MAARIFA YA JAMII

SURA YA KWANZA

MAZINGIRA

Ulipokuwa darasa la nne, ulijifunza kuhusu mazingira yana mjini na vitendo vinavyochangia uharibifu wa mazingira ya kijiji au mtaa. Pia, ulijifunza shughuli za utunzaji wa mazingira. Katika sura hii utajifunza kuhusu shughuli zinazofanywa na binadamu kama vile kilimo, ufugaji, uchimbaji madini, uvuvi, ukataji miti ovyo na shughuli za viwandani zinavyoweza kuharibu mazingira. Vilevile, utajifunza kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, vitendo vinavyoharibu vyanzo vya maji na athari zinazotokana na uharibifu wa vyanzo vya maji. Mwisho utajifunza njia za kutunza vyanzo hivyo.

Maana ya mazingira

Neno mazingira linajumuisha vitu vyote vinavyotuzunguka vikiwemo viumbe hai na visivyo hai. Hivyo, mazingira yanaundwa na vitu vya asili na vitu vya kutengenezwa na binadamu. Mazingira ni mjumuisho wa hali ya hewa, wanyama, mimea, udongo, milima, mabonde, bahari na miundombinu.

Uharibifu wa mazingira

Shughuli zote za binadamu hutegemea uwepo wa mazingira mazuri. Baadhi ya shughuli za binadamu huchangia uharibifu wa mazingira. Matumizi yasiyo sahihi ya mazingira hufanya mazingira kupoteza thamani yake, jambo ambalo husababisha binadamu kushindwa kufaidika nayo. Mazingira yanapoharibika husababisha athari mbalimbali. Kwa mfano, uharibifu wa ardhi husababisha ardhi kupoteza rutuba na kusababisha mavuno kupungua. Kuchafuliwa kwa hewa kutokana na moshi na vumbi kutoka viwandani husababisha kuongezeka kwa magonjwa ya binadamu kama vile kikohozi na mafua. Aidha, sumu za viwandani hufanya maji yanayotumika kwa shughuli mbalimbali kuchafuka.

Shughuli za binadamu zinazochangia uharibifu wa mazingira

Baadhi ya shughuli za binadamu zinazoweza kuchangia uharibifu wa mazingira iwapo,hazitafanyika kwa uangalifu ni pamoja na kilimo, ufugaji. uvuvi, viwanda na uchimbaji wa madini.

Kilimo

Kilimo ni shughuli ya uzalishaji mali inayohusisha uzalishaji wa mazao mbalimbali. Binadamu huzalisha mazao ya chakula na biashara. Baadhi ya mazao ya chakula ni mahindi, mpunga, mihogo, mtama, uwele, ndizi na karanga. Mazao ya biashara ni kama vile pamba, kahawa, katani, korosho na chai. Mazao kayo hulimwa sehemu mbalimbali nchini kutegemeana na hall ya hewa. Jedwali lifuatalo linaonesha mikoa inayolima mazao ya biashara na chakula kwa wingi nchini Tanzania.

Jedwali namba 1: Baadhi ya mikoa inayolima mazao ya chakula na biashara kwa wingi nchini Tanzania

Mazao

Maoneo yanapopatikana

Mahindi

Mbeya, iringa, Ruvuma, Morogoro, Rukwa, Dodoma, Kilimanjaro, Njombe, Katavi na Songwe

Mpunga

Mbeya, Rukwa, Morogoro, Pwani, Tabora, Mwanza na Shinyanga

Ndizi

Kagera, Arusha, Kilimanjaro na Mbeya

Mihogo

Tanga, Mtwara, Lindi, Mwanza, Ruvuma, Pwani, Morogoro, Kigoma na Mara

Chaff

Njombe, Tanga, Iringa na Mbeya

Kahawa

Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Ruvuma na Songwe

Katani

Tanga na Morogoro

Pamba

Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora

Korosho

Lindi, Mtwara na Pwani

Tumbaku

Tabora, Ruvuma, Katavi na Iringa

Faida za kilimo

Kilimo hutupatia chakula na malighafi ambazo hupelekwa viwandani kwa ajili ya kuchakata. Halikadhalika, hutupatia fedha za ndani na za kigeni ambazo hupatikana kwa kuuza mazao ya biashara na chakula. Kwa ujumla, kilimo hutoa ajira na kuitambulisha nchi katika sura ya dunia, mfano kilimo cha pamba Mwanza na korosho Mtwara.

Athari zitokanazo na shughuli za kilimo kisichofaa katika mazingira

Pamoja na faida zitokanazo na kilimo, shughuli hii huweza kuharibu mazingira.isipofanyika kwa uangaiifu. Kwa mfano, kilimo katika miteremko ya milima husababisha mmomonyoko wa udongo. Kutokana na kilimo cha kuhamahama, watu hufyeka misitu ovyo na kuichoma moto hivyo husababisha ukame. Vilevile, matumizi ya dawa na mbolea za viwandani yasiyokuwa sahihi husababisha ardhi kupoteza rutuba yake ya asili na kuua viumbe hai vinavyoishi ardhini.

Kutokana na vitendo hivi, ardhi hupoteza uoto wake wa asili na kusababisha mmomonyoko wa udongo. Aidha, vyanzo vya maji hukauka na ardhi hupoteza rutuba. Madhara yanayotokana na vitendo hivyo kwa viumbe hai kama binadamu, wanyama na wadudu ni kukosa makazi, kupata magonjwa na vifo.

Njia za kukabiliana na athari za shughuli za kilimo kisichofaa katika mazingira

Zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika katika kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na kilimo kisichofaa. Njia hizo ni kulima matuta ya kukingama na mteremko iii kuzuia mmomonyoko wa udongo. Njia nyingine ni kilimo mseto ambacho zao zaidi ya moja hulimwa katika eneo au shamba moja. Aina hii ya kilimo husaidia kuongeza rutuba katika ardhi. Pia, kulima kilimo cha kubadilisha mazao, mfano, mwaka huu mkulima akilima mahindi, mwakani analima mazao ya mikunde ambayo hurutubisha ardhi. Kupunguza matumizi ya dawa za kuulia wadudu na mbolea za viwandani iii kulinda rutuba ya asili ya udongo. Mbolea ya mboji au samadi inaweza kutumika badala ya mbolea za viwandani.

Aidha, kupanda miti katika maeneo yaliyoachwa wazi katika sehemu ambazo watu hufanya kilimo cha kuhamahama huzuia mmomonyoko wa udongo. Ni muhimu pia kupanda miti katika miteremko ya milima kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Ufugaji

Ufugaji ni shughuli inayohusu kutunza mifugo kama ng'ombe, mbuzi, kondoo, kuku na bata. Kuna aina tatu za ufugaji nazo ni ufugaji wa ndani, ufugaji wa jadi au asili na ufugaji wa kuhamahama. Katika ufugaji wa ndani sehemu maalumu hutengwa kwa ajili ya kufugia. Ufugaji huu huweza kufanywa kwa mifugo michache. Aidha, mifugo mingi kama vile ng'ombe, mbuzi na kondoo hufugwa katika mashamba makubwa yanayomilikiwa na serikali, makampuni au watu binafsi, mashamba hayo huitwa ranchi. Aina nyingine ya ufugaji ni ule wa jadi au asili. Katika aina hii wafugaji hupeleka mifugo yao malishoni asubuhi na kuwarudisha mazizini jioni. Halikadhalika kuna ufugaji wa kuhamahama. Katika aina hii ya ufugaji, mfugaji hulazimika kuhama na mifugo yake kwa ajili ya kutafuta malisho na maji. Wakati mwingine mifugo hutembea umbali mrefu kabla ya kufika mahali penye malisho na maji.

Ufugaji wa ng'ombe hufanyika zaidi katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga,Tabora, Singida, Dodoma, Kilimanjaro na Arusha. Baadhi ya makabila yanayojihusishana ufugaji huo ni Wamasai, Wabarbaig, Wasukuma, Wanyamwezi, Wameru na Wagogo. Wafugaji kama vile Wamasai, Wabarbaig na Wasukuma hufuga kwa kuhamahama kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta maji na malisho kwa ajili ya mifugo yao.

Faida za ufugaji

Ufugaji una faida nyingi. Baadhi ya faida hizo ni kutupatia nyama, maziwa, ngozi, kwato na mbolea. Ngozi hutumika kutengeneza vitu mbalimbali kama vile viatu, mabegi, mikanda na ngoma. Kwato hutumika kutengeneza gundi. Pia, mifugo hutupatia samadi kwa ajili ya kutumia kwenye kilimo kuzalisha mazao mbalimbali. Mazao hayo huzalishwa kwa ajili ya chakula na biashara. Vilevile, mifugo inapouzwa hutupatia fedha.

Athari zitokanazo na ufugaji usiofaa

Wanyama wengi wanapochungwa kwenye eneo moja, humaliza nyasi zote na uoto mwingine na kuacha ardhi wazi. Makundi makubwa ya mifugo yanapopita mahali katika eneo kwa muda mrefu huondoa uoto katika ardhi. Pia, wanyama hao hufanya ardhi kuwa tifutifu na kusababisha upepo au mvua kuimomonyoa na kusafirisha udongo wake kwa urahisi. Udongo uliomomonyolewa huweza kusababisha mabwawa kujaa na kukauka. Hatimaye kusababisha ukosefu wa maji na malisho kwa mifugo, watu na viumbe wengine.

Aidha ufugaji wa kuhamahama husababisha ukataji miti ovyo pale ambapo wafugaji hutengeneza mazizi ya kuhifadhi mifugo yao na kupata kuni za kupikia. Baada ya muda wafugaji hao huondoka mahali hapo na kwenda sehemu nyingine ambako huendelea kufanya uharibifu wa mazingira.

Njia za kudhibiti athari za ufugaji usiofaa

Njia ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ufugaji usiofaa ni kuepuka kufuga mifugo mingi katika eneo dogo. Kupunguza idadi ya mifugo kutasaidia kuepuka athari zitokanazo na shughuli za ufugaji. Hivyo, ni muhimu kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji iii wafuge mifugo michache itakayotoa mazao bora na mengi mfano maziwa ya kutosha, nyama na ngozi bora.

Viwanda

Kiwanda ni mahali panapofanyika shughuli ya kiuchumi inayohusisha uchakataji wa malighafi na kuzalisha bidhaa kwa kutumia mashine. Bidhaa hizo zinaweza kuwa nguo, magodoro, magari, bati, pikipiki, vyakula na vinywaji mbalimbali. Kuna aina mbili za viwanda ambazo ni viwanda vinavyochakata malighafi na viwanda vinavyozalisha bidhaa. Mifano ya viwanda vinavyochakata malighafi ni viwanda vya uchakataji wa pamba na kutengeneza nyuzi. Aina ya pili ya viwanda ni vile vinavyotengeneza bidhaa zinazotokana na malighafi au bidhaa za viwanda vya uchakataji. Kwa mfano kiwanda cha kutengeneza nguo kutokana na nyuzi za pamba, kiwanda cha kutengeneza mazulia kutokana na nyuzi za mkonge na kiwanda cha kutengeneza sukari kutokana na zao Ia miwa.

Faida zitokanazo na shughuli za viwanda

Viwanda husaidia kuongeza ubora na thamani ya malighafi inayozalishwa na kupata bidhaa kwa matumizi mbalimbali. Viwanda husaidia kuinua pato is taifa kwa kuingiza fedha za kigeni baada ya kuuza bidhaa hizo nje ya nchi. Aidha, viwanda hutoa ajira kwa kuwa watu wengi huajiriwa viwandani. Pia, viwanda hutoa fursa ya watu kujiajiri kwa kuanzisha shughuli za ujasiriamali katika maeneo yenye viwanda.

Athari zitokanazo na shughuli za viwanda katika mazingira

Viwanda husababisha uchafuzi wa aina mbalimbali wa mazingira kama vile kutoa hewa chafu yenye sumu, moshi, vumbi, taka ngumu, majitaka na kelele. Aina mbalimbali za gesi zinazotoka viwandani huwa ni sumu. Sumu hiyo hudhuru viumbe hai akiwemo binadamu. Uchafuzi wa hewa kutokana na shughuli za viwandani husababisha magonjwa mbalimbali kwa mfano magonjwa ya ngozi na magonjwa ya mfumo wa hewa. Pia uchafuzi wa hewa kutokana na viwanda, huchangia katika kusababisha mabadiliko ya tabia ya nchi kama vile ongezeko Ia joto, mafuriko na ukame.

Majitaka kutoka viwandani yakitiririshwa kwenye ardhi, mito na maziwa hudhuru viumbe hai wa nchi kavu na majini. Taka ngumu kama vile mifuko au chupa za plastiki zikitupwa ovyo katika mazingira kuchafua mazingira.

Njia za kudhibiti athari zitokanazo na shughuli za viwanda
Uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli za viwandani unaweza kudhibitiwa kwa kujenga viwanda mbali na makazi ya watu. Kuweka utaratibu wa kusafisha maji taka yanayotoka viwandani ili yaweze kutumika kwa shughuli nyingine. Viwanda vijengewe mashine yenye mitambo ya kupunguza moshi na kusafisha hewa yenye sum na vumbi linalotoka viwandani.

Viwanda viweke utaratibu wa urejelezaji takataka ambazo huweza kutumiwa tena kwa matumizi mengine au kutumiwa kama malighafi. Kwa mfano, karatasi zilizotumika kama vile magazeti huweza kurudishwa kiwandani na kuchakatwa iii kupata karatasi tena. Pia; karatasi huweza kubadilishwa kuwa nishati ya mkaa. Takataka nyingine zinaweza kubadilishwa kuwa mbolea. Aidha, vizuia sauti viwekwe viwandani iii kupunguza kelele za mashine.

Uchimbaji wa madini

Madini ni mkusanyiko wa maliasili zinazopatikana katika ardhi. Madini huchimbwa ardhini. Mifano ya madini ni dhahabu, almasi, chuma, makaa ya mawe, shaba na chumvi. Madini chumvi hupatikana kwa kuvukiza maji ya bahari na kubaki chumvi. Aidha chumvi inaweza kupatikana kwa kuvukiza majichumvi yaliyopo chini ya ardhi.

Uchimbaji wa madini ardhini hufanyika kwa mashine au mikono kwa kutumia vifaa rahisi kwa mfano majembe na sururu. Njia ya mikono hutumiwa na wachimbaji wadogo. Wachimbaji wakubwa hutumia mitambo mikubwa kuchimba madini ardhini.

Jedwali lifuatalo linaonesha baadhi ya madini na mahali yanapopatikana nchini Tanzania.

Aina ya madini

Mahali yanapopatikana

Dhahabu

Geita, Kahama mkoani Shinyanga, Chunya mkoani Mbeya, Mpanda mkoani Katavi, Amani mkoani Tanga, Sekenke na Manyoni mkoani Singida

Bati

Karagwe mkoani Kagera

Almasi

Mwadui mkoani Shinyanga

Tanzanite

Mererani mkoani Manyara

Makaa ya mawe

Songwe, Kiwira mkoani Mbeya na Mchuchuma mkoani Njombe

Rubi

Mahenge na Kilosa mkoani Morogoro

Chumvi

Uvinza mkoani Kigoma na mwambao wa Bahari ya Hindi

Chuma

Liganga mkoani Njombe, Mbeya, Milima ya Uluguru mkoani Morogoro na Mbabara karibu na ziwa Tanganyika

Chokaa

Chunya mkoani Mbeya, Kilwa mkoani Lindi na Tanga

Shaba

Mpanda mkoani Katavi

Ulanga

Ulanga mkoani Morogoro

Urani

Manyoni mkoani Singida, Bahi mkoani Dodoma na Namtumbo mkoani Ruvuma

Faida za madini

Uchimbaji wa madini husaidia watu kupata ajira na malighafi kwa ajili ya viwanda mbalimbali. Aidha, madini kama vile dhahabu, fedha na almasi huweza kutumika kama mapambo. Madini ya chumvi hutumika kama kiungo cha chakula na dawa. Aidha, chumvi hutumika kuhifadhi vyakula kama nyama na samaki visiharibike. Madini kama almasi hutumika kutengeneza mashine za kupata vitu vigumu viwandani, kukatia vioo na kutoboa au kuvunja miamba. Baadhi ya madini huuzwa nchi za nje na hivyo nchi hupata fedha za kigeni. Madini hutambulisha nchi. Kwa mfano,

madini ya Tanzanite ambayo hupatikana Tanzania peke yake, hufanya Tanzania itambulike na nchi mbalimbali.

Athari zitokanazo na uchimbaji wa madini katika mazingira

Uchimbaji wa madini huharibu mazingira iwapo njia bora za uchimbaji hazitatumika. Uchimbaji madini huweza kusababisha mmomonyoko wa udongo na kuacha mashimo makubwa. Mahal' palipochimbwa madini hapawezi kutumika kwa shughuli nyingine za uzalishaji mali mfano kilimo. Vumbi na moshi kutoka migodini husambaa na huweza kusababisha magonjwa kwa binadamu. Magonjwa hayo ni kama vile kifua, ugonjwa wa macho na magonjwa mengine yanayosababishwa na mzio wa vumbi. Aidha, kemikali zinazotumika katika kusafishia madini kama vile zebaki zikiingia katika vyanzo vya maji huathiri viumbe vya majini pamoja na binadamu.

Maeneo ya migodi mara nyingi hukumbwa na mafuriko. Kwa mfano, Mererani mkoani Manyara na Geita. Maeneo hayo hukumbwa na mafuriko kwa sababu uoto wa asili huondolewa na kusababisha maji kutiririka kwa kasi na kusomba udongo mwingi. Udongo huu huweza kuingia katika mito au mabwawa ambayo hujaa na kusababisha mafuriko. Maeneo ya migodi pia hukumbwa na ukame unaosababishwa na ukataji miti ovyo.

Njia za kudhibiti athari za uchimbaji wa madini

Athari zinazosababishwa na uchimbaji wa madini zinaweza kudhibitiwa kwa kusawazisha sehemu za machimbo kwa kufukia mashimo makubwa na madogo. Pia, kupanda miti na nyasi katika maeneo yaliyoharibiwa na uchimbaji madini iii kurejesha uoto wake. Vilevile, kuweka mashine za kuchuja hewa chafu na maji machafu yanayotoka migodini. Njia nyingine ni kutunga sheria ya matumizi bora ya ardhi katika maeneo ya machimbo.

UVUVI

Uvuvi ni shughuli ya kiuchumi inayohusisha uvunaji wa bidhaa za majini wakiwemo samaki. Uvuvi hufanyika katika maziwa, mito, mabwawa na bahari. Baadhi ya aina ya samaki wanaopatikana baharini ni changu, pweza, kibua, kolekole na papa. Samaki hawa ni wa maji chumvi. Samaki wa maji baridi hupatikana kwenye maziwa, mito na mabwawa. Mfano wa samaki wa maji baridi ni sato, kambale na sangara.

Faida za uvuvi

Shughuli ya uvuvi hutupatia faida nyingi. Baadhi ya faida hizo ni upatikanaji wa ajira kwa jamii zinazozunguka maeneo ya uvuvi mfano uchuuzi na ununuzi wa samaki. Vilevile, hutoa malighafi kwa ajili ya viwanda kama vile viwanda vya kusindika samaki. Samaki wanapouzwa huchangia kuongeza pato la taifa. Samaki wanapouzwa nje ya nchi hutupatia fedha za kigeni. Pia, uvuvi hutupatia chakula.

Athari zitokanazo na shughuli ya uvuvi usiofaa katika mazingira

Kuna njia mbalimbali zinazotumika katika kuvua samaki. Njia hizo zinaweza kuwa bora au njia zisizo bora. Njia bora ni zile ambazo wavuvi hutumia nyavu sahihi zenye viwango vinavyokubalika katika kuvua. Njia zisizo bora ni zile ambazo huleta uharibifu wa samaki na mazalia yake. Mifano ya njia zisizo bora ni pamoja na matumizi ya sumu na baruti. Njia hizi huharibu mazingira ya baharini au ziwani na kuharibu mazalia ya samaki. Matumizi ya kokoro ni mojawapo ya njia zisizo bora za uvuvi kwani hukamata samaki wadogo na mayai. Samaki hao wangeachwa wakue wangekuwa na manufaa zaidi kwa jamii na nchi kwa ujumla.

Mvuvi anapotumia sumu au baruti huua viumbe wengi wa majini, kwa hiyo husababisha viumbe hao kutoweka. Samaki waliovuliwa kwa kutumia sumu huweza kuleta madharakwa afya ya binadamu kama vile saratani.

Njia za kudhibiti uvuvi haramu

uvuvi usio bora huitwa uvuvi haramu. Madhara yanayotokana na uvuvi haramu yanaweza kudhibitiwa kwa kuelimisha wavuvi kuhusu madhara ya kutumia baruti, sumu na kokoro. Vilevile, sheria za kuzuia uvuvi haramu zisimamiwe vizuri iii kuboresha shughuli za uvuvi. Aidha, wavuvi wajengewe uwezo wa kutumia vifaa bora vya uvuvi kwa kupewa mikopo yenye riba nafuu.

Vyanzo vya maji

Maji ni rasilimali muhimu sana kwa maisha ya kila siku kwa viumbe hai. Kuna vyanzo vikuu vitatu vya maji:

  1. Maji yaliyopo chini ya ardhi mfano chemchemi na visima
  2. Maji yaliyopo juu ya ardhi mfano maziwa, mito na bahari
  3. Maji ya mvua

Mvua inaponyesha maji huingia ardhini mpaka kwenye miamba. Maji hayo hujitokeza tena juu ya ardhi kama chemchemi au mto.

Maji hutumika nyumbani kwa kupikia, kunywa, kufulia, kuoga na kufanya usafi. Maji hutumika pia viwandani iii kupooza mashine na kuchakata malighafi. Vilevile, maji hutumika kwa shughuli za umwagiliaji na kufua umeme. Umeme unaotokana na nguvu za maji huzalishwa kwa nguvu ya maporomoko ya maji. Mifano ya mabwawa ya kufua umeme hapa Tanzania ni Bwawa fa Nyumba ya Mungu mkoani Kilimanjaro, Mtera mkoani Iringa na Kidatu mkoani Morogoro.

Vitendo vya uharibifu wa vyanzo vya maji

Shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na binadamu huhitaji matumizi makubwa ya maji. Binadamu anapofanya shughuli za uzalishaji mali huweza kuharibu vyanzo vya maji. Vitendo vinavyoweza kuharibu vyanzo vya maji ni pamoja na kulima na kulisha mifugo kwenye vyanzo vya maji, kukata miti na kuchoma misitu. Halikadhalika, kutupa taka na kutiririsha majitaka yanayotoka majumbani, viwandani na maeneo ya biashara karibu na vyanzo vya maji huchafua na kuharibu vyanzo vya maji.

Athari zinazotokana na uharibifu wa vyanzo vya maji

Vyanzo vya maji vinapoharibiwa huleta athari kwa maisha ya viumbe hai. Athari mojawapo ni kusababisha upungufu wa maji kwa matumizi ya nyumbani na viwandani. Uharibifu huo pia huathiri shughuli za kilimo na uvuvi. Pia, uharibifu wa vyanzo vya maji husababisha magonjwa kama homa ya matumbo, kipindupindu, kuhara na kuhara damu. Vilevile, kuweka makazi ya watu karibu na vyanzo vya maji, husababisha maji kukauka hivyo kuleta usumbufu kwa watu.

Njia zinazotumika kutunza vyanzo vya maji

Kwa kuzingatia umuhimu wa maji ni vema kutunza vyanzo vya maji kwa kupanda miti inayohifadhi maji kama vile mkuyu, kutokulima au kujenga karibu na vyanzo vya maji na kutokutupa takataka za majumbani na zile za viwandani katika vyanzo hivyo. Pia, kuepuka kukata miti hasa ya asili na kuchoma moto katika maeneo ya vyanzo vya maji. Viievile, kuweka sheria inayozuia kufanya shughuli za kiuchumi katika maeneo ya vyanzo vya maji. Aidha, jamii ielimishwe kuhusu umuhimu wa maji na njia za kutunza vyanzo hivyo.

www.learninghubtz.co.tz

Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256