Sura Ya 02 : Maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa

Utangulizi

Fasihi ya Kiswahili imepiga hatua kubwa za maendeleo ndani na nje ya mipaka ya jamii za Afrika Mashariki. Katika sura hii, utajifunza kuhusu maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa kabla ya uhuru na maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa baada ya uhuru. Vilevile, utajifunza athari za sayansi na teknolojia katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa. Uelewa utakaojenga utakuwezesha kuelewa kwa undani maendeleo ya fasihi ya Kiswahili na kutambua kazi za fasihi ya Kiswahili zinazoweza kutumika ndani na nje ya mipaka ya Afrika Mashariki.

Fasihi ya Kiswahili kabla na baada ya uhuru

Shughuli ya 2.1

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya maktabani na mkondoni, eleza kwa mifano hatua za maendeleo zilizofikiwa na jamii ya Waswahili Afrika Mashariki kabla ya uhuru.

Maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa kabla ya uhuru

Kabla ya kupata uhuru, maendeleo ya fasihi ya Kiswahili katika eneo la Afrika Mashariki yaliathiriwa na wenyeji na wageni. Kabla ya kuja kwa wageni, wenyeji wa kila jamii walikuwa wanatekeleza matukio yaliyohusisha utendaji wa tamaduni mbalimbali za fasihi simulizi. Matukio hayo yalihusisha: kuimba, kutambika, kutumia semi na tamathali mbalimbali katika mazungumzo yao, kutamba hadithi, na kughani mashairi na tenzi. Hali hiyo iliyodumu kwa muda mrefu ilihifadhiwa sana na ujio wa wageni (hasa Waarabu, Wajerumani, na Waingereza) ambao walileta Uislamu na Ukristo. Kwa ujumla, utendaji wa fasihi simulizi ya Kiswahili katika kipindi hicho ulikuwa unafanyika zaidi ndani ya mipaka ya jamii. Hivyo, katika kipindi hicho, fasihi simulizi ya Kiswahili haikupata mawanda mapana kimataifa.

Kwa upande wa fasihi andishi ya Kiswahili, chimbuko na maendeleo yake katika jamii za Afrika Mashariki kunahusishwa na juhudi za awali za wageni. Hii ni kwa sababu fasihi andishi ya Kiswahili ilianza wakati jamii hizo zilipoanza kuweka amali zao kama vile historia na tamaduni katika maandishi. Hati za maandishi zililetwa na wageni waliotoka mabara ya Asia na Ulaya. Wageni hao ni Waarabu, Wazungu, Wajerumani, na Waingereza. Ujio wa hati hizo katika jamii za Waswahili ulienda sambamba na ujio wa elimu ya kigeni iliyovletwa na wageni hao. Hati ya Kiarabu ilianza kutumika kuandika Kiswahili tangu karne ya 9 (inaikisiwa miaka ya 800 BK). Maandiko ya kale ya Kiswahili, hasa tendi, tenzi na tarihi, yaliandikwa kwa hati hiyo. Mifano niUtendi wa Tambuka (Bwana Mwengo, 2019) na Utenzi wa Al-Inkishafi (Sayyid Abdallah bin Ali bin Nasir, 1800).

Kuanzia karne ya 19, hati ya Kirumi ilijengezwa na Wajerumani na Waingereza katika jamii za Waswahili. Hati hiyo ya Kirumi ilienezwa kupitia mfumo wa elimu. Hati hiyo imeendelea kutumika hadi hivi sasa; na ndiyo imekuwa hati inayotumiwa katika uandishi wa fasihi andishi ya Kiswahili. Hii inaamanisha kuwa, maendeleo ya fasihi andishi ya Kiswahili kabla ya uhuru yana uhusiano mkubwa na wageni hao. Inachezwa kwamba wageni hawa walipofika Pwani ya Afrika Mashariki kuanzia karne ya 16 walileta hati na elimu ya jinsi ya kuzitumia hati hizo. Ndiyo maana baadhi ya tenzi za zamani kama vile Fumo Liyongo zilikuwa hapo kabla ya hati za maandishi katika Kiswahili na ziliwekwa katika maandishi baadaye. Tenzi hizi zilitokana na nyimbo za wenyeji.

Pamoja na kuhusika kwa wageni katika shughuli mbalimbali zinazohusisha fasihi andishi ya Kiswahili, bado mawanda ya kazi hizo kabla ya uhuru yalikuwa ndani ya maeneo ya Waswahili. Kazi za fasihi andishi ya Kiswahili zilijusu na wandani ya kimataifa baada ya kuanza kufasiriwa kwa kutumia lugha mbalimbali. Japo kuwa lengo la kufasiri kazi hizo katika lugha mbalimbali lilikuwa kufundisha na kukuza lugha, kwa namna moja au nyingine, hali hiyo ilichangia kuzifikisha kazi hizo kwa wasomaji wa mataifa yaliyotokea. Mfano wa kazi zilizotandikwa au kutafsiriwa kwa lugha za mataifa yaliyotawala eneo la Afrika Mashariki ni: Swahili Tales as Told by the Natives of Zanzibar (1870) kilichotafsiriwa na Edward Steere na Prose and Poetry der Suaheli (1907) kilichoandikwa na Carl Velten.

Kadiri muda ulivyopenda, Waafrika walianza kuandika kazi za kinathari. Miongoni mwa kazi hizo ni Maisha ya Hemed bin Muhammed el Murjebi au Tippu Tip (Wilfred Whiteley, 1902) (Mhariri, 1950), Mwaka katika Mnyororo (Samweli Shoza, 1921), Tulivyoona na Tulivyofanya Uingereza (Martin Kayamba, 1932), Uhuru wa Watumwa (James Mbotela, 1934), na Habari za Wakilindi (Abdalla Hemed el Ajemi, 1972).

Riwaya nyingi za mwanzo zilifuata mkondo wa hekaya na ngano. Kimaudhui, riwaya nyingi ziliielezea mambo ya mila na desturi kama njia ya kutunza maadili. Baadhi ya riwaya hizi ziliathiriwa na fasihi ya Kiarabu kwa mfano: Kisa cha Mwna wa Mfalme Mohamed bin Suleiman (Akida Waziri, 1944) na Jeshuri katika Nyumba ya Sultani (David Diva, 1949). Aidha, riwaya zilizoandikwa na Waafrika zilihusu mila na desturi za jamii. Maandiko hayo pia yalihusu maadili mbalimbali na changamoto zilizohusu jamii ya wakati huo.

Vilevile, baadhi ya maandiko hayo yalisisitiza utu. Miongoni mwa kazi hizo niAdili na Nduguze (Shaaban Robert, 1952) na Kurwa na Doto (Mohamed Saleh Farsy, 1960). Kazi nyingine zilionesha madhara ya watawala wasio na utu. Miongoni mwa hizo niKufikirika (1951) na Kusadikika (1952) za Shaaban Robert. Hali kadhalika, kulikuwa na kazi mbalimbali za fasihi zilizoathiriwa na tamaduni za Kizungu, ingawa ziliandikwa na wazawa wa nchi za Afrika Mashariki. Kazi hizi zilikuwa na maudhui yanayohusu upelelezi na ujambazi wa kutumia silaha. Miongoni mwa kazi hizo ni riwaya ya Mzimu wa Watu wa Kale (Mohammed Said Abdulla, 1957). Pia, walikuwapo waandishi walioandika vitabu vya ushairi. Mifano ya waandishi hao ni: Seadan Kandoro (Mashairi ya Saadani, 1972), Mathias Mnyampala (Waadhi wa Ushairi, 1965), na Kaluta Amri Abedi (Sheria za Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri, 1954). Hata hivyo, baadhi ya kazi za waandishi hawa zilichapishwa miaka ya mwanzo baada ya uhuru.

Shughuli ya 2.2

Kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya maktabani na mkondoni, eleza mchango wa taasisi mbalimbali zilizosaidia kukuza na kuendeleza fasihi ya Kiswahili kabla na baada ya uhuru.

Maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa baada ya uhuru

Fasihi ya Kiswahili ilipata mafanikio makubwa sana katika na kimataifa baada ya uhuru, ambapo waandishi wengi walijitokeza na kutumia Kiswahili kama nyenzo kuu ya kupaza sauti zao kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kisiasa, na kiutamaduni. Katika kipindi hiki, fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa iliendelea kupata sura mpya kulingana na mahitaji ya wakati huo. Kazi nyingi za fasihi zilikuwa za kushangilia uhuru. Pamoja na kushangilia uhuru, wanafasihi waliandika pia kazi za kusisitiza ukombozi wa wananchi. Mathalan, kutokana na mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964, Tanzania Visiwani kulibuka kazi za fasihi ambazo zilihusu ukombozi wa mnyonge. Baadhi ya kazi hizo niKasri ya Mwinyi Fuad (1978) na Kati (1979) za Shah Abdam Sharif; Nyota ya Rehema (Mohamed Suleiman Mohamed, 1978), Dunia Mti Mkavu (1980), Sikate Tamaa (1980), na Utengo (1980) za Said Ahmed Mohamed; na Utenzi wa Ukombozi wa Zanzibar (Muhammed Seif Khatib, 1978).

Mnamo mwaka 1967, yapata miaka sita baada ya uhuru, Azimio la Arusha lilitangazwa. Falsafa kuu ya Azimio la Arusha ilikuwa Ujamaa na Kujitegemea. Pamoja na mabadiliko mengine, fasihi andishi pia ilipata sura mpya. Fasihi ya kipindi hicho ililenga kutukuza maadili na amali zilizotokana na tamko la Azimio la Arusha. Kazi nyingi za fasihi za wakati huo zilisifu Azimio la Arusha. Miongoni mwazo ni: Madunda ya Azimio (Wah. Lucas Hornero, Tigiti Sengo, na Shaaban Ngole, 1980), Mashairi ya Miaka Kumi ya Azimio la Arusha (UKUTA, 1977), na Ngonjera za UKUTA (Mathias Mnyampala, 1970).

Kutokana na Azimio la Arusha kusisitiza vijiji vya ujamaa pamoja na shughuli za kilimo,baadhi ya kazi za fasihi andishi zilisawiri ubora wa maisha ya vijijini ikilinganishwa na yale ya mijini. Kazi zenye maudhui ya aina hiyo ni kama vile: Mtu ni Utu (George Mhina, 1971), Kijiji Chetu (Ngalimecha Ngahyoma, 1975), Ndoto ya Ndaraja (John Ngomoi, 1975), na Njozi za Usiku (William Seme, 1975), Shida (Ndyanao Balisidya, 1975), na Hatia (Penina Muhando, 1972). Pamoja na kuwapo kwa kazi zilizosifu Azimio la Arusha, zipo kazi nyingine ambazo zilikosoa na kuonesha kushindwa kwa Azimio la Arusha kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baadhi ya viongozi kushindwa kulielewa Azimio hilo; hivyo, kushindwa kusimamia utekelezaji wake. Miongoni mwa kazi hizo ni: Njia Iliyopotea (Claude Mung'ong'o, 1979) na Lina Ubani (Penina Muhando, 1984). Nyingine niDunia Uwanja wa Fujo (1978), Maya Waziri wa Maradhi (1978), Gamba la Nyoka (1978), na Kaputula la Marx (1999) za Euphrase Kezilahabi.

Katika miaka ya 1970 na 1980, lilibuka wimbi la riwaya na hadithi fupi zenye maudhui ya upelelezi na mapenzi. Waandishi wengi wa mkondo huu waliandika ili kuchuma fedha. Kazi zao ziliisisimua na kuvutia wasomaji. Kwa upande mwingine, baadhi ya kazi hizi zilitimiza masharti ya mfumo wa kibopari kwa sababu hazikujishughulisha na matatizo halisi ya watu wa kawaida. Hata pale zilipoyashughulikia, zilipotosha ukweli na uhalisi wake. Hali hii ilitokana na kazi hizo kutoa majibu ya mkato kama vile kutumia polisi, mahakama na jela. Pamoja na kuzuka kwa riwaya pendwa, wapo waandishi walioandika kazi zao kueleza hali halisi ya jamii. Mifano ya kazi hizo ni: Fungate ya Uhuru (Muhammed Seif Khatib, 1974), Raha Karaha (Theobald Mvungi, 1982), Chungu Tamu (Theobald Mvungi, 1985), na Kunga za Ushairi na Diwani Yetu (Mugyabuso Mulokozi na Kulikoyela Kahigi, 1979).

Mwishoni mwa miaka ya 1980, zilibuka riwaya za kimajaribio zilizolizuka au kutengua baadhi ya kaida za uandishi wa riwaya. Baadhi ya sifa za riwaya hizo ni kukosa msuko ulio dhahiri, simulizi kukosa mhusika mkuu aliye dhahiri, na matumizi ya mfumo wa wakati tofauti na iliyozoweleka. Mara nyingi, riwaya za aina hiyo huwa na maudhui yenye uchangamani mkubwa. Mifano ni riwaya za Nagona (1990) na Mzingile (1991) (Euphrase Kezilahabi), Babu Alipofufuka (Said Ahmed Mohamed, 2001), na Bin-Adamu (Kyallo Wamitila, 2002). Kwa ujumla, maendeleo ya fasihi yanaonekana kufuata mwelekeo wa mifumo ya maisha ya wakati ambao kazi husika zinaandikwa; na baadhi zimekwenda mbele ya wakati.

Umaarufu wa fasihi andishi ya Kiswahili haukuishia katika mipaka ya Afrika Mashariki pekee bali ulivuka na kusomwa maeneo mengine duniani kutokana na tafsiri. Fasihi andishi ya Kiswahili imefanikiwa kutafsiriwa katika lugha mbalimbali kama vile Kijerumani, Kichina, Kiingereza, Kiitaliano, Kijapani, Kiarabu na Kifaransa. Kutafsiriwa huko kumesaidia kuongeza idadi ya wapokezi (wasomaji na wahakiki) wa maudhui ya kazi za fasihi andishi ya Kiswahili. Mifano ya kazi za fasihi ya Kiswahili zilizotafsiriwa katika lugha nyingine ni: Tutarudi na Robo Zetu?ya Ben Mtobwa (iliyotafsiriwa katika lugha ya Kiingereza kama Zero Hour) na Aliyeonja Pepo ya Farouk Topan (iliyotafsiriwa katika lugha ya Kiingereza kama A Taste of Heaven). Pia, kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili zimetafitiwa na wataalamu wa fasihi wa nchi za nje ya mataifa ya Waswahili.

Shughuli ya 2.3

Wataalamu mbalimbali wamejadili fasihi ya kitaifa na kimataifa kabla na baada ya uhuru. Kwa kurejelea wataalamu hao, jadili tofauti iliyopo kati ya fasihi ya kitaifa na kimataifa kabla na baada ya uhuru.

www.learninghubtz.co.tz

Zoezi

1. Jadili kwa mifano maendeleo ya fasihi ya Kiswahili nchini Tanganyika na Zanzibar kabla ya uhuru kwa kuhusianisha na maendeleo ya sasa.

2. Eleza kwa kifupi aina za fasihi ya Kiswahili zilizokuwepo baada ya uhuru na mchango wake kwa jamii.

3. Kwa kutumia mifano, eleza mbinu za kisanaa zilizotumika katika fasihi ya Kiswahili kabla ya uhuru.

4. Tathmini nafasi ya tuzo za uandishi wa kazi mbalimbali za fasihi katika kukuza fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.

Shughuli ya 2.4

Teknolojia imekuwa na athari chanya na hasi katika maendeleo ya Kiswahili kitaifa. Thibitisha kauli hii kwa kurejelea vyanzo mbalimbali.

Athari za sayansi na teknolojia katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa

Sayansi na teknolojia imekuwa na athari kubwa katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa. Watunzi mbalimbali wa kazi za fasihi simulizi na andishi ya Kiswahili wamefanikiwa kutumia vipengele mbalimbali vya sayansi katika kuumba maudhui ya kazi zao. Mfano mojawapo wa kazi za fasihi simulizi ambazo zina athari ya kisayansi ni methali isemayo, ukiona vyaelea, ujue vimeundwa. Pia, kuna kazi mbalimbali za fasihi andishi ambazo zimeathiriwa na maendeleo ya kisayansi kama vile bunilizi za kisayansi ambazo zinaangazia maudhui yanayohusu uhalifu, upelelezi na ujasusi.

Teknolojia ni zao la fikra za kisayansi katika kuunda nyenzo mbalimbali za kurahisisha maisha ya mwanadamu. Kwa hiyo, teknolojia imetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya fasihi simulizi na andishi ya Kiswahili. Watunzi na hadhira ya kazi za fasihi wamenufaika kupitia matumizi ya nyenzo mbalimbali za kiteknolojia. Nyenzo hizo hujumuisha programu na vifaa. Kwa mfano, kuna programu za kuandikia na kuhariria maandishi ambazo huwasaidia watunzi wa kazi za fasihi kuzalisha kazi. Pia, kuna programu mbalimbali zinazosaidia kusambaza, kutangaza na kuuza kazi za fasihi. Programu hizo zinajumuisha majukwaa ya mitandao ya kijamii na maduka ya kidijiti. Kwa upande wa vifaa vya kiteknolojia, watunzi wa kazi za fasihi ya Kiswahili hunufaika na matumizi ya kompyuta, simu, na vishikwambi ambavyo hutumika kwa kufanya tafiti, kuandikia, kuhariria, kutafsiria, kukalimania, kuhifadhi, na kuuza kazi zao. Kwa ujumla, sayansi na teknolojia imesaidia kukuza soko la fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.

Shughuli 2.5

Kwa kutumia vyanzo vya maktabani na mkondoni, tathmini kazi za kifasihi zilizoandikwa na wataalamu mbalimbali, kisha eleza athari za kisayansi zinazojitokeza katika kazi hizo.

Tamrini

1. Bainisha waandishi watatu wa fasihi ya Kiswahili wa baada ya uhuru na eleza kwa kifupi mchango wao katika maendeleo ya fasihi.

2. Tathmini namna kazi za fasihi ya Kiswahili zilizochapishwa nchini baada ya uhuru zinavyofungamana na uhalisi wa maisha.

3. Kwa kutumia mifano, eleza changamoto zinazoyakabili maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa tangu uhuru.

4. Jadili mambo yaliyofanya nchi za Afrika Mashariki zilivyokuza fasihi ya Kiswahili baada ya uhuru.

5. Eleza mambo yaliyochangia kuwapo kwa tofauti za kimaudhui ya fasihi ya Kiswahili kabla na baada ya uhuru.

6. Kwa kutumia mifano, eleza namna kazi za fasihi ya Kiswahili zilivyochangia katika upatikanaji wa uhuru katika nchi za Afrika Mashariki.

7. Jadili changamoto zinazoyakabili maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kimataifa, licha ya juhudi zinazofanyika tangu uhuru.

8. Eleza ni kwa namna gani teknolojia inaathiri uandishi na usomaji wa fasihi ya Kiswahili.

9. Bainisha njia tano ambazo wadau wa fasihi wanaweza kuzitumia kupambana na changamoto za ubwakuzi zinazosababishwa na matumizi ya teknolojia.

Majibu ya Tamrini:

1. Bainisha waandishi watatu wa fasihi ya Kiswahili wa baada ya uhuru na eleza kwa kifupi mchango wao katika maendeleo ya fasihi.

(i) Shaaban Robert

Mchango:

  • Aliikuza riwaya, insha na ushairi wa Kiswahili.

  • Alitumia fasihi kufundisha maadili na uzalendo.

  • Alikuza matumizi ya lugha sanifu ya Kiswahili.

Mfano wa kazi: Kusadikika, Kufikirika, Adili na Nduguze.

(ii) Euphrase Kezilahabi

Mchango:

  • Alianzisha mtindo mpya wa riwaya na ushairi.

  • Aliibua maudhui ya falsafa na ukombozi wa fikra.

  • Alihamasisha ubunifu katika fasihi ya Kiswahili.

Mfano wa kazi: Rosa Mistika, Nagona, Mzingile.

(iii) Penina O. Mlama

Mchango:

  • Aliendeleza tamthilia ya Kiswahili.

  • Alitetea usawa wa kijinsia kupitia fasihi.

  • Alikuza maigizo ya kijamii.

Mfano wa kazi: Hatia, Lina Ubani.


2. Tathmini namna kazi za fasihi ya Kiswahili zilizochapishwa nchini baada ya uhuru zinavyofungamana na uhalisi wa maisha.

Kazi hizo zinafungamana na maisha kwa sababu:

  1. Zinaonesha matatizo ya umaskini.

  2. Zinazungumzia rushwa na ufisadi.

  3. Zinakosoa uongozi mbaya.

  4. Zinahamasisha elimu.

  5. Zinapinga ukandamizaji wa wanawake.

  6. Zinahimiza uzalendo.

  7. Zinahamasisha uwajibikaji.

  8. Zinatoa suluhisho la changamoto za jamii.

Mifano: Rosa Mistika, Dunia Uwanja wa Fujo, Kigogo, Kuli.


3. Kwa kutumia mifano, eleza changamoto zinazoyakabili maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa tangu uhuru.

  1. Upungufu wa wasomaji.

  2. Ushindani kutoka lugha za kigeni.

  3. Ubwakuzi wa kazi za fasihi.

  4. Ukosefu wa fedha za kuchapisha vitabu.

  5. Teknolojia kutumika vibaya.

  6. Upungufu wa tafsiri za kazi za Kiswahili.

  7. Masoko madogo ya vitabu.

  8. Kushuka kwa utamaduni wa kusoma.

Mifano: Uchapishaji haramu wa vitabu katika mtandao na usambazaji wa PDF bila ruhusa.


4. Jadili mambo yaliyofanya nchi za Afrika Mashariki zilivyokuza fasihi ya Kiswahili baada ya uhuru.

  1. Kuifanya Kiswahili kuwa lugha ya taifa.

  2. Kuanzishwa kwa BAKITA na BAKIZA.

  3. Kufundishwa Kiswahili mashuleni na vyuoni.

  4. Kuongezeka kwa wachapishaji wa vitabu.

  5. Mashindano ya uandishi.

  6. Kuanzishwa kwa taasisi za utafiti wa Kiswahili.

  7. Matumizi ya Kiswahili kwenye vyombo vya habari.

  8. Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.


5. Eleza mambo yaliyochangia kuwapo kwa tofauti za kimaudhui ya fasihi ya Kiswahili kabla na baada ya uhuru.

Kabla ya Uhuru

  • Kupinga ukoloni.

  • Kueneza dini.

  • Kuhifadhi mila.

  • Kudai uhuru.

  • Kupinga unyonyaji.

Baada ya Uhuru

  • Kujenga Taifa.

  • Rushwa.

  • Demokrasia.

  • Ukimwi.

  • Utandawazi.

  • Teknolojia.

  • Haki za binadamu.

  • Uongozi bora.


6. Kwa kutumia mifano, eleza namna kazi za fasihi ya Kiswahili zilivyochangia katika upatikanaji wa uhuru katika nchi za Afrika Mashariki.

  1. Ziliwahamasisha wananchi kupigania uhuru.

  2. Zilifichua ukandamizaji wa wakoloni.

  3. Zilijenga uzalendo.

  4. Zilihamasisha umoja.

  5. Zilikosoa sera za kikoloni.

  6. Ziliamsha ari ya mapambano.

Mifano:

  • Mashairi ya Muyaka bin Haji.

  • Nyimbo za harakati za TANU.

  • Tamthilia mbalimbali za ukombozi.


7. Jadili changamoto zinazoyakabili maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kimataifa, licha ya juhudi zinazofanyika tangu uhuru.

  1. Lugha za kigeni kutawala.

  2. Tafsiri chache.

  3. Fedha ndogo za utafiti.

  4. Upungufu wa wachapishaji wa kimataifa.

  5. Ubwakuzi wa kazi.

  6. Teknolojia kutumiwa vibaya.

  7. Idadi ndogo ya wataalamu wa Kiswahili duniani.

  8. Masoko madogo ya vitabu vya Kiswahili.


8. Eleza ni kwa namna gani teknolojia inaathiri uandishi na usomaji wa fasihi ya Kiswahili.

Athari Chanya

  1. Huwezesha uchapishaji wa kidijitali.

  2. Huongeza wasomaji kupitia vitabu pepe.

  3. Hurahisisha utafiti.

  4. Hukuza usambazaji wa kazi za fasihi.

  5. Huwarahisishia waandishi kuchapisha kazi zao.

Athari Hasi

  1. Ubwakuzi wa kazi.

  2. Kushuka kwa ununuzi wa vitabu.

  3. Kutegemea taarifa zisizo sahihi.

  4. Kupungua kwa usomaji wa vitabu vya karatasi.

  5. Matumizi ya AI na programu nyingine kunakoweza kupunguza ubunifu wa baadhi ya waandishi ikiwa vitatumika bila uwajibikaji.


9. Bainisha njia tano ambazo wadau wa fasihi wanaweza kuzitumia kupambana na changamoto za ubwakuzi zinazosababishwa na matumizi ya teknolojia.

  1. Kusajili hakimiliki za kazi za fasihi.

  2. Kutekeleza sheria za hakimiliki kwa ukamilifu.

  3. Kutumia mifumo salama ya usambazaji wa vitabu vya kidijitali.

  4. Kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ubwakuzi.

  5. Kuwachukulia hatua za kisheria wanaokiuka hakimiliki.

  6. Kutumia teknolojia za kulinda faili za kidijitali (Digital Rights Management – DRM).

  7. Kuuza vitabu kupitia majukwaa rasmi ya mtandaoni.

  8. Kushirikiana na taasisi za hakimiliki na wachapishaji kufuatilia ukiukaji wa kazi za fasihi.

Hitimisho:
Maendeleo ya fasihi ya Kiswahili tangu uhuru yamekuwa makubwa kutokana na mchango wa waandishi, taasisi za lugha, elimu na teknolojia. Hata hivyo, changamoto kama ubwakuzi, ushindani wa lugha za kigeni na kupungua kwa utamaduni wa kusoma zinahitaji ushirikiano wa serikali, waandishi, wachapishaji na wasomaji ili kuhakikisha fasihi ya Kiswahili inaendelea kukua kitaifa na kimataifa.

www.learninghubtz.co.tz

ZOEZI LA MARUDIO : MAENDELEO YA FASIHI YA KISWAHILI

SEHEMU A: Maswali ya Chagua Jibu Sahihi

1. Maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kabla ya uhuru yaliathiriwa zaidi na:

  1. Wamarekani
  2. Waarabu, Wajerumani na Waingereza
  3. Wahindi pekee
  4. Wareno pekee

2. Hati ya kwanza iliyotumika kuandika Kiswahili ilikuwa:

  1. Hati ya Kirumi
  2. Hati ya Kigiriki
  3. Hati ya Kiarabu
  4. Hati ya Kiebrania

3. Hati ya Kirumi ilianza kutumika sana katika Kiswahili kuanzia:

  1. Karne ya 9
  2. Karne ya 12
  3. Karne ya 19
  4. Karne ya 21

4. Azimio la Arusha lilitangazwa mwaka:

  1. 1961
  2. 1964
  3. 1967
  4. 1977

5. Falsafa kuu ya Azimio la Arusha ilikuwa:

  1. Ubepari
  2. Ujamaa na Kujitegemea
  3. Ukomunisti
  4. Uliberali

6. Riwaya Nagona imeandikwa na:

  1. Shaaban Robert
  2. Euphrase Kezilahabi
  3. Mohamed Said Abdulla
  4. Penina Muhando

7. Kazi za fasihi za baada ya uhuru zilijikita zaidi katika:

  1. Kusifu ukoloni
  2. Kushangilia uhuru na ukombozi wa wananchi
  3. Biashara pekee
  4. Michezo ya watoto

8. Teknolojia imechangia maendeleo ya fasihi kwa:

  1. Kupunguza usomaji pekee
  2. Kuongeza uchapishaji, usambazaji na utafiti
  3. Kufuta vitabu vya fasihi
  4. Kuzuia tafsiri

9. Ni ipi kati ya zifuatazo ni kazi ya Shaaban Robert?

  1. Kusadikika
  2. Nagona
  3. Mtu ni Utu
  4. Kijiji Chetu

10. Tafsiri za kazi za fasihi ya Kiswahili zimechangia:

  1. Kupungua kwa wasomaji
  2. Kuenea kwa fasihi kimataifa
  3. Kufutwa kwa Kiswahili
  4. Kupungua kwa waandishi

SEHEMU B: Maswali Mafupi

11. Eleza maana ya maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

12. Taja mambo manne yaliyochangia maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kabla ya uhuru.

13. Eleza nafasi ya Waarabu katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

14. Eleza nafasi ya Wajerumani na Waingereza katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

15. Taja kazi nne za fasihi zilizoandikwa kabla ya uhuru.

16. Eleza kwa kifupi maendeleo ya fasihi ya Kiswahili baada ya uhuru.

17. Taja waandishi watano wa fasihi ya Kiswahili wa baada ya uhuru.

18. Eleza mchango wa Azimio la Arusha katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

19. Taja athari tano chanya za sayansi na teknolojia katika fasihi ya Kiswahili.

20. Taja athari tatu hasi za teknolojia katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

SEHEMU C: Maswali ya Insha

21. Jadili maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa kabla ya uhuru.

22. Kwa kutumia mifano, eleza maendeleo ya fasihi ya Kiswahili baada ya uhuru.

23. Jadili mchango wa wageni katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kabla ya uhuru.

24. Kwa kutumia mifano, eleza mchango wa Azimio la Arusha katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

25. Jadili tofauti za maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kabla na baada ya uhuru.

26. Kwa kutumia mifano, eleza jinsi fasihi ya Kiswahili ilivyochangia ukombozi wa jamii baada ya uhuru.

27. Jadili mchango wa teknolojia katika uandishi, uchapishaji na usambazaji wa kazi za fasihi ya Kiswahili.

28. Tathmini athari chanya na hasi za sayansi na teknolojia katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili.

29. Kwa kutumia mifano, jadili sababu zilizoifanya fasihi ya Kiswahili kuvuka mipaka ya Afrika Mashariki.

30. Jadili nafasi ya tafsiri katika kueneza fasihi ya Kiswahili duniani.

31. Kwa kutumia mifano, linganisha maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kabla na baada ya uhuru kwa kuzingatia:

  • Waandishi
  • Maudhui
  • Lugha
  • Hadhira
  • Athari za kisiasa

32. "Uhuru ulileta mageuzi makubwa katika fasihi ya Kiswahili." Jadili kauli hii kwa hoja nane.

33. Jadili mchango wa waandishi wa fasihi ya Kiswahili katika maendeleo ya jamii ya Tanzania baada ya uhuru.

34. Kwa kutumia mifano, tathmini mchango wa sayansi na teknolojia katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili kitaifa na kimataifa.

35. "Teknolojia imekuwa baraka na changamoto katika maendeleo ya fasihi ya Kiswahili." Thibitisha kauli hii kwa hoja zenye mifano.

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256