Sura Ya 02 : Mifumo ya ulinzi na usalama wa Taifa

Utangulizi

Katika kujenga misingi ya amani na utulivu, ni muhimu kuwa na mifumo imara ya ulinzi na usalama dhidi ya vitisho vya ndani na nje ya nchi. Katika sura hii, utajifunza kuhusu chimbuko la mifumo ya ulinzi na usalama wa Taifa, mabadiliko yaliyofanyika baada ya kupata uhuru, pamoja na nafasi ya maadili katika kujenga mifumo hiyo. Aidha, utajifunza umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika shughuli za ulinzi na usalama. Umahiri utakaoujenga utakusaidia kuthamini na kushiriki ipasavyo katika juhudi za kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa.

Fikiri

Mifumo ya ulinzi na usalama wa Taifa

Dhana ya ulinzi na usalama wa Taifa

Ulinzi na usalama wa Taifa ni msingi muhimu wa ustawi wa taifa, kwani bila uhakika wa ulinzi na usalama, maendeleo endelevu hayawezi kupatikana. Ulinzi wa Taifa unahusisha jitihada mahsusi za kulinda uhuru, mipaka na maslahi ya nchi dhidi ya vitisho mbalimbali, vikiwamo vya kijeshi, kiuhalifu, kimazingira na kisiasa, ambavyo vinaweza kutoka ndani au nje ya nchi. Shughuli za ulinzi hujikita zaidi katika kuzuia mashambulizi ya kijeshi, kama vile vita au uvamizi.

Kwa upande mwingine, usalama unahusu zaidi shughuli za ndani zinazolenga kulinda raia, mali zao, amani ya kitaifa na uhuru wa taasisi za serikali. Katika muktadha wa Tanzania, mfumo wa usalama unajumuisha vyombo mbalimbali vya kitaifa, kama vile Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania Intelligence and Security Service – TISS, Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Aidha, mfumo wa ulinzi na usalama unahusisha pia maeneo ya sera na utekelezaji, yakiwamo usalama wa kiuchumi, usimamizi wa rasilimali na nishati kama gesi na maji, usalama wa mazingira, usalama wa mtandao (cybersecurity), usalama wa jamii unaojumuisha huduma za afya, elimu na haki za binadamu, pamoja na usalama wa miundombinu muhimu kama barabara, viwanja vya ndege, madaraja, mawasiliano na umeme. Vilevile, mfumo huu unahusisha ushirikiano wa kimataifa na diplomasia kupitia mikataba ya kiusalama na mataifa mengine. Kwa ujumla, mfumo wa ulinzi na usalama wa Taifa ni wa ushirikiano, ambapo vyombo vyote husika hufanya kazi kwa pamoja kwa ufanisi ili kulinda maslahi ya taifa na ustawi wa raia wake, huku vikizingatia mwongozo, kanuni, sheria na heshima ya haki za binadamu.

Umuhimu wa mifumo ya ulinzi na usalama nchini Tanzania

(a) Kulinda amani na utulivu wa taifa: Mifumo ya ulinzi na usalama husaidia kuzuia vurugu, uasi na mashambulizi ya kisiasa, hivyo kulinda utulivu wa ndani na kuimarisha amani ya taifa kwa ujumla.

(b) Kulinda raia na mali zao: Vyombo vya usalama, kama vile Jeshi la Polisi na vyombo vya kijeshi, hutoa ulinzi kwa wananchi na mali zao dhidi ya uhalifu, ugaidi, ujasusi na vitisho vingine, jambo linaloongeza kiwango cha usalama kwa raia.

(c) Kukuza maendeleo ya kiuchumi: Usalama wa taifa huwezesha kuwapo kwa mazingira bora ya uwekezaji na biashara. Pale ambapo raia na wawekezaji wanapokuwa na imani kuwa usalama ni thabiti, huvutiwa kuwekeza zaidi, hali inayochochea ukuaji wa uchumi.

(d) Kulinda rasilimali muhimu: Tanzania ina rasilimali muhimu kama gesi asilia, maji na madini. Mfumo wa usalama una wajibu wa kuhakikisha rasilimali hizi zinalindwa, zinatumika kwa manufaa ya taifa na hazitumiwi vibaya au kupotea kutokana na vitisho vya ndani au nje.

(e) Kushughulikia vitisho vya kiteknolojia: Katika zama za sasa, mashambulizi ya mtandao cyber-attacks ni tishio kubwa kwa usalama wa taifa. Mifumo ya ulinzi na usalama inapaswa kuimarisha uwezo wa kulinda taarifa, data na mawasiliano ya serikali na raia dhidi ya udukuzi na uharibifu wa kiteknolojia.

(f) Kuwa tayari kwa dharura na majanga: Usalama wa taifa unahitaji kuwapo kwa mifumo madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili, kama vile mafuriko, ukame na matetemeko ya ardhi, pamoja na vitisho vingine vya kimazingira. Hatua hizi ni muhimu katika kupunguza madhara kwa raia na miundombinu ya taifa.

(g) Ushirikiano wa kimataifa: Mifumo ya usalama huiwezesha Tanzania kushirikiana na mataifa mengine kupitia mikataba ya kiusalama, mazoezi ya kijeshi na mipango ya pamoja. Ushirikiano huu huimarisha ushawishi wa kimkakati wa taifa na kusaidia kuzuia vitisho vya kimataifa.

(h) Kuimarisha uaminifu wa raia kwa serikali: Pale ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kwa ufanisi, uwazi na haki, raia hujenga imani kubwa kwa serikali. Hali hii ni muhimu kwa kudumisha utulivu wa kisiasa na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maendeleo ya taifa.

(i) Kusaidia usimami wa sheria za kitaifa: Vyombo vya ulinzi na usalama husaidia serikali kutekeleza na kusimamia sheria na sera za kitaifa, ikiwamo kulinda Muungano, kuhifadhi uhuru wa taifa na kuimarisha mshikamano wa kitaifa, mambo ambayo ni msingi wa taifa imara.

Kazi ya kufanya 2.1

Fanya mahojiano na watu mbalimbali kuhusu shughuli za ulinzi na usalama zinazotekelezwa katika eneo lao. Kusanya maelezo yao, kisha andika ripoti inayoeleza kwa ufasaha aina ya shughuli hizo, namna zinavyotekelezwa, pamoja na umuhimu wake kwa jamii.

Chimbuko la mifumo ya ulinzi na usalama wa Taifa

Mifumo ya ulinzi na usalama wa Taifa ina chimbuko na historia ndefu inayoanzia kipindi cha kabla ya ukoloni, ikaendelea wakati wa ukoloni, na kufuatiwa na mabadiliko makubwa baada ya uhuru. Ili kulielewa chimbuko hili kwa kina, ni muhimu kuchambua sababu na mabadiliko yaliyotokea katika vipindi hivyo vitatu: kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya uhuru.

Ulinzi na usalama kabla ya ukoloni

Shughuli za ulinzi na usalama zilianza tangu kipindi cha kabla ya ukoloni. Katika kipindi hiki, jamii nyingi zilikuwa na mifumo ya ulinzi wa jadi iliyomhusisha kila mwanajamii. Ulinzi wa jadi ulikuwa msingi mkuu wa usalama wa jamii zote katika kipindi hicho. Silaha zilizotumika kulinda jamii zilijumuisha pinde, mikuki, mishale, panga na sime. Kila jamii ilikuwa na utaratibu wa kuwaandaa vijana wake kujifunza matumizi ya silaha za jadi, na baadaye vijana hao walipewa jukumu la kulinda jamii zao.

Wakati wa amani, vijana waliokuwa wakijihusisha na ulinzi waliendelea na shughuli zao za kawaida za kiuchumi na kijamii. Katika kipindi hiki cha kabla ya ukoloni, jukumu la ulinzi na usalama wa jamii lilikuwa likitekelezwa zaidi na wanaume, huku wanawake wakijihusisha zaidi na shughuli za uzalishaji mali na majukumu ya kifamilia.

Aidha, mifumo ya ulinzi na usalama kabla ya ukoloni ilihusisha ushirikiano wa koo na jamii mbalimbali katika kulinda maeneo yao. Baadhi ya jamii zilikuwa na mifumo imara ya ulinzi na usalama; kwa mfano, jamii ya Wangoni ilikuwa na wapiganaji wa kudumu waliobobea katika mbinu za kivita. Vilevile, jamii ya Wasukuma ilikuwa na utaratibu wa kuwaandaa wanajamii katika vikundi maalumu vya ulinzi na usalama. Kwa ujumla, katika jamii nyingi, mifumo ya ulinzi na usalama ilikuwa imara, ambapo karibu kila kijana wa kiume alikuwa sehemu ya ulinzi na usalama wa jamii yake.

Sababu kuu zilizochangia kuanzishwa kwa mifumo ya ulinzi na usalama ni pamoja na:

  1. Ulinzi dhidi ya maadui kutoka jamii nyingine;
  2. Ulinzi dhidi ya makundi yaliyokuwa yakiteka watu kwa ajili ya biashara ya watumwa; na
  3. Ulinzi wa rasilimali muhimu, kama vile mifugo, ardhi na vyanzo vya maji.

Mfano wa jamii za Kitanzania zilizokuwa na mifumo ya jadi ya ulinzi ni ule wa Mtemi Mirambo, aliyedhibiti njia za biashara kutoka ukanda wa Maziwa Makuu na magharibi mwa Tanzania kuelekea pwani. Kupitia udhibiti wa biashara hiyo, alipata kodi na silaha za moto, jambo lililoimarisha uwezo wake wa kijeshi. Kielelezo 2.1 kinamwonesha Mtemi Mirambo, aliyekuwa mahiri katika mbinu za kivita na aliyewatumia wapiganaji wa kukodi, maarufu kama rugaruga, ambao wengi wao walikuwa wapiganaji hodari kutoka jamii ya Wangoni.

Vilevile, Mtemi Isike wa Unyanyembe (Tabora) alikuwa mjuzi wa mbinu za kivita na alisaidiwa na vijana wapiganaji waliokuwa mahiri. Kutokana na umahiri huo, aliweza kupambana na jeshi la Wajerumani mwanzoni mwa mwongo wa mwisho wa karne ya 19. Kadhalika, katika Uhehe, wapiganaji wa Mkwawa walipambana kwa ujasiri mkubwa dhidi ya Wajerumani katika mwongo wa mwisho wa karne hiyo. Viongozi wengine wa Kitanzania waliopigana dhidi ya Wajerumani kupinga ukoloni ni pamoja na Abushiri ibn Salim al-Harthi, aliyeongoza harakati za upinzani kati ya mwaka 1888 na 1889, Mangi Sina wa Kibosho, pamoja na Kinjeketile Ngwale aliyeongoza Vita vya Majimaji kati ya mwaka 1905 na 1907. Katika mapambano haya, askari wa jadi walitumika kwa kiasi kikubwa na walitegemea zaidi silaha za jadi katika kupambana na maadui zao. Kielelezo 2.2. kinawaonesha askari wa jadi wakiwa na zana mbalimbali za ulinzi.

Kielelezo 2.1: Mtemi Mirambo wa Wanyamwezi

Kielelezo 2.2: Askari wa jadi wakiwa na silaha za jadi

Kazi ya kufanya 2.2

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, ikiwemo mitandao, soma kuhusu mifumo tofauti ya ulinzi na usalama iliyotumiwa na jamii za Kitanzania kabla ya ukoloni. Kisha, eleza namna mifumo hiyo inaweza kutumika au kuboreshwa ili kuendana na mazingira ya sasa.

Ulinzi na usalama wakati wa ukoloni

Ujio wa utawala wa Kijerumani uliambatana na kuanzishwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya kikoloni. *Schutztruppe* lilikuwa jina rasmi la jeshi la kikoloni la Ujerumani katika eneo la Afrika ya Mashariki ya Wajerumani (*German East Africa*). Utawala huo ulianza rasmi mwaka 1885 baada ya Mkutano wa Berlin kuidhinisha madai ya Carl Peters kwa niaba ya Kampuni ya Kijerumani ya Afrika ya Mashariki. Awali, Kansela Otto von Bismarck hakuwa na mpango wa kuunda jeshi la serikali, bali alitegemea makampuni ya biashara yaliyopewa hati ya kikoloni kugharamia na kuendesha shughuli za ulinzi na usalama. Hata hivyo, kuongezeka kwa upinzani kutoka kwa jamii za Kitanzania katika miaka ya 1888–1889 kulimlazimisha Bismarck kuidhinisha uundwaji wa kikosi cha kijeshi cha kudumu cha kikoloni.

Vilevile, Wajerumani waliunda *Polizeitruppe* (polisi wa kikoloni) katika Afrika ya Mashariki ya Wajerumani. Askari wengi katika vyombo hivi walikuwa Waafrika waliotumika kufanya doria na kukandamiza upinzani wa jamii za Kiafrika. Jamii zilizotoa idadi kubwa ya askari ni pamoja na Wanyamwezi, Waswahili na Wamanyaema. Aidha, Wanubi kutoka Sudani na Washangaan kutoka Inhambane (Msumbiji) walijumuishwa katika vikosi vya mwanzo vilivyoanzishwa na serikali ya Kijerumani. Katika kipindi cha utawala wa Waingereza (1919–1961), Tanganyika ilikuwa makao ya vikosi vya *King's African Rifles* (KAR), ambavyo vilikuwa mhimili mkuu wa ulinzi hadi wakati wa uhuru. Baada ya ushindi wa Waingereza katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1916 na kupokea hati ya udhamini (*mandate*) mwaka 1919, Waingereza walianza kuajiri na kuunda vikosi vya KAR ndani ya Tanganyika. Wakati wa upanuzi wa KAR mwaka 1917, baadhi ya askari wa zamani wa Kijerumani (*Schutztruppe*) walijiunga na jeshi hilo.

Kupitia Tangazo la Mei 1919 la kuanzishwa kwa Idara ya Polisi na Magereza (*Police and Prisons Proclamation of May 1919*), Jeshi la Polisi na Huduma ya Magereza ya Tanganyika zilianzishwa rasmi mwezi Agosti 1919 (*Tanganyika Police Force and Prisons Service*). Hatua hii iliweka misingi wa kuwapo kwa polisi wa kiraia, tofauti na jeshi, pamoja na huduma ya magereza kama taasisi za udhibiti wa sheria. Aidha, utawala wa kikoloni ulianzisha mfumo wa sheria kupitia *Tanganyika Order in Council* ya mwaka 1920, uliyoingiza Sheria ya Kiingereza (*Common Law*) kama msingi wa mfumo wa sheria wa Tanganyika. Mwaka 1930, ilitungwa Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Tanganyika (*Tanganyika Penal Code*) kama msimbo mkuu wa makosa ya jinai na adhabu zake. Tarehe 25 Agosti 1931, Huduma ya Magereza ilitenganishwa na Jeshi la Polisi na kufanywa idara kamili ya serikali. Hatimaye, mwaka 1933, kulifanyika marekebisho ya Sheria ya Magereza (*Prisons Ordinance*) yaliyodumisha muundo huo na kuimarisha misingi ya kisheria na kiutawala.

Uundwaji wa mifumo ya ulinzi na usalama wakati wa ukoloni ulitokana na sababu mbalimbali. Kwanza, serikali za kikoloni ziliunda vyombo hivyo ili kukandamiza upinzani wa wenyeji, kama ilivyodhihirika katika Vita vya Majimaji vya mwaka 1905–1907. Pili, vyombo hivyo vililenga kulinda maslahi ya kiuchumi ya wakoloni, yakiwamo mashamba makubwa, reli na makazi ya walowezi. Tatu, vilitumika kuhakikisha upatikanaji wa askari wa kushiriki katika Vita vya Dunia, hususan kupitia askari wa Kiafrika wa KAR. Nne, mifumo hiyo ilitumika kudhibiti jamii na kuhakikisha utekelezaji wa sheria na maagizo ya kikoloni, hasa kupitia polisi na magereza kama vyombo vya nidhamu na udhibiti wa kijamii.

Mfumo wa ulinzi na usalama baada ya uhuru

Baada ya Tanganyika kupata uhuru tarehe 9 Desemba 1961, ilirithi Jeshi la Tanganyika Rifles (TR) kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza. Jeshi hili lilikuwa muendelezo wa Jeshi la King's African Rifles (KAR), na licha ya kubadilishwa jina mwaka 1962, falsafa, muundo na uongozi wake uliendelea kubeba sura ya kikoloni. *Tanganyika Rifles* ilikuwa na rejimenti moja yenye vikosi viwili: Kikosi cha Kwanza kilichokuwa Dar es Salaam (Lugalo) na Kikosi cha Pili kilichokuwa Tabora. Vikosi vyote viwili viliongozwa na makamanda Wazungu, isipokuwa kombania moja tu iliyokuwa chini ya uongozi wa Mwafrika.

Mwaka 1963, sehemu ya Kikosi cha Tabora ilitumwa kuanzisha kambi ya jeshi Nachingwea. Hatua hii ilifanyika katika kipindi ambacho pia kulishuhudiwa kuanzishwa kwa Jeshi la Ukombozi la Zanzibar tarehe 12 Januari 1964, mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar. Uasi wa Tanganyika Rifles ulizuka tarehe 20 Januari 1964, ukianzia Dar es Salaam kabla ya kusambaa hadi Tabora na Nachingwea. Sababu kuu za uasi huo zilihusisha malalamiko ya wanajeshi Waafrika kuhusu kuendelea kuwapo kwa uongozi wa Wazungu, tofauti kubwa za mishahara kati ya askari Waafrika na Wazungu, pamoja na madai kwamba jeshi lilipaswa kuongozwa na wazalendo baada ya uhuru. Uasi huo uliakisi athari za mifumo ya kikoloni iliyorithiwa na upendeleo uliowagawa Waafrika na Wazungu. Hali ilizidi kuwa tete wakati Tanganyika na Zanzibar zilipokuwa katika mchakato wa kuunganisha majeshi yao kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama, Serikali ya Tanganyika iliomba msaada wa Uingereza. Jeshi la Wanamaji la Uingereza lilitumwa nchini na kufanikiwa kuzima uasi kwa kuwanyang'anya silaha wanajeshi walioasi. Baada ya kurejesha utulivu, wanajeshi wa Uingereza waliendelea kulinda usalama nchini hadi Mei 1964. Baadaye, serikali ilialika Jeshi la Nigeria kutoa mafunzo na kusaidia katika uundaji wa jeshi jipya. Mara baada ya wanajeshi wa Nigeria kuwasili, vikosi vya Uingereza viliondoka, na hatua hiyo ikawa mwanzo wa kurejesha udhibiti wa ndani katika masuala ya ulinzi wa taifa. Katika mazingira haya ya mpito, Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964, Tarehe 1 Septemba 1964, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianzishwa kama muungano wa Tanganyika Military Force na Jeshi la Ukombozi la Zanzibar. Jeshi la Ukombozi la Zanzibar lilikuwa limeanzishwa mara baada ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964, wakati Waafrika walio wengi, kupitia Chama cha Afro-Shirazi (ASP), walipovunja utawala wa Sultani na kuchukua madaraka.

Baada ya mapinduzi kukamilika, Jeshi la Ukombozi la Zanzibar liliundwa kwa lengo la kulinda mafanikio ya mapinduzi na kuwezesha serikali mpya kudhibiti usalama wa visiwa hivyo. Kwa ujumla, jeshi jipya la Muungano liliundwa kwa misingi ya uzalendo, uadilifu na nidhamu, likiwa na lengo la kuondoa athari za mifumo ya kikoloni iliyokuwa imedhoofisha usawa, uwajibikaji na uaminifu katika taasisi za ulinzi na usalama.

Kazi ya kufanya 2.3

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, ikiwemo mitandao, soma matini kuhusu mifumo ya ulinzi na usalama wakati wa ukoloni, kisha ufanye tathmini ya mifumo hiyo.

Mabadiliko ya mifumo ya ulinzi na usalama baada ya uhuru

Wakati Tanganyika ilipopata uhuru tarehe 9 Desemba 1961, mifumo ya ulinzi na usalama ilikuwa bado imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na urithi wa kikoloni, ambapo vyombo kama Polisi na Magereza vilikuwa vimeundwa zaidi kulinda maslahi ya wakoloni. Baada ya uhuru, serikali iliona umuhimu wa kufanya mageuzi katika mifumo hiyo ili iendane na mahitaji ya taifa huru. Hivyo, ilianzisha na kuimarisha vyombo vipya vya ulinzi na usalama, kama vile Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Jeshi la Mgambo, Magereza na Idara ya Usalama wa Taifa, kwa lengo la kulinda mipaka ya nchi, kudumisha amani, na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Mabadiliko ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)

Jeshi hili lilianzishwa rasmi tarehe 1 Septemba 1964 kwa kuunganisha Jeshi la Ukombozi la Zanzibar na Tanganyika Military Forces. Aidha, vijana kutoka Umoja wa Vijana wa vyama vya TANU na ASP, pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), waliandikishwa na kuunganishwa katika jeshi hilo. Mkuu wa kwanza wa Majeshi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alikuwa Jenerali Mirisho Hagai Sarakikya, aliyepandishwa cheo kutoka Kapteni hadi kuwa Mkuu wa Majeshi. Kielelezo 2.3 kinamwonesha Mkuu wa kwanza wa JWTZ, Jenerali Mirisho Hagai Sarakikya.

Kielelezo 2.3: Mkuu wa kwanza wa majeshi Jenerali Mirisho Hagai Sarakikya

Mabadiliko mbalimbali ya kimfumo na kimuundo yalifanyika ili kulifanya jeshi liendane na mahitaji na malengo ya Watanzania baada ya uhuru. Hatua hizo zililenga kuondoa athari za mfumo wa kikoloni uliokuwa umetawala katika muundo wa Jeshi la Tanganyika Rifles. Baada ya uasi wa mwaka 1964, jeshi lilisitishwa mara moja. Viongozi wote waliohusika katika uasi huo walifukuzwa kazi, huku baadhi yao wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini. Maafisa na askari ambao hawakuhusika na uasi waliendelea kubaki jeshini, na jina la jeshi likabadilishwa kutoka Tanganyika Rifles kuwa Tanganyika Military Force. Hata hivyo, jina hilo lilitumika kwa muda mfupi kabla ya kuundwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Uundwaji wa JWTZ uliambatana na mabadiliko mbalimbali, yakiwamo yafuatayo:

Uandikishaji wa askari wazalendo: Tofauti na mfumo wa kikoloni uliotumia vigezo vya urefu na afya pekee katika kuandikisha askari, JWTZ lilizingatia zaidi uzalendo na uaminifu kwa taifa kama vigezo vikuu. Vijana waliokuwa wanachama wa TANU walipewa kipaumbele katika uandikishaji kwa kuwa chama hicho kilikuwa na mtandao mpana nchini na kilitambulika kwa misingi yake ya kizalendo. Baada ya kuanzishwa, JWTZ lilikuwa kwa kasi kutoka kuwa na vikosi vitatu vya jeshi la ardhini hadi kuwa jeshi kamili lenye brigedi na divisheni zilizosambaa nchi nzima. Mwaka 1966, JWTZ lilianzisha vikosi vya mizinga.

Aidha, shule na vyuo mbalimbali vya kijeshi vilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo na kuendeleza utaalamu wa kijeshi, sambamba na kujenga moyo wa uzalendo kwa wanajeshi. Mafunzo ya awali yaliweka mkazo mkubwa katika siasa na itikadi ya taifa, ambapo muda maalumu ulitengwa kwa ajili ya kujifunza sera za chama, nafasi ya JWTZ katika serikali, na wajibu wake katika jamii.

Mafunzo na uandikishaji wa askari: Ili kuandaa askari shupavu na wazalendo, mafunzo ya awali yalifanyika katika kambi mbalimbali nchini. Mafunzo ya kwanza ya askari wa jeshi jipya yalianza rasmi katika Kambi ya Mgulani tarehe 3 Machi 1964 na kukamilika tarehe 1 Septemba mwaka huo huo. Askari wapatao 1,000 waliapishwa mbele ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Katika sherehe hizo, Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naye alihudhuria. Askari hao walihitimisha mafunzo yao ya awali na kuingizwa rasmi katika JWTZ.

Uimarishaji wa jeshi na mafunzo nje ya nchi: Juhudi za kuliimarisha jeshi jipya zilianza mara moja ili kulijengea taifa jeshi imara na la kitaifa. Maafisa wa jeshi walitumwa kupata mafunzo katika nchi rafiki, zikiwamo Canada, Uingereza, Israeli, India, China na Pakistani. Kutokana na hitaji kubwa la kuwa na maafisa na askari wenye ujuzi wa juu, serikali ililazimika kupeleka askari wengi nje ya nchi kwa mafunzo ya uafisa, licha ya gharama kubwa zilizohusika. Ikumbukwe kuwa kabla na hata baada ya uhuru, Tanganyika ilikuwa na fursa ya kupeleka afisa mmoja tu kwa mwaka kwenda Uingereza kwa mafunzo, jambo ambalo lingechukua takribani miaka hamsini kupata maafisa hamsini. Ili kuharakisha mchakato huo, TANU ilitumia mbinu mbadala kwa kupeleka vijana 15 wa chama hicho kupata mafunzo ya uafisa nchini Israeli mwaka 1963.

Mabadiliko ya majina ya kambi za jeshi: Baada ya kuanzishwa kwa JWTZ, jeshi liliendelea kutumia vikosi vitatu vya askari wa miguu, lakini majina ya kambi yalibadilishwa ili kuipa taswira ya taifa huru. Kambi zilizokuwa na majina ya kigeni zilipewa majina ya kizalendo. Kwa mfano, Kambi ya Lugalo ilibadilishwa kutoka *Colito Barracks* kwa heshima ya Mtwa Mkwawa wa Wahehe (Iringa), aliyepambana vikali dhidi ya Wajerumani katika eneo la Lugalo. Aidha, Kambi ya Kalewa iliyopo Tabora ilipewa jina la Mtemi Mirambo, ili kumuenzi kwa ujasiri wake katika kupinga uvamizi wa wafanyabiashara wa Kiarabu katika maeneo yake.

Kazi ya kufanya 2.4

Soma matini mbalimbali kuhusu historia ya JWTZ, kisha tathmini namna mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji yaliyokidhi ulinzi na usalama wa Taifa kati ya 1961 na 1966.

Kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)

Kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kulitokana na mawazo ya Umoja wa Vijana wa Chama cha TANU (*TANU Youth League*), yaliyowasilishwa wakati wa Mkutano Mkuu wa chama uliofanyika Tabora tarehe 25 Agosti 1962. Baadaye, tarehe 19 Aprili 1963, Baraza la Mawaziri la Tanganyika, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lilipitisha azimio la Umoja wa Vijana wa TANU na kuamua kwa kauli moja kuanzishwa kwa JKT. Hatimaye, tarehe 10 Julai 1963, JKT lilianza rasmi, na hivyo kutangazwa kuwa ndilo tarehe rasmi ya kuasisiwa kwake. Kisheria, JKT lilianzishwa kupitia Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (*National Service Act*), Namba 16 ya mwaka 1964.

Katika uzinduzi wa JKT, Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa umuhimu wa jeshi hilo unatokana na haja ya taifa kuwa na vijana walioko tayari kuitikia wito wa kulitumikia taifa lao kwa jukumu lolote watakalohitajika. Tangu kuanzishwa kwake, JKT lilianza kuandikisha vijana wa kujitolea waliokuwa na elimu ya darasa la saba. Hata hivyo, kufikia mwaka 1966, sheria ilirekebishwa ili kuruhusu uandikishaji wa vijana wenye elimu ya juu zaidi, kuanzia kidato cha nne na kuendelea, kwa mujibu wa mahitaji ya taifa. Moja ya malengo muhimu ya kuanzishwa kwa JKT ilikuwa ni kuondoa aina zote za ubaguzi katika jamii ya Watanzania, hali iliyokuwa imesababishwa na sera ya kikoloni ya "Gawa Uwatawale" (*Divide and Rule*). Sera hiyo ilichochea migawanyiko ya kikabila, kidini, kirangi na kitabaka kwa misingi ya kipato. Ili taifa huru la Tanganyika liweze kufikia maendeleo ya kweli, lilihitaji wananchi wake kushirikiana, kupendana, kuheshimiana, kusaidiana na kudumisha umoja wa kitaifa. Jukumu kuu la JKT lilikuwa ni kuwaelimisha na kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuwa wazalendo, waadilifu, wenye nidhamu na raia wema wanaopenda kulitumikia na kulinda taifa lao. JKT lilitoa fursa kwa vijana kujifunza kwa vitendo umuhimu wa kazi na kujitolea kwa taifa bila kutegemea ujira. Kupitia mafunzo na malezi hayo, vijana walijengewa misingi ya kujitegemea, uwajibikaji na uzalendo.

Mnamo mwaka 1966, JKT lilipewa jukumu la kutoa mafunzo ya lazima ya kijeshi kwa vijana wote wa Kitanzania, hususan wale waliokuwa wakihitimu masomo ya kidato cha sita, vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu. Ili kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, JKT lilifungua kambi tatu za awali ambazo ni Mgulani (Dar es Salaam), Ruvu (Pwani) na Mafinga (Iringa). Aidha, JKT liliendelea kuwa na lengo la kukuza malezi yenye tija, kujenga moyo wa uzalendo na kuimarisha uwezo wa vijana kujitegemea. JKT limekuwa na nafasi muhimu katika malezi ya vijana kama taasisi ya kitaifa inayofanya kazi kama "familia ya pili," ambapo vijana huunganishwa bila kujali kabila, rangi, dini, kiwango cha elimu, jinsia au ulemavu, kwa lengo la kujenga udugu, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Kuanzishwa kwa Jeshi la Mgambo

Jeshi la Mgambo liliundwa baada ya uasi wa Tanganyika Rifles wa mwaka 1964 na kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kama sehemu ya mkakati wa ulinzi shirikishi unaowahusisha wananchi. Serikali iliona umuhimu wa kuwashirikisha raia katika ulinzi wa taifa changa, ambalo wakati huo lilikuwa na jeshi dogo. Kwa muktadha huo, Jeshi la Mgambo lilipewa jukumu la kuwa nguvu ya akiba ya JWTZ na kuwa kiungo kati ya jeshi la kitaifa na wananchi. Kuanzishwa kwa Jeshi la Mgambo kulichochewa na changamoto kadhaa. Kwanza, uasi wa jeshi wa mwaka 1964 ulidhihirisha udhaifu wa jeshi dogo lililorithiwa kutoka kwa wakoloni. Pili, kulikuwapo uhitaji mkubwa wa kulinda mipaka mirefu ya taifa, hali iliyokuwa vigumu kutekelezwa na JWTZ pekee. Tatu, sera za uzalendo za chama cha TANU zilihamasisha wananchi, hususan vijana, kushiriki moja kwa moja katika shughuli za ulinzi kupitia Jeshi la Mgambo na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Aidha, mazingira ya kimataifa ya wakati huo yalikuwa na vitisho vikubwa vya kiusalama. Uwepo wa utawala wa kikoloni na ubaguzi wa rangi katika nchi jirani, pamoja na uvamizi wa majeshi ya Wareno na makaburu, ulihatarisha usalama wa Tanzania. Hali hii ilikuwa nyeti zaidi kutokana na uwepo wa wapigania uhuru wa Msumbiji na Afrika Kusini waliokuwa wameweka kambi zao nchini Tanzania. Mara kadhaa, majeshi ya Wareno yaliwafuatilia wapigania uhuru hao hadi ndani ya mipaka ya Tanzania walipokuwa wakikimbia mashambulizi nchini Msumbiji. Kutokana na matukio hayo ya mara kwa mara, ilionekana kuwa vigumu kuitegemea JWTZ pekee katika kulinda mipaka ya nchi nzima, hivyo serikali ikaamua kuwashirikisha wananchi katika kulinda maeneo na vijiji vyao.

Kuanzishwa kwa Jeshi la Mgambo pia kulitokana na falsafa ya Rais Mwalimu Julius K. Nyerere ya kuwa na jeshi dogo la kitaalamu linaloungwa mkono na wananchi wengi kupitia Jeshi la Mgambo. Kifungu cha 21 cha Mwongozo ya Chama cha TANU kilisisitiza kuwa msingi wa ulinzi na usalama wa Tanzania ni wananchi wenyewe. Dhana hii ilieleweka kwa urahisi na Watanzania kwa kuwa haikuwa ngeni katika jamii zao. Katika jamii za jadi, kila mwanaume mwenye uwezo alitarajiwa pia kuwa mpiganaji wakati wa mahitaji ya ulinzi. Kisheria, Jeshi la Mgambo liliwekwa chini ya Wizara ya Ulinzi na JWTZ, huku uandikishaji wake ukifanyika kupitia ofisi za chama na serikali za mitaa. Wananchi waliandikishwa walipatiwa mafunzo ya muda mfupi kuhusu matumizi ya silaha ndogo, mbinu za ulinzi wa maeneo, nidhamu na uzalendo, ili kuwaandaa kushiriki katika kulinda taifa dhidi ya vitisho vya ndani na nje.

Jeshi la Mgambo liliundwa kama nguvu ya akiba ya JWTZ. Lilikusudiwa kusaidia katika nyakati za dharura, kushiriki katika ulinzi wa ndani, na kulinda mipaka ya taifa, sambamba na kuimarisha malezi ya kizalendo miongoni mwa wananchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Kitaifa ya Ulinzi ya mwaka 1966, majukumu ya Jeshi la Mgambo ni pamoja na yafuatayo:

  1. Kupata mafunzo na kushirikiana na viongozi wa umma katika kudumisha usalama, sheria na utulivu katika maeneo yao;
  2. Kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia wakati wa dharura za kitaifa;
  3. Kufanya kazi kama akiba ya kujitolea ya vikosi rasmi vya ulinzi; na
  4. Kulinda miundombinu na mitambo muhimu katika maeneo yao.

Malengo mengine ya kuanzishwa kwa Jeshi la Mgambo yalikuwa ni kujenga hali ya uwajibikaji wa pamoja katika jamii na kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa taifa. Kwa ujumla, uanzishaji wa Jeshi la Mgambo uliimarisha mkakati wa kuwa na jeshi dogo la kitaalamu la JWTZ linaloungwa mkono na wanamgambo wengi, na hivyo kuiwezesha jamii ya Kitanzania kujilinda kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.

Kazi ya kufanya 2.5

Soma matini kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika kuhusu historia ya majeshi nchini Tanzania, kisha eleza changamoto zilizojitokeza katika kuanzisha JWTZ, JKT na Jeshi la Mgamb Mabadiliko katika Jeshi la Magereza.

Jeshi la Magereza lilianzishwa wakati wa utawala wa kikoloni wa Waingereza mwaka 1931. Kabla ya hapo, Jeshi la Polisi lilikuwa likitekeleza pia majukumu ya magereza. Awali, Jeshi la Magereza lilijulikana kama Idara ya Jela na jukumu lake kuu lilikuwa ni kusimamia wafungwa na kuwalazimisha kufanya kazi ngumu bila kuzingatia maslahi yao au manufaa kwa taifa. Katika kipindi hicho, taasisi za magereza zilijengwa zaidi katika miji na wilaya kwa madhumuni ya kudhibiti upinzani dhidi ya ukoloni.

Baada ya kupata uhuru, kulifanyika mageuzi ya kisheria na kiutendaji yaliyolenga kubadilisha dhana na mtazamo wa magereza. Jeshi la Magereza lilianza kuendeshwa kwa kuzingatia haki za binadamu katika kuwahudumia wafungwa na watuhumiwa. Mageuzi hayo yaliendana na mahitaji ya taifa jipya, ambapo Jeshi la Magereza lilibadilishwa kuwa chombo muhimu cha ulinzi, usalama na maendeleo ya kijamii.

Kwanza, Jeshi la Magereza liliimarishwa ili kudumisha ulinzi na usalama wa taifa kwa kudhibiti wafungwa kwa nidhamu na utaratibu wa kijeshi, hivyo kulinda amani ndani ya magereza na kuzuia kuendelea kwa vitendo vya uhalifu katika jamii. Pili, lililenga kuimarisha nidhamu, uzalendo na uwajibikaji miongoni mwa wafungwa na askari, kwa kuunganisha mfumo wa magereza na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wa taifa. Tatu, Jeshi la Magereza lilibadilishwa kuwa sehemu ya nguvu kazi ya taifa, kwa kushirikishwa katika shughuli za uzalishaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, sambamba na vyombo vingine kama Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Mgambo. Sheria ya Magereza ilitilia mkazo haki za msingi za binadamu, hali iliyowezesha kuanzishwa kwa shughuli za uzalishaji mali na mafunzo ya ufundi kwa wafungwa. Kupitia mpango huo, wafungwa waliwezeshwa kupata ujuzi na stadi zitakazowasaidia kujitegemea baada ya kumaliza vifungo vyao. Hivyo, Jeshi la Magereza lilianzisha vyuo vya ufundi katika mikoa ya Mbeya na Morogoro, ambavyo vilitoa mafunzo na vyeti vya ujuzi kwa wafungwa wenye vifungo vya muda mrefu.

Aidha, mfumo wa utoaji elimu kwa wafungwa uliimarishwa kwa kuanzisha elimu ya msingi kwa watu wazima, masomo ya jumla ya kitaaluma, pamoja na elimu ya shule za msingi kwa wafungwa waliokuwa wameacha shule wakiwa na umri mdogo. Sambamba na hayo, askari wa magereza walipewa mafunzo maalumu ili kuwajengea uwezo wa kufundisha wafungwa na kubadilisha mtazamo wa utoaji huduma kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu, marekebisho ya tabia na urekebishaji wa wahalifu.

Mabadiliko katika Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi nchini Tanganyika lilianza wakati wa utawala wa kikoloni wa Wajerumani, ambapo lilijulikana kama *Polizeitruppe*. Mwaka 1892, Wajerumani waliunda kikundi maalumu cha watu kilichotekeleza kazi za polisi kwa lengo la kurahisisha na kuimarisha shughuli za utawala wa kikoloni. Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Tanganyika iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza. Tarehe 25 Agosti 1919, utawala wa Waingereza ulitangaza rasmi kuanzishwa kwa Jeshi la Polisi la Tanganyika kupitia Gazeti la Serikali namba 21-2583. Makao makuu ya jeshi hilo yaliwekwa Lushoto chini ya uongozi wa Meja S. T. Davis. Mwaka 1921, shule ya mafunzo ya polisi ilianzishwa mjini Morogoro, na mwaka 1925 kituo cha kwanza rasmi cha polisi kilifunguliwa Lupa Tingatinga katika eneo la machimbo ya dhahabu ya Chunya. Mwaka 1930, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi yalihamishwa kutoka Lushoto kwenda Dar es Salaam.

Aidha, mwaka 1949 kikosi maalumu cha kutuliza ghasia kilianzishwa, ambacho kwa sasa kinajulikana kama *Field Force Unit* (FFU). Katika kipindi hicho, kulikuwapo hamasa kubwa ya kuajiri vijana wa Kiafrika, ambapo wahitimu wa shule za sekondari walichaguliwa kujiunga na Jeshi la Polisi na kupewa nafasi za ukaguzi chini ya uangalizi (*probation inspectors*). Mwaka 1952, kikosi cha mawasiliano ya simu bila waya (*Signal Branch*) kilianzishwa, na mwaka 1958 askari polisi wanawake walianza kujiunga na Jeshi la Polisi kwa idadi kubwa. Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, Jeshi la Polisi lililoachwa na Waingereza lilibaki na muundo wa kikoloni na liliendelea kuongozwa na makamanda wa kigeni. Hatua ya kwanza ya mageuzi ilikuwa ni uafrikishaji wa uongozi, ambapo askari wazawa walianza kupandishwa vyeo na kushika nafasi za juu zilizokuwa zikishikiliwa na Wazungu. Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi lilianza kubadilika kutoka kuwa chombo cha kulinda maslahi ya wakoloni na kudhibiti raia, na kuwa chombo cha kulinda amani, kusimamia sheria na kuhakikisha haki kwa wananchi wa taifa huru.

Serikali ya Mwalimu Julius K. Nyerere ilipanga majukumu ya Jeshi la Polisi ili yaendane na mwelekeo wa taifa jipya. Majukumu hayo yalijumuisha kudhibiti uhalifu wa ndani na kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kulinda usalama wa taifa. Mwaka 1962, nafasi ya Kamishna Mzungu ilichukuliwa na Mwafrika, Elangwa Shaidi. Pamoja na uteuzi wake, maafisa kumi Waafrika waliteuliwa kushika nafasi za Wakuu wa Polisi wa Mikoa (*Regional Police Commanders* – RPC). Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, Jeshi la Polisi lilifanywa kuwa la Muungano. Kutokana na hatua hiyo, Kamishna Elangwa Shaidi alipandishwa cheo na kuteuliwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), na hivyo kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama inavyoonesha katika kielelezo 2.3.

Kielelezo 2.4: *Inspekta Jenerali wa kwanza wa Polisi Elangwa Shaidi 1962-1972

Aidha, Jeshi la Polisi liliendelea kukua na kuboreshwa zaidi kila wakati kulingana na mahitaji ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Maboresho yaliyofanyika ni pamoja na kuwa na vyuo vya mafunzo ya upolisi Moshi, chuo cha Maafisa wa Polisi Kurasini, Dar es Salaam na kuongezeka kwa idara za polisi na vitengo.

Mabadiliko katika Idara ya Usalama wa Taifa

Usalama wa taifa ni mkusanyiko wa hatua na mikakati inayochukuliwa na serikali ili kujilinda dhidi ya vitisho vinavyoweza kuhatarisha utulivu, uhuru na maslahi ya taifa. Nchini Tanzania, jukumu hili hutekelezwa kwa kiasi kikubwa na Idara ya Usalama wa Taifa (Tanzania Intelligence and Security Service – TISS), ambayo ni chombo cha kijasusi na kimkakati chenye lengo la kulinda usalama wa taifa kupitia ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa taarifa muhimu za kiusalama. Idara ya Usalama wa Taifa hufanya kazi kwa siri na kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa taarifa nyeti kuhusu vitisho vinavyoweza kujitokeza ndani na nje ya nchi zinapatikana kwa wakati, zinachambuliwa kwa ufanisi, na kufikishwa kwa mamlaka husika. Kikatiba, idara hii inawajibika moja kwa moja kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu na kiongozi mkuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Kabla ya Tanzania kupata uhuru, shughuli za kijasusi zilikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza na ziliendeshwa na kitengo maalumu kilichojulikana kama *Special Branch*. Kitengo hiki kililenga kulinda maslahi ya wakoloni kwa kudhibiti harakati za kisiasa na vitendo vyote vilivyoonekana kuwa tishio kwa utawala wa kikoloni. Hivyo, mfumo wa kijasusi wa kipindi hicho haukulenga usalama wa raia, bali ulihudumia maslahi ya ukoloni na udhibiti wa jamii. Baada ya Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961, serikali ilirithi mfumo huo wa kijasusi lakini ilifanya maboresho ya kimuundo na kiutendaji ili kuubadilisha na kuufanya kuwa taasisi ya kitaifa inayolenga kulinda usalama wa wananchi na taifa kwa ujumla. Aidha, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 ulihitaji mfumo jumuishi wa ulinzi na usalama, hivyo shughuli za kijasusi ziliimarishwa zaidi ili kulinda Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhakikisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.

Majukumu makuu ya Idara ya Usalama wa Taifa

Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania, ina majukumu yafuatayo:

Ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za kiusalama: Mojawapo ya majukumu ya msingi ya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ni kukusanya na kuchambua taarifa za kijasusi zenye maslahi kwa taifa kutoka vyanzo mbalimbali. Taarifa hizo hutumika kumshauri Rais na Serikali kuhusu hali ya usalama wa nchi na hatua stahiki za kuchukua.

Kulinda usalama wa taifa: Usalama wa taifa ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa msingi huo, Idara ya Usalama wa Taifa ina jukumu la kufuatilia, kutambua na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali kuhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi. Vitendo hivyo ni pamoja na ugaidi, uchochezi, hujuma, uhalifu wa kupangwa na upotoshaji wa taarifa wenye madhara kwa taifa. Aidha, idara hii huchangia kuimarisha ulinzi wa miundombinu muhimu ya kitaifa, ikiwemo bandari, viwanja vya ndege, mitambo na mabwawa ya kuzalisha umeme, maji, pamoja na mifumo ya mawasiliano.

Kulinda usalama wa nje ya nchi: Kwa kushirikiana na vyombo vya kimataifa na taasisi rafiki za kijasusi, TISS hufanya uchunguzi na uchambuzi wa vitisho vinavyotoka nje ya nchi. Vitisho hivyo ni pamoja na ujasusi wa mataifa mengine na shughuli za mitandao ya uhalifu wa kimataifa ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa Tanzania.

Kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama: Idara ya Usalama wa Taifa hufanya kazi kwa karibu na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kama vile Jeshi la Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na vikosi vingine vya usalama. Ushirikiano huo huongeza uwezo wa taifa kukabiliana na mabadiliko ya vitisho vya kiusalama na kujenga mfumo imara na endelevu wa ulinzi na usalama wa taifa.

Kufanya upekuzi wa kiusalama (security vetting): TISS ina jukumu la kufanya upekuzi na uchunguzi wa kiusalama kwa watu mbalimbali, wakiwamo wale wanaoteuliwa au kupendekezwa kushika nyadhifa za umma, watu wanaohusika na taarifa nyeti au zilizoruhusiwa, pamoja na waombaji wa uraia wa Tanzania. Hatua hii husaidia kulinda maslahi ya taifa na kuzuia hatari zinazoweza kujitokeza.

Kutoa ulinzi binafsi: Idara ya Usalama wa Taifa pia ina jukumu la kutoa ulinzi binafsi kwa viongozi wakuu wa serikali kama ilivyobainishwa katika Sheria ya Usalama wa Taifa. Viongozi hao ni pamoja na wagombea wa urais wakati wa uchaguzi mkuu, pamoja na mtu mwingine yeyote atakayeteuliwa na Rais kwa kuzingatia ushauri wa Mkurugenzi Mkuu wa TISS.

Kazi ya kufanya 2.6

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa za kuaminika ikiwamo mtandao, soma matini kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa kisha, tathmini mchango wa mabadiliko Idara ya Usalama wa Taifa katika kuimarisha usalama nchini tangu uhuru.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

1. Kwa kutumia mifano eleza jinsi jamii za Kitanzania zilivyojilinda dhidi ya uvamizi kutoka kwa jamii nyingine.

2. Chambua mikakati iliyotumiwa na wakoloni wa Kijerumani na Kingereza kuimarisha ulinzi na usalama katika Tanganyika.

3. Chambua namna ambavyo mfumo wa kijasusi wa kikoloni (Special Branch) ulivyoathiri maendeleo ya Idara ya Usalama wa Taifa baada ya Tanzania kupata uhuru.

4. Fafanua jinsi ambavyo Idara ya Usalama wa Taifa inachangia katika kusimamia na kuimarisha maadili ya taifa.

Sababu za mabadiliko katika mifumo ya ulinzi na usalama baada ya uhuru

Baada ya kupata uhuru, kulijitokeza haja ya kufanya mageuzi katika mifumo ya ulinzi na usalama ili iendane na malengo na mahitaji ya taifa huru. Mageuzi haya yalichochewa na sababu mbalimbali za kijamii, kisiasa, kiusalama na kimataifa, kama ifuatavyo:

(a) Kutoka utawala wa kikoloni kwenda katika uhuru: Baada ya Tanganyika kupata uhuru, ilirithi jeshi la kikoloni lililoundwa kulinda maslahi ya wakoloni badala ya wananchi. Jeshi hilo halikuweza kuendana na matarajio ya taifa huru. Ingawa lilibadilishwa jina na kuitwa Tanganyika Rifles (TR), liliendelea kuwa na maafisa wengi wa kikoloni, jambo lililoibua tofauti za kimaadili na kisera, pamoja na hofu kwamba halikukidhi mahitaji ya nchi. Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Tanganyika iliamua kuanzisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kulinda mipaka ya taifa, kudumisha amani ya ndani, na kushirikiki katika shughuli za maendeleo.

(b) Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliibua haja ya kuunganisha mifumo ya ulinzi na usalama ya pande zote mbili. Hatua hii ililenga kuunda jeshi moja lenye sera, malengo na mwelekeo wa pamoja, jambo lililosaidia kuimarisha usalama wa kitaifa na kudumisha umoja wa nchi. Mabadiliko hayo yaliwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi kwa uratibu chini ya Serikali ya Muungano.

(c) Sera za ulinzi na usalama zinazoendana na mazingira ya siasa za kimataifa: Mivutano ya kisiasa kati ya mataifa makubwa duniani ilileta changamoto mpya za kiusalama, hivyo kuhitaji mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji katika vyombo vya ulinzi na usalama. Kipindi cha Vita Baridi kilisababisha dunia kugawanyika katika kambi mbili pinzani, ya Mashariki na Magharibi. Tanzania, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, ilijiunga na Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement – NAM). Uamuzi huo ulihitaji mfumo madhubuti wa ulinzi na usalama ili kukabiliana na shinikizo na ushawishi kutoka pande zote mbili, na kuhakikisha kuwa Tanzania haigeuki kuwa uwanja wa migogoro ya kisiasa au kijeshi ya mataifa makubwa.

(d) Harakati za ukombozi barani Afrika: Tanzania ilijitolea kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi za Afrika dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi. Kuanzia miaka ya 1960, nchi iliwapokea wapigania uhuru kutoka vyama vya ukombozi, kama vile African National Congress (ANC) ya Afrika Kusini na FRELIMO ya Msumbiji. Msaada huo ulihitaji kuwapo kwa mfumo thabiti wa ulinzi na usalama wenye uwezo wa kushirikiana na harakati hizo bila kuhatarisha usalama wa taifa. Hivyo, jeshi na vyombo vingine vya usalama vilibadilishwa ili kuimarisha ulinzi wa mipaka, kutoa mafunzo, na kudhibiti shughuli za vikundi vya ukombozi vilivyokuwa ndani ya nchi.

(e) Matukio ya uasi na migogoro ndani ya jeshi la zamani: Uasi wa Tanganyika Rifles uliojitokeza Januari 1964 ulionesha wazi udhaifu wa jeshi lililorithiwa kutoka kwa wakoloni. Uasi huo uliashiria ukosefu wa uaminifu, uzalendo na uungwaji mkono wa wananchi, hali iliyodhihirisha kuwa jeshi lililokuwapo halikuweza kuhakikisha usalama wa taifa ipasavyo. Tukio hilo lilikuwa kielelezo cha wazi cha kushindwa kwa mfumo wa kikoloni wa ulinzi, na hivyo kulazimisha kuundwa kwa jeshi

(f) Sera ya ulinzi inayomshirikisha mwananchi: Mfumo mpya wa ulinzi ulilenga kuanzisha jeshi la wananchi linalokuwa chini ya udhibiti wa kiraia na lisiloegemea maslahi ya kikoloni. Jeshi hili lililenga kuunganisha wananchi na vyombo vya ulinzi kwa kushirikisha vijana wengi kupitia harakati za kisiasa na kijamii. Lengo lilikuwa ni kujenga jeshi ambalo wananchi wanalitambua kama lao, si jeshi la kigeni, hivyo kuimarisha uhusiano kati ya jeshi, serikali na wananchi, na kuhakikisha kuwa ulinzi wa taifa unalenga usalama wa wote.

Mchango wa maadili katika kujenga mifumo ya ulinzi na usalama

Mifumo ya ulinzi na usalama nchini Tanzania imejengwa juu ya misingi ya kulinda amani, uhuru na mshikamano wa taifa. Hata hivyo, nguvu za kijeshi au kisheria pekee haziwezi kudumisha usalama wa kudumu bila kuwapo kwa msingi imara wa maadili. Maadili ni sehemu muhimu ya mfumo wa ulinzi na usalama kwa kuwa yanahusisha viwango vya tabia njema, uadilifu na uwajibikaji vinavyowaongoza watoa huduma za usalama pamoja na wananchi kwa ujumla.

Maadili ndiyo msingi wa nidhamu na uaminifu katika vyombo vya ulinzi na usalama, jambo linalohakikisha matumizi sahihi ya mamlaka na nguvu kwa haki na uwajibikaji. Aidha, huimarisha mshikamano, uzalendo na utiifu kwa mamlaka ya kiraia, sambamba na kulinda heshima na haki za binadamu. Jeshi lenye maadili hujenga imani ya wananchi, huepuka vitendo vya rushwa na dhuluma, na hukiacha kuwa chombo cha kulinda taifa badala ya kukandamiza raia. Kwa ujumla, maadili huongeza mshikamano wa kitaifa na kuimarisha ufanisi wa vyombo vya ulinzi na usalama ndani na nje ya mipaka ya nchi. Mchango wa maadili katika kujenga mifumo imara ya usalama ni kama ifuatavyo:

Kujenga nidhamu ya askari: Vyombo vya ulinzi na usalama hutegemea nidhamu na utiifu wa askari wao. Nidhamu hii hujengwa juu ya maadili ya uaminifu, uwajibikaji na heshima kwa sheria. Nidhamu ni nguzo kuu ya utendaji wa kijeshi kwa kuwa huwezesha askari kutii amri kwa wakati, kudumisha mshikamano wa kikosi na kuhakikisha uwajibikaji wa pamoja. Askari mwenye nidhamu hujiepusha na vitendo vya rushwa, uzembe, ulevi au ukaidi vinavyoweza kudhoofisha ulinzi wa taifa. Aidha, nidhamu huimarisha uaminifu wa wananchi kwa vyombo vya ulinzi kwa kuwa askari hutenda kwa heshima na uwajibikaji. Katika nyakati za vita au dharura, nidhamu ndiyo msingi wa mshikamano na ufanisi wa jeshi katika kulinda amani, uhuru na mshikamano wa kitaifa.

Kuunganisha vyombo vya usalama na wananchi: Mifumo ya ulinzi na usalama hufanya kazi ndani ya jamii na si katika ombwe. Maadili huimarisha imani ya wananchi kwa vyombo vya usalama kupitia uwajibikaji, heshima kwa haki za binadamu na utoaji wa huduma kwa usawa. Wananchi wanapowaona maafisa wa usalama wakiwa waadilifu, hujitokeza kushirikiana nao kwa hiari, kutoa taarifa muhimu na kushirikiki katika kulinda amani ya taifa. Vilevile, maadili huzuia matumizi mabaya ya madaraka, ukatili na rushwa, vitendo vinavyoweza kudhoofisha uhalali wa vyombo vya usalama mbele ya jamii.

Kujenga uhalali kwa umma: Maadili hutoa msingi wa uhalali wa kimaadili kwa mfumo wa ulinzi na usalama. Ingawa jeshi, polisi au chombo kingine cha usalama kinaweza kuwa na mamlaka ya kisheria ya kutumia nguvu, bila kuzingatia maadili yanayoheshimu utu wa binadamu, haki na usawa, hujikuta kinakosa uhalali mbele ya wananchi. Mfumo wa ulinzi unaongozwa na maadili hujenga imani ya raia, ambayo ni muhimu kwa ushirikiano, upatikanaji wa taarifa za kiusalama na ustahimilivu wa taifa kwa muda mrefu.

Kujenga ushirikiano wa kitaifa na kikanda: Tanzania ni mwanachama wa jumuiya mbalimbali za kikanda, zikiwemo Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Ushirikiano wa kikanda hujengwa juu ya maadili ya uaminifu, usawa, uwajibikaji na mshikamano. Maadili haya huimarisha uaminifu kati ya nchi wanachama katika masuala ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi, hivyo kupunguza hofu na mashaka. Aidha, heshima kwa haki za binadamu na matumizi ya diplomasia huchangia kudumisha amani na usalama wa kikanda. Maadili pia huimarisha uwajibikaji kupitia mifumo ya kisheria, kama vile Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, kwa ajili ya kutatua migogoro kwa haki na amani, na kuhimiza maendeleo ya pamoja kupitia miradi ya miundombinu, elimu na biashara.

Kuwezesha utekelezaji wa sheria na kuheshimu haki za binadamu: Uwepo na uendeshaji wa vyombo vya ulinzi na usalama hutegemea misingi ya kisheria ya taifa na mikataba ya kimataifa. Wanajeshi na maafisa wa usalama huapa kulinda Katiba na sheria za nchi, hivyo maadili ni nguzo muhimu katika kuhakikisha kuwa mamlaka hayo yanatumika kwa kuzingatia sheria na kuheshimu haki za binadamu. Vyombo vya usalama vinapozingatia maadili ya haki, usawa na utu wa binadamu, huhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria haukiuki haki za raia. Hali hii hujenga mfumo wa usalama unaoheshimika ndani na nje ya nchi, kwa kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu mara nyingi hudhoofisha mshikamano wa jamii na kuondoa uhalali wa taasisi za usalama.

Shughuli ya kufanya 2.7

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya taarifa vinavyoaminika, ikiwemo mtandao, soma kuhusu vigezo vya kimaadili vilivyotumika katika uandikishaji wa vyombo vya ulinzi na usalama mara baada ya uhuru. Kisha, linganisha vigezo hivyo na vinavyotumika katika mazingira ya sasa, ukionesha kufanana, tofauti na sababu zinazochangia mabadiliko hayo.

Umuhimu wa wananchi kushiriki katika shughuli za ulinzi na usalama

Ni muhimu kwa wananchi kushiriki katika shughuli za ulinzi na usalama kwa kuwa usalama wa taifa ni jukumu la kila mwananchi, na si la vyombo vya dola pekee. Ushiriki wa wananchi hujenga hali ya uwajibikaji, uzalendo na umoja katika kulinda amani na mipaka ya nchi. Aidha, ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama huwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu vitendo vya uhalifu vinavyoweza kuhatarisha usalama wa taifa. Umuhimu wa wananchi kujihusisha katika shughuli za ulinzi na usalama ni kama ifuatavyo:

Hujenga uhalali na imani kwa vyombo vya ulinzi na usalama: Ushirikishaji wa wananchi hujenga imani na uhalali wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwafanya raia wajione kuwa sehemu ya taasisi hizo na kuzitambua kama vyombo halali vya kulinda maslahi yao. Kupitia ushirikiano huu, uwazi na uwajibikaji huimarika, huku wananchi wakishiriki kutoa taarifa na kushuhudia matokeo chanya ya mchango wao. Aidha, ushirikiano unaozingatia heshima na maadili hupunguza hofu na kuondoa dhana ya ukatili. Matokeo yake ni kuimarika kwa imani ya jamii kwa vyombo vya ulinzi na usalama, hata katika nyakati ambazo inahitajika kutumia nguvu ya kisheria kwa kiwango cha wastani ili kurejesha amani na utulivu.

Huwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu: Wananchi ni "macho na masikio" ya kwanza ya vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo mchango wao ni muhimu katika upatikanaji wa taarifa za kiusalama. Wananchi wanaweza kutoa taarifa za mapema kuhusu mienendo inayotia shaka kupitia Polisi Jamii, Jeshi la Mgambo au kamati za ulinzi, pamoja na kutumia teknolojia ya mawasiliano kama simu, mitandao ya kijamii na namba za dharura kuripoti matukio kwa wakati. Vilevile, kwa kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi, wananchi huchangia kudumisha amani, kulinda rasilimali na miundombinu muhimu kama reli, barabara, viwanja vya ndege, mabwawa na mitambo ya umeme. Ushirikiano huu huwezesha vyombo vya usalama kupata taarifa sahihi na kwa wakati, hivyo kuimarisha ulinzi wa taifa kwa ujumla.

Kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa: Ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama huimarisha mshikamano wa kitaifa kwa kuwa raia hujihisi kuwa sehemu ya jukumu la kulinda taifa lao. Ushirikishaji huu huzuia migawanyiko ya kijamii, kikabila au kisiasa, na huongeza fahari na mshikamano wa jamii. Kupitia mifumo kama Polisi Jamii, Jeshi la Mgambo na vikundi vya ulinzi wa mitaa au wa jadi, wananchi hushiriki moja kwa moja katika kulinda maeneo yao, hivyo kuzuia uhalifu na migogoro kabla haijakuwa mikubwa. Aidha, ushiriki huu huimarisha uzalendo na hisia za uwajibikaji wa pamoja, na kuweka msingi imara wa amani endelevu.

Huzuia matumizi mabaya ya nguvu: Ushirikishaji wa wananchi katika shughuli za ulinzi na usalama huongeza uwajibikaji wa pande zote na kusaidia kuzuia matumizi mabaya ya nguvu na ukiukwaji wa haki za binadamu. Kwa kuwapo kwa uwazi na ushirikiano wa karibu, vyombo vya ulinzi na usalama hulazimika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, maadili na haki za raia. Ushirikiano huu huondoa hofu, hupunguza vitendo vya ukatili, rushwa au upendeleo, na hutoa ridhaa ya kijamii kwa matumizi ya nguvu kwa mujibu wa sheria pekee. Aidha, huwakumbusha askari umuhimu wa nidhamu, utu na heshima kwa haki za binadamu, jambo linaloongeza imani ya wananchi na kuimarisha uhalali wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Huchochea uzalendo na uwajibikaji: Ushirikishaji wa wananchi katika shughuli za ulinzi na usalama huamsha uzalendo na kuimarisha uwajibikaji, kwa kuwa kila raia hutambua kuwa ana jukumu la moja kwa moja la kulinda mipaka, amani na rasilimali za taifa. Jamii inaposhiriki kwa karibu katika shughuli hizi, ikiwa ni pamoja na uratibu, utoaji wa taarifa na ufuatiliaji wa wananchi hujiona kuwa wamiliki wa vyombo vya ulinzi na usalama. Hisia hii ya umiliki huimarisha uzalendo, mshikamano wa kijamii na kuongeza ufanisi wa kulinda usalama wa jamii nzima.

Kujenga mfumo endelevu wa usalama: Kwa kuwa vitisho vya kiusalama hubadilika kulingana na nyakati, ushiriki wa wananchi huongeza uwezo wa taifa kukabiliana navyo kwa pamoja na kujenga mfumo imara na endelevu wa ulinzi na usalama. Ushirikishaji wa vikundi vya kijamii, kama vile Sungusungu, katika kusimamia ulinzi katika maeneo yao husaidia kupunguza matukio ya wizi wa mifugo, uvamizi wa wanyama wakali na aina mbalimbali za uhalifu. Aidha, malezi ya jadi yanayounzia katika familia, ukoo na jamii kwa ujumla huchangia kuandaa kizazi chenye uadilifu, nidhamu na utiifu, jambo linalosaidia kupatikana kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama wenye maadili mema na uwajibikaji.

Njia zilizotumika kuwashirikisha wananchi katika ulinzi na usalama

Njia mbalimbali zilitumika kuwashirikisha wananchi katika ulinzi na usalama, zikiwemo zifuatazo:

Kuanzishwa kwa vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama: Baada ya uhuru, serikali ilianzisha vyombo mbalimbali kwa lengo la kulinda nchi na kuhusisha wananchi katika ulinzi wa taifa kwa misingi ya kisheria na kiutendaji. Kwanza, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) tangu kuanzishwa kwake limekuwa chombo muhimu cha malezi ya uzalendo, nidhamu na huduma ya vijana kwa taifa. Pili, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliweka mifumo ya akiba ya raia kupitia mfumo wa kawaida (Regular Reserve) na mfumo wa kujitolea (Volunteer Reserve) ili kupanua wigo wa ushiriki wa wananchi katika ulinzi wa taifa. Tatu, Sheria za Wanamgambo kwa Wananchi (People's Militia Acts) za mwaka 1973 na 1975 ziliwahusisha raia kama wanamgambo kwa kuweka utaratibu wa fidia iwapo watajeruhiwa au kufariki, na kuwapa mamlaka ya kukamata na kufanya upekuzi chini ya uangalizi wa kisheria, hivyo kurahisisha ulinzi shirikishi katika ngazi ya jamii.

Kuingiza vikundi vya kijamii katika ulinzi na usalama: Baada ya uhuru, serikali iliunganisha vikundi vya ulinzi wa jadi, ikiwemo Sungusungu, katika mfumo rasmi kwa kutumia hatua za kisheria na kiutawala. Sheria za Wanamgambo kwa Wananchi ziliboreshwa ili kutoa mamlaka ya kukamata na kufanya upekuzi, huku zikibainisha kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye mwenye mamlaka ya juu, kuhusu ya wanamgambo na mwenye uwezo wa kutunga kanuni za kuwaongoza. Aidha, Sheria za Serikali za Mitaa za mwaka 1982 na Sheria ya Mabaraza ya Kata ya mwaka 1985 (Ward Tribunals Act, 1985) ziliweka misingi ya kiutawala ya ushiriki wa jamii katika kudumisha amani. Kwa pamoja, sheria hizi zilifanya ulinzi shirikishi kuwa sehemu ya miundombinu ya usalama wa taifa.

Uhamasishaji wa vijana wa TANU kujiunga na shughuli za ulinzi: Umoja wa Vijana wa TANU ulitumika kama nguvu ya ulinzi wa jamii kwa kusaidia doria, ukusanyaji wa taarifa na kudumisha nidhamu ya umma kabla na baada ya uhuru. Vijana hawa pia walishiriki katika kazi za kijasusi kwa kukusanya taarifa kutoka maeneo mbalimbali na kuziwasilisha kwa vyombo vya usalama. Baadaye, shughuli hizi ziliwekwa chini ya mfumo rasmi wa dola kupitia TYL. Tarehe 5 Februari 1977, TYL iliunganishwa na ASP kufuatia muungano wa TANU na ASP, na hivyo kuzaliwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM). Hata hivyo, utaratibu wa kuhusisha vyama vya siasa na shughuli za ulinzi ulisitishwa baada ya kurejea kwa mfumo vya vyama vingi kufuatia marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992.

Kuanzishwa kwa Mabaraza ya Kata: Mabaraza ya Kata yaliundwa kwa lengo la kusuluhisha migogoro, kulinda amani na kuimarisha mfumo wa haki-jamii katika ngazi ya kata kwa kushirikisha wananchi. Kazi kuu ya mabaraza haya ni kulinda amani na maelewano kwa kutanguliza upatanishi na kutafuta suluhu za haki kati ya wahusika. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabaraza ya Kata (Ward Tribunals Act), utaratibu huu huwezesha upatikanaji wa haki kwa urahisi na kwa gharama nafuu. Aidha, kwa kuwa wajumbe wa mabaraza huchaguliwa kutoka kwa wenyeji wa kata husika, uhalali wa kijamii na utii wa maamuzi huimarika, huku migogoro midogo ikizuiwa kugeuka vitisho vikubwa vya usalama.

Mfumo wa ubalozi wa nyumba kumi: Mfumo wa ubalozi wa nyumba kumi ni nguzo ya ulinzi shirikishi katika ngazi ya jamii. Mfumo huu ulitegemea usajili wa kaya na ufuatiliaji wa wageni au mienendo isiyo ya kawaida ili kubaini viashiria vya hatari mapema na kurahisisha utambuzi wa wahusika wa matukio ya uhalifu. Kihistoria, utaratibu huu uliimarishwa tangu miaka ya 1960, ingawa una mizizi ya muda mrefu katika baadhi ya jamii hata kabla ya uhuru. Ubalozi wa nyumba kumi umekuwa kiungo muhimu kati ya wananchi, serikali za mitaa na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama wa watu na mali zao.

Kupitia mfumo huu, mabalozi hukusanya taarifa za kiusalama (intelijensia ya jamii), kuratibu doria za majirani na kufikisha mrejesho kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua stahiki zichukuliwe kwa haraka. Aidha, mfumo huu huwezesha uhamasishaji wa kazi za pamoja zinazopunguza mazingira ya uhalifu, kusaidia utatuzi wa migogoro midogo kabla haijawa tishio la amani, na kuoanisha usalama wa kijamii na miundo mingine ya ulinzi shirikishi. Kwa msingi huo, ubalozi wa nyumba kumi umeendelea kuwa "mshipa wa damu" wa uendeshaji wa ulinzi na usalama katika ngazi ya chini kabisa ya jamii.

Kazi ya kufanya 2.8

Chunguza changamoto za kiusalama katika jamii unayoishi, kisha andaa mpango kazi wa kuimarisha ulinzi na usalama katika jamii hiyo.

Zoezi

1. Eleza kwa namna gani mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanaathiri mabadiliko ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa sasa.

2. Kwa kutumia mifano, jadili hoja kwamba mabadiliko ya mifumo ya ulinzi na usalama baada ya uhuru lilikuwa jambo lisilo epukika.

3. Tathmini namna ushiriki wa wananchi katika kudumisha ulinzi na usalama unavyoweza kupunguza vitendo vya uhalifu katika jamii.

4. Jadili athari za kupungua kwa maadili miongoni mwa watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ustawi wa Taifa.

5. Pendekeza mikakati ya kukuza maadili kwa vijana katika kudumisha ulinzi na usalama wa Taifa.

MAJIBU YA ZOEZI

1. Eleza kwa namna gani mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanaathiri mabadiliko ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa sasa.

Jibu

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamebadilisha namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyofanya kazi kwa kuongeza ufanisi, kasi na usahihi katika kulinda raia na mali zao.

(a) Matumizi ya TEHAMA

Vyombo vya ulinzi hutumia kompyuta, mifumo ya kidijitali na intaneti katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa.

Mfano: Mfumo wa taarifa za uhalifu wa Jeshi la Polisi.

(b) Matumizi ya kamera za usalama (CCTV)

Kamera husaidia kufuatilia maeneo ya umma na kutambua wahalifu kwa haraka.

Mfano: Kamera zilizowekwa katika baadhi ya miji kama Dar es Salaam na Dodoma.

(c) Mawasiliano ya kisasa

Redio za kisasa, simu na satelaiti huwezesha mawasiliano ya haraka kati ya vikosi vya usalama.

(d) Uchunguzi wa kisayansi (Forensic Science)

Teknolojia ya alama za vidole, DNA na ushahidi wa kidijitali hutumika katika uchunguzi wa uhalifu.

(e) Matumizi ya ndege zisizo na rubani (Drones)

Drones hutumika kufuatilia mipaka, misitu na maeneo yenye uhalifu.

(f) Usalama wa mtandao (Cyber Security)

Vyombo vya usalama vinapambana na uhalifu wa mtandaoni kama wizi wa taarifa na utapeli wa kimtandao.

(g) Maboresho ya vifaa vya kijeshi

Teknolojia imeboresha silaha, magari ya doria na vifaa vya mawasiliano.

Hitimisho

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yameongeza uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda raia, mali na mipaka ya nchi kwa ufanisi zaidi.

2. Kwa kutumia mifano, jadili hoja kwamba mabadiliko ya mifumo ya ulinzi na usalama baada ya uhuru lilikuwa jambo lisiloepukika.

Jibu

Baada ya uhuru mwaka 1961, Tanzania ilihitaji kubadilisha mfumo wa ulinzi na usalama uliokuwa ukilinda maslahi ya wakoloni na kuujenga mfumo unaolinda maslahi ya wananchi na taifa.

Sababu za mabadiliko

(a) Kulinda uhuru wa taifa

Vyombo vya ulinzi vilipaswa kulinda mamlaka ya nchi huru.

(b) Kuanzishwa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)

Mwaka 1964, JWTZ lilianzishwa kuchukua nafasi ya King's African Rifles (KAR).

(c) Kuimarisha Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi lilibadilishwa ili kuhudumia wananchi badala ya kulinda maslahi ya kikoloni.

(d) Kuanzishwa kwa vyombo vya usalama

Vyombo kama Usalama wa Taifa vilianzishwa kulinda maslahi ya taifa.

(e) Kukabiliana na vitisho vipya

Baada ya uhuru kulijitokeza changamoto mpya kama ugaidi, uhalifu wa kimataifa na uhalifu wa mtandaoni.

(f) Kulinda mipaka ya taifa

Jeshi lilipewa jukumu la kulinda mipaka dhidi ya uvamizi wa nje.

Mifano

  • Kuanzishwa kwa JWTZ mwaka 1964.

  • Vita vya Kagera dhidi ya Uganda (1978–1979).

  • Ushiriki wa Tanzania katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Hitimisho

Mabadiliko ya mifumo ya ulinzi na usalama yalikuwa muhimu ili kukidhi mahitaji ya taifa huru na kulinda usalama wa wananchi.

3. Tathmini namna ushiriki wa wananchi katika kudumisha ulinzi na usalama unavyoweza kupunguza vitendo vya uhalifu katika jamii.

Jibu

Wananchi wana nafasi muhimu katika kudumisha amani na usalama kwa kushirikiana na vyombo vya dola.

(a) Kutoa taarifa za uhalifu

Wananchi wakitoa taarifa mapema, wahalifu wanaweza kukamatwa kwa haraka.

(b) Polisi jamii

Ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi hupunguza vitendo vya uhalifu.

(c) Kulinda mali za umma

Wananchi hulinda shule, hospitali na miundombinu dhidi ya uharibifu.

(d) Kukemea uhalifu

Jamii inaweza kukataa vitendo kama rushwa, matumizi ya dawa za kulevya na wizi.

(e) Elimu ya uraia

Wananchi wanaelimishwa kuhusu wajibu wao wa kulinda amani.

(f) Ushirikiano wa viongozi wa mitaa

Viongozi wa vijiji na mitaa husaidia kutatua migogoro kabla haijawa mikubwa.

(g) Ushiriki katika kampeni za usalama

Wananchi hushiriki katika kampeni za kuzuia ajali, moto na uhalifu.

Hitimisho

Ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama ni msingi wa kupunguza uhalifu na kudumisha amani nchini.

4. Jadili athari za kupungua kwa maadili miongoni mwa watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ustawi wa Taifa.

Jibu

(a) Kuongezeka kwa rushwa

Rushwa huathiri utekelezaji wa sheria kwa haki.

(b) Kupungua kwa imani ya wananchi

Wananchi hukosa imani kwa vyombo vya dola.

(c) Kuongezeka kwa uhalifu

Wahalifu wanaweza kukwepa sheria kutokana na vitendo vya rushwa au uzembe.

(d) Ukiukwaji wa haki za binadamu

Baadhi ya watendaji wanaweza kutumia madaraka vibaya.

(e) Kudhoofika kwa utawala wa sheria

Sheria haziwezi kutekelezwa kwa usawa.

(f) Kuharibu taswira ya taifa

Nchi inaweza kupoteza heshima mbele ya jumuiya ya kimataifa.

(g) Kupunguza uwekezaji

Wawekezaji hukwepa maeneo yenye ukosefu wa usalama na rushwa.

Hitimisho

Maadili mema katika vyombo vya ulinzi na usalama ni msingi wa amani, haki, maendeleo na ustawi wa taifa.

5. Pendekeza mikakati ya kukuza maadili kwa vijana katika kudumisha ulinzi na usalama wa Taifa.

Jibu

(a) Kutoa elimu ya uraia na maadili

Shule na vyuo viwafundishe vijana kuhusu uzalendo, uwajibikaji na kuheshimu sheria.

(b) Kuimarisha malezi ya familia

Wazazi na walezi wawajengee vijana tabia njema tangu wakiwa wadogo.

(c) Kushirikisha vijana katika shughuli za maendeleo

Vijana washiriki katika miradi ya kijamii na uzalishaji ili kupunguza ushawishi wa uhalifu.

(d) Kupambana na matumizi ya dawa za kulevya

Kuelimisha vijana kuhusu madhara ya dawa za kulevya na pombe kupita kiasi.

(e) Kuimarisha nafasi ya viongozi wa dini

Viongozi wa dini wahubiri maadili, amani na kuheshimu sheria.

(f) Matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii

Vijana waelimishwe kutumia teknolojia kwa njia chanya na kuepuka uhalifu wa mtandaoni.

(g) Kuendeleza programu za uzalendo

Shughuli kama makambi ya vijana na mafunzo ya uzalendo ziwajenge vijana moyo wa kulipenda na kulitumikia taifa.

(h) Kuimarisha ajira na ujuzi

Kupanua fursa za ajira na mafunzo ya ufundi ili kupunguza ushawishi wa kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Hitimisho

Kukuza maadili kwa vijana kunahitaji ushirikiano wa familia, shule, viongozi wa dini, jamii na serikali. Vijana wenye maadili mema, uzalendo na uwajibikaji watakuwa nguzo muhimu katika kulinda amani, usalama na maendeleo endelevu ya Tanzania.

www.learninghubtz.co.tz

Tamrini

1. Jadili mchango wa JKT katika kujenga maadili ya vijana kwa mazingira ya sasa.

2. Eleza changamoto za kutekeleza mfumo wa ubalozi wa nyumba kumi katika mazingira ya sasa.

3. Kwa kutumia mifano, eleza nafasi ya Jeshi la Mgambo katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao.

4. Jadili ni kwa namna gani rushwa inaweza kuathiri ulinzi na usalama wa Taifa.

5. Eleza jinsi mfumo wa ubalozi wa nyumba kumi unaweza kutumika katika mazingira ya sasa.

6. Tathmini mchango wa makundi mbalimbali ya jamii (mf. Taasisi za dini, asasi za kiraia na shule) katika ulinzi na usalama kwa Taifa.

7. Chambua namna mila na desturi za Kitanzania zinavyoweza kusaidia kuimarika kwa ulinzi na usalama wa taifa.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256