FORM FOUR KISWAHILI NECTA 2014

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA NATIONAL EXAMINATIONS COUNCIL

CERTIFICATE OF SECONDARY EDUCATION EXAMINATION

021 KISWAHILI

(Kwa Watahiniwa Walioko na Wasiokuwa Shuleni)

Muda: Saa 3 Jumanne, 04 Novemba 2014 mchana

Maelekezo

  1. Karatasi hii ina sehemu A, B, C, D na E.

  2. Jibu maswali yote katika sehemu A, B na D, swali moja   (1)  kutoka sehemu C na maswali matatu (3) kutoka sehemu E. Swali la 15 ni lazima.

  3. Zingatia maagizo ya kila sehemu na ya kila   swali.

  4. Simu za mkononi haziruhusiwi katika chumba cha mtihani.

  5. Andika Namba yako ya Mtihani katika kila ukurasa wa kijitabu chako cha kujibia.

SEHEMU A (Alama 10)

Jibu maswali yote katika sehemu hii.

UFAHAMU

1. Soma kifungu cha habari kifuatacho kisha jibu maswali yanayofuata:

Karibu masikio ya watu wa mahali pengi yalijaa habari za Karama na mashtaka yake. Umaarufu wake wa ghafla ulizungumzwa karibu na mbali. Mtu yeyote wa desturi anapozuka katika umaarufu, huyavuta masikio na macho ya watu wengi kwa sababu jambo kama hili hutokea nadra sana kwa watu ambao bahati mbaya imeshughulika kuwaweka nyuma. Kwa hiyo, siku ya tatu ya baraza ilihudhuriwa na mfalme, watu wenye vyeo mbalimbali, pamoja na nusu moja ya umati mkubwa wa Kusadikika. Fikra zilizochanganyika ziliushika umati huu. Baadhi ya watu walimwajabia Karama wakamhesabu kama mtu bora wa karne yao. Hawa walitumaini ataokoka lakini wengine waliwaza kuwa Karama alikuwa kama mjinga aliyekuwa akicheza na hatari kubwa iliyofunua taya mbele yake.

Waliokuwa wakimtazamia kuokoka walikuwa na wasiwasi wao; na wale waliokuwa wakimtazamia kuanguka walikuwa na fadhaa yao. Walakini hapana mtu hata mmoja aliyepata kulisema wazo lake.

Bila ya kujua alivyoajabiwa Karama aliendelea kusema mbele ya baraza, “Watu wanaoteswa ndio wanaoyajua mateso yao.” Kusadikika ilikuwa chini ya mateso makubwa sana. Maisha yao yalizungukwa na maradhi na mauti, uadui usiokwisha, nchi iliyokaribia kugeuka jangwa na mwamba na madhila mengine mazito yaliyowakabili watu. Wanakusadikika walitaka faraja katika mateso haya. Kila jitihada ilijaribiwa ili kuirekebisha saa ya maendeleo ya nchi, lakini mara kwa mara majira yake yalirudishwa nyuma. Kama hili lilifanywa kwa makosa ama kwa makusudi ni siri iliyo ng’ambo ya fahamu zangu hata sasa. Lakini kama siri njema hufichika, ile iliyo mbaya haifichiki hata kidogo. Uchaguzi wa wajumbe ulikuwako lakini hathibitisho ya matokeo ya ujumbe hayakupatikana.

Kusadikika iliishi kuona mjumbe baada ya mjumbe kuadhiriwa na kuadhibiwa vibaya. Kama washauri hawakudhuriwa na hili lakini watu wengine walidhuriwa sana. Kazi njema za wajumbe wawili zilipotea bure. Manung’uniko ya lawama hii yalikuwa katika hewa yote ya Kusadikika.

Hili lilipotokea serikali iliombwa ima faima kufanya ujumbe mwingine. Basi mjumbe wa tatu alitakikana ajitolee mwenyewe kwa ujumbe wa Kusini. Wito wa mjumbe wa tatu uliitikiwa na Kabuli; mtu mwenye busara, haya na mcheshi. Yeye alipatikana upesi kabisa kuliko ilivyokuwa kwa mara ya pili na ya kwanza. Misiba ya Buruhani na Fadhili ilikuwa mikubwa ya kutosha kuikongoa mioyo ya bidii katika bawaba zake. Kabuli aliyajua haya yote lakini alikuwa mtu wa moyo wa namna nyingine kabisa. Alikuwa na bidii kubwa kama ile ya siafu athubutiye kukivuka kijito kwa daraja iliyofanywa kwa maiti ya siafu wengine walioelea majini huko na huko. Maji yalijulikana kuwa na asili ya rutuba, mvuke na umeme. Nguvu nyingine za namna mbalimbali zipo pia katika maji. Kama siafu mdudu mdogo na kipofu wakati mwingine haogopi kuzikabili nguvu hizo pamoja na hatari zake kwa sababu njema, basi ni dhahiri kuwa viongozi wa wanadamu wanapoteswa bure bidii za wafuasi wao hutanuka ajabu.

Hapana tishio liwezalo kuukomesha mwendo huu. Kwa hakika utafululiza kuwako duniani mpaka mateso yakome kabisa, na labda wakati huo dunia hii itakuwa njema kama itamaniwavyo kuwa.

Buruhani na Fadhili walitoa sadaka zao bora ili kuyahimiza majilio ya wakati uliotakikana sana. Kabuli aliwaona watu wawili hawa kama wafadhili wakubwa wa ulimwengu. Alitaka kuwa mshirika wao kwa thamani yoyote ya maisha yake.

Kama ilijulikanavyo, Kusini na upande wa dunia yatokako matufani makubwa na baridi kali sana. Kabuli aliyakabili mashaka haya bila ya kigeugeu. Naam, alikuwa kama mtu aliyekuwa akinywa uchungu bila ya kigegezi. Mara mbili alikamatwa akafanywa mahabusu.

Maswali

(a) Eleza maana ya maneno yafuatayo kama yalivyotumika katika kifungu cha habari:

  1. Fadhaa

  1. Madhila

  1. Kuadhiriwa

  2. Ima faima
  3. Kigeugeu
  4.  Kigegezi.
View Ans


(b) Eleza mchanganyiko wa fikira walizonazo wana wa Kusadikika kuhusu Karama.

View Ans


(c) Kwanini bidii ya mjumbe wa Kusini imelinganishwa na bidii ya siafu? Toa sababu mbili.

View Ans


(d) Ujumbe wa mwandishi wa kifungu hiki unahusu nini?

View Ans


2. Fupisha habari uliyosoma katika swali la kwanza kwa maneno yasiyopungua mia moja na hamsini (150) na yasiozidi mia mbili (200).

View Ans


SEHEMU B (Alama 25) SARUFI NA UTUMIZI WA LUGHA

Jibu maswali yote katika sehemu hii.

3. Fafanua utata uliopo katika sentensi zifuatazo:

  1. Mama anafurahia pango.

  2. Mwalimu analima barabara.

  3. Alimpigia ngoma.

  4. Kijana amepata fomu.

  5. Baba anaunda.

View Ans


4. Tumia neno “Paa” katika sentensi kuunda dhana zifuatazo:

  1. Nomino

  2. Kitenzi

  3. Kielezi

  4. Kivumishi

  5. Shamirisho

View Ans


5. Bainisha mzizi wa asili kwa kila neno katika maneno yafuatayo:

  1. Anawaandikisha

  2. Mkimbizi

  3. Mlaji

  4. Muumbaji

  5. Nisingelipenda

  6. Kuburudika

  7. Sadifu

  8. Aliokota

  9. Walichopoka

  10. Kipambanuliwe

View Ans


6. Vibadilishe vitenzi vifuatavyo viwe katika kauli ya kutendeka:

  1. Badili

  2. Kata

  3. Komboa

  4. Zuia

  5. Fika

  6. Zoa

  7. Jenga

  8. Remba

  9. Tumia

  10. Lima

View Ans


7. Fafanua maana ya neno “chenga” kwa kutumia sentensi tano tofauti.

View Ans


SEHEMU C (Alama 10) UANDISHI

Jibu swali moja (1) kutoka sehemu hii.

8. Andika insha yenye maneno yasiopungua mia mbili (200) na yasiozidi mia tatu (300) kuhusu methali isemayo “Samaki Mkunje angali mbichi”.

View Ans


9. Wewe ni mwenyekiti wa mtaa ambao umekumbwa na mafuriko lakini wananchi wako wanakataa kuhamia makazi mapya. Andaa hotuba utakayoitoa kwa wananchi wa mtaa wako ili kuwashawishi kuondoka katika sehemu hiyo. Jina la mtaa ni Kwamachombo na eneo la makazi mapya linaitwa Kitivo.

View Ans


SEHEMU D (Alama 10) MAENDELEO YA KISWAHILI

Jibu swali la kumi (10)

  1. Kwa kutumia hoja tano, fafanua jinsi utawala wa Waingereza ulivyoimarisha Kiswahili nchini Tanzania kwa kupitia mfumo wa elimu.

View Ans


SEHEMU E (Alama 45) FASIHI KWA UJUMLA

Jibu maswali matatu (3) kutoka katika sehemu hii. Swali la 15 ni la lazima.

11. Kutokana na mabadiliko yanayoikumba jamii, baadhi ya methali zimepitwa na wakati. Thibitisha hoja hiyo kwa kutumia methali sita.

View Ans


12. “Ustadi wa msanii hudhihirishwa na fani”. Dhihirisha kauli hiyo kwa kutumia vipengele vitatu vya lugha kwa kila diwani kutoka katika diwani mbili ulizosoma.

View Ans


13. Jadili kukubalika kwa wahusika wawili kama kielelezo halisi cha wanajamii kati ya Takadini, Maman’tilie na Brown Kwacha kutoka katika riwaya mbili ulizosoma. Toa hoja tatu kwa kila mhusika.

View Ans


14. “Kujenga jamii bora ni dhima ya mwandishi.” Thibitisha kauli hii kwa kutumia hoja tatu toka katika kila tamhtiliya kati ya tamthiliya mbili ulizosoma.

View Ans


15. Tunga tamthiliya fupi kuhusu umuhimu wa elimu kwa vijana wa Tanzania ya leo. Tamthiliya hiyo isipungue maneno mia tatu (300).

ORODHA YA VITABU

Ushairi

Wasakatonge - M.S. Khatibu (DUP)

Malenga Wapya - TAKILUKI (DUP)

Mashairi ya Chekacheka - T.A. Mvungi (EP & D.LTD)

Riwaya

Takadini - Ben J. Hanson (MBS)

Watoto wa Maman’tilie - E. Mbogo (H.P)

Joka la Mdimu - A.J.Safari (H.P.)

Tamthiliya

Orodha - Steve Reynolds (MA) Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe - E. Semzaba (ESC)

Kilio Chetu - Medical Aid Foundation (TPH)

View Ans


Download Learning
Hub App

For Call,Sms&WhatsApp: 255769929722 / 255754805256