lake. Mfano mwingine unaohusu namna kazi za fasihi ya Kiswahili zinavyotumika kuleta furaha, ambapo ni kipengele muhimu katika maisha ya mwanadamu. Kwa kawaida, mwanadamu awapo katika shughuli za kuendesha maisha yake, huweza kukumbana na msawajiko au msongo wa mawazo. Fasihi ya Kiswahili hutumika kuleta furaha kwa jamii kwa njia ya burudani. Kwa mfano, wasomaji au wasikilizaji huweza ama kupunguza au kuondoa kabisa msongo wa mawazo na kuchangamsha akili kupitia nyimbo za jamii mbalimbali, taarabu, na nyimbo za kizazi kipy.

Pia, fasihi ya Kiswahili huchochea fikra tunduizi, yaani kuchambua jambo kwa kina ili kupata maana na kufikia hitimisho au kufanya uamuzi mwafaka. Misingi ya kufikiri kitunduizi ni mantiki, usahihi na uwazi. Mtu anayefikiri hutakiwa kuwa katika hali ya utulivu ili akili yake iweze kuelekeza jambo analolikabili tu, na si mengine. Hata hivyo, anatakiwa aweke makini ya kutosha katika kulikabili jambo linalohusika. Watu hufikiri kitunduizi wakati wa kusikiliza au kusoma kazi za fasihi. Aghalabu, kazi za fasihi hutumia lugha yenye mbinu mbalimbali za kisanaa. Mbinu hizo hujumuisha mafumbo, ishara, tamathali za semi, na visa vilivyopangiliwa katika muundo maalumu. Utanzuaji wa mbinu hizo, humtaka hadhira kufikiri kitunduizi ili kupata maana. Hii huwafanya watu kuchambua kwa mtazamo mbalimbali mawazo ya mwandishi au mtunzi wa simulizi husika kulingana na muktadha na muda wa utunzi wa kazi husika. Kwa kufanya hivyo, hadhira na jamii kwa ujumla hujenga tabia ya kutumia mantiki katika kufanya jambo lolote katika maisha ili kuelewa barabara kabla ya kulitolea uamuzi. Tabia hii hatimaye huwezesha jamii kuwa na ufanisi na ustawi katika maisha.

Shughuli ya 1.2

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa, ikiwamo mtandao, soma kazi anuai za fasihi ya Kiswahili, kisha eleza maana, sifa na umuhimu wa fasihi kwa Kiswahili.

Dhana ya fasihi kwa Kiswahili

Wataalamu mbalimbali wameielezea dhana ya fasihi kwa Kiswahili kuwa ni tafsiri ya fasihi ya mataifa mengine kwa lugha ya Kiswahili. Dhana hii imebuka kutokana na kuenea kwa Kiswahili ndani na nje ya Afrika Mashariki, na hata nje ya Bara la Afrika. Pia, imeibuliwa kutokana na utangamano kati ya wazungumzaji wa Kiswahili na mataifa mengine (Mulokozi, 2017). Hivyo, fasihi kwa Kiswahili ni aina ya fasihi iliyoandikwa au kusimuliwa kwa kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, bila kujali imetoka katika jamii gani. Ifuatayo ni mifano ya kazi za fasihi kwa Kiswahili: Hadithi za Alfu Lela Ulela, Barua Ndefu kama Hili, Mashimo ya Mafule Suleimani, Juliasi Kaizari, Mabepari wa Venisi, na Hadithi za Aesopo. Mfano mwingine ni: Nitaolewa Nikipenda, Takatifu, na Usaliti Mjini.

Sifa za fasihi kwa Kiswahili

Fasihi kwa Kiswahili ina sifa bainifu zinazoi­pambanua dhidi ya fasihi ya Kiswahili. Miongoni mwa sifa hizo ni kuandikwa kwa lugha ya kigeni (kama vile Kiingereza, Kiarabu na Kifaransa), kisha kutafsiriwa au kukalimaniwa kwa lugha ya Kiswahili. Kazi hizo hubadilishwa na kuwa katika kwa lugha ya Kiswahili ili ziweze kusomwa na jamii ya Waswahili. Aghalabu, kazi za fasihi kwa Kiswahili huwakilisha maudhui ya jamii ya lugha chanzi. Huwa vipengele kama vile mtazamo, falsafa, utamaduni, na itikadi za jamii hizo. Hivyo, kwa ujumla, huangazia fikra na maisha ya jamii za lugha chanzi. Hufanya hivyo kwa kutumia vipengele mbalimbali vya kifani (kama vile lugha, mandhari, na wahusika) vinavyoakisi uhalisi wa jamii hiyo. Hivyo, hubeba utambulisho wa jamii hizo kwa kusawiri vipengele mbalimbali vya maisha yao.

Umuhimu wa fasihi kwa Kiswahili

Fasihi kwa Kiswahili imekuwa na umuhimu wa kiuchumi kwa jamii za Kiafrika. Kufasiriwa kwa kazi mbalimbali za lugha za kigeni kuwa katika lugha ya Kiswahili kumesaidia kukuza kipato kwa wafasiri, waandishi na watunzi. Hii hutokana na mauzo ya kazi zao kama vile vitabu, maonesho ya tamthiliya, mashindano ya utunzi, na kutafsiri kazi mbalimbali. Pia, kufanya hivyo huongeza pato la taifa. Fasihi kwa Kiswahili pia imekuwa ikitumika katika kuhimiza na kuendeleza Kiswahili kupitia kutafsiri kazi mbalimbali za kifasihi ambazo hufasiriwa kwa kutumia lugha fasaha iliyoseheni misemo, nahau, tamathali za semi na methali, hivyo kurifanya fasihi kubaki hai. Vilevile, imekuza uhusiano wa Kimataifa, kwani huakisi desturi, mila na tajiriba za nchi iliyotokea. Hivyo, kitendo cha kutafsiri kazi hizo kwa lugha ya Kiswahili huzifanya kuwa daraja madhubuti la kujenga uhusiano baina ya jamii za lugha chanzi na jamii ya Waswahili. Utangamano huo, hatimaye, huwezesha Waswahili kujifunza tamaduni na historia za jamii za kigeni. Hata hivyo, katika kuchochea fikra linganishi, Waswahili wanapopokea kazi za fasihi kwa Kiswahili hupata maudhui na fani inayohusiana na kazi hizo. Kutokana na hilo, hadhira hiyo huweza kupata wazo la kuinganisha hali inayoasawiriwa katika kazi hizo na uhalisi wa maisha au kazi za fasihi ya Kiswahili. Mathalan, hadhira ya jamii ya Waswahili huweza kulinganisha mbinu za utunzi wa matini mbalimbali yanayomkuta mtu mmoja mmoja au jamii kadri zilivyosawiriwa katika kazi hizo. Hatimaye, ulinganisho huo husaidia kuinua usawiri wa kazi za fasihi ya Kiswahili na hata ustawi wa maisha ya Waswahili kwa ujumla.

Shughuli ya 1.3

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwamo mtandao, chunguza kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili, kisha chambua mbinu za kifasihi zilizomo katika kazi hizo.

Shughuli ya 1.4

“Isingekuwapo fasihi ya Kiswahili, pasingekuwapo na fasihi kwa Kiswahili”. Jadili kauli hii kwa kurejelea hoja za wataalamu mbalimbali.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

  1. Kwa kutumia mifano, tofautisha dhana za fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili.
  2. Chagua riwaya mbili teule za Kiswahili zilizofasiriwa, kisha eleza uhusiano uliopo kati ya fasihi kwa Kiswahili na maendeleo ya jamii.
  3. Kulingana na muktadha wa sasa, fasihi kwa Kiswahili ina umuhimu gani kwa jamii ya Kiafrika?
  4. Eleza sababu zinazochangia kuongezeka kwa tafsiri za kazi za fasihi kwa Kiswahili kutoka nje ya Afrika Mashariki.

Mchango wa fasihi ya Kiswahili katika maendeleo ya fasihi kwa Kiswahili

Fasihi ya Kiswahili imechangia kuwapo kwa Fasihi kwa Kiswahili. Uelewa na uzoefu wa kutunga na kusoma kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili umetoa msukumo kwa baadhi ya wataalamu kutafsiri kazi za fasihi za kutoka katika jamii nyingine katika lugha ya Kiswahili. Pia, kuwapo kwa kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili kumehamasisha kuwapo kwa wapokezi (wasomaji na wasikilizaji) wa kazi hizo. Kuwapo kwa wasomaji hao wa kazi za fasihi ya Kiswahili kunachukuliwa kama soko zuri kwa kazi za fasihi za jamii nyingine. Hivyo, kumechangia kupatikana kwa wazo na msukumo wa kutafsiriwa kwa kazi za fasihi za jamii nyingine na kutumia hadhira ya Waswahili kama soko. Vilevile, shughuli za utunzi, usomaji, uhakiki, na utafiti wa mambo mbalimbali kuhusu na kazi za fasihi ya Kiswahili zimechangia kuibua wazo la kulinganisha kazi za fasihi ya Kiswahili na za jamii nyingine. Wazo hilo, lilichangia kutafsiriwa kwa kazi za fasihi kutoka katika jamii nyingine ili kuendeleza fasihi kwa Kiswahili.

Shughuli ya 1.5

Umealikwa kushiriki katika mdahalo unaohusu mchango wa fasihi ya Kiswahili katika maendeleo ya fasihi kwa Kiswahili. Andaa hoja zisizopungua tano utakazowasilisha katika mdahalo huo.

Mchango wa fasihi kwa Kiswahili katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili

Kuwapo kwa kazi za fasihi kwa Kiswahili kumechochea ongezeko la shughuli za utafiti wa masuala mbalimbali ya fasihi katika jamii za Waswahili. Wataalamu mbalimbali wa fasihi katika jamii za Waswahili wamekuwa wakifanya tafiti kuhusiana na kazi za hadithi fupi, riwaya, tenzi, tamthiliya, na mashairi yaliyo tafsiriwa kutoka katika lugha nyingine. Kufanya hivyo kumesaidia kutoa maarifa na ujuzi wa wataalamu wa fasihi ya Kiswahili; hivyo kukuza fasihi hiyo. Vilevile, kazi za fasihi kwa Kiswahili zimekuwa chimbuko la fasihi ya kisasa katika fasihi ya Kiswahili. Kwa kuzingatia kuwa sehemu kubwa ya kazi za fasihi zilizotafsiriwa zimetoka katika jamii tofauti na zile za Waswahili, wapokezi wa kazi hizo (wasomaji, watazamaji, wasikilizaji, wahakiki, na watafiti) wamekuwa wakipata vionjo vipya vinavyopatikana katika kazi hizo.

Pia, kazi za fasihi kwa Kiswahili zimeongezea jitihada ya kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili nje ya maeneo ya jamii za Waswahili. Hii ni kutokana na kazi zilizokuwa zimeandikwa au kusimuliwa kwa lugha za kigeni kufasiriwa kwa Kiswahili, hivyo kuwafanya watunzi wa awali kujifunza lugha ya Kiswahili ili waweze kujisomea au kusikiliza kazi zao. Kutokana na kusoma na kusikiliza kazi hizo, wageni hao wameweza kukuza msamiati pamoja na mitindo ya lugha na tamathali za semi. Hali kadhalika, kazi za fasihi kwa Kiswahili zimeboresha utunzi wa kazi za fasihi ya Kiswahili. Kazi hizo za fasihi kwa Kiswahili zimechochea waandishi wengi kuandika kazi bunifu kwa Kiswahili. Zaidi ya hayo, zimesaidia kuimarika kwa mbinu mbalimbali za kiutunzi ambazo waandishi wa jamii za Waswahili wamekuwa wakizichota katika kazi za fasihi kwa Kiswahili; hatimaye kuchangia katika kupanua fasihi ya Kiswahili.

Shughuli ya 1.6

“Fasihi kwa Kiswahili isingeweza kuendelea bila kuhusishwa na fasihi ya Kiswahili kama ilivyo sasa”. Jadili hoja hii kwa kutumia kazi za waandishi mbalimbali.

Tamrini

  1. “Fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili ni kazi zinazo­tegemeana na kushirikiana.” Thibitisha kauli hii kwa mifano thabiti.
  2. Eleza umuhimu wa kuandika kazi za fasihi kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
  3. Ni kwa namna gani fasihi ya Kiswahili inaweza kuleta mabadiliko katika jamii?
  4. Jadili mchango wa fasihi kwa Kiswahili katika kukuza lugha ya Kiswahili.
  5. Eleza mchango wa watafiti wa fasihi katika kuendeleza fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili.
  6. Kwa kutumia mifano, tathmini mchango wa waandishi wa kazi za fasihi katika kukuza fasihi ya Kiswahili.
  7. Tathmini hatima ya uhusiano wa fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili katika kipindi hiki cha utandawazi.

www.learninghubtz.co.tz

ZOEZI LA MARUDIO

SEHEMU A: Maswali ya Chagua Jibu Sahihi (Alama 20)

1. Fasihi ya Kiswahili ni:
 A. Fasihi yote iliyoandikwa kwa lugha yoyote.
 B. Fasihi iliyoandikwa kwa Kiswahili na kuakisi utamaduni wa Waswahili.
 C. Fasihi yote ya Afrika.
 D. Fasihi ya tafsiri pekee.

2. Kazi ipi ni mfano wa fasihi kwa Kiswahili?
 A. Kufikirika
 B. Nagona
 C. Juliasi Kaizari
 D. Kiu

3. Sifa mojawapo ya fasihi ya Kiswahili ni:
 A. Kuandikwa kwa Kifaransa.
 B. Kutafsiriwa kutoka lugha nyingine.
 C. Kuakisi utamaduni wa Waswahili.
 D. Kutotumia lugha ya Kiswahili.

4. Fasihi kwa Kiswahili hutokana na:
 A. Kazi za fasihi zilizoandikwa kwa Kiswahili tangu mwanzo.
 B. Tafsiri za kazi za lugha nyingine.
 C. Mashairi ya Waswahili pekee.
 D. Hadithi simulizi za Waswahili.

5. Umuhimu mmoja wa fasihi ya Kiswahili ni:
 A. Kupunguza matumizi ya Kiswahili.
 B. Kuhifadhi utamaduni wa Waswahili.
 C. Kuondoa mila zote za Kiafrika.
 D. Kukuza lugha za kigeni.

SEHEMU B: Maswali Mafupi

6. Fasili fasihi ya Kiswahili.

7. Fasili fasihi kwa Kiswahili.

8. Taja sifa nne za fasihi ya Kiswahili.

9. Taja sifa nne za fasihi kwa Kiswahili.

10. Eleza umuhimu wowote watano wa fasihi ya Kiswahili.

11. Eleza umuhimu wowote watano wa fasihi kwa Kiswahili.

12. Tofautisha fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili kwa hoja nne.

13. Taja mifano mitano ya kazi za fasihi kwa Kiswahili.

14. Eleza maana ya falsafa na itikadi kama zinavyojitokeza katika fasihi ya Kiswahili.

15. Eleza jinsi fasihi ya Kiswahili inavyoakisi historia ya Waswahili.

SEHEMU C: Maswali ya Insha

16. Kwa kutumia mifano mwafaka, jadili sifa sita za fasihi ya Kiswahili.

17. Jadili umuhimu wa fasihi ya Kiswahili katika maendeleo ya jamii ya Tanzania.

18. Kwa kutumia mifano, eleza tofauti kati ya fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili.

19. Jadili mchango wa fasihi ya Kiswahili katika maendeleo ya fasihi kwa Kiswahili.

20. Jadili mchango wa fasihi kwa Kiswahili katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

21. "Fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili ni taaluma zinazotegemeana." Thibitisha kauli hii kwa hoja sita.

22. Eleza jinsi fasihi ya Kiswahili inavyochangia kukuza lugha ya Kiswahili.

23. Jadili nafasi ya fasihi kwa Kiswahili katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa.

24. Kwa kutumia mifano, tathmini umuhimu wa tafsiri katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

25. "Fasihi ni kioo cha jamii." Jadili kauli hii ukirejelea fasihi ya Kiswahili.

Maswali ya Mtindo wa NECTA (Uchambuzi)

26. Kwa hoja zisizopungua sita, eleza kwa nini fasihi ya Kiswahili ni nyenzo muhimu ya kuhifadhi utamaduni wa Waswahili.

27. Jadili namna fasihi kwa Kiswahili ilivyochangia maendeleo ya fasihi ya Kiswahili katika kipindi cha utandawazi.

28. Linganisha na ulinganishe fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa Kiswahili kwa kuzingatia:

  • Chanzo
  • Lugha
  • Maudhui
  • Utamaduni
  • Mchango katika jamii

29. Kwa kutumia mifano ya kazi za kifasihi, eleza jinsi fasihi inavyojenga fikra tunduizi kwa jamii.

30. "Bila fasihi ya Kiswahili, fasihi kwa Kiswahili isingekuwepo." Jadili kauli hii kwa hoja nane.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256